Nasema
mapema kwa hili wana wa Danganyika hii mmenikera na ndiyo sababu miye sitaki
kuhusika maana simo tena simo kabisaaaaa. Ala! Kwani si mwezi
mtukufu wa ramadhani si umeingia na ati siku moja kabla ya mwezi kuanza
wengi wenu mlikuwa na sherehe ya kuvunja vyungu kwa vile kwa mwezi mzima
hamtakula!?. Naapa mwamtania Mungu enyi wana.
Naapa kwa jina la Babu yangu mzee Mlalahoi wa
Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika, nyie mwamtania Mungu. Nasema mmemgeuza
Mungu kuwa babu yenu na miye humo msinihusishe. Ala! Si nimeshuhudia mwenyewe
ambavyo jana wengi wenu hamkuwamo majumbani kwenu na hata mmedhulumu haki za
'ndoo' za wenzi wenu kwa kuvunja vyungu vyote ati kwa vile mwezi huu hampiki
ila mwala magengeni na sasa vungu vya nini!? Naapa laana mmelaaniwa enyi wana na
miye humo simo. Sitaki, tena nasema sitaki kuwashawishi mkubaliane na mimi katika
kila nisemacho lakini ni kweli kwamba ama hizi dini zimekuwa kwenu kama kongwa
la utumwa ni vyema mungelizivua mkatembea huru katika uhuru wa mwendawazimu
kuliko huu wazimu wa usiku muufanyao naapa mmenikera enyi wana. Na sasa
najiuliza wakati ninapowatakia wale wenye nia safi Ramadhani karim, nyie
wengine ambao jana mmefanya kufuru ya kuvunja vyungu vyetu niwaambieje? Poleni
na starehe?. Simo.
Nasema kwa kitendo chenu hiki nashindwa kujua niwaiteje
maana kuwaita wafuasi wa dini itakuwa kuikosea adabu dini yenyewe maana ikiwa
hao mitume walioleta kwenu dini hiizi wangefufuka leo, bila shaka na ongezeko
hili la magonjwa yasiyokuwapo enzi zao wangekufa mara ya pili mara hii kwa
magonjwa ya moyo kama si sononi na humu najitoa maana simo.
Haya, wacheni nijiropokee maana humu ndani naweza kuropoka
tu bila hofu kwa vile mimi ni Mdanganyika tena mlipakodi na ninafahamu nyie
wenye kuvunja vyungu vyetu ili wote tushinde njaa kama ninyi hamna mahusiano ya
karibu na wale wasiojulikana na hivyo sikuogopeni katu. Nasema nyie si
wafungaji ni washinda njaa na mwaiongoezea kaya yetu mzigo wa kuuguza wagonjwa
wa vidonda vya tumbo na magonjwa yake kwa kujisindisha njaa ilhali nafsi zenu
zili dhalili na humu mnitoe.
Ala! Kwani hayakuwatosheni maovu ya mwaka mzima hadi
mlipoamua kufanya kufuru za mwaka mzima “ini advansi” kwa vile funga
imekurubia?. Ha ha ha ha ha ha ha!!!! Najiuliza wadanganyika nyie mwajidanganya
na nini kuwaza kwamba huyu Mungu anawaza kama muwazavyo ninyi na hivyo
atawaosheni na maovu yenu ya makusudi muyatendayo kwa kujikinahi!?. Hayo
nakuachieni nyinyi maana hata mimi ni muovu mwana wa uovu na yamkini hata mimba
yangu ilitungwa hatiani lakini kwa hili msijifananishe name maana simo.
Nasema mimi na ninyi hatufanani kwa sababu binafsi
najifahamu kwamba sihitaji kujishindisha njaa kwa sheria tu ilhali nikiwa muovu
na hivyo wakati wenzangu jana mmevunja vyungu vyote mtaani, mimi nimenunua
magudulia ya chuma nasonga ugali nile nishibe ili nikuchekeni nyie wenye
kujivisha ngozi za kondoo ilhali ndani ni mbwa mwitu wakali.
Hivi, nyie si ndiyo wale mliohusiwa juu ya vita vilivyo bora
zaidi yaani vita vya kuishinda nafsi!?
Mbona sasa mmekuwa watumwa wa nafsi zenu wakati ingekuwa rahisi kwenu kula
mkashiba mkafanya kazi na kuongeza uchumi wa jamii zenu huku mkiwa na afya
njema na nafsi safi bila kulazimika kuwa wanafiki!? Naapa huu wa wavunja vyungu
ni unafiki tena unafiki mtupu!.
Kasirikeni mkasirikavyo lakini jueni kwamba mwana wa
muhangaikaji kwa hili mmenikera lakini sina hasira sana kama nilivyo na huruma.
Ninawahurumia na ndiyo sababu ya kukuandikieni waraka huu ili mwenye masikio ya
kupona asikie hizi dawa lakini ikiwa ni wa kufa basi ziba masikio kwa hasira na
visingizio. Ndiyo, najua mtaleta visingizio kwamba ati Chokoraa miye nimeitusi
dini nasema huo utakuwa ni unafiki wa radaja la pili maana miye siitusi dini
ila nawauliza wenye kujifanya mwaifuata dini kana kwamba kwa shuruti huku
mkifanya kufuru, mmejihoji ni wangapi kati yenu mliokumbuka kula pipi zenu
kwenye maganda ama huko nako mlivunja vyungu!? Naapa ikiwa na hilo nalo
mlilivunjia vyungu, basi jiulizeni ni wangapi kati yenu mlioambukizwa kale
kaungonjwa na mnaojiandaa kunilaumu Chokoraa nikikataa kuja kuwaona mlazwapo
hospitali na wengine kusema nawanyanyapaa!? Kwa hili naapa niiteni mnyanyapaa
lakini hata kwa Mungu sina hatia ikiwa nitawanyanyapaa kwa kujisulubisha wakati
wa kuvunja vyungu maana kuna tofauti ya makusudi na bahati mbaya msiolijua hilo
jilaumuni wenyewe na humu simo.
Haya, na wale ambao mliwatoroka wazazi wenu na kwenda kwa
vibwana vyenu huku mkidhani mwawafurahisha kumbe mwajitafutia majukumu ya ulezi
msiyoyaweza bado na mwisho wa siku mwataka jamii ibebe mzigo wa kunilea
Chokoraa miye na wadogo zangu akina mzembe na mzururaji!? Hivi na hili nalo
linahitaji “sirikali” kukupeni onyo mapema?.
Komeni. Nasema komeni hasa nyie mjiitao “wana haraka tu”
kuipigia kele ‘siri kali’ ati kwa kutofanya chochote kuwasaidia ‘watoto wa
mitaani’. Nasema mkome. Ndiyo, najua wengine ni rafiki zangu lakini
nisikilizeni maana kwa hili siropoki nasema hakuna mtoto wa mtaani maana kila
mtoto ana baba na mama yake na ni lazima wawajibike wao kwanza kuondoa watoto
wao mitaani na ndipo sisi wengine tutafuata!?. Ala! Mwataka tu nyie mfanye fujo
zenu na kuvunja vyungu vyetu bila mipango wala mikakati ya kukabiliana na
matokeo ya uvunjaji vyungu huo kisha siye tuwajibike!? Nani kasema!?. Simo humu
namo.
Ha ha ha ha ha ha!!! Hongera zenu wajasiria mlo maana nina
hakika kwa siku ya jana nyie jana mlikuwa na “ugeni” mkubwa na hata wengine
walilala sebleni na hata wako waliopitisha muda wao kwenye maliwato na huko
kote wakivunja vyungu. Kwani viliwakosea nini?. Ama kosa la vyungu hivi ni
kuwapikieni mwaka mzima na sasa kwa vile mwezi huu mwabadili ratiba ya kula
basi vyungu havina thamani tena?. Nasema nyie mliovunja vyungu jana hamjafunga
hata kidogo. Mmebadili tu muda wa kula kwa kuacha kula mchana mzima huku
mkifakamia milo yote usiku maana kufunga huanzia kwenye nafsi na nyie nafsi
zenu mmeziuza kwenye kuvunja vyungu.
Haya, najua wako wale ambao kwa nia ya kweli ujio wa
ramadhani umewakuta wamejiandaa nafsi zao kwa ajiri ya muumba wao. Kwenu nyie
salamu zangu ni chache tu. Muombeni huyo Mwenye Enzi yote aliyevifanya vyote
atufanyie wepesi hasa kwenye kaya yetu hii itafunwayo kila siku na dini huku
wote tukifanya juhudi kumtafuta Mungu huyo huyo. Kwenu nyie nasema ‘kun faya
kun’ mnisamehe ikiwa neno hili limekosewa lakini ikiwa yeye mwenye kusema kuwa
likawa angetaka wote tuwe dini moja isingeshindikana na hivyo muombeni
aturudishie mioyo ya subira tujue kuvumiliana na kuchukuliana katika
kutofautiana kumwamini kwentu maana Mungu ni mmoja tu hajakuwako mwingine kabla
wala baada yake hatakuwako mwingine sasa sisi twagombea nini? Twagombea mapokeo
yaliyoletwa na wale walioleta tena kwa maslahi yao binafsi wakituchonganisha
ili watuibie? Naapa huo nao ni uduni wetu wa kufikiri na humo miye simo.
Tuombeeni. Wala smituombee atujaze mapesa mifukoni maana
amani na furaha ya kweli haitokani na kuwa na mifedha kedekede lakini atujaalie
akili njema na uwezo wa kuziona na kuzitumia fursa kujitendea na kuwatendea
wengine mema. Tuombeeni atujaalie kujua kwamba yaliyowekwa wazi ni yetu na
watoto wetu ili tuyatende nay ale yaliyofichwa ni yak wake ili tumche na
kumwabudu na siri ya kwanini Chokoraa namwamini hivi na wewe waamini vile si
yetu ni yake tuache kuyachokonoa yasiyo yetu.
Mwisho niombeeni na mimi ndugu yenu Chokoraa mwana wa
Muhangaikaji walau nitengeneze mkate hata kama ni wa unga wa mahindi badala ya
kuokoteza kila siku maana akina kaka muishiwa hawataki kunitupia tena vipande
vikubwa wanasema nikishiba sana nawapigia kele na hivyo nile kidogo ili nguvu
zinipungue wanitawale.
Ni mimi ndugu yenu, Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa
Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika nawasalimu. Ramadhani Karim.Salaam nawasalimia.