Monday, April 22, 2013

TUKANANENI WAKATI WADANGANYIKA TWALIWA.



Salaam nawasalimia.
Nasema tofauti kati ya jana na leo hutambulika na mwerevu kwa mjinga ni usumbufu na mimi sina haja hata kuieleza tofauti yenyewe maana muda na nafasi havinitoshi, hivyo naishia tu kuwasalimu, salaam nawasalimia.
Ingawa Chokoraa mwana wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika nimekuwa mpenzi sana wa kale kamchezo ka kizazi hiki ka kuwa “bize”, kwa hili imenilazimu nikae chini ya ukuta wa pagala hasa baada ya kula kipande cha mkate niliiokota jana, niwatumieni salamu enyi ndugu zangu Wadanganyika walipa kodi. Ati! Wakataa nini kwamba wewe si Mdanganyika ama si Mlipa kodi!. 

Nasema juzi juzi binafsi nimeshuhudia akina kaka na dada ‘Muishiwa’ si tu wakibishana bali nimeshuhudia wakimwagiana mitusi na mara hii siyo tu ya nguoni bali hata ya msalani, mnisamehe.  Nasema ukubwa si miaka wala akili maana ikiwa utaamua kupima akili ya samaki kwa kumlazimisha kupanda mti, utaendelea kuwa mjinga kwa kudhani samaki hana akili na humu mnitoe.  Pia ukubwa si majukumu maana hata mtoto mchanga analo jukumu la kula na kulala na ikiwa atashindwa kulitekeleza vyema basi matabibu wataitwa ili waone kwanini ameshindwa jukumu lake, na humu najitoa. Ukubwa ni kutambua, kukubali na kuheshimu upana na mipaka ya majukumu yako tena kwa uadilifu mkubwa ingawa naapa si hizi uadilifu ni msamiati mpya kwenu nyie wana wa Mdanganyik mlio na umaarufu wa harufu na humu nitoeni. 

Ala! Ati mwataka sasa kwa vile na Chokoraa miye nimeghadhibika kwa kunichafulia shati langu jeusi kwa utomvu wenu wa nidhamu nimwage mitusi ili tufanane!? Sihusiki. 

Nauliza, kwani nyie wenye nguvu ya ukinzani kazi mliyopewa na Mdanganyika ni ipi? Nauliza ikiwa mlitumwa huko kilingeni ili mtumie uwezo wenu wa kukinzana ili mkinzane mpaka na yale yaliyo ya asili yetu kama busara na adabu!?. Nasema kwenye hili mi simo. Kwani hatuwezi kukinzana kwa hoja na hata tukaelewana bila kulazimika kutumia ubabe usio na faida? Si nimeshuhudia baadhi yenu mkitunisha misuli kujaribu kubaki kilingeni baada ya mwenyekigoda kutoa amri ya ‘auti’?.  Nani alidanganya nikadanganyika Chokoraa miye kwamba ati wenye nguvu ya ukinzani basi wanao pia uwezo madhubuti wa kuitumia nguvu hiyo kunitetea mimi na wadogo zangu wale wawili akina Mzembe na Mzururaji?. Si mmechomolewa mjengoni baada ya kupandishwa jazba kidogo na watu wakajipitishia ulaji wao bila hata haraka! Ha ha ha ha ha ha ha ha!!! Kama akili ni nywele basi kumbe ndiyo maana mwenye kigoda wenu naye kaamua kuzitia zake mafuta ya kizungu ili ziwe na mng’aro kwa waonao. Simo humu. Hivi kwani mlichokuwa mkijadili mle ndani ni maonevu mnayotendewa na ‘watwawala” ama mipango ya mapato na matumizi ya kodi ya Mdanganyika mlipa kodi!? Nasema mlipoamua kuendesha gari mkielekea usoni ilhali macho yako kwenye vioo pembe mlinunua shubiri kuitia mahala pa sukari na miye najitoa.

Ha ha ha ha ha ha ha!!! Nicheke kama mazuri mwana wa Kabwela miye. Ala! Kwani hamkujua nyie kwamba wakati jinsi ilipotumika kama kigezo pekee cha kuwachagulia mwenye kigoda, siyo tu makubaliano ya ajira kati yenu na mzee Mlipa Kodi yalivunjika, bali pia mlichumiwa vimbo ya akiba ili iwatieni adhabu pasina sababu wala adabu kwa wakati wake!? Naapa asiyeiona tofauti ya jana na leo kesho yake ina taabu na mimi simo. 

Haya, na nyie wenye kunitawala badala ya kuniongoza najiuliza nini kilikusukumeni na nyie kumwaga mitusi kedekede!?. Wenye ukinzani naweza kuwaelewa ikiwa wanaghadhibika na hata kutupa matusi ijapo kusema kweli sehemu kubwa ya kilichotamkwa ni kile ambacho zamani kiliitwa ‘maoni binafsi’ kwa vile ikiwa ninaamini kwamba ‘mdogo anamtawala mkubwa na nikasema hivyo’ kosa langu ni kuamkia salamu ya mchana ilhali ni asubihi hilo nalo ni ukosefu wa hekima, lakini walau nimekusalimia . Nasema naweza kuwaelewa kwa sababu yawezekana wanataka Mdanganyika mimi mwenye kukasirika nisipige mtu bali kura wakati ukifika wa hasira yangu niwapigie wao badala ya ninyi na hivyo wanchofanya ni kukutieni utomvu wa mashati yenu ‘matukufu’ kwa weupe wa mkorogo ili mchafuke, na mimi nauliza, ilikuwaje basi mkaamua kuyavua na kuyachovya wenyewe kwenye utomvu wa wakinzani wenu!? 

Hii michezo ya kukimbizana na kunguru aliyekwiba taulo lako ukiwa maliwatoni itakuponzeni naapa. Simo.
Hata hivyo si lengo langu kuwakosoeni bali kuwasalimia. Nasema mwisho wa yote binafsi nawasifu kwa ujuzi na weredi mkubwa mliionyesha kwa ama kutiana jazba na kutupana nje ya jengo huku mkiwa mmejipitishia bajeti za kutafuna kodi za wadanganyika bila tafakuri ya kina kwa vile wote mlikuwa kasi kurushiana mitusi na kuzinduka mshapitisha ulaji, na kwa kuwazidi akili Mbwa wa wadanganyika waliokabidhiwa jukumu la kulinda kodi zao hata mkazitafuna huku wao wakiwa bize kupandisha jazba. Ha ha ha ha ha ha ha!!!! Kweli, hamzumgumzi na mbwa na hata wenye mbwa hawana uwezo wa kuzungumza nayi.  Simo humu namo.

Salaama nawasalimia.