Nimepata ujumbe unasema
nijihadhari na haya ‘matakataka’ yangu niyamwagayo kwenye milango ya majumba ya ‘waishiwa’ maana
ati yanatoa harufu mbaya yenye kuwakela waishipo kwenye mahekalu yao hayo
ambayo ati nayo wameyapata si kwa halali. Nimekusikia ndugu yangu na ndiyo maana sijathubutu kwa karibu majuma
kadhaa sasa kupita mitaani kwao ila leo nimelazimika kuja kumsalimu mkulu wa
sungusungu wa kijiji, mkulu salaam nakusalimia, shikamoo mkulu wa sungusungu.
Wanasema ati wewe umetumia muda wako mwingi tangu ulipotoka
pale kwenye jando la kijiji lililoko Mlimani, ukiwa nje ya kaya yetu hii ati tena ukifanya kazi na wale wenye rangi
nyeupe na kutudanganya siye kwa tabasamu na hivyo mkulu wa kaya alipokuteua
wewe kuwa mshika “manati za ndhungu” mkuu wa kitengo hiki cha sungu sungu,
Wadanganyika walipakodi walikuwa na matumaini makubwa na wewe lakini ati kwa
kadri siku zilivyokwenda sasa Wadanganyika hawa hawa wanawaogopa vijana wako
kiasi wewe hawakuogopi bali wanakuabudu na humo miye simo maana nimekuja tu kukusalimu,
shikamoo mkulu wa sungusungu.
Ndiyo nasema na wewe mtoto wa mtu Mwema ambaye kwa wema
wake alikutuma wewe kwenye jando la kijiji ili ukiisha kuyapata mafunzo ya
jando uje tena hapa kwenye kaya yetu
utusaidie sisi watoto wa mzee Mdanganyika Mlipa kodi na ati vile visenti
vilivyokupeleka wewe jandoni vilikopwa kwa baba yetu mzee Mdanganyika wa Mlipa kodi na ndiyo maana miye nakusalimu,
shikamoo mkulu wa sungusungu.
Ngoja! Nielewe na uniamini
ewe mwana maana sina dhihaka hata kidogo nisemapo “niko chini ya miguu
yako” kwa vile ni kweli unanikanyaga na wala siwezi hata kujaribu kujiinua
maana ni bora unikanyage wewe kuliko nidunguliwe na ‘manati’ za vitegemezi
vyako na humo miye unitoe maana simo.
Kinachonitisha miye si kule kujua kwamba hata salaam hizi
zaweza ama kupelekea miye kudunguliwa na manati za ndhungu zilizo mikononi mwa
vitegemezi vyako ati kwa vile miye “nimewakosea adabu” sungusungu wa kaya yetu,
lakini nasikia ati huko uliko wewe mkulu wa sungusungu mumeanzisha mchezo wa
kuoshana maji moto mkibabuana sura kama mwataka kutengeneza staftahi kwa sura
za wenzenu na miye humo msinihusishe maana simo.
Wacha niliseme hili walau niondoe funda lililonikaba kooni
maana uhai naupenda na uzima kuliko maradhi lakini uhuru wa kweli huja kwa
fikra sahihi na hizo huja kwa lugha sahihi na miye humu sasa nahusikaje?. Aala!
Usinitanie. Nasema mzaha wako utatumbua usaha we mwana sikiliza Chokoraa
nikueleze yaliyo ya kweli maana unajua yaliyokuwa kwa wale waliokuwa kwenye
kiti chako kabla yako na jinsi ambavyo leo hawana heshima isipokuwa nyumbani
kwao na hivyo limetanguka lile lililonenwa na manabii kuwa nabii hana heshima
kwao, ama hawakuwa manabii na hivyo haliwahusu hilo la nabii kukosa heshima
kwao.
Nani hajui kwamba zilikuwa enzi katika kaya yetu hii hii
ambazo watu ati alitumwa tu binti ‘fatuma’ akavunja malango ya watu na wafuasi
wakanyang’anya mali na uhai!?
Hayo sasa yamepita na sasa mwamwagiana ‘mtindi mkali’ na
humu miye sasa nahusikaje!?. Simo naapa. Nasema Wadanganyika sasa wamehama
makwao wanaishi nyumba za jirani yao Yule mzee mwenye sura mbaya Hofu wa Uoga
ati kwa vile kuishi kwao uwaogofya sana hadi wamezoea kuishi “na” kama si
kuishi “kwa” Hofu na ndiyo maana miye salaam nakusalimia.
Nasema ingawa umewapunguzia mzigo wadogo zangu wale wawili
Mzembe na Mzururaji wenye umaarufu wa
harufu na hata majina yao siyasikii yakitajwa sana kama ilivyokuwa kwa watangulizi
wako, lakini ati kaka yangu Machinga wa Muhangaikaji siku hizi ndiye amechukua
zamu ya kusumbuliwa, na ati wadanganyika wanadai imekuwa sawa alivyosema
Mkufunzi enzi za uhai wake kwamba ati ‘siri kali’ ikiishakuwa imetoboka inavuja
basi hubakia kukimbizana na vijitu vidogo mabarabarani, kwa vile akina kaka
mkubwa Mstahiki wa Mtukuka huwa ati wewe na vijana wako mwaogopa kuwagusa kwa
vile watakataa “kuja” ila miye humo simo.
Nasema mimi jina langu halisi ni Chokoraa wa Muhangaikaji
naomba msinifananishe na wale vijana wawili wa mzee Si Hasa akina Mchochezi na
Mropokaji ingawa tumekua pamoja ila mwenzao
majalala yamenifunda kuwa na adabu ndiposa mkulu miye nakusalimia,
shikamoo mkulu wa sungusungu. Sisemi, ndiyo, sisemi kwamba akina mzembe na
mzururaji na hata kaka yangu Machinga wa Muhangaikaji wanaruhusiwa kukosa adabu
ati kwa vile akina kaka Mstahiki na hata Yule kaka yetu mkubwa Muishiwa wa
Mbadhilifu wanaukosea adabu msaafu na mafunzo ya kaya yetu, lakini nasema
imekuwaje hata imekuwa kwamba nyie wenye kuijua siri ya mzazi wa Amani bi Haki
binti Wajibu na nyie mmekuwa ndumilakuwili mkiufuata msemo wa waswahili kwamba
haja kubwa ya ng'ombe mbolea ya bata uchafu!?.
Haya, nasikia sasa si salama hadi kwenye viota vyenu wenyewe
na miye nasema hivi na nyie mlishiriki kula pesa ya sanda ya marehemu Uadilifu
hata mkasababisha mzee yule kuzikwa pasipo sanda!?. Ha ha ha ha ha ha !
Nicheke miye maana ikiwa na nyie mlio na taa haramu ya kumulika ili wengine
tuone mwatembea gizani kwa uzembe wa kuitia kandiri mafuta, itakuwaje basi yule
mama yangu bi kikongwe Shida wa Matatizo wa Taabu wa Muhangaikaji!?.
Naona kama muda unaniishia nachelea nisikute paka na mbwa wamemaliza vile vilivyotupwa jana jalalani ndiyo maana nakuomba uniruhusu tena
juma lijalo nije nikuletee ujumbe nilioagizwa na dada na kaka zangu watoto wa
Mdanganyika. Ndiyo, nitakuja tena kwa ajiri ya kukuletea salaam baada ya
kuuguza vidonda vya mkong’oto niliopokea kutoka kwa vijana wako nilipojaribu
kuukaribia mlango wa afisi yako ili nikusalimu. Mmoja wa vijana wako aliponiona
ati akaniita jina si langu eti “we kibaka, watafuta nini karibu na Muishiwa
Mkulu wa Sungusungu?”, ile kujaribu kujieleza kwamba miye ni Chokoraa wa
Muhangaikaji na si Kibaka, kidundo nilichoambulia ukichanganya na uzito wa
ujumbe nilio nao kutoka huko kwetu, ndiyo maana sauti yanitetema nizungumzapo
ingawa nina hakika salaam zitafika, salaam nakusalimia.
Ni mimi mdharauliwa wako, Chokoraa wa Muhangaikaji wa
Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika wa Mlipakodi nakusalimia,
shikamoo mkulu wa Sungusungu.