Salaam nawasalimia. Karibuni kwenye kilinge cha Chokoraa
enyi Wadanganyika wana wa Mlipakodi mnisikize kaka yenu Chokoraa mwana wa
Muhangaikaji, maana niyaonayo miye huku majalalani yatosha kunitia fahamu na
kutaka salam kuwatumieni, Salaam wadanganyika.
Ukiamka asubuhi huku tumbo lakusumbua, usikimbilie kupiga
ramli ama kufakamia kikombe cha babu bali tafakari ulichokula jana yake na hiyo
ndiyo busara enyi wana, salaam ndugu yenu Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi
wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika Mlipakodi nawasalimia.
Ati!. Wakataa nini? Kwamba wewe si Mdanganyika ama si mwana
wa Mlipakodi!?. Ha ha ha ha ha!!! Nicheke miye kitukuu wa Kabwela maana
nijuavyo Wadanganyika nyie sasa mwahoji hata asili ya mzazi wa mzee Utaifa wa
Uzalendo wa Uadilifu na miye humu nahusikaje!?. Ndiyo, kwani siku hizi si
Wadanganyika wote wamekuwa ‘wana haraka tu’?.
Nani alinidanganya nikadanganyika Chokoraa miye kwamba
harakaharaka haina Baraka maana siku hizi ati mwauthamini zaidi msemo ule
kwamba ngojangoja yaumiza matumbo pasina kutafakari kwamba ‘haraka tu’ zenu za
kula hata visivyoliwa na wazee wenu kabla yenu, ndiyo sababu ya matumbo yenu
kukusoketeni na wala si subira yenye kuvuta heri iliyo chanzo cha mgogoro wa
matumbo yenu!?. Naapa humu miye msinhusishe maana simo.
Siku hizi ati kila Mdanganyika ni ‘mwana haraka tu’ na miye
nauliza, hizi haraka zenu zakupelekeni wapi enyi wana mbona mwanishangaza!.
Nasema mapema ili yatokeapo msijenihusisha mchakuraji miye maana miye yangu
majalala huku nikichakurachakura nione ikiwa nitapata kipande cha boflo nipooze
njaa ya tumbo langu.
Ama kweli kusoma kwingi si kujua mengi bali maisha ndiyo
kipimo cha akili kama walivyosema wale waliokuwa kabla yangu miye mwana wa
Muhangaikaji. Najiuliza hivi mbona kila siku kwaibuka ‘wana haraka tu’ na mbona
wote waibuka kunifunda kudai haki na hakuna kati yenu awekezaye muda walau
kiduchu kunifunza wajibu!?. Nani alikudanganyeni kwamba haki huja bila wajibu
wenyi wana mbona mwapotea njia mchana kweupe kwa uzembe wa kuuliza?.
Haki ya mtoto, haki ya mwanamke, haki ya kichaa, haki ya
mlevi, haki…. na miye nakuulizeni haki zenye kuja bila wajibu mwayajua madhala
yake nyie?. Ha ha ha ha ha!!! Oneni sasa mnavyolalama kwamba ati Yule mzee wa
siku nyingi wa kaya yetu almaarufu Maadili ya Mdanganyika yu taabuni kama si
taabani. Mwalalama nini ikiwa mmeshindwa kujua kwamba hamuwezi kuendelea
kumlisha mzee huyu sumu iliyomuua Maadili ya Wageni na mkataraji ati kwa vile
huyu na yule wafanana majina tu lakini si ndugu basi sumu itageuka kuwa dawa
kwenu!?. Simo nasema.
Nasema ijapo mtasema wajuaje weye tofauti ya uchafu na
chakula bora ama dawa na sumu kali ilhali wala majalalani na kulala mitaroni
lakini nasema hekima si kama pesa kwamba ukiwa nayo yakutia kiburi na dharau na
maneno ya mwenye hekima ni bora ijapokuwa hekima ya maskini haithaminiwi na
hata maneno yake hayasikizwi na ndiposa nawasalimu, shikamooni Wadanganyika.
Haya, nakumbuka wakati wa kukua kwa wadogo zangu wale akina
Mzembe na Mzururaji na hata mimi kaka yao Chokoraa wa Muhangaikaji, fimbo
ilikuwa ufunguo uliiondoa ujinga kichwani mwa mtoto lakini sasa mwasema ni haki
ya mtoto kutopigwa bali ipigwe ngoma na miye nakuungeni mikono na miguu yote,
lakini wacheni kulalama basi ikiwa heshima ya juzi na jana zina tofauti maana
hiyo ni haki ya mwendawazimu peke yake. Ala! Kwani si haki ilipaswa kuja na
wajibu!?. Nasema ikiwa mwanifunda tu juu ya haki yangu na kudhani wajibu wangu
nitaufahamu ikiwa tu nitapewa haki yangu, jiandaeni basi kwa madhila ya kizazi
cha nipe nipe maana ndivyo mtakavyo na miye humu nahusikaje!?.
Ati! Wengine mnalalama ni kwanini kila mkirejea majumbani
mwenu mwakuta ‘ndoo’ zimevunjika na sasa vijana hamzitaki hata ‘ndoo’ zenyewe
badala yake mwanunua mabeseni ya karatasi ambayo mkiishaogea mwayatupa huko
huko maliwatoni!?. Mwalalama nini!?. Kwani mlipoamua kutangaza haki na usawa
kati ya jinsi zenu bila hata kufafanua yale yapasayo kuwa sawa na yale yasiyopasa
na badala yake mmeifanya jamii yote kuwa na watu wenye maumbile ya Adamu na Hawa
lakini wenye kufikiri kama Adamu tu mlidhani madhara yake nini!?. Nasema
chakula cha fahamu ni maneno na mifano na kile wanachokisikia wanenu na
kukuoneni nyie mkitenda ndicho watakachotenda na wao kwa juhudi kubwa kuliko
watangulizi wao na miye humu mnitoe maana simo.
Wacha nikomee hapa hadi tutakapokutana juma lijalo kwenye
kijiwe hiki, wacha nijaribu kumeza vipande vya boflo hivi na maji ya chumvi ila
salaam zangu zikufikieni enyi Wadanganyika.
Wasalaam, ni mimi ndugu yenu Chokoraa wa Muhangaikaji wa
Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika, nawasalimia. Shikamooni
Wadanganyika.
No comments:
Post a Comment