Wednesday, October 15, 2014

Mwaujua Ugonjwa wetu enyi wana!?



Salaam nawasalimia. Nasema tofauti ya mjinga na mwerevu ni ipi ikiwa nilijualo hulijui na ulijualo silijui na ujinga ni kutojua jambo enyi wana salaam nawasalimia. Ha ha ha ha ha ha!!! Nicheke miye! Kwani si mlikuwa mwalalama ati mwataka makubaliano mapya nyie mwaita katiba ya kugawana kaya yenu? Haya, kiko wapi sasa enyi msiojua majira na nyakati hata mwalana na kuraruana mkigombea fito ilhali mwajenga nyumba ileile?. Naapa humu simo. 

Ona huyu naye ati niwachilie mbali viapo kwa vile viapo vyazuiwa na mila za kikoloni pasina kujua kiapo ni ukomo wa uwezo wa mwanaadamu, na mimi katika kukueleweni nimefika ukomo na naapa mwaniapisha enyi wana na miye humu simo. 

Shikamooni Wana wa Haraka Tu. Ndiyo, salaam nawasalimia kwa vile haraka zenu zakuponzeni mwapotea njia mchana kweupe kwa uvivu wa kuuliza na miye humo nahusikaje!?. Simo. 

Ala! Mwadhani ati kwa vile Chokoraa miye hushinda majalalani nikichakura nipate cha kuwalisha vitegemezi vyangu wana wa mama yangu Shida wa Matatizo wa Taabu wa Maisha magumu mke wa mzee wangu Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu kilembwe wa Mdanyika Mlipakodi, basi siijui tofauti ya adhuhuri na jioni!? Mwanitania enyi wana na miye humo simo. 

Nasema wachilieni mbali uzandiki wenu ashakumu si matusi ila ikiwa kwenu kuuita uovu kwa jina lake matusi, basi miye salaam nawasalimia. Ndiyo, nakumbuka sana miaka ile ya kipindi kile cha Yule kitukuu wa Nchumali Ntoto wa Chilingi mwana wa Chipuputa mlivyokuwa mkiiandama ‘siri kali’ tena kwa kuivisha koti la chama cha upinde wa zamani, na kudai ati inakataa kuanza mchakato wa katiba na hivyo kuwahujumu wanyonge. Naapa wanyonge wa kaya hii wamekosa msemaji na miye humu nitoeni. Ala! Kwani mwadhani sioni jinsi ambayo kwa Mkwere huyu kukuruhusuni mfanye huo mchakato wenu mlivyowageuza ‘wana wa kaya’ kuwa ngao katika vita yenu ya panzi!?. Nasema msinitanie enyi wana maana miye si babu japo kusema kweli kwenu nyinyi pia si mjukuu na humu pia nitoeni. 

Nauliza maana kuuliza si ujinga, kwani ‘Waishiwa’ ninyi si ‘wana wa kaya’ ati kwa vile tu mko kwenye hilo genge lenu la wahuni wajuao kuvaa mavazi na tabasamu za kikoloni? Kama na nyie ni wana kaya, inakuwaje mwagombana na kila mmoja akidai anatetea maslahi ya Wana wa Mdanganyika wa Mlipakodi? Naapa mwatufanya mazuzu enyi wana na miye humu sitaki katu kuhusika maana simo, tena simo kabisaaaaa! 

Ati! Hivi mwadhani shekeli za baba yetu Mdanganyika wa Mlipakodi mnapoziswaga kama Ng’ombe waendao machinjioni kwa kisingizio cha kutuandalia  ka tiba kaliko bora bila kuufahamu vyema ugonjwa wetu, sisi nao ni wajinga tusioifahamu janja yenu!? Wacheni dharau enyi weledi wenye kwenda mbele ilhali macho yatazama mtokako na miye humu nahusikaje!? Simo.

Haya, mwabishana na kugombana kila mara ati muwe na siri ngapi za kuzitunza pasina kujiuliza hizo mlizokuwa nazo zimevujaje hata kutufikia sisi akina Chokoraa kama mwafahamu kutunza vyema hizo ‘siri zenu kali?’. Naapa ujinga hauna tafsiri na miye humu nitoeni.
Kwani nyie si ndiyo mliokuwa vinara wa kumnukuu Yule mzee mwana wa Mzalendo na hapa namsema Mkufunzi wa Mzalendo wa Mdanganyika, ki wapi sasa kile mlichokuwa mkituaminisha sisi wadharauliwa wenu kwamba “wale” wameasi misingi iliyotiwa na Mkufunzi na “ninyi” ndiyo manabii pekee mliobaki kuirejesha kaya yetu kwenye msingi?. Ha ha ha ha ha!!! Nasema penye pongezi zitolewe na mimi nakupongezeni maana mwauweza vyema mchezo wa ‘si hasa’ isipokuwa izi za mara hii ni zile za majitaka yasiyofaa kwa kunywewa ama kilimo cha umwagiliaji kama mjitapavyo na miye humu simo. Ala! Mlipoona misingi ya huyo mkufunzi mwenyewe inakinzana na tamaa za mioyo yenu, si nilikusikieni baadhi yenu mkimtusi hadharani kama wana wasio malezi wenye kutukana wazazi? Naapa laana mmelaaniwa enyi wana na miye humo simo. 

Nani kakudanganyeni Chokoraa miye na wadogo zangu ukoo wa Mdanganyika Mlipakodi ugonjwa wetu ni idadi ya ‘siri’ zenu!? Kwanza hatutaki hata kuzijua hizo siri zenyewe, ziongezeni ukali hata tusizikaribie kama mwataka, lakini hakikisheni kaya yetu inabaki moja kama alivyoiwacha mwana wa Mzalendo na msipotenda hayo, naapa hatutaiwachia historia kuwahukumu bali tutawahukumuni sisi wenyewe na  miye humo simo tena simo kabisaaaa, ila salaam nawasalimia. 

Ni mimi Mdharauliwa wenu, Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdangayika wa Mlipakodi nawasalimia. Salaam Waishiwa.  

Friday, January 3, 2014

Mgeni Njoo Mwenyeji Akome.



Salaam nawasalimia. Najua mwaka wa jana umekwenda na najua wengi wenu bado mngali kwenye zile nyumba zenu zenye baridi ya kutengeneza huku mkijituma wengine kuijenga na wengine kuivunja kaya ya wadanganyika na ati bado mwashangaa kwanini jengo halikamiliki. Mwashangaa nini?. Nasema ikiwa walio wengi mnafanya kazi ya kubomoa ilhali wachache tena wenye nguvu chache wanafanya kazi ya kujenga si ajabu itawachukua miaka dahali walau kulifikisha jengo kwenye ‘renta’ ila humo miye simo bali salaam nawasalimia. Shikamoooni Wadanganyika. 

Nisemeje!?. Mwataka nirudie kuwakumbusha madhila yaliyotukuta kwa mwaka uliopita?. Katu. Nasema siendi safari ya maili kumi elfu kinyumenyume asomaye na afahamu ila mi salaam nawasalimia. Jana imepita na kesho si yetu lakini ikitumika vyema leo walau kesho yaweza kuwa na matumaini na miye hapa nawasalimia. Kwa mwaka huu naapa sitasema matukio bali mazoea na tabia zenu maana tabia hutengeneza utamaduni wa jamii na miye nakuulizeni enyi wana  wa Mdanganyika Mlipakodi nani aliyekundanganyeni kwamba kuna kaya nyingine mtakwenda baada ya Danganyika yenu hii?. Ala! Washangaa nini?. Kwani si miye nakuoneni mnavyoishi kama watalii tu hapa kwenye kaya yetu kila mmoja akijaribu kuwa kama wale waliowatawala babu zetu bila kujua kwamba twatofautiana siyo tu ngozi bali mtizamo na miye humu nitoeni.

Ha ha ha ha ha ha!!!! Nakumbuka Mkulu wa Kaya kabla ya ule “Uchafuzi Mkuu” wa mwaka uleeeee ulitukasirisha sisi Wadanganyika hata tukapiga kura na kumpa yeye aslimia zaidi ya thamanini ya ‘kula’ zetu huku tukisahau kwamba tuna zaidi ya asilimia tisini ya familia za kulishwa na ‘kula’ hizo za bwelele, alituahidi ajiira makumi mia na sasa leo twalalama na miye nauliza twalalama nini?. 

Mwaka wa jana Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika Mlipakodi nimezunguka majalala yote tangu yale ya uswahilini kwetu kunakotupwa miiba ya dagaa hadi yale ya waishiwa kunakotupwa boflo na mapande ya nyama ati kwa vile yamekaa sana kwenye jokofu yakakosa radha, naapa mwakufuru enyi wana. Kwani mabucha hamkuyaona hadi mwanunua vyakula na kisha kuvitupa kwa kujifanya uzungu usio tija!?. Simo naapa. Kwani msipotupa Chokoraa miye nitakula nini? Lakini walau jifunzeni kumheshimu Mwenyezi aliyekupeni nyie kusaza siyo kwamba mtupe jalalani bali mtupe siye tusio hata na kidogo na miye humo nahusikaje?. Simo.
Nasema katika kuzurura kwangu nimejifunza jambo moja kuu na hapa salaamu nawasalimu wale sungu sungu wa mipaka yetu na wale manyapara wenye jukumu la kusimamia vibarua vya kaya yetu, shikamooni waishiwa. Nauliza, hivi waishiwa nyie mnafahamu  uzito na upana wa majukumu yenu au kwavile kama wasemavyo  wadogo zangu wale akina Mzembe na Mzururaji kwamba kaya imeuzwa basi na nyie mmeamua kuuza na utu wetu? Naapa humu miye nisihusishwe. 

Nasema kuanzia kule kwa akina Ngosha kwenye viwanda vya samaki hadi kwa akina Nchumali kwenye Korosho wadanganyika nyie hamna chenu  ati kisa mnatekeleza sera ya ‘Ukewenzaji’ na miye nauliza mbona ‘Ukewenzaji’ huu mwabakwa nyie na sisikii hata lalamiko?. Ha ha ha ha ha ha!!!!! Ninyamaze miye maana si ajabu mkaniuliza kanituma nani wakati miye ni salaam tu nawasalimia. 

Hivi wakati mlipoamua ‘kubinua na kufisha’ viwanda vyetu vyote tulivyorithi kutoka kwa wazee wetu Waishiwa nyie mliamua kubinua na kufisha hata ajira zetu?. Ha ha ha ha ha!!! Chokoraa miye nimepita na kukutana na wageni wakikaa kwenye majumba ya viyoyozi huku wakiwa hawajui hata kuandika idadi ya mali inayoingia na kutoka viwandani zaidi ya utaalamu wa kujua kuvaa na tabasamu za kikoloni na ujasiri wa macho wa kuwatazameni usoni mnaposhikana mikono kusalimiana na miye nauliza, hivi hakuna kati ya Wadanganyika wataalamu wa kufanya kazi hizi hadi mwatuletea wataalamu “feki” wenye kujua tu tabasamu na “hendisheki” ilhali utendaji wote wafanywa na akina “sabani” asomaye na afahamu?!!! Simo humu. 

Nani hakumbuki jinsi ambavyo kwenye migodi ya dhahabu kulikuwa na wageni waliokuwa wakiitwa “sekyurite sipeshialisiti” ati kwa vile wanatokea Unepali ilhali kwao walikuwa makplo na masajenti huku makapteni na maluteni wetu wastaafu wakisota mitaani kutafuta ugali wa kulisha watoto!? Naapa historia inajurudia na miye humu simo. 

Bado kidogo. Sijamaliza, naomba kuuliza wakati “wakewenzaji” hawa wanapoleta msururu wa “wataa haramu” hawa na kuwavusha kwenye stendi za mabasi ya hewani, wanawaeleza wataalamu wetu wa uhamiaji kwamba wanakuja ‘kuisaidia’ kaya yetu kwa lipi?. Au ndiyo yale yale ya kiazi kuitwa kwa lugha ya kitaalamu “potato”?!!!!. Naapa sihusiki.  Haya, endeleeni na michezo hii ya mbuni ya kuficha vichwa mchangani ili mkirudishe kizazi chetu kwenye ukoloni kule ambako babu zetu walipigana kufa na kupona kututoa sisi halafu na nyie mtakapolala na baba zenu mkiiendea njia ya watu wote mkumbukwe kama wasaliti wa juhudi za wazee wenu na miye humo nisihusishwe maana simo tena simo kabisaaaaa, sihusiki. 

Haya, na nyie mjiitao wakulu wa kazi na ajira wa kaya yetu, mmeshindwa nini kutengeneza torati ya kulinda ajira za wadanganyika wenzenu na kuzisimamia?. Ha ha ha ha ha ha!!!! Najua, najua mwaniona mjinga kwa vile wadogo wakisimamisha pembe wakubwa wapewa bahasha na mambo yanakwisha na miye humo nahusikaje? Lakini niseme miye nisijehukumiwa na kizazi kijacho kuwa mnafiki maana najua kama mungetaka kuyatenda yawapasayo yangetendeka lakini hiyari yashinda shuruti na miye humu nahusikaje?. Simo naapa. 

Haya, leo akina "Sabani" wamebaki kufukia hivyo "vidigirii" chini ya magodoro ya bibi zao huku wakipika chai na kufagia na kisha kwenda kufanya kazi za taaluma zao ili kuwafurahisha "mabosi" wasiojua hata kusoma na kuandika lakini wenye vibali halali tena vya kufanya kazi za taaluma kwenye kaya yetu na miye humu nahusikaje maana simo. Nauliza katika kutembea kwenu kote huko mwendako mmeshindwa kujifunza kwamba kaya za wenzetu hata kabla hujaenda wanakupima hata magonjwa wajiridhishe juu ya usalama wao na watu hao?. Nani aliyekurogeni enyi wana wa kushi?. Simo naapa. 

Ni mimi ndugu yenu Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika Mlipakodi nawasalimia, Shikamooni Wadanganyika Walipakodi.