Kaka Mkulu wa Kaya, salaam
nakusalimia,
Nasema kuwa huru si rahisi kama ilivyo si rahisi kuwa rais
na sasa Chokoraa nawasalimia. Kubadili majalala huku kuna siku nitaingia kwenye
jalala la tindikali naapa kwa jina la bibi yangu mzaa mama yangu Shida wa
Matatizo msinihusishe. Nasema msitake niseme kwa mtiririko maana yaliyonijaa
kwenye koo ni mengi na njia ya ama kuyameza ama kuyatema ni ndogo na hivyo
wacheni niyatapike liwalo na liwe maana ni bora moja kuliko sifuri na humu miye
nahusikaje!?.
Kwani nani kaiona ramani ya kaya yetu, ile ramani halisi ya
Danganyika ya Wadanganyika tuliyoachiwa na wazee wetu kabla haijabadilishwa na
hawa wenye kujitangazia uhuru kila uchao kisa “uhuru na haki za raia” na mimi
nauliza ni nini uhuru na haki za rais na kwa hili mnitoe maana simo.
Kaka mkulu wa kaya, nimetumwa na wadogo zangu akina Muuza
Mayai na Karanga, na hata mama yangu mdogo Mama Ntilie kanituma
nikusalimie. Hawa wawili wanasema
wanakumbuka kabla ya kufariki baba wa kaya yetu na kabla ya wewe kuteuliwa na
kikao kilichopita cha ukoo kuwa Mkulu wa Kaya na kuongoza kundi la akina kaka
Muishiwa wa Maadili na Kiongozi Mbadhilifu katika kuiwakilisha kaya yetu hii,
tulikuwa sisi wote ni wamoja watoto wa mzee Mdanganyika Mlipakodi na mama yetu
Bi Mzalendo.
Ati wanasema baada ya kufariki baba yetu, kundi lenu
likiongozwa na akina kaka Muishiwa walimpendekeza kaka yenu mkubwa Mtukutu
kutuelekeza kule yalikofichwa maisha tarajari ya kaya yetu na ati baada ya siku
chache kaka yetu huyu kujitangaza kuwa ‘Mtukufu’ watu wakaogopa lakini kwa vile
ati kilikuwa kizazi kilicholelewa vyema na marehemu baba yetu kwa kutohoji yale
yafwanywayo na wale wenye kuvaa lile joho lefu la baba na wenzake lenye rangi
ya Kiongozi, basi wakakaa kimya. Hata hivyo yale yaliyotendeka ati yalitendeka
na hata akina Mlalahoi wakaanza kujenga maghorofa kwa kuuza vitunguu swaumu
nisikuchoshe na historia, salaam nakusalimia.
Baadaye ndipo kijiti alipopewa kaka mkubwa Muishiwa.
Wanasema ati huyu naye kwa sehemu alizingatia sehemu ya mafunzo ya marehemu
mama yetu Mzalendo binti Mdanganyika ijapokuwa ni kweli kwamba yeye kijiko
chake kilikuwa kikubwa maakulini ukizingatia na sisi wengine, lakini walau
alijenga daraja na siyo ukuta, nasema nisikuchoshe ila salaam nakusalimia.
Sasa kuna Yule dada yetu mkubwa ambaye hasa ndiye
aliyenifanya nikuandikie waraka huu hasa kwa vile binafsi naweza nisipate
nafasi ya kuonana na wewe mwaka huu, si kwa sababu sipendi ama ati kwa vile naogopa
wale walinzi wako kama mjomba, lah! Bali kwa vile lile daraja kutoka huku kwetu
kuja huko kwenu lina mushkeli kidogo hasa baada ya juzi tu wadanganyika
kuchoshwa na kuamua kutenda watendavyo mradi iwe iwavyo, salaam nakusalimia.
Nasema watu wakichoshwa ni heri ya punda mzee kubeba mzigo
yeye na mwana kuliko mtu ama aliyeshiba mema au asiyekula kabisa maana wote
huwa na wazimu kwa sababu tofauti na mimi humu sihusiki.
Dada yetu mkubwa Mjasiriamali ameniagiza nikusalimie na
kisha nikueleze kwamba kwake yeye ijapokuwa hapendi hata kidogo jinsi ati
unavyotuhumiwa kwa mjomba na shangazi kuwa na sauti nzito kuliko wewe
kwenye kaya yetu, lakini walau alikuwa
bado angali na imani na ile “Siri kali” labda kwa vile ilikuwa imefichwa na
haikujulikana kwake na hivyo si kwamba aliiamini “Siri kali” bali aliamini
kwamba kuna siku na yeye atakuwa sehemu ya wale wenye kuifahamu siri hiyo
ifichwayo kwa udi na uvumba na hilo linanifanya salaam nakusalimia.
Anasema baada ya hivi majuzi watu wasiojulikana kujitangazia
mamlaka bila madaraka na kuufunga mji wa Mtwara tena pasina kupata upinzani
wowote kutoka kwa walinzi wa “Siri kali”, dada yangu mjasiriamali amejiuliza
maswali kadhaa ambayo machache yake amenitaka nikuulize na mimi sasa nakuuliza;
Hivi ni kweli kwamba ile “Siri kali” yetu imevuja na sasa kila aliyeko nje
anaona ndani kama aliyeko ndaniaonavyo nje!? Nasema usijesema miye sina adabu
ninazo tena tele lakini najiuliza inawezekanaje kwamba genge la “wahuni”
linafunga mji kiasi Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa
Kabwela wa Mdanganyika na hata dada yangu chakaramu Mjasiriamali hatuwezi
kutoka ndani na kwenda kuokoteza mkate wa siku? .
Samahani unisamehe, si hoja yangu ya msingi ikiwa ni sahihi
kwako kujenga njia ya panya na kupitisha gesi, oil ama mafuta hiyo kwangu si
hoja. Nasema yafaa nini mimi kuhoji ikiwa hilo ni sahihi ama si sahihi ikiwa
mimi Mdanganyika sina haki wala hadhi ya kuhoji usahihi ama tafsiri ya usahihi
wenyewe?.
Kinachonikera mimi na dada yangu Mjasilia ni kwanini na hasa
inawezekanaje kwamba ‘watu wasiojulikana’ wanaweza kufunga mji na biashara zake
zote na hadi sasa wakawa bado “hawajajulikana”?.
Ati! Utani wa kuniambia tena ati ni “kundi la wahuni”
wanaohatarisha maisha ya wadanganyika wa Ntwara tafadhali tuuacheni maana
wahuni hawa sasa wamepevuka mno kutoka daraja la kawaida la uhuni sasa
wanaelekea kuwa ‘waahini’ na mimi humo sihusiki. Hivi inawezekanaje kwamba watu
‘wasiojulikana’ ama “wahuni” kama ambavyo baadhi yenu mtataka nisadiki, kwa
kutumia ‘vikaratasi’tu wameufunga mji na
biashara zote kusimama?.
Nasema kwa hili msinihusishe hata kidogo. Haya, ebu niwaze
kichokoraa. Hivi wakati ‘tanchi’ la kwanza lilipopigwa, vipeperushi si vilikuwa
vimeanza kusambazwa tangu jumatatu na tanchi lilipigwa ijumaa! Nani kasema unahitaji
‘kadigirii’ kujua kwamba hapo katikati kulikuwa na jumla ya siku tatu nzima na
jumla ya saa sabini na mbili za kuwasaka na kuwatia ‘mtaroni’ agha! Samahani,
kuwatia mbaroni ‘wahuni’ wanaoongoza vitendo hivi!? Hivi siku hizi wale ‘sungusungu’
wako wa kaya nao wamekuwa butu hawana meno kazi yao imebakia kututishia siye
vitukuu wa mdanganyika lakini linapokuja suala la usalama wa kaya nao hawajui
cha kufanya!? Kama ni kweli wanafanya kazi “araundi ze kloku” kama msemavyo
ninyi, nini kilifanya hadi ‘tanchi’ la ijumaa 17 likatokea?
Ha ha ha ha ha ha ha!!! Nicheke kama mazuri. Kwani hamkujua
kwamba kwa kuruhusu watu hawa ‘wasiojulikana’ kuufunga mji siku moja mliwatumia
salaam kwamba wanaweza kufunga mji wakati wowote watakao! Haya sasa wameanza
kuufunga kila wanapotaka na mimi humu sasa nahusikaje?.
Haya, hili sasa limekwishatokea. Lakini hivi ni kweli kwamba
wale wanaohamasisha vurugu hizi wanatumia maneno matupu kama mnavyotaka niamini
miye kitukuu wa Pangupakavu!? Naapa humu miye sihusiki. Nakataa kuhusika maana
ikiwa ni uhafidhina wangu ama ni kweli waliyosema wale waliosema kale, basi “maneno
matupu hayavunji mfupa” sasa nyie mwaniambiaje ati wanaoshawishi vurugu hizi
wanasema maneno matupu yasiyo mashiko!? Sasa mbona mfupa unanjika!? Nitoeni nasema.
Au mwataka niamini upinduzi
kwa kutumia ‘propara lenye maganda’ kwamba wadogo zake na Nchumali wa Chipoku ni wachoyo
wa ‘asili mali’ zilizoko kwenye ardhi yao ilhali wao wamefaidi za wenzao?
Nasema na kwa hili mnitoe. Haya, basi tumieni wingi wa busara mlizojaaliwa na
hata tukawaamini kuwavisha majoho mvaayo kujibu walau kwa kiwango cha uelewa
wao ni kwanini viwanda vya sangara viko Mwanza, migodi ya Dhahabu iko Geita na
Mara na viwanda vya Pamba na Kahawa viko mahala pa mazao hayo lakini vile vya
kusindika Gesi vyajengwa huko kwingineko!? Sisemi hamna majibu ya swali hili,
lakini yatoeni basi na kwa namna ya kueleweka hili na mimi nisishangae kama
ninavyoendelea kushangaa. Bhaaaaa!! Mwanishangaza enyi wana.
Nasema mzaha mzaha hutumbua usaa, au kwa vile ninyi ni wa
kisasa mwaamini mzaha mzaha huwafanya watu kucheka na hivyo kuongeza siku za
kuishi!? Naapa ninyi ni kizazi cha wenye hekima na mtakapokufa ninyi basin a hekima
nayo itakoma na humo nitoeni.
Haya, nijuzeni na nyie wenye kufunga mji mwamkomoa nani!?
Nasema hawa waliishauza nafsi zao na konzi la kifaranga halimuumizi Kicheche
enyi wana. Kwani mnadhani ikiwa mmefunga bishara na kuharibu uchumi wenu kwa
siku kadhaa ndipo mmeweza kuwakomesha hawa ‘wezi’ wenu? Naapa wao
walikwishashiba halali na mlungula kilichowasalia wao ni heshima na uishiwa na
labda kesho ya vizazi vyao ambayo wao wanakusudia kuipata iwe kwa kumaliza
vizazi vyenu ama kuharibu kesho ya wanenu, basi tumieni busara badala ya mabavu
ilhali mli hali dhoofu kwa kula kidogo na kutenda kazi sana.
Wacha niyamaze miye maana nasikia kaya yetu hii mama mkwe
akitembea uchi unaruhusiwa tu kuwaza kwamba mama mkwe yu utupu lakini ukisema
hivyo dhambi. Ati! Kwani mnadhani kama kweli mngekuwa mnaitia mafuta bawaba
enyi wenye nyumba, zingetoka wapi kele za mlango ijapokuwa kusema kweli
haziwakoseshi usingizi!?. Simo nasema.
Basi kaka yetu, mkulu wa kaya hii ya Wadanganyika walipa
kodi. Wacha nikomee hapa nikatafute sehemu ya kuegesha kichwa changu maana lile
pagala nililokuwa nikilala juzi na jana mmelibomolea mbali wakati wenye “siri
kali” mlipokuwa mkipambana na “wahuni” katika kujaribu kulinda “siri kali” yenu
isivuje pasina kujiuliza kinachoivujisha ni sakafu iliyoloa ama tundu kwenye
chombo chenye kutunza “siri” yenyewe?. Ama kweli fahari wawili wapiganapo,
ziumiazo nyasi na mara hii Chokoraa nimekuwa nyasi kavu kwenye uwanja wa vita
vya fahari wa Faru na Sisimizi. Simo.
Salaam Mheshimiwa, ni mimi mdharauliwa wako Chokoraa wa
Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika nakusalimia.