Salaam nakusalimia. Hizi ni Salamu kwako wewe, ndiyo wewe
mkulu wa kaya ya Wadanganyika walipa kodi kutoka kwangu Chokoraa wa
Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika nakusalimu,
Shikamoo Mheshimiwa.
Nasema tena kama nilivyowahi kusema hapo kabla kwamba
shikamoo si salaam bali mazao ya ukoloni mkongwe lakini wacha niitumie kwako
kwa vile hasa ni ukweli usiopingika kwamba niko chini ya miguu yako, shikamoo
Muishiwa, aha! Samahani, shikamoo Mheshimiwa.
Nataka , nimesema nataka wala siombi maana Chokoraa miye
sifungwi na ‘proto kali’ ninapotaka kuzungumza na mkulu wa kaya yangu kwa vile
yaliyonijaa moyoni ni mazito maana yanatishia heshima ya Mdharauliwa miye kwako
wewe Mheshimiwa sana mkulu wa kaya yangu na hapa salaam nakusalimia.
Hivi! Kwani heshima ni kitu cha bure kama wasemavyo
waswahili wa Danganyika yetu!? Si kweli. Naapa ni uongo kuniambia ati heshima
ni kitu cha bure maana nijuavyo miye mwana wa Muhangaikaji heshima hulipiwa
gharama kubwa ya juhudi, utu, kujituma, kutenda mema na kutumia nafasi na
vipawa ulivyojaaliwa na mwenyezi na pia
kuaminiwa na wadanganyika wenzako kwamba waweza kusema na hata kutenda kwa
niaba yao na hapa salaam nakusalimia.
Wala! Wala usinichukulie miye mwana wa Mdanganyika kuwa
mmoja wa waungaji mkono wako mbumbumbu ambao hawawezi katu kukwambia ukweli
pale unapovurunda katika kutenda yale tuliyoyakasimu kwako kutenda lakini pia
si mnafiki miye kitukuu wa Mlalahoi wa kutokusifia unapotenda zaidi ya
nilivyotaraji. Nimesema unapotenda zaidi siyo unapotenda kwa kiwango tarajari
na humu sasa najitoa maana simo. Nasema kwangu kama unayo masikio ya popo basi
yafunike maana ikiwa nitayaona nitasema hadharani kwamba mfalme ana masikio
kama popo.
Hilo si lengo la waraka wangu leo hata hivyo hizo zilikuwa
salaam tu na kusalimia mkulu wa kaya ya Wadanganyika Walipa Kodi. Leo ninataka
kukueleza kuhusu Heshima ya Mheshimiwa wewe ambaye Mdharauliwa miye ili
nikufikie na kukusalimu ni lazima kwanza nitambae mwendo mrefu nikijiangusha
chini kila baada ya hatua kadhaa ati kwa vile heshima siku hizi ni shikamoo,
basi shikamoo Mheshimiwa.
Nasema ni juzi tu hapa Yule Mnyarwanda alikutupia matusi ya
nguoni kwa kumshauri jinsi ya kuishi vyema nyumbani kwake ati kwa kisingizio
cha kwamba unaingilia mambo yake ya ndani ilhali kila anapogombana na mkewe
wewe ndiye unawapa wanae malazi na chakula. Nadhani huyu ameifanya hii kuwa
mbinu ya wewe kumlelea wanae na hii si hoja yangu lakini ni sehemu ya salamu,
shikamoo Mheshimiwa.
Kilichonifanya nikuandikie leo ni kukupa pole kwa msiba,
msiba mzito wa walinzi wa kaya yetu hii ya wadanganyika walipa kodi nasema kwa
hili wakati ninapoandika Chokoraa machozi yanilengalenga. Silii kwa sababu ya
msiba wenyewe maana twafwa sote tu kama upepo upitao na kwenda zake na siku
zetu si nyingi juu ya dunia gunia letu hili lakini kinachonisikitisha ni
mazingira yenyewe ya vifo vyao.
Najiuliza ni wapi ulipochorwa ule mstari mwekundu unaoweka
tofauti kati ya amani na vita na ikiwa kwa hili mstari huu haujavukwa maana
mbele naona giza, ila bado nakusalimu, shikamoo mheshimiwa.
Hivi hawa wanaopigana na kuuana kila kuitwapo leo
“watwawala” wao si wameamua kwa makusudi kuwateketeza vijana wao walio
matumaini ya jamii yao kwa maslahi binafsi hadi pale walipokuja kushtuka maji
yashazidi unga na wakaomba kuwapo kwa msaada kutoka kwa jirani?. Ndiyo, na sisi
tukawatumia wajumbe wa amani na nani alisema ni mjumbe hauawi!? Naapa aliyenena
hili ama alitudanganya au tulijidanganya wenyewe kwa kumsadiki maana wajumbe wa
amani wameuawa kwenye uwanja wa vita na mimi nasema huu ni upuuzi.
Ndiyo. Ni upuuzi kumtuma mwalimu darasani bila chaki wala
kitabu ama mkulima shambani bila jembe au hata Chokoraa jalalani bila mfumo wa
Rambo asomaye na afahamu na sasa ndugu zetu hawa wamekwenda.
Ndugu zetu hawa wamekwenda tena walio wengi wamekwenda na
ndoto zao, na matumaini yao ya kesho yamezimika na hata wale waliobaki nyumbani
ambao matumaini yao yalifungwa kwa hawa basi hawa waliokwenda wamekwenda nayo
na itawachukua waliobaki miaka kama si dahali kujenga matumaini mapya na kama
ilivyo kovu alisafishwi kwa sabuni likaisha, hawa wamekwenda.
Kinachonifanya nikuandikie siyo tu kukupa pole bali kukutaka
ujivike wewe viatu vya wale waliobaki nyuma ya hawa waliokwenda na ambao siku
za usoni pia watakwenda kama ambavyo pia mimi na wewe tutakwenda hiyo njia ya
watu wote lakini kwa sasa tuvae viatu vya walio hai maana waliokwenda
wamekwenda na hakuna njia ya kurudia huko waendako watu wote.
Najua, najua utataka kutumia tena busara kwenye hili na hapa
mwana wa Muhangaikaji naomba nijitoe maana simo. Ala! Kwani si nimeona tangu
umekalia kitu hicho jinsi ambavyo matumizi ya busara yamezaa hasara nyingi
kuliko faida ama wataka nikukumbushe kidogo!?. Haya, ebu kumbuka wale walioanza
kuhubiri upuuzi wa kipuuzi na kutugawa kwa misingi ya dini, kwani habari hizi
hazikufika mezani kwako kwa wakati na ukaamua kutumia busara kukabiliana nao!?
Ona sasa tulipofika ambapo hata majalalani Machokoraa twaulizana dini kabla ya
kupeana kipande cha boflo na wali uliolala ukatupwa asubuhi. Humu namo simo.
Tazama, tazama jinsi ambavyo wale waliotuhumiwa kwa ufisadi
mkubwa na wakathibitika ulivyotumia busara ya kuwataka warudishe walichoiba
badala ya kufichua mwizi na kumwadhibu kwa kadri ya miiko na vijiko vya kaya
yetu na mwisho wa siku ni hao hao waliotangaza ati wewe ni dhaifu na hasira
zikawapanda wale walio na ngazi za kupandisha hasira hizo miye nikajitoa kama
ambavyo hata sasa najitoa.
Ona jinsi ambavyo ati baada ya fedha kedekede za
wadanganyika kutumika kununua Rada na hawa wadanganyika tukatakiwa kula nyasi
kama Mbuzi kwa ajiri hiyo bado wanyama wetu walipakiwa kwenye dege tena la
kijeshi na kurushwa nje ya kaya yetu na hata sasa bado imetumika busara. Sitaki
kusemea wale walioua waandishi na wengine wengi na madhila ya kila leo
yawapatayo wadanganyika ilhali wewe mkulu wa kaya ukiwa unaendelea kutumia
busara.
Leo sicheki, nasema sicheki kwa vile nina huzuni na hasira
maana nakumbuka kuna wakati wako walioomba ati uwe mkali walau kiduchu tu ili
heshima ya uheshimiwa ilindwe lakini naamini hata hao nao ulitumia busara
kutowasikiliza kama ambavyo unatumia busara kuwaachilia wale waliokuwa kituoni
na wenye wajibu wa kulinda raia na mali zao wanapovamiwa na kuibiwa na hata
sasa bado busara ingali inatumika na ndiyo maana najitoa.
Nakuandikia nikuombe kwa hili muishiwa, aha! Nisamehe,
mheshimiwa sana mkulu wa kaya ya Danganyika ya Wadanganyika walipa kodi
usitumie busara hata kidogo. Nasema si sahihi kuwa sahihi mara zote maana hilo
humaanisha kwamba ustaarabu kwa mpumbavu huonekana kuwa uoga na ndiyo maana
hata wale tuliowale na kuwalisha leo wanatutukana na wewe unatumia busara
ilhali matusi yao hayaishii kwako tu maana shati ulilovaa kipande chake nimevaa
mimi na wadogo zangu wengine watoto wa baba yetu Mdanganyika na hivyo utomvu
wao wa nidhamu watuchafua wote japo kusema kweli wewe wachafuka sana maana uko
hukoooo mbele yetu.
Kwani hatuwajui wakuu wa hawa wauaji waliowaua vijana wetu?
Wako wapi akina Sikamona na wenzie ama waliishia tu kwenye mawazo ya akina
Mtobwa na hivyo Danganyika yetu haina tena mashujaa wa Salaamu toka kuzimu ili
wawapelekee salamu wajinga hawa kwa ujinga wao wa kuwaua wajumbe wetu wa amani
ilhali wanajua fika mjumbe hauawi!?.
Nasema ni wakati sasa vijana wetu wavuke mipaka wakawatafute
wahalifu hawa na kuwaleta hapa kwenye kaya yetu ili tuwakalishe kwenye ule
mbuyu mkubwa na kuwazodoa kwa mawe na maembe mfu na ujumbe ufike kwa jirani
kwamba kila atakayemgusa Mdanganyika pasipo kuzingatia taratibu atazodolewa.
Nasema sisi kwa sisi tugombane na kuumizana maana mwanao
ukimpiga mwenyewe unajua kiwango cha adhabu lakini anapopigwa na jirani huna
budi kujua sababu vinginevyo umeshindwa kuwa baba na kumfunda mwanao kuwalinda
wanawe baada yake na humu miye simo ila salaamu nakusalimia.
Nasikia umemtumia salaam mkulu mwenzio wa kaya ya jirani
afanye “haraka” kumtafuta nyoka aliyeuma vijana wetu maana yumo humo ndani
mwake na kwamba ikiwa atashindwa kumpata “haraka” basi utawatuma vijana wako
kumkamata mwenyewe huyo nyoka na Chokoraa nauliza tafsiri yako ya “haraka” mara
hii inamaanisha nini !!?.
Ni mimi Mdharauliwa wako, Chokoraa wa Muhangaikaji wa
Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika Mlipakodi nakusalimia. Shikamoo Mheshimiwa.