Salaam nawasalimia. Najua mwaka wa jana umekwenda na najua
wengi wenu bado mngali kwenye zile nyumba zenu zenye baridi ya kutengeneza huku
mkijituma wengine kuijenga na wengine kuivunja kaya ya wadanganyika na ati bado
mwashangaa kwanini jengo halikamiliki. Mwashangaa nini?. Nasema ikiwa walio
wengi mnafanya kazi ya kubomoa ilhali wachache tena wenye nguvu chache
wanafanya kazi ya kujenga si ajabu itawachukua miaka dahali walau kulifikisha
jengo kwenye ‘renta’ ila humo miye simo bali salaam nawasalimia. Shikamoooni
Wadanganyika.
Nisemeje!?. Mwataka nirudie kuwakumbusha madhila
yaliyotukuta kwa mwaka uliopita?. Katu. Nasema siendi safari ya maili kumi elfu
kinyumenyume asomaye na afahamu ila mi salaam nawasalimia. Jana imepita na
kesho si yetu lakini ikitumika vyema leo walau kesho yaweza kuwa na matumaini
na miye hapa nawasalimia. Kwa mwaka huu naapa sitasema matukio bali mazoea na
tabia zenu maana tabia hutengeneza utamaduni wa jamii na miye nakuulizeni enyi
wana wa Mdanganyika Mlipakodi nani
aliyekundanganyeni kwamba kuna kaya nyingine mtakwenda baada ya Danganyika yenu
hii?. Ala! Washangaa nini?. Kwani si miye nakuoneni mnavyoishi kama watalii tu
hapa kwenye kaya yetu kila mmoja akijaribu kuwa kama wale waliowatawala babu
zetu bila kujua kwamba twatofautiana siyo tu ngozi bali mtizamo na miye humu
nitoeni.
Ha ha ha ha ha ha!!!! Nakumbuka Mkulu wa Kaya kabla ya ule “Uchafuzi
Mkuu” wa mwaka uleeeee ulitukasirisha sisi Wadanganyika hata tukapiga kura na
kumpa yeye aslimia zaidi ya thamanini ya ‘kula’ zetu huku tukisahau kwamba tuna
zaidi ya asilimia tisini ya familia za kulishwa na ‘kula’ hizo za bwelele,
alituahidi ajiira makumi mia na sasa leo twalalama na miye nauliza twalalama
nini?.
Mwaka wa jana Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu
wa Kabwela wa Mdanganyika Mlipakodi nimezunguka majalala yote tangu yale ya
uswahilini kwetu kunakotupwa miiba ya dagaa hadi yale ya waishiwa kunakotupwa boflo
na mapande ya nyama ati kwa vile yamekaa sana kwenye jokofu yakakosa radha,
naapa mwakufuru enyi wana. Kwani mabucha hamkuyaona hadi mwanunua vyakula na
kisha kuvitupa kwa kujifanya uzungu usio tija!?. Simo naapa. Kwani msipotupa
Chokoraa miye nitakula nini? Lakini walau jifunzeni kumheshimu Mwenyezi
aliyekupeni nyie kusaza siyo kwamba mtupe jalalani bali mtupe siye tusio hata
na kidogo na miye humo nahusikaje?. Simo.
Nasema katika kuzurura kwangu nimejifunza jambo moja kuu na
hapa salaamu nawasalimu wale sungu sungu wa mipaka yetu na wale manyapara wenye
jukumu la kusimamia vibarua vya kaya yetu, shikamooni waishiwa. Nauliza, hivi
waishiwa nyie mnafahamu uzito na upana
wa majukumu yenu au kwavile kama wasemavyo
wadogo zangu wale akina Mzembe na Mzururaji kwamba kaya imeuzwa basi na nyie
mmeamua kuuza na utu wetu? Naapa humu miye nisihusishwe.
Nasema kuanzia kule kwa akina Ngosha kwenye viwanda vya
samaki hadi kwa akina Nchumali kwenye Korosho wadanganyika nyie hamna
chenu ati kisa mnatekeleza sera ya ‘Ukewenzaji’
na miye nauliza mbona ‘Ukewenzaji’ huu mwabakwa nyie na sisikii hata lalamiko?.
Ha ha ha ha ha ha!!!!! Ninyamaze miye maana si ajabu mkaniuliza kanituma nani
wakati miye ni salaam tu nawasalimia.
Hivi wakati mlipoamua ‘kubinua na kufisha’ viwanda vyetu
vyote tulivyorithi kutoka kwa wazee wetu Waishiwa nyie mliamua kubinua na
kufisha hata ajira zetu?. Ha ha ha ha ha!!! Chokoraa miye nimepita na kukutana
na wageni wakikaa kwenye majumba ya viyoyozi huku wakiwa hawajui hata kuandika
idadi ya mali inayoingia na kutoka viwandani zaidi ya utaalamu wa kujua kuvaa
na tabasamu za kikoloni na ujasiri wa macho wa kuwatazameni usoni mnaposhikana
mikono kusalimiana na miye nauliza, hivi hakuna kati ya Wadanganyika wataalamu
wa kufanya kazi hizi hadi mwatuletea wataalamu “feki” wenye kujua tu tabasamu
na “hendisheki” ilhali utendaji wote wafanywa na akina “sabani” asomaye na
afahamu?!!! Simo humu.
Nani hakumbuki jinsi ambavyo kwenye migodi ya dhahabu kulikuwa
na wageni waliokuwa wakiitwa “sekyurite sipeshialisiti” ati kwa vile wanatokea Unepali
ilhali kwao walikuwa makplo na masajenti huku makapteni na maluteni wetu
wastaafu wakisota mitaani kutafuta ugali wa kulisha watoto!? Naapa historia
inajurudia na miye humu simo.
Bado kidogo. Sijamaliza, naomba kuuliza wakati “wakewenzaji”
hawa wanapoleta msururu wa “wataa haramu” hawa na kuwavusha kwenye stendi za
mabasi ya hewani, wanawaeleza wataalamu wetu wa uhamiaji kwamba wanakuja ‘kuisaidia’
kaya yetu kwa lipi?. Au ndiyo yale yale ya kiazi kuitwa kwa lugha ya kitaalamu “potato”?!!!!.
Naapa sihusiki. Haya, endeleeni na
michezo hii ya mbuni ya kuficha vichwa mchangani ili mkirudishe kizazi chetu
kwenye ukoloni kule ambako babu zetu walipigana kufa na kupona kututoa sisi
halafu na nyie mtakapolala na baba zenu mkiiendea njia ya watu wote mkumbukwe
kama wasaliti wa juhudi za wazee wenu na miye humo nisihusishwe maana simo tena
simo kabisaaaaa, sihusiki.
Haya, na nyie mjiitao wakulu wa kazi na ajira wa kaya yetu, mmeshindwa nini kutengeneza torati ya kulinda ajira za wadanganyika wenzenu na kuzisimamia?. Ha ha ha ha ha ha!!!! Najua, najua mwaniona mjinga kwa vile wadogo wakisimamisha pembe wakubwa wapewa bahasha na mambo yanakwisha na miye humo nahusikaje? Lakini niseme miye nisijehukumiwa na kizazi kijacho kuwa mnafiki maana najua kama mungetaka kuyatenda yawapasayo yangetendeka lakini hiyari yashinda shuruti na miye humu nahusikaje?. Simo naapa.
Haya, leo akina "Sabani" wamebaki kufukia hivyo "vidigirii" chini ya magodoro ya bibi zao huku wakipika chai na kufagia na kisha kwenda kufanya kazi za taaluma zao ili kuwafurahisha "mabosi" wasiojua hata kusoma na kuandika lakini wenye vibali halali tena vya kufanya kazi za taaluma kwenye kaya yetu na miye humu nahusikaje maana simo. Nauliza katika kutembea kwenu kote huko mwendako mmeshindwa kujifunza kwamba kaya za wenzetu hata kabla hujaenda wanakupima hata magonjwa wajiridhishe juu ya usalama wao na watu hao?. Nani aliyekurogeni enyi wana wa kushi?. Simo naapa.
Ni mimi ndugu yenu Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa
Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika Mlipakodi nawasalimia, Shikamooni
Wadanganyika Walipakodi.