Ngoja kwanza nicheke. Ha ha ha ha ha ha ha!!! Nacheka miye Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangu Pakavu wa Kabwela wa Mdanganyika. Leo, tofauti na siku zote ni furaha. Ndiyo, mwaka huu umeanza kwa mafanikio makubwa na kwa hilo namshukuru ‘Mulungu’. Ona huyu naye anakereka ati kwa vile nimemwita kikwetu huyu ambaye yeye angetaka aitwe “God” ili ajiridhishe kwamba yeye ni mtumwa. Naapa simo.
Nina furaha kwa vile mwaka huu Chokoraa nimepanda daraja, halafu nimepanda daraja mwanzoni mwa mwaka, ha ha ha ha ha ha!! Unashangaa!! Kwa sasa Chokoraa silali tena kwenye mitaro na huko hunikuti, nimepanga kichumba changu kimoja huku kwetu Uswazi kwenye kajumba ka mama Chausiku na hivyo silali tena chini ya daraja. Nani kasema hilo ni jambo dogo!?
Japo misosi yangu ni kule kule majalalani kama kawaida, lakini mara hii nafikiri hata majalala yangu itabidi yabadilike kidogo hasa kwa vile inabidi niwe kibiashara zaidi ili niweze kulipa kodi. Hilo nitakuhadithia ila leo, nataka kukueleza kero moja tu iliyonikuta. Kero ya mlango.
Kila mara “Ng’waaaaa!! Ng’waaaaaa!! Mlango huu wa bati unapiga kelele kila unapofunguliwa na Chokoraa hili linanikera lakini kinachonishangaza ni kwamba mama Chau na watoto wake wala hilo haliwasumbui, nasema kweli mi nashangaa sana. Ene wei, baada ya kuishi hapa walau kwa wiki mbili, nimeanza kuzoea hali hii na hivyo na mimi sasa naweza kulala na hiyo kelele hainisumbui sana isipokuwa pia hunisaidia nyakati fulani fulani, hilo nitakueleza siku nyingine.
Ndipo siku moja nikiwa nimejilaza hapa kwenye kitanda change cha kamba na hasa kwa vile siku hiyo nilikuwa sijatia kitu kinywani hadi hiyo saa sita ya usiku, nikabaki kuhesabu ‘kenchi’ na misumari na kupata nafasi ya kutafakari na hata kuzilinganisha kero za hapa kwa mama Chau na kero za kelele za wadanganyika walipa kodi kama ambavyo nimekuwa nikishuhudia kwenye kurasa za magazeti.
Ngoja kwanza! Nani kasema Chokoraa huwa sisomi magazeti!? Mwongo. Huwa sinunui magazeti hasa kwa vile matukio mengi yanayotokea huku mtaani huwa nayaona mwenyewe na sitaki kuyanunua tena yakishatiwa nakshi za wino hasa kwa vile huwa tayari yamechakachuliwa ili kuleta radha ya si hasa, lakini huwa nasoma magazeti na hapa kwangu si ajabu ukakuta magazeti kadha wa kadha kuanzia yale yaliyofungiwa maandazi, vitumbua, samaki au hata chips dume na kila nipatapo nafasi huwa najisomea hivyo vipande na usiniambie eti siyo magazeti.
Ndiyo. Nakumbuka Wadanganyika walivyokuwa wamedanganyika na kuhamasika hadi kutaka kuingia barabarani kuandaa mana ili iliwe na watoto wao baada yao ati kwa vile walichoshwa kula nyama ilhali wakifyatua matofari ya utumwa na hivyo wakajiandaa kuandaa mana. Weeee!!! Koma. Kwani waliandaa mana hata hivyo!? Wapiii!! Walifanya maandalizi yao yoote na matangazo na kila kitu halafu ati kuna jamaa mmoja mwema katika wema wake akagundua kuna mashababi mjini wanataka ati kuwadungua wadanganyika wote watakao andaa mana, basi kwa wema wake akawaonya wadangayika na wao wakanyewa kimyaaa!! Ama kweli rahisi sana kuwadanganya wadanganyika.
Ni juzi tu wakati nasoma hiki kipande cha gazeti kuhusu hayo maandalizi ya kuandaa mana na jinsi yalivyozimwa kwa wema wa mwema na vijana wake, ndipo nilipogundua kumbe wadanganyika wengi wanaishi kama milango ya nyumba ya mama Chausiku. Nasema usidhani nakutusi ewe mdanganyika mlipa kodi, lakini nakuuliza, ziko wapi zile hasira ulizokuwa nazo na kampeni kubwa ulizofanya ili kuandaa mana kwa ajiri ya kizazi kijacho baada yako hasa kwa kuzingatia kwamba ikiwa hivyo vijisenti yako uchwara vingelipwa kwa ajiri ya kusafisha hilo “Doa la Nzi” kwenye shati jeusi lenye harufu ya kinyesi, basi vizazi vijavyo vingepata hasira itokanayo na hasara na hata kufikia kuukana udanganyika wao?! Kwani hao mashababi walikuwa wangapi hata nchi nzima inasiamama wima kuwaacha hawa jamaa wapite!? Hata kama walikuwa wengi na waliojisheheneza sira nzitonzito na za maangamizi, walikuwa wapi na walikusudia kukaa muda gani au ndiyo wamehamia na hivyo sasa hatuwezi kufanya lolote kwa sababu kila tutakapojaribu kutoka nje ya milango yetu basi tutapambana na hawa mashababi!!? Nafikiri katika wema wake, huyu nduyu yetu mwema angetwambia basi kwamba hawa mashababi ama wamedibitiwa au wamekwishaondoka na hivyo tuendelee na maandalizi yetu ya kuandaa mana ili kizazi chetu kisifie jangwani kwa ukosefu wa chakula!. Humu mimi simo.
Nikakumbuka pia kwamba baada ya maandalizi ya mana kushindikana, waheshimiwa wawili akina Mbu na Nge nao wakaja kwa umoja wao wa Mbu-Nge kutaka nyogeza ya posho na hapa wadanganyika wakakasirika hadi povu kuwatoka midomoni. Nikahisi labda mara hii, wadanganyika hawa hawatadangayika. Wapi!! Kwa mara nyingine wakazidiwa na kile kibinti huwa nakiona kwenye vile visanduku vya picha kikisema kwa sauti kubwa “Sidanganyikiii” maana wandanganyika ghafla wakadanganyika na matukio ya mafuriko na mengineyo na kusahahu kwamba kuna visenti vyao kibao vyaliwa na ule umoja wa “Mbu-Nge” na wao wakibakia kuwa wadanganyika walipa kodi.
Mara mlango wa nje wa hapa nyumbani kwa mama chiku ukasukumwa ila mara hii polepole nafikiri kwa vile huyu anayefungua anajua kwamba watu wameanza kulala na hataki kuwasumbua na hivyo japo ulipiga kelele kama kawaida yake, lakini bado nasikia mikoromo ya usingizi ya mama Chiku na vitegemezi vyake ndipi nikakumbuka, kweli kele za mlango, hazimzuii mwenye nyumba kuuchapa.
Salaam nakusamilia, ni mimi nduguyo Chokoraa wa Muhangaikaji ,wa Mlalahoi, wa Pangu Pakavu, wa Kabwela ,wa Mdanganyika.