Salaam nawasalimia. Nasema tofauti ya mjinga na mwerevu ni
ipi ikiwa nilijualo hulijui na ulijualo silijui na ujinga ni kutojua jambo enyi
wana salaam nawasalimia. Ha ha ha ha ha ha!!! Nicheke miye! Kwani si mlikuwa
mwalalama ati mwataka makubaliano mapya nyie mwaita katiba ya kugawana kaya
yenu? Haya, kiko wapi sasa enyi msiojua majira na nyakati hata mwalana na
kuraruana mkigombea fito ilhali mwajenga nyumba ileile?. Naapa humu simo.
Ona huyu naye ati niwachilie mbali viapo kwa vile viapo
vyazuiwa na mila za kikoloni pasina kujua kiapo ni ukomo wa uwezo wa
mwanaadamu, na mimi katika kukueleweni nimefika ukomo na naapa mwaniapisha enyi
wana na miye humu simo.
Shikamooni Wana wa Haraka Tu. Ndiyo, salaam nawasalimia kwa
vile haraka zenu zakuponzeni mwapotea njia mchana kweupe kwa uvivu wa kuuliza
na miye humo nahusikaje!?. Simo.
Ala! Mwadhani ati kwa vile Chokoraa miye hushinda majalalani
nikichakura nipate cha kuwalisha vitegemezi vyangu wana wa mama yangu Shida wa
Matatizo wa Taabu wa Maisha magumu mke wa mzee wangu Muhangaikaji wa Mlalahoi
wa Pangupakavu kilembwe wa Mdanyika Mlipakodi, basi siijui tofauti ya adhuhuri
na jioni!? Mwanitania enyi wana na miye humo simo.
Nasema wachilieni mbali uzandiki wenu ashakumu si matusi ila
ikiwa kwenu kuuita uovu kwa jina lake matusi, basi miye salaam nawasalimia.
Ndiyo, nakumbuka sana miaka ile ya kipindi kile cha Yule kitukuu wa Nchumali
Ntoto wa Chilingi mwana wa Chipuputa mlivyokuwa mkiiandama ‘siri kali’ tena kwa
kuivisha koti la chama cha upinde wa zamani, na kudai ati inakataa kuanza
mchakato wa katiba na hivyo kuwahujumu wanyonge. Naapa wanyonge wa kaya hii
wamekosa msemaji na miye humu nitoeni. Ala! Kwani mwadhani sioni jinsi ambayo
kwa Mkwere huyu kukuruhusuni mfanye huo mchakato wenu mlivyowageuza ‘wana wa kaya’
kuwa ngao katika vita yenu ya panzi!?. Nasema msinitanie enyi wana maana miye
si babu japo kusema kweli kwenu nyinyi pia si mjukuu na humu pia nitoeni.
Nauliza maana kuuliza si ujinga, kwani ‘Waishiwa’ ninyi si
‘wana wa kaya’ ati kwa vile tu mko kwenye hilo genge lenu la wahuni wajuao
kuvaa mavazi na tabasamu za kikoloni? Kama na nyie ni wana kaya, inakuwaje
mwagombana na kila mmoja akidai anatetea maslahi ya Wana wa Mdanganyika wa
Mlipakodi? Naapa mwatufanya mazuzu enyi wana na miye humu sitaki katu kuhusika
maana simo, tena simo kabisaaaaa!
Ati! Hivi mwadhani shekeli za baba yetu Mdanganyika wa
Mlipakodi mnapoziswaga kama Ng’ombe waendao machinjioni kwa kisingizio cha
kutuandalia ka tiba kaliko bora bila
kuufahamu vyema ugonjwa wetu, sisi nao ni wajinga tusioifahamu janja yenu!?
Wacheni dharau enyi weledi wenye kwenda mbele ilhali macho yatazama mtokako na
miye humu nahusikaje!? Simo.
Haya, mwabishana na kugombana kila mara ati muwe na siri
ngapi za kuzitunza pasina kujiuliza hizo mlizokuwa nazo zimevujaje hata
kutufikia sisi akina Chokoraa kama mwafahamu kutunza vyema hizo ‘siri zenu
kali?’. Naapa ujinga hauna tafsiri na miye humu nitoeni.
Kwani nyie si ndiyo mliokuwa vinara wa kumnukuu Yule mzee
mwana wa Mzalendo na hapa namsema Mkufunzi wa Mzalendo wa Mdanganyika, ki wapi
sasa kile mlichokuwa mkituaminisha sisi wadharauliwa wenu kwamba “wale” wameasi
misingi iliyotiwa na Mkufunzi na “ninyi” ndiyo manabii pekee mliobaki
kuirejesha kaya yetu kwenye msingi?. Ha ha ha ha ha!!! Nasema penye pongezi zitolewe
na mimi nakupongezeni maana mwauweza vyema mchezo wa ‘si hasa’ isipokuwa izi za
mara hii ni zile za majitaka yasiyofaa kwa kunywewa ama kilimo cha umwagiliaji
kama mjitapavyo na miye humu simo. Ala! Mlipoona misingi ya huyo mkufunzi
mwenyewe inakinzana na tamaa za mioyo yenu, si nilikusikieni baadhi yenu
mkimtusi hadharani kama wana wasio malezi wenye kutukana wazazi? Naapa laana
mmelaaniwa enyi wana na miye humo simo.
Nani kakudanganyeni Chokoraa miye na wadogo zangu ukoo wa
Mdanganyika Mlipakodi ugonjwa wetu ni idadi ya ‘siri’ zenu!? Kwanza hatutaki
hata kuzijua hizo siri zenyewe, ziongezeni ukali hata tusizikaribie kama
mwataka, lakini hakikisheni kaya yetu inabaki moja kama alivyoiwacha mwana wa
Mzalendo na msipotenda hayo, naapa hatutaiwachia historia kuwahukumu bali
tutawahukumuni sisi wenyewe na miye humo
simo tena simo kabisaaaa, ila salaam nawasalimia.
Ni mimi Mdharauliwa wenu, Chokoraa wa Muhangaikaji wa
Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdangayika wa Mlipakodi nawasalimia.
Salaam Waishiwa.
No comments:
Post a Comment