Kiherehere hiki!
Leo ati Chokoraa na mimi nimejikusanya na baadhi ya wananzengo hapa mtaani kwetu, tumekazunguka haka kasanduku kanakoonyesha sura za watu wakiongea na sauti zao twazisikia ati ninyi mwaita tivii. Uliza sasa tunaangalia nini! Duh! Nachoka miye mwana wa Muhangakaji kitukuu wa Kabwela.
Tumekaa tunaangalia Taarifa na Habari. Wewee!! Nani kasema nimekosea?! Nani!!! Tena!!! Angalia usiniudhi mapema nikazira kukuhadithia hata tukio lenyewe. Kwani ile ni “Taarifa ya Habari, Taarifa za Habari, Taarifa na Habari?!!. Nadhani lile baraza la wanaokifahamu Kiswahili kuliko sisi wengine inabidi watusaidie kwenye hili.
Ala! Unaona sasa!! Hadi nimesahau nilichotaka kukwambia kwa vile umenitia hasira. Hata hivyo nadhani nimejaribu sana kutumia lugha yenu ya kistaarabu sana ilhali mi siifahamu hiyo lugha yenyewe. Wacha nitwange kichokoraa sasa ndo tuelewane. Simo.
Nasema kwenye hili la kulalamika na kunung’unika kwa kila kitu simo, tena simo hata kidogo, simo kabisaaaaa! Ala! Hivi, si kila mwisho na mwanzo wa mwaka kumekuwapo na lundo la ajari barabarani na nyingi zikisababishwa pamoja na mambo mengine uzembe wa madereva na kukosa ujuzi na sifa stahiki za kuendesha magari!? Kwani kuna mtu kati yetu hajui kwamba hali hii imechangiwa kwa kiasi kikubwa na uzembe wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama hasa wa barabarani yaani ile mamlaka ya kuzibiti barabara na maji almaarufu kama ‘chuma tule’ na vikosi vya ‘usaha alama za barabarani’ kwa umoja wao? Hilo halinikasirishi hata hivyo.
Linalonikasirisha hadi nimewaandikia waraka huu, ni hili la wadanganyika walipa kodi kujifanya kulaumu “sirikali” kwa kila kinachofanywa hata kama ni kizuri. Hivi si nimeona mkipaza sauti mishipa ya shingo kuwasimama mkilalamikia kukatizwa safari zenu kwa sababu ya zoezi la ukaguzi wa “liseni’ za udereva ili kujua wale walio ‘liseni’ darasani kabla ya kuanza kuendesha na wale ambao wanaendesha bila kuanza ‘kuliseni’!! Nasema kwa hili mnitoe.
Ona sasa. Yaani wakati watendanaji wa ‘sirikali’ walipojipanga ki ‘stratejiki’ kabisa kwa kuzingatia ‘taimingi’ ya muda ambao ajari zinazidi na kujaribu kuokoa maisha ya wadanganyika, mwalalama! Mwalalama nini enyi wana wa danganyika yetu!? Naapa simo humu. Ona hyu naye anachukia ati kwa vile nachanganya kikoloni katikati ya sentensi zangu. Utajuaje kwamba “Nshomile mpaka fomu fooo!!!” Kalagabaho kama hujaelewa, kwani hilo mi Chokoraa lanihusu!? Simo nasema.
Nasema kwenye hili, badala ya hasira zangu kuzielekeza kwa hawa wana usalama japo si salama, ningezielekeza kwa wamiliki wa haya madude yaliyofanyika wajumbe wa malaika mtoa roho kila mwanzoni mwa kila mwaka. Washangaa nini!! Ningezielekeza hasira zangu kwao kwa vile kila mwajiri anapomwajiri dereva anamuuliza kuhusu leseni na ikiwa mwenye gari anaruhusu dereva asiye na leseni kuendesha gari lake, mwataka nisimwelekezee hasira zangu kwa nini!!? Naapa kwa hili tutashindana sana, lakini simo.
Halafu!! Ebu niwaulize enyi wana wa usalama japo si salama, huu utaratibu wenu wa kuvamia tu maeneno na kuanza kutekeleza majukumu yenu bila hata kuzingatia kwamba Chokoraa miye mwana wa Muhangaikaji, naam, mimi huyu mjukuu wa Mlalahoi kilembwe wa Kabwela, mara nyingine ninatoka nyumbani na tiketi tu na ziada ya shilingi elfu mbili kwa ajiri ya maji na nauli ya ‘bodaboda’ nikifika huko niendako na hayo mengine namuachia maulana, mmeianza lini!?
Naapa kwa ubabe huu sina hakika kama mnafanya ‘upolisi jamii’ kwa sababu mnashindwa kuzingatia mahitaji ya jamii yenyewe katika utekelezaji wa majumu yenu kwa sababu hasa mahitaji ya Chokoraa miye hayaishii kwenye kusafiri na kufika salama bali pia kuzingatia matumizi ya kila ‘shekeli’ (iite ‘sinyingi’ kama hilo ndilo jina ulipendalo) ninayoitumia na ninavyoitumia wakati wa safari na ndiyo maana japo naona kama lengo lilikuwa zuri lakini kwenye utekezaji wake simo, tena simo kabisaaa!.
Nasema iweni na huruma na maisha ya sisi wajukuu wa Pangu Pakavu kwa sababu kila mara tumekuwa tukisema tieni mchuzi lakini hamtaki, naapa simo. Hivi mnadhani wale wadogo zangu akina Mzembe na Mzururaji ambao walikuwa wameng’ng’ana kuishi mjini humu kwa kuningezea shughuli ya kuwalinda na kuwahudumia mimi kaka yao Mkubwa, tajiri wa ukoo kwa kipato cha kunanga, Chokoraa wa Kabwela, na sasa walikuwa wameamua kurudi kijijini, si wamehairisha baada ya magari kuchelewa kuondoka na wamerudi kwenye lile pagala tunakojikusanya usiku na kujirundika tukipitiwa na usingizi ilhali tukiita huko ni kulala!?. Nasema hamjui ni kiasi gani ya gharama na maumivu ya moyo mmeniongezea mwaka huu na ndiyo kwanza unaanza. Naapa mpaka umelizike, tutaonana wabaya. Simo.
Na nyie ‘chuma tule’ hivi kweli na akili zenu zoote mmeshindwa kutengeneza ‘mpango mkakati’ (naogopa kusema ‘sitrateji’ msijesema napenda sana kikoloni) wa jinsi ya kukagua walio ‘liseni’ na kuwa lessen wale wasio nazo bila kunisumbua miye Mdanganyika Mlipa kodi!!? Naapa utaalamu umesafiri kwenye inchi ya wadanganyika walipa kodi. Simo, tena simo kabisaa.
Haya, tekelezeni majukumu yenu na wala msijesema mimi nawakataza kutekeleza majukumu yenu maana nafahamu mnayo sheria ya kuitumia kuniyamazisha miye hati kwa vile nimekuwa domo kaya wakati huyo ni mpwa wangu mimi jina langu ni lile lile le siku zote, Chokoraa wa Mdanganyika wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangu pakavu wa Kabwela.
Haha ha ha ha ha ha ha! Nicheke niongeze siku miye.
Salaam nawasalimia,
Chokoraa wa Muhangaikaji.
No comments:
Post a Comment