Thursday, October 11, 2012

Chokoraa nahama 'Mjini'.



Nawaomba msihoji uzalendo wangu na wala msinione mwoga ila nasema wazi Chokoraa nahama mjini.  Naapa kwa jina lake mama yangu Shida wa Matatizo binti Huzuni wa Sikitiko wa Taabu Mateso Mengi humu simo , tena simo kabisaaa. 

Nasema tena msijesema sikusema na naweka kumbukumbu sawa kabla sijafunga vilango kurejea zangu shamba kwenye kile kibanda cha marehemu bibi yangu alichoachiwa na marehemu mumewe Kabwela wa Mdanganyika, na hapo ni ikiwa hakijauzwa kwa bei chee kwa mkulima wa matuta hamsini ya nyanya ila mwenye umaarufu wa harufu kwa vile anapaka yale marashi ya siku hizi yajulikanayo humu mjini kwenu kama ‘Ukewenzaji’ na humu simo.  Simo.
Salaale!! Mwanitisha enyi wana na sasa sijui ikiwa nikitoka kwenye pagala langu kwenda kuokoteza majalalani niwaambieje wadogo zangu akina Mzembe na Mzururaji ama kwamba ‘tutaonana jioni’ ama niage kabisa!? 

Ati washangaa!? Washangaa nini ikiwa siku hizi kukiwako tu na taarifa za “kiintelijensia” kwamba Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika anaunda mabomu ya ‘nyuki hulia’ hakuna anayejali hata kutaka kutumia walau sehemu kiduchu ya ‘intelijensi’ yake kupima ikiwa kweli ‘intelijensia’ hizo ni sahihi anachofanya ni kuvuta  “manati ya ndhungu” na halengi miguu bali kichwa!? Naapa, kaya ya wadanganyika si salama kwa akina Chokoraa, labda kaka zetu akina Mstahiki na Muishiwa wao kwa vile wanafanya makosa yaliyofanyiwa upembuzi yakinifu. Wallahi twahitaji tena akina Nyerere na Kwame Nkurumah na humu mi naapa sihusiki. 

Kwani mmeanza leo enyi walinzi wa amani mliogeuka kuwa wavuruga amani na sasa mmekuwa tishio la raia!? Nani hajui  Wambeya walivyopoteza vitegemezi vyao kwenye ‘risero’ na bado tukaambiwa na ‘kamati teule’ juu ya ‘makosa ya kiufundi’ na kwamba hatua za miguu zimechukuliwa kukomesha vifo hivi!? Hamkutosheka enyi wana na sasa kila aliye na “manati ya ndhungu” akijisikia anadungua yeyeote amtakaye!  Naapa kwa Muumba wa mbingu na ardhi Chokoraa nina mashaka na kichwa changu maana mawe ya manati zenu yanaviona zaidi vichwa vya Kunguru kuliko Mbuni kisa si kwamba Kunguru ni mwizi sana, lakini anawanyima usingizi akina Mbuni waishio kwenye majumba ya starehe na humu miye simo. 

Kwani nini tofauti kati ya Punda na Farasi au Kunguru na Mbuni isipokuwa aina ya maisha waishiyo ilhali wote wakiwa ni ndege na wayama na humu miye nahusika kwani!? Kama haikuwatosheni enyi wenye dhamana ya uhai na mamlaka ya kuutwaa wa kwetu na kuutoa sadaka huku mkijisafi kwa ‘mizimu weupe’ kwa damu zetu na wao wakiwapa ‘manati’ zaidi kwa vile hilo hasa lawaongezeeni ninyi uishiwa na wao ‘shekeli’ zitokanazo na ‘mali asili’ za ardhi yenu hii ya wana wa Hamu, mkawachukua baadhi ya kaka zetu na kuwapeleka kwenye ule msitu mkuubwa mtoleako sadaka za damu ya wana wa Adamu na kuwachinjilia mbali na kisha mkatwambia  “yarikuwa yakipambana na ‘hofu ya raia” tukakaa kimya si kwa vile tuliwakubalia bali kwa vile tuliogopa kesho isiwe zamu yetu. 

Nasema hata pale mlipoanza kuchunguzana huku mkikonyezana na kuzungumza kwa uchungu wa kujifanya, Chokoraa nilijua igizo hili limemkosa tu Muhogo Mchungu lingenoga lakini sikufumbua kinywa hadi ati “siri kali” ilipopoteza kwenye shauri hilo watoto na wake wa ‘wajasiria mlo’ wale wakabaki wajane na yatima likaisha. Nina uchungu lakini simo. 

Kama haikuwatosha ni hivi majuzi tu mkaamua kumuua sisimizi kwa risasi ya Tembo ati kwa vile sisimizi huyu ni mmoja wa wale wenye kupanda kwa siri kwenye nguo zenu na kuyajua yale tusiyoyajua na kisha kuyaanika hadharani, naapa hii tabia ya “hivi unanijua!” itawamaliza wanaobaki mjini maana Chokoraa siji tena mjini na humo wala msinihusishe maana simo. 

Haya, jiosheni muosheke basi kwa wana na mjane wa Yule mliyemtandika bomu la machozi na kumtoa damu ya uhai kama mwaweza.  

Haya, tena juzi juzi  tu wanafunzi wakiwa kwenye michezo ya kujificha kwenye eno la hifadhi, wenye manati za ndhungu, tena za ‘siri kali’ ya kaya yao, wamewakomelea hadi umauti na Chokoraa nauliza, hivi mwawapima vyema hawa mnaowakabidhi hizi manati au kila mmoja sasa anaweza kubeba manati na akiogopa kidogo tu basi anadungua!? Jibu msinipe, lakini wafundeni basi walau kwamba watumia ‘intelijensi’ zao kuamua ikiwa intelijensia wanazopata zinatosha kuwapa kibali cha kudungua ama lah, vinginevyo Chokoraa sirudi mjini na humu mi sihusiki.


Ni mimi ndugu yenu Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa mDanganyika nawasalimia. Simo.

No comments:

Post a Comment