Najua, najua kwamba hatutakubaliana wote lakini kwenye hili
ni lazima ukweli usemwe na kama hakuna anayeusema ukweli basi tunabaki gizani
na si rahisi kusogea na huenda hiki ndicho baadhi yenu mnachotaka, kwamba
tuendelee kuwa gizani na ninyi mliopaswa kumulika mishumaa mwaiwasha huku
mmeifunika vitambaa vyeusi.
Tuwe wakweli, Tanzania inatafunwa na ugonjwa mbaya kuliko
yote na huu ni ugonjwa wa ‘Udini’ na sina shaka kusema haya ni matokeo ya matendo na hata maneno ya viongozi wa dini.
Nakumbuka kipindi fulani Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
aliwataka viongozi wa dini wasiilaumu serikali kwa kuwapo kwa tuhuma nyingi za
rushwa ndani ya taasisi zake kwa vile wala rushwa hao ni waumini wa viongozi wa
dini na wako waliombeza, lakini nasema kwa hili Mheshimiwa Mizengo Pinda
alisema ukweli isipokuwa tu kwa sababu wengi wa watanzania sasa hivi tunapenda
kusikia maneno laini na matumaini matupu kuliko ukweli uumizao, basi alibezwa.
Kwani ni kipi alichosema Waziri Pinda wakati huo ambacho
hakikuwa na ukweli wowote?. Ebu tutafakari pamoja. Ni ukweli ulio wazi kwamba
dini inayo athari kubwa ya jinsi ambavyo mtu anaishi na kuishi kunajumuisha
kutekeleza majukumu yake ya kila siku akitumia elimu na vipawa vya kimaumbile
aliyojaaliwa na mwenyezi Mungu. Hili si jambo la Tanzania peke yake, ni jambo
linalogusa hata mataifa makubwa duniani kama Marekani taifa lenye kujionyesha kuwa kinara wa
demokrasia duniani.
Kwenye gazeti la Los Angels Times la huko Marekani la tarehe
16/03/2007, msemaji wa mgombea urais wa wakati huo na aliye sasa Rais wa taifa hilo Barak Obama,
Bw. Robert Gibbs katika waraka wake kwa waandishi wa habari, aliwaambia wapiga
kura kwa kuwahakikishia kwamba Barak Obama alikuwa Mkristo na kwamba hajawahi
kuwa Muislamu. Alisema katika waraka huo kwamba “Obama siyo na wala hajawahi
kuwa Muislamu” na walio wengi wakajiuliza kama ambavyo wanaendelea kujiuliza
leo kwamba je, kama Obama angekuwa muislamu asingechaguliwa kuwa rais?. Je,
ikiwa leo rais Obama atatangaza kubadili dini yake na kuwa muislamu basi
ataondolewa madarakani? Na kadhalika na kadhalika. Jambo moja ni wazi hata
hivyo, kwamba dini inao mchango mkubwa kwenye maisha ya kisiasa ya wanadamu na
hatuwezi kuitenga dini na siasa.
Binafsi naona dini na siasa kufanana kwenye maeneo mengi ikiwamo
ukweli kwamba viwili hivi vinaendeshwa kwa misingi ya imani. Ndiyo. Mfuasi wa
chama chochote cha siasa anaamini kwamba sera za chama chake na uongozi mzuri
wa chama hicho ndiyo msingi wa maendeleo yake na ndiyo maana anakipigia kura kimtawale. Vivyo
muumini wa dini yoyote anaamini kwamba dini yake ndiyo bora kuliko ile ya
mwenzake na ndiyo maana anayaacha mafundisho ya dini hiyo kutawala matendo na
hata maneno yake.
Kwa hiyo ni sahihi kusema dini ni siasa kama siasa ilivyo
dini. Ni ukweli wa kihistoria kwamba kumekuwapo na tawala nyingi duniani kwa
karne na miongo mingi zenye kujiendesha kwa kufuata mfumo wa kidini yaani
‘serikali za kitheokrasia’. Katika serikali hizi, huaminika kwamba Mungu (kwa
tafsiri ya watu ama jamii inayoongozwa na mfumo huu) ndiye mwenye kuongoza
taifa na kwamba kiongozi mkuu wa nchi ni mteule mwenye mahusiano ya hali ya juu
na ya kipekee na mungu huyo na hata maelekezo yake kuhusu jinsi ya kutatua
migogoro na matataizo ya jamii yake huaminika kuwa yanatoka kwa Mungu. Mifano iko
mingi lakini mfano wa jinsi Mussa alivyowaongoza waisraeli kutoka mikononi mwa
Farao ama Firauni kama ajulikanavyo na baadhi ya misahafu, unaweza kutuonyesha
vyema jinsi dini ilivyo na siasa ndani yake.
Lakini pia Siasa na Dini vyote hufanana kwa kuzingatia
kwamba vyote huishi na kufaulu kwa kutumia nguvu ya ushawishi. Neno siasa
linatafsiriwa na msomi wa kiarabu iliyo lugha yenye kuchagia maneno mengi
kwenye Kiswahili kuliko lugha nyingine yoyote, Shaikh 'Alee Hassan Al-Halabee
ya kwamba “ Ni kuhami na linda masuala ya umma”, neno Politics ambalo hutumiwa
kumaanisha siasa kwa kiingereza linatafsiriwa kuwa ni ‘uwezo wa kuhamasisha
jamii ya watu ama mtu mmoja katika kufikia malengo ya kiutawala”. Hivyo basi ni
sahihi kusema kwamba dini na siasa haviwezi kutenganishwa na maisha ya kila
siku ya mwanadamu kwa vile tunafanya vyote viwili kwa wakati mmoja tunapotenda
majukumu yetu ya kila siku.
Hayo hapo juu hata hivyo hayafanyi hoja ya waziri mkuu
kuwataka viongozi wa dini wajitafakari wenyewe badala ya kuilaumu serikali kuwa
na mashiko sana ila mantiki yake kwamba wala rushwa ni waumini wa dini hizi
ndiyo hoja ya msingi.
Viongozi wa dini ndiyo watu wenye dhamana ya kuamua muelekeo
wa kidini wa watu wetu, na si hilo tu lakini kama alivyowahi pia kusema Rais wa
awamu ya tatu Mh. Benjamini Mkapa kwamba maneno ya viongozi wa dini yanaaminika
kuwa maneno ya Mungu miongoni mwa waumini, ni kweli kwamba sisi wengine kwa
ujumla wetu tumewaachia viongozi wa dini watuongoze kuhusu masuala mazima ya
kidini na bila kuwaingilia na hivyo ikiwa dini leo inageuka kuwa tatizo zito
kiasi cha kutishia utaifa wetu, basi wa kulaumiwa wakiwa wa kwanza ni viongozi
wa dini.
Ndiyo, tunawalaumu wanausalama kunapokuwapo na uzagaaji wa
siraha za moto na kuhatarisha usalama wa watu na hata usalama wa taifa si kwa
kuwaonea bali kwa sababu kwa mwanachi wa kawaida hapa Tanzania hawezi
kutofautisha hata milio ya risasi tu kutoka bunduki moja hadi nyingine kwa vile
hiyo ni tasinia iliyo na wenye taaluma,
ujuzi na ufahamu nayo ambayo jamii nzima imewaamini na kuwapa jukumu siyo tu la
kumiliki na kutumia siraha hizo kwa niaba yetu, bali kuhakikisha usalama wa
siraha zenyewe, sasa kwanini mnataka tusiwalaumu wale waliopewa jukumu la
kusimamia na kuhakiki usahihi wa mafundisho yatolewayo kwetu wakati jamii inapohitaji miongozo ya kiimani?.
Kuwaweka kando viongozi wa dini na kuilaumu serikali kwenye
suala la udini ni sawa na kuibiwa mali kwenye ghala na kumweka kando mtunza
ghala na kumlaumu muhasibu ati kwa vile tu majukumu yao yanaingiliana bila
kuzingatia kwamba mtunza ghala alikabidhiwa majukumu maalumu kutunza ghala hilo
hata kama muhasibu anahusika kusimamia matumizi ya rasilimali za shirika.
Sisemi serikali haina sehemu katika madhila haya
yanayoikumba jamii yetu leo, lakini nasema ikiwa kwa namna yoyote wanasiasa
wametumia dini kujipatia matakwa yao ya kisiasa na hivyo kuyumbisha mfumo mzima
wa jamii kwa kutojulikana mipaka kati ya dini na siasa, si kosa la wanasiasa
bali la wanazuoni wetu ambao kwa makusudi ama kwa uzembe wameshindwa kusimamia
misingi ya kiimani kuhusu uwajibikaji binafsi wa waumini wao kwa Mungu wao,
waumini ambao ndiyo wanasiasa wanaolaumiwa.
Nasema ikiwa kiongozi anawalaumu wale anaowaongoza kwa
kushindwa kutekeleza yale waliyopaswa kuyatekeleza, kiongozi huyu ameshindwa
kuongoza hana budi kukaa kando awaanchie wengine waongoze.
Yanayojitokeza leo kwenye majumba ya ibaada ni matokeo ya
viongozi wa dini kujichanganya wenyewe na kushindwa kusimamia misingi ya
utakatifu na heshima kwa Mungu waliyepaswa kumtumikia. Nani haoni vile ambavyo
leo mimbari zimegeuka majukwaa ya kisiasa tena yakitumiwa na wanasiasa ambao
wana tuhuma nzito kwenye jamii zao wakiwa wamejichafua kwenye ulingo wa siasa
na kukimbilia kujiosha kwenye majumba ya dini!?
Najua wako ambao mtasema si kazi ya viongozi wa dini
kuwatenga wakosefu bali kuwapokea na kuwasaidia lakini nasema Mungu mwenyewe
hatoi msamaha kwa wasiotubu na hata manabii na mitume walilifundisha hili na
hakuna kati yao aliyesema unaweza kumsamehe mkosefu kimya kimya tu bali
“akitubu msamehe” na mimi najiuliza hivi watuhumiwa hawa ambao wamekataa hata kujibu tuhuma zao (japo kusema
kweli si tuhuma za kisheria bali za kijamii) na kujisafisha mbele ya jamii na
badala yake kukimbilia mbele ya viongozi wa dini ili wawasafishe, watazuiwa na
nini kesho wapatapo nafasi kuvurunda tena na kuwataka muwasafishe kama mwanzo?.
Niseme kama alivyowahi kusema Yesu “…chumvi ikipoteza radha
yake yafaa nini….” Na mimi najiuliza viongozi wa dini wanaofanya michezo hii
wanajua madhara ya kukumbatia watu wenye tuhuma bila kuwawajibisha ma madhara
yake?. Najiuliza itakuwaje ama mtamlaumu nani ikiwa tutafika mahala ambapo watu
hasa vijana tutakataa kuja kwenye majumba yenu ya ibada kwa vile kumbe huko
nako ni kunajisi kama ilivyo kwenye siasa na badala yake kuamua kubaki nje kwa
vile ndani na nje kote kunanyesha na hivyo ni bora kulowa huku ukitembea maana
mwisho utakuwa umesogea hatua kuliko kuloa ukiwa mahala pamoja?.
Viongozi hawa wa dini ndiyo wanaoshadidia mafundisho yenye
kusababisha mitafaruku mikubwa kwenye jamii yetu na si ajabu kwamba leo vijana
wa kitanzania ni wazalendo zaidi kwa dini zao kuliko walivyo wazalendo kwa
jamii yao. Si ajabu vijana wengi wa kitanzania wanaamini jamii yao ni wale
wenye imani ya kidini sawa na wao na wale wenye imani tofauti si sehemu ya
jamii yao na hivyo hakuna ndani ya akili za vijana hawa ile iliyojulikana
miongoni mwetu kwa miaka mingi kama jamii ya Kitanzania.
Pita kwenye mahubiri na mihadhara mingi utawasikia viongozi
wa dini wakiwahubiri vijana wao juu ya umuhimu wa kujitazama kwa “wao” kwa
maana ya dini zao badala ya kutumia mwanya wa kuwafundisha imani ya dini ili
kuitumia kutatua matatizo yao na jamii zao. Yako mabaraza mengi ya kidini nchi
hii na yote yamengukia kwenye mkumbo ule ule. Si mabara ya maaskofu wala masheihk
yanayochukua hatua kuwakemea wajinga wachache, natumia neno wajinga na si
wapumbavu, wanaojaribu kueneza chuki miongoni mwetu na ndiyo maana kukawa na
wachungaji wenye kutumia vituo vyao vya redio kutukana na kupandisha jazba
waumini wa dini nyingine hadi serikali ilipoamua kuvifungia. Nauliza wakati
wote wahubiri hawa wanahubiri sumu hizi ndani ya jamii yetu, mabaraza ya kidini
ya dini hizi yalikuwa yakifanya kazi gani!? Kwani jukumu la mabaraza haya ni
nini kama si pamoja na kuhakikisha kwamba mafunzo ya dini hizi hayapotoshwi?.
Kwani wale waliojiita masheikh waliokuwa wakiendesha
mihadhara yenye kuchochea chuki na kusambaza CD za chuki hizo walikuwa kwa
namna yoyote hawawajibiki kwa mabaraza ya kidini? Mbona viongozi wa mabaraza
hayo wasikemee upuuzi huo hadi damu zimemwagika ndipo ati polisi inawatafuta na
wao kukimbilia nje ya nchi?. Najiuliza je, viongozi wa kidini wanafurahishwa
na mafundisho haya yenye kuibomoa jamii
yetu? Kwa faida ya nani!?
Ni unafiki. Ni unafiki leo viongozi wa dini kusimama na bila
aibu kuilaumu serikali kwamba ndiyo inayochochea udini wakati dini ni tasnia
pekee ambayo kwa miaka mingi haikuingiliwa na serikali ndani ya nchi hii hadi
pale wenyewe wanaposhindwa kuendesha mambo yao na kusababisha vurugu. Ni ajabu
kwamba hata inapofikia hapo bado serikali inapoingilia utawasikia viongozi hawa
hawa wakilalamika kwamba serikali inaingilia uhuru wa kuabudu wakati
wameshindwa kuutumia uhuru na kuufanya kuwa uendawazimu. Maana uhuru usio
mipaka ni uendawazimu.
Wakati viongozi wa dini wanapojitafutia umaarufu kwenye
vyombo vya habari kwa kuzungumzia masuala yasiyowahusu kana kwamba wao ndiyo
wasemaji wa taasisi za umma ama kujitokeza kwenye vyombo vya habari kuzitaka
taasisi za umma kujibu hoja zao na bado wakaendelea kudai wasiingiliwe uhuru
wao wa kuabudu, binafsi ninaona kama wameiondoa ibada kwenye milango ya
mahekalu na masinagogi na kuipeleka kwenye malango ya ikulu jambo ambalo ni
kinyume na katiba na ni kuingilia uhuru wa taasisi nyingine.
Wako ambao hadi leo wanalalamikia kauli za kiongozi mmoja wa
dini ya kikristo kufuatia vurugu za Mwembechai mnamo February 13, 1998 ambapo
baada ya vurugu hizo, kiongozi mmoja wa dini alijitokeza mbele ya waandishi wa
habari akisema “jeshi la polisi halikutumia nguvu kubwa bila sababu na kwamba
ilikuwa sahihi kutumia siraha za moto kwa sababu raia(akiwataja kwa dini yao)
nao walikuwa na mawe na kwamba mawe nayo yanaweza kuua….”. Ni kauli za jinsi
hii na zifanazo ambazo zimechangia kuchochea migogoro ya kidini kufikia hapa
ilipo leo kwa sababu kiongozi huyu hakupaswa kwa namna yoyote kusema aliyosema
hata kama yeye aliamini ni sahihi na hata kama kwa mujibu wa katiba anao uhuru
wa kutoa maoni yake, lakini alipaswa kuzingatia nafasi yake na kutafakari
madhara ya yeye kutoa maoni hayo maana hekima ni uwezo wa kusema neno sahihi,
mahala sahihi kwa wakati sahihi na kwa namna sahihi. Ikiwa utanisalimu salamu
ya asubuhi wakati wa machweo, utakuwa umefanya kitu sahihi kwamba umenisalimia,
ila utakuwa umekosa hekima kwa kunisalimu salamu ya asubuhi wakati wa jioni.
Ni wakati sasa viongozi wa dini wajichunguze na warudi nyuma
kufanya mambo kadhaa waliyoyaacha. Viongozi hawa waache kukubali kuwa daraja la
wanasiasa na wahakikishe kwamba wanawaunga mkono wanasiasa katika mambo ya
maendeleo lakini pia wapime upepo na kutazama sifa ya mwanasiasa katika jamii
na ni lazima wahakikishe kwamba wanasiasa wanajua kwamba ikiwa watajichafua
kwenye utendaji wao, dini hazitakuwa mahala pa kujisafishia.
Viongozi wa dini wakemee watu wanaoibuka kila leo na
kufundisha mambo yaliyo kinyume na upendo na amani na hata mshikamano wa watu
wa jamii yao badala ya kuingia kwenye makundi ama kuoneana aibu ati kwa vile
huyo anayekosea ni wa mlengo wa dini yangu na hivyo siwezi kumkosoa hadharani.
Ni lazima viongozi wa dini wanaopotoka kutoka kwenye misingi ya kidini na
kuvunja hata sheria za nchi kwa mahubiri ama mafunsidho yao wakemewe na
viongozi wenzao wa dini na ikibidi hadharani ili dini zirudi kuwa mahala ambapo
mizaha ya hatari haiwezi kuruhusiwa kamwe.
Ni lazima tuache kuwashabikia watu wenye kufanya vitendo vya
kipuuzi na kuumiza binadamu wenzao ati kwa kisingizio cha dini lakini pia
tusiwakalie kimya na kisha kusimama tukijiosha kwamba hao ni “wahuni” maana
wanachofanya hakikubaliki na dini, ni lazima tuseme hadharani mapema kwamba
hawa wanachofanya hakikubaliki na tuwapinge badala ya ama kuwavisha mavazi ya
heshima ama kuwakalia kimya hadi serikali inapoonyesha kukasirika ndipo ati na
sisi tunaibuka na kauli za kujiosha.
Viongozi wa dini walinde heshima ya mimbari na pia wasimame
ndani ya mipaka yao badala ya kujitwalia mamlaka ya kusema kuhusu kila kitu
maana miluzi mingi humpoteza mbwa na ni busara kunyamaza kuliko kusema ikiwa
kusema kwenyewe ni kwenye kuchochea moto unaochoma nyumba tayari. Ikiwa bado
viongozi wa dini mnataka kujiingiza kwenye siasa na kisha kuwalaumu wanasiasa
mi nadhani ni wakati sasa mfike mahala muone haya kwa haya yanayotokea.
Ni mimi ndugu yenu Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika, nawasalimia.