Wananchi wakiondoka kwa amani kwenye mkutano uliofanyika juzi kwenye viwanja vya Bima ambapo mkutano wa leo umekwisha kwa vurugu..
Kwa sababu dunia imebadilika kiasi cha kuruhusu kila mtu
kutoa maoni yake kwa urahisi na uhuru, na kwakuwa matumizi ya mitandao ya
kijamii yametengeneza jukwaa pana zaidi kwetu sote kutumia nafasi na vipaji
vyetu kuonyesha uwezo wetu, naamini ni kwa sababu hiyo baadhi ya wasomaji wangu
japo kusema kweli ni wachache humu mtandaoni wananipa nafasi kubwa ya kusema
kwao na hata wakakubali juu ya ninachokisema japo walio wengi wana sifa moja na
mimi kwamba sisi ni watu wasio na nafasi huru za kusema.
Ndiyo maana basi kwa hili nimeona vyema niseme kwa sababu
wasomaji wangu hawa wanategemea niwe na cha kusema na kwa hilo Chokoraa
nawaandikia. Siwaandikii hili wote mkubaliane na mimi lakini najaribu kwa kadri
niwezavyo kupata uhuru wangu wa kusema.
Pamoja na kwamba nimekuwa Mtwara kwa karibu miezi sita sasa,
leo nimepita katika mji wa Mtwara ukiwa katika kile ambacho kwangu binafsi kama
Chokoraa kimenitisha. Nimeogopa. Nimetishwa na kuamka na kugundua kwamba kumbe
Tanzania ile tuliyolala jana, inaweza kuamka ikiwa ni Tanzania nyingine ambayo
watu wanaishi kwa hofu na mashaka kiasi hiki?
Mji wa Mtwara ulitanda askari Polisi waliokuwa
wamejisheheneza vilivyo kwa ajiri ya kupambana na wananchi wa Mtwara
waliokuwa kwenye mkutano wa kupinga Gesi
asilia kuondolewa Mtwara.
Inasemekana maandamano ya leo hayakukusidiwa kuwa maandamano
ya fujo bali lengo lilikuwa kufanya mkutano mkubwa ambapo wananchi kutoka
wilaya zote za mikoa ya Lindi na Mtwara
wangekutanika kwenye uwanja wa mashujaa ikiwa ni mwendelezo wa kuishinikiza
serikali kutokuondoa gesi ghafi Mtwara.
Wakati maandalizi ya mkutano yakiendelea mara umeme
ukakatika kwenye eno la mkutano na baadhi ya wananchi wakahisi hiyo ni hujuma
kutaka mkutano usiendelee kama ulivyopangwa kwa vile vipaza sauti zisingefanya
kazi bila umeme na ndipo kimbembe kilipoanza.
Wananchi waliteremka mabarabarani na kuanza vurugu na fujo
huku wakielekea zilipo ofisi za Tanesco na polisi wakaingia kuwadhibiti,
kilichofuata ni milipuko ya mabomu, kurushwa mawe, magogo ya miti kupangwa
barabarani na kufunga kabisa mji wa Mtwara. Barabara kuu ya Mtwara ilifungwa
kabisa ambapo hakuna gari liliweza kupita barabara hiyo na hata makutano ya
barabara eneo la Bima yalifungwa kwa magogo.
Maduka yalifungwa na mji mzima ulikuwa umepooza mnamo wa
majira ya saa saba hadi tisa za jioni nilipojichomoa mjini na kuamua kujiridia
kibandani kwangu kujificha na yatokanayo.
Si lengo langu kusema juu ya nini msimamo wangu binafsi juu
ya hili kwenye makala hii lakini niseme
nilichokiona leo kimenitisha sana. Si kwa sababu nyingine yoyote bali kwa kuwa
leo kwa mara ya kwanza (najua wako ambao wameshudia hili mara nyingi)
nimeshuhudia barabara zikiwa zimefungwa kwa magogo ya miti, polisi wakiwama na
siraha mikononi kukabiliana na wananchi waliokuwa na mawe na fimbo mikononi.
Kauli za waandamanaji wakifananisha mji huu na Libya ni
jambo lingine lililonitisha. Wananchi wenye morali walisikika wazi wazi
wakisema “Kama Libya…..damu itamwagika sana….” Na wengine kutishia askari
Polisi wanaoishi uraiani kuhamishia familia zao kituoni.
Si lengo langu kusema juu ya nini msimamo wangu binafsi juu
ya hili kwenye makala hii lakini niseme
nilichokiona leo kimenitisha sana. Si kwa sababu nyingine yoyote bali kwa kuwa
leo kwa mara ya kwanza (najua wako ambao wameshudia hili mara nyingi)
nimeshuhudia barabara zikiwa zimefungwa kwa magogo ya miti, polisi wakiwama na
siraha mikononi kukabiliana na wananchi waliokuwa na mawe na fimbo mikononi.
Kilichonitisha zaidi ni pale ambapo mpaka sasa serikali
imekaa kimya bila kutoa majibu yoyote kwa hoja za wananchi hawa na badala yake
imeishia kudharau vuguvugu hili huku hali hiyo ikihatarisha usalama wa wananchi
na amani ya nchi kwa ujumla.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ndiye kiongozi mkubwa kabisa mkoani
humu ambaye kauli yake kwa wananchi imeibua kero na manung’uniko hata miongoni
mwa maafisa wa serikali yenyewe pale alipowaita wananchi hawa ‘wapuuzi’ na
wasiosoma.
Nasema kwa hili serikali itoe majibu yanayoeleweka kwa
wananchi wake ama bunge lichukue hatua ya kuitana haraka na kuzungumza kuhusu
jambo hili ama mgogoro mkubwa utakaobadili historia ya nchi unaweza kutokana na
ukimya huu. Ikiwa bunge limekuwa likiunda tume kuchungunza mambo kama pesa
zilizofichwa nje ambazo bado kitendawili chake hakikajulikana ikiwa ni kweli au
si kweli, basi ni wakati bunge lichukue hatua kwa hili.
Wananchi bado wana imani na bunge lao japokuwa hawana imani
na serikali na ni wakati wabunge ambao ndiyo waajiriwa wa wananchi kuisimamia
serikali, waamke na kufanya kazi waliyotumwa na wananchi wao.
Kazi hii wala wasiachiwe wabunge wa Mtwara peke yao. Nasema
hivi kwa sababu inaonekana wazi kwamba kazi hii imewashinda kwa sababu maneno
haya hayakufikia hapa kwa kuzaliwa leo asubuhi na kufikia hali hii bali
yamekuwako kwa wanajamii muda mrefu na ikiwa ama wabunge hawakujua kwa sababu
hawana ukaribu na wananchi wao ama walijua na kudharau kwamba ni maneno ya
hovyo, basi wameshindwa kuwa na uwezo wa kuaminiwa tena na wananchi kumaliza
suala hili na hivyo ni wakati Bunge kama taasisi ijiingize kwenye hili.
Wananchi wanachotaka ni kusikilizwa na kupewa majibu kwa
hoja zao na kwa kuwa wamepoteza imani na majibu yanayotolewa na serikali, ni
wakati kwa ajiri ya amani ya nchi, taasisi ya Bunge ijiingize kwenye jambo hili
kuepusha umwagaji damu mkubwa.
Nilipotazama kwamba wengi wa waandamanaji ni vijana wadogo
ambao hata hawajawa na familia bado, nikajifunza kwamba hili litakuwa jambo
gumu sana kulimaliza kwa ubabe kwa sababu kimsingi vijana hawa hawana cha
kupoteza kwa kufanya wafanyao.