Shikamoo Mkulu wa Gunia.
Shikamoo si salaam mwana wa Muhangaikaji nilikataa tangu zama ila sasa, shikamoo mkulu
wa gunia. Nasema shikamoo si kwa kukuamkua maana ningekuamkua ningesema salaam
nakusalimia lakini nasema tena kwa sauti ya juu unisikie ijapo kusema kweli
akina kaka Muishiwa wamenifungia juu ya dari ya nyumba tena kwenye paa la choo
ili nisionekane mbele yako, ila naamini sauti yangu itakufikia ewe mkuu wa
gunia hili tambala bovu tuishilo sisi wana wa Adamu, shikamoo mkulu wa gunia.
Ha ha ha ha ha ha!!! Nimekumbuka zamani enzi zile wakati
wazee wangu hasa mama yangu Shida wa Matatizo wa Taabu Malingumu alipokuwa
akiniamsha lukwiri ili niende huko kwenye jando la kikoloni kufundwa ujinga wa
kuidharau ‘ilimu’ ya babu na babu zangu kwa kuuita ushenzi ilhali tamaduni za
mgeni zikiitwa uungwana, hilo si lengo la waraka huu, shikamoo mkulu wa gunia.
Nakumbuka enzi hizo ikiwa Mkulu wa kaya ama wasaidizi wake
walitembelea kijiji chetu, wote tuliambiwa tuoge, tuchane nywele zetu kwa
mitindo ya kurithishwa na wakoloni wenyewe ati wakiita ‘kisasa’ bila kuheshimu
ukweli kwamba hakuwezi kuwapo na sasa bila zamani na mjukuu ni matokeo ya babu,
humu namo simo ila, shikamoo mkulu wa gunia.
Tulijipanga mabarabarani na enzi hizo barabara zenyewe
zilikuwa za vumbi tupu na ole wetu ikiwa ulikuwa msimu wa mvua na siye na shati
zetu nyeupe kwa weupe wa mkorogo, letu lilikuwa tope na maji machafu wakati
walinzi wa ‘mkulu wa kaya’ wakipita na magari yao na siye tukijitahidi kupunga
mikono na kulazimisha tabasamu nasema enzi ni enzi na kumbe historia hujirudi,
shikamoo mkulu wa gunia.
Mkulu wa Gunia, mwana wa wana wa Hamu ndugu wa Shemu na
Yafethi kwa mujibu wa misaafu iliyoletwa na wale uwatawalo leo, nimemua kupaza
sauti kwanza nikukumbushe japo najua wajua ya kwamba shikamoo humaanisha niko
chini ya miguu yako na hilo ndilo ninalotaka kukwambia leo, niko chini ya miguu
yako na kusema kweli unanikanyaga. Sikulaumu. Wala! Hata kidogo. Nani kasema
nakulaumu? Miye sikulaumu kwa vile kama walivyofanya babu zako ambao walipokuja
wageni wenye pua ndefu na tabasamu za unafiki uonekanao kama urafiki,
waliwakuta babu zetu wakiwazika machifu mikononi mwa walio hai na waliozikwa
hao ati kumsindikiza chifu kwenye safari yake ya mwisho walikufa kwa ujasiri
ati kwa vile walikuwa mashujaa na mimi ni shujaa mtukufu mkulu wa gunia.
Mimi ni shujaa ila si shujaa wako bali shujaa wa kaka
Muishiwa kwa vile tangu ulipotangaza kwamba waja huku kwetu mimi niko chini ya
miguu yako na hata mkate wa wanangu niliokuwa nimeukumbatia kifuani kwangu nao
sasa umesagika kwa kule tu mimi kuwa chini ya miguu yako.
Ha ha ha ha ha ha!!! Usitake nikutajia jina la marehemu bibi
yangu mzaa mama yangu wewe aliyeniambia mbwa mwitu na mbuzi hukaa kundi moja
tena bila kuchokozana ama kuogopana Simba anapoingia kichakani na sasa kwa
sehemu nasadiki.
Ati! Nasema uji wako kwenye ardhi ya wadanganyika walipa
kodi umenikumbusha mambo mengi mojawapo ni mzee yule aliyekuwa mwenye kigoda
cha kijiji chetu. Pamoja na kuwa mtu mkubwa sana wa enzi zake lakini hakuwa na
shati hata moja lisilo na tobo mabegani na siku moja Mkufunzi alipotembelea
darasa lake na kuamua kukagua usafi, yule mzee kwa vile alijua Mkufunzi
angekagua mavazi alikuwa amevaa koti zuri juu ya shati lake ila kwa vile
mkufunzi alipoamuru huyo mzee avue koti lake ndipo tukagundua kumbe mabega na
mgogo vilikuwa wazi. Ha ha ha ha ha ha!!! Nicheke kama mazuri Chokoraa miye.
Najua!!! Najua, najua unashangaa kusikia
Mkufunzi alitutembelea na kumvua yule mzee shati lake kwenye ukaguzi wa usafi
wakati unajua mkufunzi huwa anakagua wanafunzi pekee ila ulichosahau ama
kudharau ni kwamba wakati huo kaya yetu yote ilikuwa shule na mkufunzi alikuwa
mmoja akituongoza kama Mussa na Israel hayo unayajua kwa hiyo , shikamoo mkulu
wa gunia.
Wacha nikumalizie kisa hicho halafu ninyamaze maana najua
akina kaka Muishiwa kwa sasa wamenuna ati Chokoraa nampigia kele mgeni na ndiyo
maana ati kwa vile miye siujui ‘ustaarabu’ wamenikataza kuja mjini. Mkufunzi
baada ya kumvua koti yule mzee na kumkuta amevaa shati lililochanika akaamuru
atandikwe viboko sita pale pale na mimi nikajihoji, kwanini kumtandika mtu
aliyejaribu kujiheshimu mbele ya mgeni!? Mkufunzi akanisikia wakati najihoji
inawezekana nilijisahau nikawa nazungumza kwa sauti, akaniita mbele. Weeeee!
Hukuwapo maana ungecheke sana jinsi nilivyokuwa nikitetema.
Nilijua leo na miye
vyangu sita ninavipata lakini mzee yule Mkufunzi alikuwa heshi visa, ati
akaanza kunifafanulia Chokoraa miye ni kwanini alimtandika mzee yule viboko
sita. Akasema kwa kitendo cha mzee yule kuficha shati lake lililochanika,
mkufunzi angeondoka kijijini ameridhika kwamba mambo yako barabara maana hata
mwenye kigoda kava suti kumbe ndani malapulapu na hivyo asingetuma tena “kilimpilini”
pale kijijini mwaka huo labda baada ya miaka sita na hivyo aliamua kumtandika
kwa vile mwenyekigoda alimficha ukweli wa mambo. Ha ha ha ha ha ha!!! Natamani
na wewe mkulu wa gunia ungekuwa na busara ya kujua kilichojificha nyuma ya jiji
safi unalolipitia unapotokea kwenye stendi ya mwewe! Lakini waaaapi! Kwani
watakwambia!?.
Hata wakikwambia kwani utawafanyaje zaidi ya kuwapongeza kwa
juhudi ya kusafisha jiji? Nasema uchafu waliouondoa ni mimi na ndugu zangu
akina Seremala, makenika, machine na yule Ntilie, mdogo wake na mama yao Mama
Lishe, na miye nauliza, kwani sisi sasa ni takataka kwenye kaya yetu wenyewe
ati kwa ajiri ya ujio wako? Naomba kujua unaoga maji ama maziwa!?. Ila bado
zijajiinua wasijeniangushia vitu vilipukavyo, bado niko chini ya miguu yako
mkulu wa gunia.
Nasema kumbe ukweli na uwazi ni mchezo mgumu kuucheza na
yawezekana wanaohofia na wanachokihofia miye nakijua. Ati! Sikia huyu naye! Ati
wanahofia usalama wako? Nani kasema! Hawana mashaka na usalama wako maana kama
wao wenyewe tu wako salama iweje wewe na maguvu yote uliyo nayo na ‘utukutu’
uliojifunika nao usiwe salama katika kaya ya amani na utulivu!? Na huyu, ati
wanahofia maandamano na si hasa!? Hilo nalo si kweli maana hayo yaweza kutokea popote
na vyovyote ila wadanganyika siye hatuna kawaida ya kuwafanzia fujo wangeni
kuuana twauana wenyewe lakini mgeni yuko salama.
Wanachohofia mimi nitakwambia
ijapo najua ukiondoka nitakiona cha mtema kuni. Ndiyo, ukiwapo hawanigusi kwa
vile, niko chini ya miguu yako.
Wanaogopa usije ukawauliza zile shekel, noti na mifedha
kedekede uliyowapa walete kuboresha maisha ya wadanganyika imefanya nini ikiwa
miaka hamsini ati baada ya bendera bado wadanagnyika wanaishi chini ya nusu
dola kwa siku!? Nani kasema wanaishi chini ya dola moja? Kwani dola moja si
sawa na “si nyingi” zetu harufu mbili! Naapa wako wadanganyika miongoni mwetu
ambao wanaamka na kuzitafuta “si nyingi” tamo mia na wasizipate hao wanaishije
chini la dola moja!?. Wanaogopa utawauliza
kuhusu magari yao ya kifahari wanayoendesha ilhali mama Ntilie na Machinga
hawajui watakula nini na hivyo wanapotuondoa akina siye mjini utakaoukutana nao
ni “wao” na hivyo hutojua kundi la akina siye tuko wapi na kuondoka ukidhani na
“sisi” ni kama “wao” kumbe pana tofauti kubwa. Natamani kuendelea kusema lakini
naonga kama uzito wako unaongezeka na mimi pumzi zinapungua kwa sababu, niko
chini ya miguu yako.
Wasalaam, ni mimi Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahio wa
Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika nakusalimia. Shikamoo Mkulu wa Gunia.