Salaam,
Leo siandiki ati kwa sababu nahitaji msomaji, na wala sina kile kiherehere cha kujaribu kujithibitishia kwamba naweza kuandika. Lah! Ninaandika kwa sababu ya kuandika tu hasa kwa vile kuandika kama kusema huyatoa yale yaliyoko moyoni yaani huyafanya mawazo kuwa maneno na ustaarabu wote wa binadamu umejengwa juu ya mambo mawili makubwa, mawazo yaliyotendwa ambayo kifupi huitwa matendo, na mawazo yaliyosemwa ambayo kifupi huitwa maneno na neno hili maneno hutumika mara nyingine kuelezea mawazo yaliyoandikwa kama haya ya kwangu ambayo mara nyingi huitwa maandiko.
Tofauti iliyoko hata hivyo kati ya maandiko, maneno na matendo ni muda wa kudumu na kukumbukwa kwa hizi njia zote tatu za kuwasilisha mawazo. Matendo, hudumu muda mrefu na huonwa na wengi, hata hivyo kwa kadri kizazi kimoja kinavyoondoka na kuruhusu kizazi kingine, basi yale yaliyokuwa matendo makubwa na yenye nguvu na maana kwa kizazi kimoja hubadilika kuwa tu msingi wa matendo bora zaidi, lakini hayaleti tena ule msisimko wa awali.
Fikiria kwa mfano juu ya wazo la mvumbuzi wa simu. Wakati alipowaza kwamba binadamu wangeweza kuwa na njia bora ya kuwasiliana kwa mazungumzo wajapokuwa umbali fulani ikiwa tu watakuwa na chombo chenye uwezo wa kusafirisha mazungumzo yao kutoka upande mmoja hadi mwingine na kurudi, bila shaka kama angerudi leo kwenye dunia yetu hii na kuona jinsi ambavyo sasa teknolojia ya mawasiliano imekuwa hata kizazi chetu hiki kinaamini kwamba kinaishi katika ulimwengu wa teknolojia ya habari na mawasiliano, asingeshangazwa kuona wazo lake la msingi kuwa likiishi hadi sasa, bali angeshangazwa na ukweli kwamba matendo yake yaani chomo alichotengeneza hakitumiki kabisa leo. Mifumo na vyombo vitumikavyo leo kwenye mawasiliano kama tuyajuavyo leo, ni matokeo ya uboreshaji wa mawazo ya yule aliyewaza kwanza juu ya mfumo huo na kuyatia mawazo yake katika vitendo. Ni jambo linaloshawishi kuamini kwamba hakuwa akiwaza mawasiliano kwa mifumo na viwango tulivyo navyo sasa. Na hivyo kazi yake kwa maana ya vile alivyoyatendea kazi mawazo yake vile alivyoyawaza imesahahulika na leo wako wengine wanaoutukuzwa kwa uvumbuzi bora wa mifumo na vyombo vya mawasiliano kuliko Alexander Bell ambaye mtambo wake aliotengeneza yaweza kuwa kwamba hauko leo hata kwenye majumba ya makumbusho . Kinachosemwa hapa ni kwamba matendo japo huwa makubwa na huacha nyuma yake mchango usiopingika, lakini usahauliwa upesi zaidi katika mifumo yote hii mitatuu ya uwasilishaji wa mawazo.
Maneno ya hekima huwa kama msumari uliogongomewa sana katika mioyo ya wale wasikiao, lakini maneno husahaulika haraka zaidi na utuzanji wake hata kwenye ulimwengu ulioendelea kama huu wa kwetu wa sayansi na teknolojia bado ni mgumu sana ukilinganisha na maandiko. Inawezekana pia kwamba maneno hupata zaidi maana yake kutoka kwenye sauti na nota wakati wa kutamka na hivyo japo ni rahisi kusema fulani kasema hivi ama vile, lakini si rahisi kuwasilisha kwa jinsi alivyosema yeye wakati aliposema kwa vile sauti yake ni yake na mvumo wa sauti hiyo wakati akisema neno hilo ulikuwa wa maana sana ili kulipa neno lenyewe maana.
Ndiposa binaadam tangu kale amefahamu umuhimu wa kuandika na sehemu kubwa ya historia ya binadamu iliyotunzwa hata sasa imetunzwa kwa kuandika japo si kuandika kule tukujuako leo. Wamayani kwa mfano, ndiyo jamii yenye historia tajiri kuliko nyingi na ambayo yaonekana kuwa na mchango mkubwa kwenye mambo mengi yatumikayo na binaadamu wa leo, na sehemu kubwa ya maandiko yao yameendelea kutafsiriwa kizazi hadi kizadi yakitufunulia kile walichokijua wakati huo na walichokitegemea kwenye ulimwengu ujao baada yao.
Imani zote za dini duniani, zimejengwa pia kwenye maandiko yaliyoandikwa na wale waliokuwako kabla ya baba zetu na hata sisi na yatakuwako baada yetu na watoto wetu japo imani na uchaji wake hutofautiana toka kizazi hadi kizazi.
Kwa kutambua maana, heshima na nafasi ya kuandika ndiyo maana leo naandika.
Naandika mawazo kwa vile kila binadamu huwaza, naam, hata wale ambao wanadhani hawana muda wala haja ya kusoma, kusikia ama kufahamu mawazo ya wengine, nao huwaza na wanalo hitaji la kufahamiwa na hata kuheshimiwa mawazo yao na ingewasaidia kujua kwamba wako watu wengine wawazao kama wao au hata kinyume chao juu ya mambo kadha wa kadha katika ubinadamu wao.
Kama umesoma mpaka hapa, maana yake umekubali kwamba na wewe huwaza na kwamba unalo hitajio la kujua mawazo ya wengine hata kama hukubaliani nayo na ama unayaona kuwa ni upuuzi lakini bado unajua kwamba ni mawazo.
Labda sasa umebaki ukihitaji kujua ni mawazo juu ya nini? Hili jibu lake ni rahisi tu. Ni mawazo juu ya mawazo kwa sababu maisha yote na ustaarabu wote wa binadamu ni mawazo yaani matendo ni mawazo yaliyotendwa, maneno ni mawazo yaliyosemwa na hata maadiko ni mawazo yaliyoandikwa na hivyo huwezi kumtenga binadamu na mawazo.
Hivyo leo nimeamua wakati nilipoamua kuandika, hilo lilikuwa ni wazo lililotokana na wazo juu ya muda na hivyo nitakushirikisha mawazo yangu kuhusu muda.
Miasha ya binadamu yanaonekana kupata tafsiri yake kwa kutumia muda walau hayo ndiyo mawazo yangu. Wakati tunapozungumzia umri wa mtu, kitu ama taasisi, tunazungumzia muda ambao mtu, kitu ama taasisi husika imekuwapo.
Pia muda ni moja ya vitu adimu lakini visivyohitaji fedha kuwa navyo na ndiyo maana watu wote dunia kote wamepewa muda kwa kiasi sawa. Binadamu na awe upande wowote wa dunia, rangi yoyote ya ngozi yake na hata jinsi yoyote ya maumbile yake, anazo saa kumi na mbili za mchana na saa kumi na mbili za usiku. Katika saa hizi, binadamu hupata nafasi ya kuwaza na kusema ama kutenda mawazo yake.
Wakati binadamu anapofanya shughuli yoyote, anachofanya ni ama kutumia muda wake kutekeleza mawazo yake ama ya wengine. Ukweli unabaki kuwa kwamba binadamu anatumia muda kutekeleza mawazo iwe ni kwa kutenda ama kusema.
Kwa hiyo, kama maisha ya binadamu yangekuwa chakula ama kinywaji, basi tungesema kinywaji hiki kinahitaji mchanganyiko bora wa vitu viwili tu, navyo ni mawazo na muda na kwamba uchanganyaji wa muda na mawazo ndivyo huamua ikiwa maisha ya binadamu huyu yatakuwa mazuri ama mabaya.
Uko msemo miongoni mwetu uliosemwa na wale waliokuwa kabla yetu usema “Hekima ni uwezo wa kutenda ama kusema neno sahihi, mahala sahihi, kwa watu ama mtu sahihi, kwa wakati sahihi, na lugha sahihi”. Ni mawazo yangu kwamba usahihi woote unaweza kuharibiwa tu ikiwa tutapatia maeneo mengine ya kauli hiyo tukakosea usahihi wa muda.
Kwa hiyo kwa maelezo hayo tumeona kwamba mawazo na muda huwekwa pamoja kuleta ama madhara au faida kwa binadamu.
Ni mawazo yangu kwamba muda ni sawa na fedha iwekwayo kwenye akaunti ya benki. Ebu fikiri hivi, kwamba kila siku asubuhi, fulani hukuwekea fedha kiasi cha shilingi themanini na sita elfu na mia nne, na kukwambia utumie fedha hizo kwa kila siku na kwamba ikiwa utabakisha, kiasi utakachobakisha hakitaweza kuingizwa kwenye akaunti yako kesho, bali kesho utapewa kiwango kile kile cha fedha.
Hii ingemaanisha kwamba ungetumia shilingi elfu tatu na mia sita kwa saa moja na kile ambacho ungenunua kwa fedha hizo ni juu yako. Ndivyo na muda. Unazo sekunde 3600 kwa kila saa moja na unachofanyia sekunde zote hizo ni juu yako. Kwa mfano, muda unaotumia kusoma makala haya, utakuwa umetumika kabisa na kuptea milele na ikiwa hutapata faida yoyote kwa kusoma makala haya, basi utakuwa umepata hasara ya muda wote uliotumia kuisoma.
Wakati nikiwaza haya na jinsi muda ulivyo wa muhimu katika matumizi yake, nikaona nikuandikie ili nikueleze ujibidishe kutumia muda wako kuwaza na kutekeleza mawazo yako. Mimi nimewaza kuandika makala haya na nimekuandikia.
Wasalaam,
Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangu pakavu wa Kabwela wa Mdanganyika.