Wednesday, June 27, 2012

Rafiki yangu kipenzi Udadisi Chautundu - 2

Najua! Naam, bado nakumbuka ahadi niliyokuahidi kwamba nitakueleza zaidi kuhusu yule jamaa maarufu wa harufu hapa mjini kwa jina la Maisha Magumu, lakini ngoja kwanza nimalizie kila kisa cha Chokoraa wa Muhaingaikaji wa Mlalaohi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika kufikishwa kwenye kituo kikuu cha walinzi wa ‘muishi miwa’ saaaaana Dola.

 Bila shaka unakumbuka nilipokomea kwenye kukuhadithia tukio zima na jinsi ambavyo nilitandikwa kibuti cha mgongo na kuishia kunyamaza kimya ili kuokoa uhai wangu, lakini nakuapia ndugu yangu bado nigali na hasira kwa kitendo kile japo kadhia nzima imepita sasa. Aala! Yaani kufikishwa tu kituoni tena si mahala pa usalama bali kashfa matusi na vipigo? Naapa humu miye simo. Ati kila anayefikishwa kwenye “sentro” basi ni mhalifu hata kama hajaonana na pilato na hawa walinzi wanaanza kumpa majina kwa kadri watakavyo mara wakuite Mhalifu wa Mkosaji, mara wakuite Kibaka wa Mwizi, mara Jambazi wa Sugu na mengine mengi, naapa kwenye yote hayo hakuna hata jina langu.

 Nilitamani nikuite ndugu yangu Udadisi ili uwaambie hawa jamaa kwamba mimi naitwa Chokoraa wa Mdanganyika lakini nikahofia kukuingiza na wewe kwenye msambwe na kadhia ya kupachikwa majina ya ajabu ajabu huku ukitandikwa kwa kadri watakavyo wanaotaka katika kutaka kwao na humu simo. Basi ndugu yangu, baada ya kuulizwa maswali kadha wa kadha ya kuudhi nikasukumizwa ‘lokapu’ bila hata kujua kosa langu na kama nilivyokuahadithia hapo awali, nikaamua kukaa kimya kwa vile nilijua tu kwamba kesho yake wababe hawa wangenipeleka tu kwa pilato na huko ningesema bila hofu wala mashaka kwa sababu huko hawaruhusiwi kunifanyia ubabe wao huu.

Yaliyonikuta humo ndani hata sitaku kukuhadithia ndugu yangu Udadizi na nakuonya kwa sababu ya jina lako usije ukajaribu kuingia huko kwa ajiri ya kujua kunani maana naapa hakufai. Kesho ilifika hata hivyo, asubuhi na mapema nikaamshwa na kukabidhia tena “kobazi” zangu niziitazo viatu na sehemu ya vikaratasi vyangu vilivyokuwa mfukoni na ambavyo nilinyang’anywa wakati nikitiwa ‘lokapu’, noti yangu ya shekeli kadha wa kadhaa iliyokuwa mpya niliikuta imebadilishwa na moja iliyokuwa chakavu karibu na kuchanika, lakini walau kuzeeka kwa noti hakuondoa thamani ya fedha humu namo simo, nikaitia mfukoni na kupakiwa kwenye gari na watu wengine niliowakuta ‘lokapu’ jana yake.

Kilichonishangaza hadi nakaribia kuanguka na kuzimia si kufika kwa pilato na kugundua jinsi ambavyo wababe hawa wa muishi miwa sana Dola walivyogeuka kuwa wapole na waungwana ghafla, hapana, hilo nililitaraji lakini nilishangazwa na mashtaka niliyosomewa mbele ya Pilato wa Mwamuzi. Nakwambia ilikuwa kama mchezo wa kuigiza, mshitaki akajipanga vizuri na kurekebisha ‘ulimi wa mbwa’ shingoni mwake na kisha akajikohoza kidogo kuweka sauti sawa, kisha kwa sauti yenye mikwaruzo kidogo, na nadhani mikwaruzo hii ni kwa sababu ya kunywa sana mvinyo ila humo namo simo, akasema; “Chokoraa wa Mdanganyika, unashitakiwa mbele ya ‘kilinge’ hiki cha ‘muheshimiwa’ Pilato kwa kosa la Uzembe na Uzururaji, kwamba siku ya juzi mnamo saa tatu na dakika kidogo za usiku ulikutwa ukitenda kosa la Uzembe na Uzururaji kwenye mitaa ya kaya yetu hii kinyume na kifungu cha sheria…..” sikupata hata nafasi ya kumsikiliza hili amalize nikaamua kumkatisha’

 “...Kwanza mimi Jina langu halisi ni Profesa Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika, halafu umenishitaki kwenye ‘kilinge’ hiki kwa makosa ya wadogo zangu wawili yaani Kulwa na Doto maana wamezaliwa mapacha kwa mama yetu Shida wa Matatizo na ndiye aliyemwita Kulwa Uzembe na Doto akamwita Uzururaji, na hivyo nafikiri ama ukawatafute waje wajibu makosa yao ama unipe mimi muda nitawaleta hata nyumbani kwako ukitaka”.

Nakwambia “kilinge” chote kilikaa kimya kwa muda maana nilizungumza kwa jazba na kujihamini sana. Aala! Yaani kwanza ati nashitakiwa kwa makosa ya watu wengine! Huu sasa si uonevu? Yaani Uzembe na Uzururaji wafanye makosa halafu nishitakiwe mimi Chokoraa kwa lipi hasa!? Halafu hayo makosa yenyewe waliyoyafanya mimi hata siyafahamu, nitajibuje sasa kuhusu makosa yao ambayo hata sikuwapo wakati wakiyatenda kama kweli waliyatenda na siyafahamu? Naapa huu sasa ni uonevu. Namshukuru mwenyezi kwamba Pilato naye ni mtoto wa Muungwana na bila shaka unakumbuka jinsi yule mzee naye alivyowalea watoto wake na kuwafunza kuwa na huruma na kutenda haki, baada ya kusikiliza maneno yoote ya mlalamikaji, akalifutilia mbali shitaka lenyewe kwa vile ati aliliona halina msingi. Mimi nasema halikuwa hata na ngazi, madiirisha, milango wala paa.

 Basi bwana, nikaondoka mahakamani na kujaribu kupita dukani mgahawani ili walau nijipatie chochote kitu kwa ajiri ya kula maana njaa ilikuwa ikiniuma, lakini kutahamaki hata ile noti yangu mbovumbovu ilishakwapuliwa haikuwamo mfukoni. Nikaona sina jinsi, nikaamua kujikongoja kidogo kidogo hadi kwa yule rafiki yake na marehemu baba yetu mzee Mkulima ili walau nipate embe nitulize njaa wakati nikiangalia uelekeo na ndipo nikapitia posta na kukuta barua yako.

 Bila shaka sasa umefahamu chanzo cha ugomvi kati yangu na wadogo zangu hawa wawili Uzembe na Uzururaji. Nitakapokuandikia tena nitakueleza ni kwa nini nimekasirikia zaidi Uzembe uliko uzururaji ile kwa sasa nahitaji kwenda hospitali kumtazama mtoto wa Uzembe yule mdogo aitwaye Ulalamishi maana nasikia ni mgonjwa, damu nzito kuliko maji nakwambia.

Ati! Hujui kama Uzembe ana mtoto? Kweli wewe sasa unazeeka vibaya rafiki yangu. Haya nitakuhadithia yahusuyo huyo mtoto kwenye waraka wangu utakaofuata ila kwa sasa nikusalimie tu.

Wasalaamu, nduguyo Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika, nakusalimia.

Saturday, June 9, 2012

 Rafiki yangu kipenzi Udadisi Chautundu


Nimepata barua yako rafiki yangu kipenzi tuliyekua pamoja na kucheza pamoja “kidaso” yaani naona hata aibu kukuita rafiki maana wewe ni ndugu yangu. Umenilaumu kweli kwenye barua yako kwamba ndugu yako nimekusahau na hata jina lako huna hakika kama ningali nikilikumbuka, lakini nakuhakikishia hata ningeamshwa usingizini ghafla na kutakiwa nimtaje rafiki yangu wa karibu, ningekutaja wewe kwanza kaka yangu Udadisi Chautundu. Hata hivyo ni siku nyingi kweli tangu tulipoonana na nimegundua baada ya kusoma barua yako, kwamba kuna mambo mengi uliyoyasahau kuhusu mimi na kuna mengi pia yametokea ambayo hujayajua na inawezekana kama ungekuja mjini kunitafuta basi bila shaka ungenikosa.

 Nakupongeza hata hivyo ulivyoamua kubaki kijijini. Ndiyo, nakupongeza kwa sababu huku mjini kuna watu wana roho mbaya sana kiasi ningekuwa sina tetesi kuhusu wazazi wao, basi nisingesita kukwambia hawa si binadamu na hawakuzaliwa lakini kwa bahati kuna tetesi nyingi kuhusu wazazi wao. Kuna huyu Maisha Magumu. Huyu jamaa unapoingia tu mjini ndiye wa kwanza unayekutana naye na nakwambia huyu jamaa ni maarufu humu mjini kuliko hata ‘mkulu wa kaya’ yetu na kila siku umaarufu wake unaongezeka.

Ha ha ha ha!! Unaona sasa, umeanza kumfananisha huyu jamaa na yule mzee pale kijijini ambaye wewe rafikiri yangu Udadisi ulinifanya kila siku nifikirie maana ya jina lake bila majibu mpaka nilipokuja huku mjini. Si yule mzee alikuwa na koti lefu jeusi na kofia ambayo japo hatukujua aliifua saa ngapi lakini haikuwa ikionekana chafu kila alipoivaa!! Usijifanye umemsahau bwana, mzee Malingumu wa Maliyatabu.

Huyu maisha magumu wala hana uhusiano na hao wawili. Yeye huyu hajulikani vizuri hasa nasaba yake maana wako wanaosema anatoka kwenye ukoo wa yule mzee mwenye kitambi mheshimiwa Kiongozi Mrafi na eti ni mtoto wa mke mkubwa wa huyu mzee Bi Rushwa wa Mlungula.

 Wangine wanasema hapana, Mheshimiwa Kiongozi Mrafi anasaidia tu kumlea huyu mtoto kwa sababu wakati anamuoa mke wake Bi Rishwa wa Mlungula, Bi Rushwa alikuja na huyu mtoto kutoka kwenye ndoa yake ya kwanza kwa yule mzee kiburi sana hapa mjini Bw. Ubadhirifu wa Maliyauma. Vyovyote iwavyo, huyu jamaa amejifunza vyema kwa mama yake maana tabia zake mnh! Nitakueleza siku nyingine, leo nataka tu kujibu barua yako.

 Kwanza nikuhakikishie kwamba sijakusahau ndugu yangu na unapoona sikuandikii hata barua, ni kwa sababu ndugu yako siku hizi naishi kwenye kitongoji kimoja hapa mjini ambacho ni maarufu kwa kuwa na shughuli nyingi wenyewe wanaita “bize”. Basi mwenzako nashinda bize tangu asubihi hadi jioni na kila uzingizi ukinizidia ‘naangusha gari’ hapo hapo ninapokuwa na nikaimka naendeleza libeneke. Lakini pia yule mdogo wangu Uzembe naye anachangia hii hali ya mimi kutokukuandikia barua, lakini usijari kwa sababu sasa hivi mimi na uzembe tuna ugomvi tena mkubwa, basi nadhani kwa muda mrefu kidogo ataniacha peke yangu na hivyo nitapata nafasi ya kukuandikia kila mara.

 Unashangaa tuna ugmvo gani!!? Si ndo hayo sasa ninayokwambia ndugu yangu kwamba siku hizi kuna mambo mengi yamenitokea na wewe huyajui!! Hata! Wala sikulaumu. Najua unanipenda sana na ungependa kujua kila kinachonipata swahiba wako Chokoraa wa Muhangaikaji, lakini mara nyingine huwa nalazimika kukuficha mengine maana najua yatakuumiza hasa kwa vile wewe ulivyo Mdadisi kama jina lako, najua utaumia sana moyo ndiyo maana huwa mengine namezea.

 Haya basi, kwa vile umelazimisha, wacha nikwambia tuna ugomvi gani na Uzembe halafu hayo mengine nitakuandikia waraka ujao. Ilikuwa usiku kamaa saa tatu na nusu hivi na tulikuwa watatu tunatokea kwenye soko la “bize” kurejea ‘gheto’ kwa ajiri ya kupumzisha mbavu zetu. Basi bwana, mara ghafla tukakutana na watumishi wa ‘siri kali’ wenye jukumu la kulinda amani. Mimi soga zilikuwa zimenikolea mwenyewe hata sikuwaona hadi walipokuwa wameshatufikia karibu, kutahamaki, Uzembe na Uzururaji wakatimua mbio na kuniwacha peke yangu. Kwanza sikufahamu kwa nini walikimbia, lakini kama unijuavyo ndugu yako Chokoraa huwa sina hofu na walinzi wa mheshimiwa Dola.

 Nikasimama kwa ujasiri kabisa tena kwa kujiamini si ninajua sina matatizo mimi na mwenyekiti wetu Mheshimiwa Dola! Wapi!! Nakwambia yaani hawa walinzi hata kabla hatujasilimiana nikasikia mmoja ambaye nadhani alikuwa kubwa wao akisema kwa sauti ya ukali na ya kushutumu “Hivi hili si ndiyo linaitwa Chokoraa litoto na yule mzee marehemu Mhangaikaji?”. Akajibiwa “Ndiyo” hata sikujua ni nani aliyejibu maana tayari alishaanza kunitandika makofi huku akinipa amri mfululizo “kaa chini kachini…mikono juu.. una nini mfukoni we Chokoraaa?... huna majani mfukoni kweli wewe….?”.

Sikujua hata nijibu swali lipi kwanza na sikujua hata kosa langu, mara nikawasikia wakizungumza maneno fulani kwenye vilongalonga vyao na lugha yenyewe hata sikuifahamu ila nahisi kitakuwa ni kigagagigikoko maana sikuambulia hata sentensi moja, mara gari hilo likaja limejisheheneza walinzi wengine na hata mmoja wao akiwa amebeba ‘manati ya ndhungu’. Niliogopa nilipoiona hiyo manati wewe!!! Asikudanganye mtu ndugu yangu, manati ya ndhungu inatisha ikiwa kwenye mikono ya watu wenye hasira kama hawa walinzi wa dola. Basi bwana, nikapakiwa kwenye gari tena kwa kusukumizwa kama mzigo hadi kwenye kituo kikuu cha hawa walinzi, hapa napo nikapokelewa na maneno kadhaa ya kejeli “Mmelitoa wapi hili Chokoraa!!?” mmoja wao akauliza huku akinikwida na kunizungusha nyuma ya meza kuuubwa ajabu! Mwingine akadakia, “kwani ni Chokoraa au Jambazi kabisa hili?”.

Ala! Sasa hasira zangu zikanipanda na povu likaanza kunitoka mdomoni. Yaani wananifananisha na yule adui yangu mkubwa ambaye ndiye aliyemuua baba yangu marehemu Muhangaikaji? Nimekuwa nikimtafuta huyu jamaa na hata walinzi wa Dola waliniahidi kwamba wangemtia mbaroni sasa ni mwaka sijui wa ngapi hajapatikana na nasikia anaishi mjini humu humu tena rafiki zake wengine wanajulikana na ati ndiyo sababu ameshindikana kukamatika, leo hawa wananifananisha naye! Haiwezekani.

Nikafumbua kinywa hivyo hivyo na mapovu mdomoni. “Mimi siyo jambazi, mimi ni Chokoraa wa Muhangaikaji. Hata mimi namtafuta huyu Jambazi kwa sababu alimuua baba yangu miaka kadhaa iliyopita…” hata sikumaliza, sori ya kiatu ikatua mgongoni na kunituliza chini, nikaona ili kuokoa uhai wangu bora nikae kimya hadi nitakapofika kuonana na liwali kesho maana hawa jamaa hata hawatakki kunisikiliza. Itaendelea