Saturday, January 19, 2013

BUNGE LIINGILIE KUPUSHA MGOGORO WA MTWARA




 Wananchi wakiondoka kwa amani kwenye mkutano uliofanyika juzi kwenye viwanja vya Bima ambapo mkutano wa leo umekwisha kwa vurugu..

Kwa sababu dunia imebadilika kiasi cha kuruhusu kila mtu kutoa maoni yake kwa urahisi na uhuru, na kwakuwa matumizi ya mitandao ya kijamii yametengeneza jukwaa pana zaidi kwetu sote kutumia nafasi na vipaji vyetu kuonyesha uwezo wetu, naamini ni kwa sababu hiyo baadhi ya wasomaji wangu japo kusema kweli ni wachache humu mtandaoni wananipa nafasi kubwa ya kusema kwao na hata wakakubali juu ya ninachokisema japo walio wengi wana sifa moja na mimi kwamba sisi ni watu wasio na nafasi huru  za kusema.

Ndiyo maana basi kwa hili nimeona vyema niseme kwa sababu wasomaji wangu hawa wanategemea niwe na cha kusema na kwa hilo Chokoraa nawaandikia. Siwaandikii hili wote mkubaliane na mimi lakini najaribu kwa kadri niwezavyo kupata uhuru wangu wa kusema.

Pamoja na kwamba nimekuwa Mtwara kwa karibu miezi sita sasa, leo nimepita katika mji wa Mtwara ukiwa katika kile ambacho kwangu binafsi kama Chokoraa kimenitisha. Nimeogopa. Nimetishwa na kuamka na kugundua kwamba kumbe Tanzania ile tuliyolala jana, inaweza kuamka ikiwa ni Tanzania nyingine ambayo watu wanaishi kwa hofu na mashaka kiasi hiki?

Mji wa Mtwara ulitanda askari Polisi waliokuwa wamejisheheneza vilivyo kwa ajiri ya kupambana na wananchi wa Mtwara waliokuwa  kwenye mkutano wa kupinga Gesi asilia kuondolewa Mtwara.

Inasemekana maandamano ya leo hayakukusidiwa kuwa maandamano ya fujo bali lengo lilikuwa kufanya mkutano mkubwa ambapo wananchi kutoka wilaya zote za  mikoa ya Lindi na Mtwara wangekutanika kwenye uwanja wa mashujaa ikiwa ni mwendelezo wa kuishinikiza serikali kutokuondoa gesi ghafi Mtwara.

Wakati maandalizi ya mkutano yakiendelea mara umeme ukakatika kwenye eno la mkutano na baadhi ya wananchi wakahisi hiyo ni hujuma kutaka mkutano usiendelee kama ulivyopangwa kwa vile vipaza sauti zisingefanya kazi bila umeme na ndipo kimbembe kilipoanza.  

Wananchi waliteremka mabarabarani na kuanza vurugu na fujo huku wakielekea zilipo ofisi za Tanesco na polisi wakaingia kuwadhibiti, kilichofuata ni milipuko ya mabomu, kurushwa mawe, magogo ya miti kupangwa barabarani na kufunga kabisa mji wa Mtwara. Barabara kuu ya Mtwara ilifungwa kabisa ambapo hakuna gari liliweza kupita barabara hiyo na hata makutano ya barabara eneo la Bima yalifungwa kwa magogo.

Maduka yalifungwa na mji mzima ulikuwa umepooza mnamo wa majira ya saa saba hadi tisa za jioni nilipojichomoa mjini na kuamua kujiridia kibandani kwangu kujificha na yatokanayo.

Si lengo langu kusema juu ya nini msimamo wangu binafsi juu ya hili kwenye makala hii  lakini niseme nilichokiona leo kimenitisha sana. Si kwa sababu nyingine yoyote bali kwa kuwa leo kwa mara ya kwanza (najua wako ambao wameshudia hili mara nyingi) nimeshuhudia barabara zikiwa zimefungwa kwa magogo ya miti, polisi wakiwama na siraha mikononi kukabiliana na wananchi waliokuwa na mawe na fimbo mikononi.

Kauli za waandamanaji wakifananisha mji huu na Libya ni jambo lingine lililonitisha. Wananchi wenye morali walisikika wazi wazi wakisema “Kama Libya…..damu itamwagika sana….” Na wengine kutishia askari Polisi wanaoishi uraiani kuhamishia familia zao kituoni.

Si lengo langu kusema juu ya nini msimamo wangu binafsi juu ya hili kwenye makala hii  lakini niseme nilichokiona leo kimenitisha sana. Si kwa sababu nyingine yoyote bali kwa kuwa leo kwa mara ya kwanza (najua wako ambao wameshudia hili mara nyingi) nimeshuhudia barabara zikiwa zimefungwa kwa magogo ya miti, polisi wakiwama na siraha mikononi kukabiliana na wananchi waliokuwa na mawe na fimbo mikononi.

Kilichonitisha zaidi ni pale ambapo mpaka sasa serikali imekaa kimya bila kutoa majibu yoyote kwa hoja za wananchi hawa na badala yake imeishia kudharau vuguvugu hili huku hali hiyo ikihatarisha usalama wa wananchi na amani ya nchi kwa ujumla.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ndiye kiongozi mkubwa kabisa mkoani humu ambaye kauli yake kwa wananchi imeibua kero na manung’uniko hata miongoni mwa maafisa wa serikali yenyewe pale alipowaita wananchi hawa ‘wapuuzi’ na wasiosoma.

Nasema kwa hili serikali itoe majibu yanayoeleweka kwa wananchi wake ama bunge lichukue hatua ya kuitana haraka na kuzungumza kuhusu jambo hili ama mgogoro mkubwa utakaobadili historia ya nchi unaweza kutokana na ukimya huu. Ikiwa bunge limekuwa likiunda tume kuchungunza mambo kama pesa zilizofichwa nje ambazo bado kitendawili chake hakikajulikana ikiwa ni kweli au si kweli, basi ni wakati bunge lichukue hatua kwa hili.

Wananchi bado wana imani na bunge lao japokuwa hawana imani na serikali na ni wakati wabunge ambao ndiyo waajiriwa wa wananchi kuisimamia serikali, waamke na kufanya kazi waliyotumwa na wananchi wao.

Kazi hii wala wasiachiwe wabunge wa Mtwara peke yao. Nasema hivi kwa sababu inaonekana wazi kwamba kazi hii imewashinda kwa sababu maneno haya hayakufikia hapa kwa kuzaliwa leo asubuhi na kufikia hali hii bali yamekuwako kwa wanajamii muda mrefu na ikiwa ama wabunge hawakujua kwa sababu hawana ukaribu na wananchi wao ama walijua na kudharau kwamba ni maneno ya hovyo, basi wameshindwa kuwa na uwezo wa kuaminiwa tena na wananchi kumaliza suala hili na hivyo ni wakati Bunge kama taasisi ijiingize kwenye hili.

Wananchi wanachotaka ni kusikilizwa na kupewa majibu kwa hoja zao na kwa kuwa wamepoteza imani na majibu yanayotolewa na serikali, ni wakati kwa ajiri ya amani ya nchi, taasisi ya Bunge ijiingize kwenye jambo hili kuepusha umwagaji damu mkubwa.

Nilipotazama kwamba wengi wa waandamanaji ni vijana wadogo ambao hata hawajawa na familia bado, nikajifunza kwamba hili litakuwa jambo gumu sana kulimaliza kwa ubabe kwa sababu kimsingi vijana hawa hawana cha kupoteza kwa kufanya wafanyao.

No comments:

Post a Comment