Salaam nawasalimia!
Hivi! kwanini wengi wenu mmekuwa “mnanidipu” kwenye kitochi changu
na ati kwavile Chokoraa nina “gando” la kugandishwa nikiwapigia mnakimbilia
kuniuliza mbona siku hizi sionekani!?. Ala! Mwataka nionekane wapi!? Kwenye
vilinge vyenu vya ulevi wa “si hasa” majitaka!? Nani kasema nataka kulichafua
kaniki langu na majitaka yenu?. Simo naapa.
Ha ha ha ha ha!!! Chafuaneni maana huu hasa ndiyo wakati na
mwaka wenu, mwaka wa Uchafuzi. Na miye
humo nahusikaje!? Simo.
Nasema kama walivyokwishasema wale waliokuwa kabla yenu,
Nguruwe kwake sifa kugagaa matopeni na mimi nakupongezeni kwa juhudi zenu za
kuchafuana, na wala siwalaumu maana huu ndiyo muhula wake, muhula wa
kuchafuana, ila miye salaam nawasalimia.
Nasema kuchafuana si jambo baya kwenu hasa kwa vile hiyo
ishakuwa mila na “visturi” kwenu, ila wacheni basi kutuchezea mahepe na viini
macho tena mchana kweupe siye wana wa Mdanganyika Mlipakodi, maana michezo yenu
hii mwailipia kwa kodi za Wadanganyika hawa na miye nauliza mwataka kutudangaya
mpaka lini!?.
Ati! Kwani si nawasikia jinsi mlivyo na juhudi katika
kututaka na sisi tushiriki kuchafuana kwenye uchafuzi wa “ ka tiba” kapya ilhali hamjafanya maandalizi
tosha ya kutufikisha mahututi siye kwa tabibu!?. Ha ha ha ha ha!!! Na miye
nauliza, hivi ‘ka tiba’ haka kanatibu ule ugonjwa wenu uliomuua Maadili wa
Mdanganyika ama ugonjwa unaowaua kila
kuitwapo leo wana wa Mdanganyika wa
Mlipakodi!?. Naapa hiki ni kiini macho kwa wazima kupata ‘ka tiba’ ilhali
wagonjwa wa umaskini na “si hasa” maji taka wakiachwa wajifie kwa kadri
wawezavyo ila simo. Tena simo kabisaaa, sihusiki.
Haya, niyawache hayo miye ya ‘ka tiba’ kalikomuua badala ya
kumtibu Umoja wa Mshikamano wa Mdanyika wa Mlipakodi, japo kusema kweli
nakumbuka bado jinsi tulivyotawanyika
msibani bila hata kuanua matanga ati kwa vile sungusungu wa kijiji waliamuliwa
wawanyamzishe wote waliokuwa wakilia sana, na ati watakaogoma kunyamaza basi
wapigwe tu maana wanapenda kulia.
Nasema huu mwaka wenu tu hata mkatae enyi wana wa
Mdanganyika Mlipakodi na japo mwenye macho haambiwi tazama, lakini kutazama si
kuona na miye hapa salaam nawasalimia. Ala! Kwani si wenyewe mwajionea vituko
vya uchafuzi huu, wakati mnapofukuzana kwenye banda lenu ati kwa vile
mmeshindwa kuelewana wenyewe kwa wenyewe, ama kwa vile bwana mdogo ameshindwa
kunyamaza akasemea kwenye kashimo kwamba mfalme ana masikio kama popo!?. Ha ha
ha ha ha ha!!! Ama kweli si kila ukweli ni ukweli na si kila ulijualo yakupasa
kulisema maana ati ulimi uliponza kichwa. Simo naapa.
Nauliza ikiwa kumwendesha Farasi kwa kupeni taabu mtaiweza
nyie kasi ya Nyumbu ama na nyie mwachafuana tu kwa vile huu nao ni mwaka wa
uchafuzi!?. Pole sana wewe mwembamba lakini mzito kwa uzito wa Tembo. Nasema hili
si kosa lako hata kidogo bali ni kosa la Wadanganyika sisi tuliosahau katazo la
kumsifia Mgema na sasa umewatukana Mamba ilhali hujavuka mto, ona sasa hasira
yao inavyokuchafua. Hata hivyo si mwaka wa uchafuzi! Chafuaneni tu ila mimi humo simo katu!.
Nasema mnisamehe ikiwa pamoja na ukweli kwamba ninaumwa,
tena hoi bin taabani, bado nachelea kuchafuana kwenye uchafuzi wenu huu wa ‘ka
tiba’, japo kusema kweli najihoji, mtafanzaje bila ‘ka tiba’ ilhali mwaka huu
kale ka ugonjwa kenu ka kuchafuana kamewaanza tena!?. Ha ha ha ha ha ha!!! Nicheke
Chokoraa miye maana kuchafuana ni kama kifafa, mwaujua msimu wake na dalili
zake lakini ati mlikuwa na mambo mengi sana mkashindwa kuuandalia ‘ka tiba’ kwa
wakati na sasa mwajaribu kuutibu kwa kasi ya zimamoto. Simo naapa.
Haya, wacha nirudi zangu jalalani nikakusanye mapande ya
Boflo kwa ajiri yangu na wadogo zangu na hata Yule mama yangu kikongwe Shida wa
Matatizo wa Taabu Maisha Magumu. Naomba chonde chonde, mkiisha kupata ‘ka tiba’
ka ugonjwa huu wa kuchafuana, basi chafuaneni maana nani atakukatazeni ilhali
huu ndo msimu wake hasa! Ila chonde enyi
wana msije mkauchafua hata mchezo wenyewe wa kuchafuana ikiwa mtaamua
kujiingiza kichwa kichwa kwenye uchafuzi wa ‘ka tiba’ ati kwa vile msimu wa
ugonjwa wa uchafuzi umefika, kwani kale ka tiba kalikokutibuni miaka yote kana
nini hata mwatumia nguvu ya zimamoto kuzima barafu!!!!!?.
Wasalaamu, ni mimi ndugu yenu Chokoraa wa Muhangaikaji wa
Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika wa Mlipakodi nawasalimia,
shikamooni Wadanganyika.
naona umejiandaa na mwaka wa kuchafukwa tumbo kutokana na uchafuzi mkuu
ReplyDelete