Nasema jina baya umuua mwenye nalo chambilecho wale
waliokuwa kabla yetu na humu nasema simo. Kwenye hili la wazee wetu kukupa jina
la marehemu babu yake na babu mzaa baba marehemu Mdanganyika, walikutia
matatizoni we mwana na humu naapa unitoe.
Kwani mi si nilikuwa nimekataa kwamba usipewe jina hilo
lakini Yule shangazi yetu mke wa baba yetu mdogo Mstahiki wa Mheshimiwa
akalazimisha na mwisho ukapewa jina ambalo leo lakusumbua ewe Mdanganyika
Mlipakodi na humu mi simo nasema.
Ebu kwanza nikupe pole maana siku hizi wanao wauana kama
wanyama tu bila hata kujali na humu nasema mapema kabisa ili msijesema mi
sikusema maana simo tena simo kabisaaa.
Nasema wakati walipotutoza kodi na kununua ‘manati za ndhungu’ nani alikudanganya
kwamba zilikuwa kwa ajiri ya kuwindia ndege!? Ndege huwindwa kwa manati za
asili na si manati za ndhungu zenye nguvu na mshindo wa radi na humu mi
nitoeni. Ati! Msikie huyu naye! Kwamba zilinunuliwa kwa ajiri ya kulinda
usalama wa kaya yetu hii!? Ha ha ha ha ha ha ha!! Nicheke miye kitukuu wa Pangupakavu
maana nchi haikumaanisha akina nyie mzee Pangupakavu na wenzio bali kundi la
akina kaka mkubwa Mheshimiwa na vitegemezi vyao na ndiposa na ninyi mnapotishia
usalama wa maslahi ya vitegemezi vyao basi wakudungulieni mbali na humu mi nisihusishwe.
Kwani si mmekuwa mkidunguliwa kila mwaka na hakuna hatua
hata za miguu zinazochukuliwa dhidi ya wale waliopewa dhamana ya kushika manati
kwa niaba yenu na kisha kukudungueni!?
Nasema watu wanatumia vibaya vitu vilivyonunuliwa kwa fedha
ya wazazi wako Bi Mwananchi na mzee Mlipakodi na sasa wamevigeuza vyombo hivyo
kuwa zana za kukuangamizeni na humu simo.
Nani kasema nahusika miye humu kwenye hili! Nasema wakati ‘wadunguaji’
hawa wanaendelea kulipwa mishahara ya kuwadungueni kwa fedha za baba yangu mzee
Mdanganyika Mlipakodi, wana wa kaya ya wadanganyika sasa wako mashakani si
kutoka kwa wale waliotarajiwa maana mvua ya msimu haibomoi nyumba ya mwenye
akili kwa vile huchukua taadhari, lakini unafanyaje ikiwa dawa inageuka sumu na
humu mi nitoeni.
Hivi! Mbona mwaishi kama wasi kwao ilhali ninyi ni
Wadanganyika na babu wa babu zenu walimwaga damu na hata kuutoa uhai si kwa
ajiri yao bali kwa ajiri ya vizazi vyao ambavyo ndiyo mimi na wewe na sasa
mwachinjana wenyewe kwa wenyewe kwa faida ya nani? Naapa ni heri muumba
alivyokataza wafu kufufuka na kuona yawapatayo watoto wao baada yao maana
sidhani Mkwawa, Kinjekitile na wenzao wengine wangekubali haya muyafanyao wacha
huyu aliyeondoka juzi juzi tu Mzalendo Mwalimu wa Mkufunzi na humu mi sihusiki.
Haya, tuwachilie mbali hayo ya wale waliokwenda maana baadhi
yenu husema hao huwa wamepumzika na kwa miaka mingi nilikataa lakini sasa
navutwa kukubali. Ndiyo. Uzee una mambo we mwana nisikize Chokoraa miye
nikupashe leo na unisikize kwa makini. Shida ya uzee si kutojua njia na mwisho
wa njia yenyewe isipokuwa nguvu za kuipita na msukosuko wa maisha ni kuona wale
uliowapa nguvu na kuwakabidhi kijiti wakiiacha njia na kutumbukia maporini kwa
vile huko huwezi kuwaona wafanyao na hata ukisema wanakucheka kwa viule huwezi
kuwakimbiza na hapa namtumia salamu za pole mzee wa Uongo na Uficho kwa sababu kizazi hiki wazi twaficha na fichu
twasema na humu mnitoe. Ala! Si aliwekeza juhudi ili kuifanya Danganyika ya
wadanganyika walipa kodi isiitwe bongo ati kwa vile watu walikuwa wakiishi kwa
kutegemea bongo sana kiasi cha kuifanya
kaya yetu kuwa pango la wanyang’anyi? Najiuliza, naye anasikitika na mimi
ninaposikitika kuona kwamba sasa hii
ndiyo Bongo halisi na hivyo kumbe alishindwa vita vyake, ama nay eye alijigeuza
msanii kwenye jengo la sanaa kuniigizia ili niamini maigizo nisione uhalisia?
Naapa mi humu najitoa mapema maana simo.
Ati washangaa! Washangaa nini we mwana ikiwa hadi dawa,
narudia tena, dawa yaani ile mizizi niliyofundwa na babu yangu Pangupakavu
kwamba ingeweza kutiba homa na tetekuwanga nayo mwaitia sumu almuradi
mtajipatia chochote kitu kwa kufanya hivyo? Ha ha ha ha ha ha ha!!! Naapa wana
wa kaya hii mmekosa aibu na hofu ya muumba na humu simo.
Ati mwatengeneza dawa bandia na kuzitia sokon, matabibu
mwawa wauaji halafu na nyie mnaketi kwenye viti vyenu vireefu mkigonganisha
bilauri na kuwalaumu washika manati kwa kuuwa watu kila siku huku mkisahau
ninyi mmeua wangapi! Naapa Nyani kweli huliona kundu la mwenzie na humu mi
nitoeni.
Ndiposa Chokoraa nikasema jina baya humuua mwenye nalo maana Mdanyika wewe kweli umedanganyika. Umedanganyika kwamba ati ni kwa ajiri yako watu walinunua manati za ndhungu na kusema kweli zilinunuliwa kwa ajiri yako lakini ulidanganyika kudhani ni kwa ajiri ya kukulinda. Ha ha ha ha ha ha ha!!! Nicheke miye. Ulindwe we mwana wa Mlalahoi wa Kabwela una nini!? Zilinunuliwa kwa ajiri yako kwa vile walijua kwamba utaanza muda si mrefu kuuliza juu ya jinsi wanavyotumia kodi yako uwalipayo kila siku kwa kuendelea kuwa Mdanganyika na hivyo walikununulia wewe manati ya ndhungu. Walalama nini sasa zinapotekeleza lengo la kununuliwa kwake ilhali ulijua wamezinunua kwa ajiri yako? Simo.
Nasema ulidanganyika ulipodhani kwamba wao walio wazima wanajipanga kukutengenezea dawa wewe uliye mgonjwa ili urudie kuwa mzima na ukasahau kwamba kipande cha mkate ni kidogo na humu simo. Ona sasa wanalisha sumu kwa jina la dawa naapa kaya hii imekaa kichwa chini miguu juu. Ati! Matabibu wanapokuwa wauaji na walinzi wanapokuwa wadunguaji nani alaumiwe. Narudi zangu jalalani nisijechelewa vipande vya mkate na mabaki ya siagi ila humu mi simoe tena simo kabisaaaa, sihusiki.
Wasalaam, ni mimi nduguyo Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi
wa Pangupakavu wa Kabwelwa Mdanganyika, nakusalimia.