Kwanza ni "Usafiri" wetu. Hapa kwetu Mafia hatuna "Teksi" na wala huo upuuzi wenu wa kutumia magari hata kwa safari fupi kisa mwaonyesha ufahari wa kuwa na mafedha kedekede sisi hatumo na humu Chokoraa nilikataa kuhusika. Kuna njia mbili tu za kuingia kisiwa hiki chenye utajiri wa mali na utu na mara unapofika ama kwenye bandari yetu kongwe isiyoendelezwa bado ukitumia usaifiri wa "boti" kutokea Nyamisati au wale "waishiwa" msiochoka kuishiwa mkijifanya kutumia "ulozi wa ndhungu" kwa kupanda 'ungo' mchana kweupeeeee! Na humo simo, hata hivyo usaifiri wako wa kuzunguka mjini humu ni pikipiki iwe ya matairi mawili almaarufu "Bodaboda" ama matairi matatu almaarufu "Bajaji". Teksi zenu tupa kule!!! Simo nasema.
Halafu! Huku kwetu ule uchafu wenu muutiao barabarani mkiifanya nyeusi tiii kama mkaa ati wenyewe mwaita lami huku sisi upuuzi huo hatuna hata mmoja. Huu mji wa kitalii bwana lazima uwe "nechuro". Ha ha ha ha ha ha!!! Sihusiki miye humu naapa.
Halafu nani kasema ati wanawake wa Pwani hawajui kutafuta pesa ila akina "Manka" peke yao!!!? Nyooo!! Simo. Hapa kwetu sokoni kwa lugha ya 'Ami' yangu wa kule Mchambawima paitwa "Malikiti" akina mama wanauza kitoweo. Yaani akina baba wavua, na akina mama wauza na wote watia kipato ndani ya nyumba sasa hilo la haki sawa mwalikataa kwanini!!!? Simo humu miye.
"Si hasa" za Kaya yetu nazo zatuhusu na sisi twahusika. Hapa ni kikao cha kamati za vijiji vya Banja na Jojo kilichofanyika shule ya msingi Banja ambapo wanavijiji hawa walikutana na wataalamu wa mazingira na hapa mmoja wa wanakamati akihoji swali na kutoa maoni yake. Ha ha ha ha ha!! Nisifurahi kwanini Chokoraa miye.
Kwenye kikao hiki, ndugu yenu Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika nilikaribishwa niketi na mimi pamoja na wakuu na sikufungua kinywa kunena bali kusikiza yale yaliyosemwa na wana kaya maana simo.
Huyu si mgonjwa jamani kwamba anakandwa mkono umevunjika ama kakutwa na madhila. La hasha! Anapambwa mtoto wa kike kabla ya harusi na kama huyajui haya basi hujafika Pwani weye na mi humo simo, tena simo kabisaaaaaaaa.
Haya tena, kishapendeza mtoto wa kike asubiriwa somo hapa mambo yaanze. Ha ha ha ha ha ha! Tembea ulishe macho yako wewe! Kila siku kumshangaa Chokoraa, ohoo! mara Chokoraa ana maneno mengi! Si nimeona mengi!!!? Simo humu miye.
Somooooooooo!!!! Yuko wapi somoye harusi jamani aje hapa tuhangaike naye, nasema aje hapaa, nasema aje hapaa, nasema aje hapaaa!!!!!!!! Nahusika humu kwani miye!? Simo.
Haya, kwa leo nakomea hapa. Ni mimi ndugu yenu Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika, nawasiliamia.
No comments:
Post a Comment