Saturday, July 14, 2012

Chokoraa na 'Fotoa Foto'

Hapa ni "Ng'wanza" wenyewe mwaita 'Mwanza'. Tumekuja kushuhudia mchakato wa BSS chini ya udhamini wa Zantel.
Ha ha ha ha ha ha!!! Ati wajiuliza namaanisha nini? Kwani mbona wewe hutambai tena siku hizi!? Ndiyo, nasema na Chokoraa anakua na kuongezeka na hizo ni baraka za jalali na kama unabisha basi kwenye huo ubishi mi simo tena simo kabisa. Ala!. Haya basi, kuanzia sasa naanza kuwaletea picha kadha wa kadha ambazo Chokoraa wa Kabwela amekutana nazo kwenye kuchakulachakula majalalani huku na huko, walau kila mwisho wa Wiki.

Wiki hii, meli maarufu kwa kusaifirisha mizigo toka Bandari Salama hadi kisiwa cha Mafia iliteketea kwa moto baada ya mmoja wa wafanyakazi wake kujaribu kuwasha jenereta ili ku-pump nje shehena ya mafuta ya Tanesco yaliyokuwa ndani ya meli hiyo.

Wananchi wakishuhudia meli hiyo ikiteketea kwa moto. Wananchi wamekitupia lawama kikosi cha Zimamoto wilayani Mafia kwa kushindwa kuonyesha makeke yoyote kwenye tukio hilo. Hata hivyo, shehena ya mafuta iliyokuwemo kwenye meli hiyo iliokolewa yote ilhali kiasi cha pikipiki mbili, na gari moja vilivyokuwa mali ya watu binafsi vinaripotiwa kuteketea kabisa. Hili ni tukio la pili kwa meli iliyobeba shehena ya mafuta ya Tanesco kupata mushkeli ambapo miaka kadhaa meli nyingine ikiwa na shehena ya mafuta ya Tanesco ilizama baharini ikitokea Dare salaam kwenda kisiwani Mafia.