Nawaomba msihoji uzalendo wangu na wala msinione mwoga ila
nasema wazi Chokoraa nahama mjini. Naapa
kwa jina lake mama yangu Shida wa Matatizo binti Huzuni wa Sikitiko wa Taabu
Mateso Mengi humu simo , tena simo kabisaaa.
Nasema tena msijesema sikusema na naweka kumbukumbu sawa
kabla sijafunga vilango kurejea zangu shamba kwenye kile kibanda cha marehemu
bibi yangu alichoachiwa na marehemu mumewe Kabwela wa Mdanganyika, na hapo ni
ikiwa hakijauzwa kwa bei chee kwa mkulima wa matuta hamsini ya nyanya ila
mwenye umaarufu wa harufu kwa vile anapaka yale marashi ya siku hizi
yajulikanayo humu mjini kwenu kama ‘Ukewenzaji’ na humu simo. Simo.
Salaale!! Mwanitisha enyi wana na sasa sijui ikiwa nikitoka
kwenye pagala langu kwenda kuokoteza majalalani niwaambieje wadogo zangu akina
Mzembe na Mzururaji ama kwamba ‘tutaonana jioni’ ama niage kabisa!?
Ati washangaa!? Washangaa nini ikiwa siku hizi kukiwako tu
na taarifa za “kiintelijensia” kwamba Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa
Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika anaunda mabomu ya ‘nyuki hulia’ hakuna
anayejali hata kutaka kutumia walau sehemu kiduchu ya ‘intelijensi’ yake kupima
ikiwa kweli ‘intelijensia’ hizo ni sahihi anachofanya ni kuvuta “manati ya ndhungu” na halengi miguu bali
kichwa!? Naapa, kaya ya wadanganyika si salama kwa akina Chokoraa, labda kaka
zetu akina Mstahiki na Muishiwa wao kwa vile wanafanya makosa yaliyofanyiwa
upembuzi yakinifu. Wallahi twahitaji tena akina Nyerere na Kwame Nkurumah na
humu mi naapa sihusiki.
Kwani mmeanza leo enyi walinzi wa amani mliogeuka kuwa
wavuruga amani na sasa mmekuwa tishio la raia!? Nani hajui Wambeya walivyopoteza vitegemezi vyao kwenye ‘risero’
na bado tukaambiwa na ‘kamati teule’ juu ya ‘makosa ya kiufundi’ na kwamba
hatua za miguu zimechukuliwa kukomesha vifo hivi!? Hamkutosheka enyi wana na
sasa kila aliye na “manati ya ndhungu” akijisikia anadungua yeyeote amtakaye! Naapa kwa Muumba wa mbingu na ardhi Chokoraa
nina mashaka na kichwa changu maana mawe ya manati zenu yanaviona zaidi vichwa
vya Kunguru kuliko Mbuni kisa si kwamba Kunguru ni mwizi sana, lakini
anawanyima usingizi akina Mbuni waishio kwenye majumba ya starehe na humu miye
simo.
Kwani nini tofauti kati ya Punda na Farasi au Kunguru na
Mbuni isipokuwa aina ya maisha waishiyo ilhali wote wakiwa ni ndege na wayama
na humu miye nahusika kwani!? Kama haikuwatosheni enyi wenye dhamana ya uhai na
mamlaka ya kuutwaa wa kwetu na kuutoa sadaka huku mkijisafi kwa ‘mizimu weupe’
kwa damu zetu na wao wakiwapa ‘manati’ zaidi kwa vile hilo hasa lawaongezeeni
ninyi uishiwa na wao ‘shekeli’ zitokanazo na ‘mali asili’ za ardhi yenu hii ya wana
wa Hamu, mkawachukua baadhi ya kaka zetu na kuwapeleka kwenye ule msitu mkuubwa
mtoleako sadaka za damu ya wana wa Adamu na kuwachinjilia mbali na kisha
mkatwambia “yarikuwa yakipambana na ‘hofu
ya raia” tukakaa kimya si kwa vile tuliwakubalia bali kwa vile tuliogopa kesho
isiwe zamu yetu.
Nasema hata pale mlipoanza kuchunguzana huku mkikonyezana na
kuzungumza kwa uchungu wa kujifanya, Chokoraa nilijua igizo hili limemkosa tu
Muhogo Mchungu lingenoga lakini sikufumbua kinywa hadi ati “siri kali”
ilipopoteza kwenye shauri hilo watoto na wake wa ‘wajasiria mlo’ wale wakabaki
wajane na yatima likaisha. Nina uchungu lakini simo.
Kama haikuwatosha ni hivi majuzi tu mkaamua kumuua sisimizi
kwa risasi ya Tembo ati kwa vile sisimizi huyu ni mmoja wa wale wenye kupanda
kwa siri kwenye nguo zenu na kuyajua yale tusiyoyajua na kisha kuyaanika
hadharani, naapa hii tabia ya “hivi unanijua!” itawamaliza wanaobaki mjini
maana Chokoraa siji tena mjini na humo wala msinihusishe maana simo.
Haya, jiosheni muosheke basi kwa wana na mjane wa Yule mliyemtandika
bomu la machozi na kumtoa damu ya uhai kama mwaweza.
Haya, tena juzi juzi tu wanafunzi wakiwa kwenye michezo ya
kujificha kwenye eno la hifadhi, wenye manati za ndhungu, tena za ‘siri kali’
ya kaya yao, wamewakomelea hadi umauti na Chokoraa nauliza, hivi mwawapima
vyema hawa mnaowakabidhi hizi manati au kila mmoja sasa anaweza kubeba manati
na akiogopa kidogo tu basi anadungua!? Jibu msinipe, lakini wafundeni basi
walau kwamba watumia ‘intelijensi’ zao kuamua ikiwa intelijensia wanazopata
zinatosha kuwapa kibali cha kudungua ama lah, vinginevyo Chokoraa sirudi mjini
na humu mi sihusiki.
Ni mimi ndugu yenu Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa
Pangupakavu wa Kabwela wa mDanganyika nawasalimia. Simo.