Najua! Najua umekuwa muda sasa tangu nimepitia kijiweni hapa
walau kukusalimia na si kwamba nilikusahau, ila nilikuwa kwenye ule mchezo wa
sasa ambao kila mtu ni lazima acheze tangu mdogo hata mkubwa, maskini ama
tajiri, msomi kama wewe ama mbumbumbu kama Chokoraa, nao ni mchezo wa kuwa “bize’.
Naapa simo. Si kwamba simo kwenye mchezo wenyewe, isipokuwa kwa vile wako ambao
wako ‘bize’ kila siku na wapata chochote kitu ilhali wengine wako ‘bize’
waambulia umaarufu wa harufu, humu namo simo.
Ha ha ha ha ha ha!! Nicheke miye Chokoraa wa Muhangaikaji wa
Mlalahoi wa Pangu pakavu wa Kabwela wa Mdanganyika si kana kwamba nina furaha,
lakini nani kasema hii “gunia” yetu ni kama ile ya babu yangu Pangu pakavu
ambapo walioweza kupata habari, wachilia mbali walioweza kutoa habari walikuwa
wachache sana na wenye daraja fulani katika jamii!!? Washangaa nini! Nakumbuka
miaka hiyo kulikuwa na vyombo vichache sana vya habari na vyote vilikuwa kwenye
‘siri kali’ vikitumiwa tu na ‘watwawala’ kuwapelekea amri ‘watwaliwa’ na hata
sheria ikaweka kwamba ili iwe sheria ni lazima kwanza itangazwe kwenye gazeti
la ‘siri kali’. Ha ha ha ha ha ha!!! Leo watu wasema na sisi kupitia ‘ubunifu
wa Buibui’ na mwana wa Muhangaikaji nasikika kupitia kamchezo hako ka mdudu Buibui
na bado wataka ati nisicheke! Simo humu.
Haya, wacha basi nikupe pole kwa msiba maana siku hizi kwa
ajiri ya wadanganyika woote kuhama mitaani na vijijini kwao wakishinda “bize”
na kurudi jioni ama usiku mwingi, basi utamaduni wetu umebadilika na hata
misiba haihudhuriwi kama ilivyokuwa zama na ndiyo maana hata Chokoraa sikuwa
nimepata nafasi ya kukupa pole ya misiba. He! Ona huyu ati hajui kwamba kwenye ‘inji’
hii tumepata misiba mikubwa kadhaa na ya kitaifa kwa sababu ati naye alikuwa ‘bize’
kiasi cha kushindwa kusoma ‘udaku’ na kutazama kasanduku ka picha ama
kusikiliza ile radio ya mwenyekigoda wa kijiji chao, hata alipoingia kwenye
makaazi ya Buibui yaani ‘mtandaoni’ hakupata nafasi ya kusoma ‘niuzi’ zaidi ya
kupata ‘esi emu esi’ kadhaa kwa BBM na kuishia kulala ili adamke mapema na
kukimbilia ‘bize’, naapa utamaduni wa binadamu unafirisika kila kukicha na humu
simo.
Nasema mnitoe kwenye huu mufirisi wa ustaarabu wenu enyi
wadanganyika maana mtu asite utamaduni ni mfungwa wa kifungo cha nyumbani walau
hivyo ndivyo nijuavyo Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi na kwa hili naapa
tutashindana sana lakini simo. Hivi si ulikuwa utamaduni wenu enyi wadanganyika
wa kuheshimu watangulizi wenu iwe ni wazazi nyumbani ama viongozi kwenye hizo ‘siri’
zenu ‘kali ‘ na hata mlikuwa na ‘proto kali’ ya kutokunywa kahawa kama
mwenyekigoda hajafika? Nasema huo unaoonekana kama upuuzi kwenu ninyi masharo
wa sasa ndiyo ulikuwa misingi ya uzalendo wa watu wa inji hii na hata kujitolea kufa kwa ajiri ya ‘udanganyika’
wao kwa sababu walau walijua ‘legasi’ yao ingebaki. Sasa naapa kila mmoja
anataka kuwa “msanii” na nimtumie pole ‘mzee wa ukweli usio wazi’ kwa juhudi
zake za kutaka ati kuifanya ‘danganyika’ yake isiitwe tena ‘bongo’ kwa vile ati
‘usanii’ ulizidi. Nani anataka kuwa ‘hiro ov ze nesheni’ (naonyesha msisitizo)
kwa kutumikia inji hii ilhali anaweza kuacha ‘ligasi’ kwa watoto wake kwa kuwa
muuza sura luningani nasema mnitoe. Ati wakulu wote wa kaya wakajikusanya na kujirundika
kwenye msiba wa ‘msanii’ na kuishushia heshima ya ‘kiifitaki’ misiba ya mashujaa
wa inji hii hadi wale walioliongoza ‘geshi la waheshiwa tangu zamani’ naapa
humu simo. Nasema kwa hili Chokoraa nitasema na kurudia kwamba adabu si
shikamoo na uungwana ni vitendo, kizazi hiki kimekosa adabu kwa watangulizi
wake na namuomba jalali awajaalie mzeeke ili muone jinsi inavyoumiza kwa kizazi
kinachofuata baada yenu ‘kuikanya legasi’ yenu chini ya nyao za miguu, siyo
nawalaani nawaombea maisha mema na ya neema ila kwenye hili la dharau mimi
simo, tena simo kabisaaa.
Nasema kama mgekubali kuwa wanafunzi mgejifunza maana
waalimu wako wengi waliotenda vyema kabla yenu ili muone na kujifunza kwao
lakini nani kasema adabu inauzwa ama hukwanguliwa kama vocha!? Naapa simo. Ala!
Kwani wakati ‘mzee wa kuruhusu’ alipoamua ‘kushtuka’ (naogopa kusema kizanaki
msijesema natumia vibaya lugha ya taifa) na kujiweka pembeni ‘kuepusha
msongamano’ ilimnyima nini kuwa ‘mkulu wa kaya’ wakati ulipowadia!? Au ni kwa
sababu ninyi sasa mmeendela sana na mnaamini “riziki kama ipo ichukue kama
haipo ilazimishe” na hivyo mwaona kung’atuka ni aibu?.
Labda ni kweli kwamba hamna heshima kwa ‘wazee’ wenu tena
enyi wana wa danganyika maana nani hakusikia wakati mlipowatazama usoni wazee
wenu na kuwahoji sababu ya wao kutotumia hayo mawazo mazuri wanayokupeni
kipindi cha ‘wakati wao’ mkisahau kwamba wakati ukuta?. Naapa mna zaidi ya
kiburi enyi wana. Nasema kama ilivyokwisha kusemwa kwamba sokoni hupatikana
vyote yaani chakula na uchafu na cha pili si aghali kupatikana kwake japo
matumizi yake ni adimu na ninyi mmejifunza kwa watangulizi wenu lakini kama
waenda sokoni mmechukua uchafu mkaacha chakula ashakumu si matusi, humu simo.
Ala! Kwani si mmeamua kwa makusudi kujifunza kwa wale waliojitokeza hadharani
mbele ya visanduku vyetu vya picha, tena tunavyoviwasha kwa umeme tunaoulipia
sisi wakitwambia wala si kutuomba kwamba tugeuke mbuzi na ng’ombe tule nyasi
lakini wao wanunue “mwewe” kwa ajiri ya ‘mkulu wa kaya?”. Nasema mmejifunza kwa
hao na mmefaulu na humu mimi nakataa kuhusika, simo tena simo kabisa.
Ni hivi juzi tu, mlikulana na kuparurana makucha huko kwenye
jumba la maamuzi na kutaka hata kuvuana nguo na wala hii si mara ya kwanza ama
ya pili walau kwa siku za karibuni, lakini tofauti na mwanzo wakati watu
walipojipachika majina kama “Bangusiro’ na mengineyo, ninyi mmekataa kuwa ‘mbuzi
wa sadaka’ na badala yake mmekuwa ‘ngangari’ kwenye kuendeleza ‘yale yote
ambayo kwa moyo na nia thabiti mmekuwa mkiitendea inji hii’ na kwa hili
nakupongezeni ila mi mnitoe maana simo. Naam, mioyo na nia zenu ni thabiti katika
kutenda lakini mnatenda kama waenda sokoni maana pana faida gani kuendelea
kuonyesha njia mbele ya mtu ambaye hayuko tayari kukufuata? Naapa nilidanganyika. Ndiyo, ni uzembe wangu
kwamba nilidanganywa nikadanganyika kwamba kiongozi wa domo daraja la kwanza
ama domo class A huzingatia misingi ya ‘domo class A’ yaani utawala wa watu
kupitia watu kwa ajiri ya watu, kumbe sivyo na humu simo tena simo kabisa.
Nakataa kuwamo kwa sababu kama watu (kupitia mawakala wao) wamekataa kwamba
fulani na fulani hatutaki muendelee kutangulia huko mbele, si adabu basi kwamba
mjitenge na kuwaacha watu wachague watu wengine wa kuongoza njia ya watu kwa
ajiri ya watu ama ninyi mnayo tafsiri nyingine ya ‘domo krasi ei’?
Sitaki kuongea sana wacha haya machache yatoshe kwa leo na
niwape pole wadanganyika walipa kodi kwa misiba mikubwa ya kitaifa
iliyowakuteni ikiwamo kuondokewa na wazee wetu, waliojitolea kufa na kupona,
waliorudisha fedha za serikali kwa sababu waliamini kwamba wamelipwa zaidi ya
walivyotumia na hatuwezi kwa na mfano bora zaidi wa uwajibikaji na uzalendo
kama huu. Nasema jifunzeni kwa hawa kama bado mmebakiza sehemu ya kuingiza
mafunzo mapya kwenye fahamu zenu lakini ikiwa tayari mmekwishakuwa mbwa wazee
wasiofunzwa mbinu mpya, sina jingine la kuwaambieni isipokuwa kuwasalimiwa.
Wasalaaam, ni mimi ndugu yenu Chokoraa wa Muhangaikaji wa
Mlalahoi wa Pangu pakavu wa Kabwela wa Mdanganyika, nawasalimia.