Saturday, April 16, 2016

Mwashangaa Fatu kupigwa! Mwashangaa nini!?



Salaam nawasalimia! Najua wako baadhi yenu ambao mmepita kijiweni kwangu mara nyingi na kunikosa na hata wengine nasikia walishakula wali wa hitima. Si makosa yenu, ila miye salaam nawasalimia. Nasema sionekani kijiweni si kwa sababu sipo ila kwa sababu hamnioni. Labda pia sipendi mnione maana si siku hizi hata upele mwaita jipu na kila mmoja atafuta kuonekana tabibu na anaweza kutumbua! Nani kakwambia na miye jipu! Naapa mwanitafuta ubaya enyi wana na miye humo simo ila salaam tu miye nawasalimia. 

Ala! Kwani mi si nimekuwa nakuoneni tu tangu mlipomaliza ule mchezo wwenu kichaa jinsi ambavyo nyote mmehamia huku kwetu ‘bize’ mkimwagiana “majitaka” ilhali mwajua fika kwamba muda wa kuchafuana ushakwisha!?. Haya, endeleeni kumwagiana majitaka tu midhali si mtindi mkali, lakini nawaapia enyi wana msipokubaliana kutokukubaliana na mkasonga mbele hata kama kwa mwendo wa Kobe, huko mwendako nachelea mtaanza tumbuana wenyewe kwa wenyewe ila miye humo nahusikaje! Simo naapa. 

Leo miye nimekuja tu huku mjini kwenu mara moja  kumletea salaam za heri Mkulu wa kaya ya Wadanganyika walipakodi; ikiwa heri ni kunyamaa usinene yale wasiyopenda kuyasikia akina kaka mkubwa Muishiwa wa Mdanganyika wa Mlakodi, , salaam nakusalimia. 

Muishiwa sana Mkulu wa kaya yetu, miye ni yule nduguyo Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika Mlipakodi, ambaye siku si nyingi wapambe wako walipita kijiweni kwangu na baragumu kunitaka nikusanyike kwenye uwanja wa ‘mkung’utano’; nishuhudie jinsi mlivyokuwa mkiucheza ule mchezo wenu maarufu kwa harufu, muupendao wewe na waishiwa wenzio, mchezo wa kuchafuana. 

Ha ha ha ha ha!!! Sikuwa nimevaa rangi rangi, na sauti ya kijiweni haitoki kwa mvaa suti kwa hiyo kama hukunitambua kwa masempele yangu niliyokuwa nimejifunika ili walau msiseme natembea uchi japo kusema kweli sikuwa nimevaa, basi itakuwa shida kweli kunikumbuka, ila salaam nakusalimia, shikamoo mkulu wa kaya. 

Sitaki nikukumbushe zamani maana najua wewe waifahamu vyema historia ya kaya yetu hii na jinsi ambavyo kaka mkubwa, Mkufunzi wa Mdanganyika wa Mlipakodi alivyotuasa na kutuacha, ila miye nimekuja tu hapa mtaani kwako nikuletee  salaam za wadogo zangu wale akina Mtafutaji na Mjasiria, na hata yule aliyepewa jina la babu wa babu yake na babu mzaa baba, Mlalahoi. 

Wala sina haja ya kukumbusha jinsi Mlalahoi alivyo mtundu na hata bibi yake yaani mama yenu mkubwa Mchakarikaji anasema amechoshwa na kelele na vurugu za huyu mtoto, ila hayo unayajua.

Juzi tu wakati nafunga safari kuja mjini, mlalahoi akaniijia na majani  mabichi mkononi, unaweza kudhani nilimdharau tu kwa vile ni mtoto anacheza, lakini mimi namfahamu vyema mlalahoi, akifanya jambo ujue anataka kusema jambo. Asivyo na adabu, ati nayo akayaweka kwenye kimfuko changu cha Rambo nilimoweka pia vidaso vyangu vya kubadilisha, hapo sasa nikakasirika, nikataka kumzaba kofi, lakini kabla hata sijanyanyua mkono akanitazama na kutabasamu kitoto, kisha akasema “Kaka, hiyo dawa hiyo, uende nayo huko mjini”.

 “Dawa ya nini wewe Mlalahoi, mbona weshi vituko we mtoto?” Nikamuuliza na hata mimi sasa nilitabasamu maana kumbe ule niliowaza kuwa uchafu, ilikuwa namna yake ya kunijali nisiugue niendako.
 “Dawa ya majipu kaka, huko mjini nasikia huo ugonjwa umeenea na hata kaka yetu Muishiwa sana mkulu wa kaya, siku hizi anatumbua majipu tu...”. Nikamtazama huyu mtoto, kisha nikaanza kujihoji ameyatoa wapi mawazo hayo kichanga huyu asiyejua chochote katika dunia hii ya “si hasa” za kuchafuana hata baada ya “uchafuzi mkuu”?

Nadhani mlalahoi aliouna wasiwasi wangu, akanishika mkono na kuniashiria nikae chini, nikaketi na kumsikiza, ndipo aliponiambia nikifika mjini nikusalimu na ati nikwambie ingawa ni kweli kwamba dawa yoyote ni chungu wakati wa kunywewa kwake, na kwamba dawa ya jipu kutumbuliwa, lakini tumeagana na nyonga katika mbio hizi!?.

Ndiyo, maana huku kwetu sasa wale watoto watukutu wa mzee Mhalifu wameanza tena zile tabia mbaya za kumpiga dada “Fatuma” na ati ukiuliza unaambiwa “hali ngumu sasa tukale wapi?”, na miye swali ambalo sijalipatia jibu hadi sasa ni ikiwa ‘kumpiga fatuma’ ndiyo suluhu ya njaa yao, ila miye salaam nakusalimia.
Nasema hili ongezeko la kile ambacho sungusungu wa kijiji wanakiita “uhalifu mdogo mdogo” siyo hasa jipu, bali ni dalili za kansa inayomea na kukua upesi, na naapa mwaniapisha ikiwa hamtafuti dawa yake, tumbueni majipu lakini kansa haitumbuliwi. 

Ati! Najua wako wanaosema kwani anajua nini bananga huyu, na wako wengine watatafuta kunitumbua na miye kwa kutumia ile sindano yao ya “swahiba klaimu”, lakini miye sivunji sheria bali ni salaam tu nawasalimia. 

Ala! Kwani mmepofuka lini msione kwamba ama ongezekeo hili la ‘vibakaji’ vinavyobaka hata chakula chetu tulichokitolea jasho na damu, ni dalili ama kwamba ile bana matumizi sasa inaanza kutufikia hata sisi tuliokuwa tukipiga kelele za ufisadi bila kujua kwamba hata kuishi mjini kwa ‘misheni tauni’ ni ufisadi, ama kwamba wahalifu papa hasa wauzao sembe wameamua kuanzisha mbinu ya kuhamisha ‘atensheni’ yenu mkimbizane na ‘vijitu vidogovidogo’ ili wao wasage na kuuza sembe lao kwa amani!? Ha ha ha ha ha ha!!! Nacheka mwanichekesha miye!

Nasema ya wauza sembe msiniulize maana miye si mla nyama, mchicha na tembele ndiyo mboga yangu, lakini sembe simo hata kidogo, na hapa salaam nawasalimia, ila fumbueni macho muikate kansa hii kabla haijaenea sana na kuwazidi kimo enyi wana maana mchelea mwana kulia hulia yeye.
Ala! Kwani hamjui kwamba kuna waliokuwa wakiishi mjini kwa misimu ya sikuu za kitaifa na sasa hawana la kufanya  ili wanunue ugali kwa mama ntilie!? Ama mwajifanya mmesahau kwamba walipoamua kutoendesha magari yao kwa vile mafuta yamekuwa aghali, na vipuri vimeacha kuharibika na hivyo gereji hazina kazi!?. Nasema simo humu namo!. Mwashangaa ati inakuwaje sasa mnasikia kilio, fatuma kapigwa mtaani kwenu!? Mwashangaa nini!?

Sisemi kati msibane matumizi na wala msitumbue majibu uchungu  maana dawa ya ugonjwa tiba, lakini nauliza tu ikiwa kuna mipango mbadala ya kukabiliana na madhara yatokanayo na hatua chanya hizi ama wote tufumbe macho tusali!? 

Ni mimi ndugu yenu Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika Mlipakodi, salaam nawasalimia.

No comments:

Post a Comment