Najua! Naam, bado nakumbuka ahadi niliyokuahidi kwamba nitakueleza zaidi kuhusu yule jamaa maarufu wa harufu hapa mjini kwa jina la Maisha Magumu, lakini ngoja kwanza nimalizie kila kisa cha Chokoraa wa Muhaingaikaji wa Mlalaohi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika kufikishwa kwenye kituo kikuu cha walinzi wa ‘muishi miwa’ saaaaana Dola.
Bila shaka unakumbuka nilipokomea kwenye kukuhadithia tukio zima na jinsi ambavyo nilitandikwa kibuti cha mgongo na kuishia kunyamaza kimya ili kuokoa uhai wangu, lakini nakuapia ndugu yangu bado nigali na hasira kwa kitendo kile japo kadhia nzima imepita sasa. Aala! Yaani kufikishwa tu kituoni tena si mahala pa usalama bali kashfa matusi na vipigo? Naapa humu miye simo. Ati kila anayefikishwa kwenye “sentro” basi ni mhalifu hata kama hajaonana na pilato na hawa walinzi wanaanza kumpa majina kwa kadri watakavyo mara wakuite Mhalifu wa Mkosaji, mara wakuite Kibaka wa Mwizi, mara Jambazi wa Sugu na mengine mengi, naapa kwenye yote hayo hakuna hata jina langu.
Nilitamani nikuite ndugu yangu Udadisi ili uwaambie hawa jamaa kwamba mimi naitwa Chokoraa wa Mdanganyika lakini nikahofia kukuingiza na wewe kwenye msambwe na kadhia ya kupachikwa majina ya ajabu ajabu huku ukitandikwa kwa kadri watakavyo wanaotaka katika kutaka kwao na humu simo.
Basi ndugu yangu, baada ya kuulizwa maswali kadha wa kadha ya kuudhi nikasukumizwa ‘lokapu’ bila hata kujua kosa langu na kama nilivyokuahadithia hapo awali, nikaamua kukaa kimya kwa vile nilijua tu kwamba kesho yake wababe hawa wangenipeleka tu kwa pilato na huko ningesema bila hofu wala mashaka kwa sababu huko hawaruhusiwi kunifanyia ubabe wao huu.
Yaliyonikuta humo ndani hata sitaku kukuhadithia ndugu yangu Udadizi na nakuonya kwa sababu ya jina lako usije ukajaribu kuingia huko kwa ajiri ya kujua kunani maana naapa hakufai. Kesho ilifika hata hivyo, asubuhi na mapema nikaamshwa na kukabidhia tena “kobazi” zangu niziitazo viatu na sehemu ya vikaratasi vyangu vilivyokuwa mfukoni na ambavyo nilinyang’anywa wakati nikitiwa ‘lokapu’, noti yangu ya shekeli kadha wa kadhaa iliyokuwa mpya niliikuta imebadilishwa na moja iliyokuwa chakavu karibu na kuchanika, lakini walau kuzeeka kwa noti hakuondoa thamani ya fedha humu namo simo, nikaitia mfukoni na kupakiwa kwenye gari na watu wengine niliowakuta ‘lokapu’ jana yake.
Kilichonishangaza hadi nakaribia kuanguka na kuzimia si kufika kwa pilato na kugundua jinsi ambavyo wababe hawa wa muishi miwa sana Dola walivyogeuka kuwa wapole na waungwana ghafla, hapana, hilo nililitaraji lakini nilishangazwa na mashtaka niliyosomewa mbele ya Pilato wa Mwamuzi.
Nakwambia ilikuwa kama mchezo wa kuigiza, mshitaki akajipanga vizuri na kurekebisha ‘ulimi wa mbwa’ shingoni mwake na kisha akajikohoza kidogo kuweka sauti sawa, kisha kwa sauti yenye mikwaruzo kidogo, na nadhani mikwaruzo hii ni kwa sababu ya kunywa sana mvinyo ila humo namo simo, akasema;
“Chokoraa wa Mdanganyika, unashitakiwa mbele ya ‘kilinge’ hiki cha ‘muheshimiwa’ Pilato kwa kosa la Uzembe na Uzururaji, kwamba siku ya juzi mnamo saa tatu na dakika kidogo za usiku ulikutwa ukitenda kosa la Uzembe na Uzururaji kwenye mitaa ya kaya yetu hii kinyume na kifungu cha sheria…..” sikupata hata nafasi ya kumsikiliza hili amalize nikaamua kumkatisha’
“...Kwanza mimi Jina langu halisi ni Profesa Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika, halafu umenishitaki kwenye ‘kilinge’ hiki kwa makosa ya wadogo zangu wawili yaani Kulwa na Doto maana wamezaliwa mapacha kwa mama yetu Shida wa Matatizo na ndiye aliyemwita Kulwa Uzembe na Doto akamwita Uzururaji, na hivyo nafikiri ama ukawatafute waje wajibu makosa yao ama unipe mimi muda nitawaleta hata nyumbani kwako ukitaka”.
Nakwambia “kilinge” chote kilikaa kimya kwa muda maana nilizungumza kwa jazba na kujihamini sana. Aala! Yaani kwanza ati nashitakiwa kwa makosa ya watu wengine! Huu sasa si uonevu? Yaani Uzembe na Uzururaji wafanye makosa halafu nishitakiwe mimi Chokoraa kwa lipi hasa!? Halafu hayo makosa yenyewe waliyoyafanya mimi hata siyafahamu, nitajibuje sasa kuhusu makosa yao ambayo hata sikuwapo wakati wakiyatenda kama kweli waliyatenda na siyafahamu? Naapa huu sasa ni uonevu.
Namshukuru mwenyezi kwamba Pilato naye ni mtoto wa Muungwana na bila shaka unakumbuka jinsi yule mzee naye alivyowalea watoto wake na kuwafunza kuwa na huruma na kutenda haki, baada ya kusikiliza maneno yoote ya mlalamikaji, akalifutilia mbali shitaka lenyewe kwa vile ati aliliona halina msingi. Mimi nasema halikuwa hata na ngazi, madiirisha, milango wala paa.
Basi bwana, nikaondoka mahakamani na kujaribu kupita dukani mgahawani ili walau nijipatie chochote kitu kwa ajiri ya kula maana njaa ilikuwa ikiniuma, lakini kutahamaki hata ile noti yangu mbovumbovu ilishakwapuliwa haikuwamo mfukoni. Nikaona sina jinsi, nikaamua kujikongoja kidogo kidogo hadi kwa yule rafiki yake na marehemu baba yetu mzee Mkulima ili walau nipate embe nitulize njaa wakati nikiangalia uelekeo na ndipo nikapitia posta na kukuta barua yako.
Bila shaka sasa umefahamu chanzo cha ugomvi kati yangu na wadogo zangu hawa wawili Uzembe na Uzururaji. Nitakapokuandikia tena nitakueleza ni kwa nini nimekasirikia zaidi Uzembe uliko uzururaji ile kwa sasa nahitaji kwenda hospitali kumtazama mtoto wa Uzembe yule mdogo aitwaye Ulalamishi maana nasikia ni mgonjwa, damu nzito kuliko maji nakwambia.
Ati! Hujui kama Uzembe ana mtoto? Kweli wewe sasa unazeeka vibaya rafiki yangu. Haya nitakuhadithia yahusuyo huyo mtoto kwenye waraka wangu utakaofuata ila kwa sasa nikusalimie tu.
Wasalaamu, nduguyo Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika, nakusalimia.
No comments:
Post a Comment