Wednesday, July 10, 2013

Mwala magengeni mwezi huu; Vyungu vya nini!?





Nasema mapema kwa hili wana wa Danganyika hii mmenikera na ndiyo sababu miye sitaki kuhusika maana simo tena simo kabisaaaaa. Ala! Kwani  si mwezi  mtukufu wa ramadhani si umeingia na ati siku moja kabla ya mwezi kuanza wengi wenu mlikuwa na sherehe ya kuvunja vyungu kwa vile kwa mwezi mzima hamtakula!?. Naapa mwamtania Mungu enyi wana. 

Naapa kwa jina la Babu yangu mzee Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika, nyie mwamtania Mungu. Nasema mmemgeuza Mungu kuwa babu yenu na miye humo msinihusishe. Ala! Si nimeshuhudia mwenyewe ambavyo jana wengi wenu hamkuwamo majumbani kwenu na hata mmedhulumu haki za 'ndoo' za wenzi wenu kwa kuvunja vyungu vyote ati kwa vile mwezi huu hampiki ila mwala magengeni na sasa vungu vya nini!? Naapa laana mmelaaniwa enyi wana na miye humo simo. Sitaki, tena nasema sitaki kuwashawishi mkubaliane na mimi katika kila nisemacho lakini ni kweli kwamba ama hizi dini zimekuwa kwenu kama kongwa la utumwa ni vyema mungelizivua mkatembea huru katika uhuru wa mwendawazimu kuliko huu wazimu wa usiku muufanyao naapa mmenikera enyi wana. Na sasa najiuliza wakati ninapowatakia wale wenye nia safi Ramadhani karim, nyie wengine ambao jana mmefanya kufuru ya kuvunja vyungu vyetu niwaambieje? Poleni na starehe?. Simo.

Nasema kwa kitendo chenu hiki nashindwa kujua niwaiteje maana kuwaita wafuasi wa dini itakuwa kuikosea adabu dini yenyewe maana ikiwa hao mitume walioleta kwenu dini hiizi wangefufuka leo, bila shaka na ongezeko hili la magonjwa yasiyokuwapo enzi zao wangekufa mara ya pili mara hii kwa magonjwa ya moyo kama si sononi na humu najitoa maana simo.

Haya, wacheni nijiropokee maana humu ndani naweza kuropoka tu bila hofu kwa vile mimi ni Mdanganyika tena mlipakodi na ninafahamu nyie wenye kuvunja vyungu vyetu ili wote tushinde njaa kama ninyi hamna mahusiano ya karibu na wale wasiojulikana na hivyo sikuogopeni katu. Nasema nyie si wafungaji ni washinda njaa na mwaiongoezea kaya yetu mzigo wa kuuguza wagonjwa wa vidonda vya tumbo na magonjwa yake kwa kujisindisha njaa ilhali nafsi zenu zili dhalili na humu mnitoe. 

Ala! Kwani hayakuwatosheni maovu ya mwaka mzima hadi mlipoamua kufanya kufuru za mwaka mzima “ini advansi” kwa vile funga imekurubia?. Ha ha ha ha ha ha ha!!!! Najiuliza wadanganyika nyie mwajidanganya na nini kuwaza kwamba huyu Mungu anawaza kama muwazavyo ninyi na hivyo atawaosheni na maovu yenu ya makusudi muyatendayo kwa kujikinahi!?. Hayo nakuachieni nyinyi maana hata mimi ni muovu mwana wa uovu na yamkini hata mimba yangu ilitungwa hatiani lakini kwa hili msijifananishe name maana simo.
Nasema mimi na ninyi hatufanani kwa sababu binafsi najifahamu kwamba sihitaji kujishindisha njaa kwa sheria tu ilhali nikiwa muovu na hivyo wakati wenzangu jana mmevunja vyungu vyote mtaani, mimi nimenunua magudulia ya chuma nasonga ugali nile nishibe ili nikuchekeni nyie wenye kujivisha ngozi za kondoo ilhali ndani ni mbwa mwitu wakali. 

Hivi, nyie si ndiyo wale mliohusiwa juu ya vita vilivyo bora zaidi  yaani vita vya kuishinda nafsi!? Mbona sasa mmekuwa watumwa wa nafsi zenu wakati ingekuwa rahisi kwenu kula mkashiba mkafanya kazi na kuongeza uchumi wa jamii zenu huku mkiwa na afya njema na nafsi safi bila kulazimika kuwa wanafiki!? Naapa huu wa wavunja vyungu ni unafiki tena unafiki mtupu!. 

Kasirikeni mkasirikavyo lakini jueni kwamba mwana wa muhangaikaji kwa hili mmenikera lakini sina hasira sana kama nilivyo na huruma. Ninawahurumia na ndiyo sababu ya kukuandikieni waraka huu ili mwenye masikio ya kupona asikie hizi dawa lakini ikiwa ni wa kufa basi ziba masikio kwa hasira na visingizio. Ndiyo, najua mtaleta visingizio kwamba ati Chokoraa miye nimeitusi dini nasema huo utakuwa ni unafiki wa radaja la pili maana miye siitusi dini ila nawauliza wenye kujifanya mwaifuata dini kana kwamba kwa shuruti huku mkifanya kufuru, mmejihoji ni wangapi kati yenu mliokumbuka kula pipi zenu kwenye maganda ama huko nako mlivunja vyungu!? Naapa ikiwa na hilo nalo mlilivunjia vyungu, basi jiulizeni ni wangapi kati yenu mlioambukizwa kale kaungonjwa na mnaojiandaa kunilaumu Chokoraa nikikataa kuja kuwaona mlazwapo hospitali na wengine kusema nawanyanyapaa!? Kwa hili naapa niiteni mnyanyapaa lakini hata kwa Mungu sina hatia ikiwa nitawanyanyapaa kwa kujisulubisha wakati wa kuvunja vyungu maana kuna tofauti ya makusudi na bahati mbaya msiolijua hilo jilaumuni wenyewe na humu simo.

Haya, na wale ambao mliwatoroka wazazi wenu na kwenda kwa vibwana vyenu huku mkidhani mwawafurahisha kumbe mwajitafutia majukumu ya ulezi msiyoyaweza bado na mwisho wa siku mwataka jamii ibebe mzigo wa kunilea Chokoraa miye na wadogo zangu akina mzembe na mzururaji!? Hivi na hili nalo linahitaji “sirikali” kukupeni onyo mapema?. 

Komeni. Nasema komeni hasa nyie mjiitao “wana haraka tu” kuipigia kele ‘siri kali’ ati kwa kutofanya chochote kuwasaidia ‘watoto wa mitaani’. Nasema mkome. Ndiyo, najua wengine ni rafiki zangu lakini nisikilizeni maana kwa hili siropoki nasema hakuna mtoto wa mtaani maana kila mtoto ana baba na mama yake na ni lazima wawajibike wao kwanza kuondoa watoto wao mitaani na ndipo sisi wengine tutafuata!?. Ala! Mwataka tu nyie mfanye fujo zenu na kuvunja vyungu vyetu bila mipango wala mikakati ya kukabiliana na matokeo ya uvunjaji vyungu huo kisha siye tuwajibike!? Nani kasema!?. Simo humu namo. 

Ha ha ha ha ha ha!!! Hongera zenu wajasiria mlo maana nina hakika kwa siku ya jana nyie jana mlikuwa na “ugeni” mkubwa na hata wengine walilala sebleni na hata wako waliopitisha muda wao kwenye maliwato na huko kote wakivunja vyungu. Kwani viliwakosea nini?. Ama kosa la vyungu hivi ni kuwapikieni mwaka mzima na sasa kwa vile mwezi huu mwabadili ratiba ya kula basi vyungu havina thamani tena?. Nasema nyie mliovunja vyungu jana hamjafunga hata kidogo. Mmebadili tu muda wa kula kwa kuacha kula mchana mzima huku mkifakamia milo yote usiku maana kufunga huanzia kwenye nafsi na nyie nafsi zenu mmeziuza kwenye kuvunja vyungu. 

Haya, najua wako wale ambao kwa nia ya kweli ujio wa ramadhani umewakuta wamejiandaa nafsi zao kwa ajiri ya muumba wao. Kwenu nyie salamu zangu ni chache tu. Muombeni huyo Mwenye Enzi yote aliyevifanya vyote atufanyie wepesi hasa kwenye kaya yetu hii itafunwayo kila siku na dini huku wote tukifanya juhudi kumtafuta Mungu huyo huyo. Kwenu nyie nasema ‘kun faya kun’ mnisamehe ikiwa neno hili limekosewa lakini ikiwa yeye mwenye kusema kuwa likawa angetaka wote tuwe dini moja isingeshindikana na hivyo muombeni aturudishie mioyo ya subira tujue kuvumiliana na kuchukuliana katika kutofautiana kumwamini kwentu maana Mungu ni mmoja tu hajakuwako mwingine kabla wala baada yake hatakuwako mwingine sasa sisi twagombea nini? Twagombea mapokeo yaliyoletwa na wale walioleta tena kwa maslahi yao binafsi wakituchonganisha ili watuibie? Naapa huo nao ni uduni wetu wa kufikiri na humo miye simo.
Tuombeeni. Wala smituombee atujaze mapesa mifukoni maana amani na furaha ya kweli haitokani na kuwa na mifedha kedekede lakini atujaalie akili njema na uwezo wa kuziona na kuzitumia fursa kujitendea na kuwatendea wengine mema. Tuombeeni atujaalie kujua kwamba yaliyowekwa wazi ni yetu na watoto wetu ili tuyatende nay ale yaliyofichwa ni yak wake ili tumche na kumwabudu na siri ya kwanini Chokoraa namwamini hivi na wewe waamini vile si yetu ni yake tuache kuyachokonoa yasiyo yetu. 

Mwisho niombeeni na mimi ndugu yenu Chokoraa mwana wa Muhangaikaji walau nitengeneze mkate hata kama ni wa unga wa mahindi badala ya kuokoteza kila siku maana akina kaka muishiwa hawataki kunitupia tena vipande vikubwa wanasema nikishiba sana nawapigia kele na hivyo nile kidogo ili nguvu zinipungue wanitawale. 

Ni mimi ndugu yenu, Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika nawasalimu. Ramadhani Karim.Salaam nawasalimia.

Tuesday, July 9, 2013

Udini Tanzania; Viongozi wa Dini Oneni Haya.



Najua, najua kwamba hatutakubaliana wote lakini kwenye hili ni lazima ukweli usemwe na kama hakuna anayeusema ukweli basi tunabaki gizani na si rahisi kusogea na huenda hiki ndicho baadhi yenu mnachotaka, kwamba tuendelee kuwa gizani na ninyi mliopaswa kumulika mishumaa mwaiwasha huku mmeifunika vitambaa vyeusi. 

Tuwe wakweli, Tanzania inatafunwa na ugonjwa mbaya kuliko yote na huu ni ugonjwa wa ‘Udini’ na sina shaka kusema haya ni matokeo ya  matendo na hata maneno ya viongozi wa dini. Nakumbuka kipindi fulani Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania aliwataka viongozi wa dini wasiilaumu serikali kwa kuwapo kwa tuhuma nyingi za rushwa ndani ya taasisi zake kwa vile wala rushwa hao ni waumini wa viongozi wa dini na wako waliombeza, lakini nasema kwa hili Mheshimiwa Mizengo Pinda alisema ukweli isipokuwa tu kwa sababu wengi wa watanzania sasa hivi tunapenda kusikia maneno laini na matumaini matupu kuliko ukweli uumizao, basi alibezwa. 

Kwani ni kipi alichosema Waziri Pinda wakati huo ambacho hakikuwa na ukweli wowote?. Ebu tutafakari pamoja. Ni ukweli ulio wazi kwamba dini inayo athari kubwa ya jinsi ambavyo mtu anaishi na kuishi kunajumuisha kutekeleza majukumu yake ya kila siku akitumia elimu na vipawa vya kimaumbile aliyojaaliwa na mwenyezi Mungu. Hili si jambo la Tanzania peke yake, ni jambo linalogusa hata mataifa makubwa duniani kama Marekani  taifa lenye kujionyesha kuwa kinara wa demokrasia duniani. 

Kwenye gazeti la Los Angels Times la huko Marekani la tarehe 16/03/2007, msemaji wa mgombea urais wa wakati huo  na aliye sasa Rais wa taifa hilo Barak Obama, Bw. Robert Gibbs katika waraka wake kwa waandishi wa habari, aliwaambia wapiga kura kwa kuwahakikishia kwamba Barak Obama alikuwa Mkristo na kwamba hajawahi kuwa Muislamu. Alisema katika waraka huo kwamba “Obama siyo na wala hajawahi kuwa Muislamu” na walio wengi wakajiuliza kama ambavyo wanaendelea kujiuliza leo kwamba je, kama Obama angekuwa muislamu asingechaguliwa kuwa rais?. Je, ikiwa leo rais Obama atatangaza kubadili dini yake na kuwa muislamu basi ataondolewa madarakani? Na kadhalika na kadhalika. Jambo moja ni wazi hata hivyo, kwamba dini inao mchango mkubwa kwenye maisha ya kisiasa ya wanadamu na hatuwezi kuitenga dini na siasa. 

Binafsi naona dini na siasa kufanana kwenye maeneo mengi ikiwamo ukweli kwamba viwili hivi vinaendeshwa kwa misingi ya imani. Ndiyo. Mfuasi wa chama chochote cha siasa anaamini kwamba sera za chama chake na uongozi mzuri wa chama hicho ndiyo msingi wa maendeleo yake na  ndiyo maana anakipigia kura kimtawale. Vivyo muumini wa dini yoyote anaamini kwamba dini yake ndiyo bora kuliko ile ya mwenzake na ndiyo maana anayaacha mafundisho ya dini hiyo kutawala matendo na hata maneno yake.
Kwa hiyo ni sahihi kusema dini ni siasa kama siasa ilivyo dini. Ni ukweli wa kihistoria kwamba kumekuwapo na tawala nyingi duniani kwa karne na miongo mingi zenye kujiendesha kwa kufuata mfumo wa kidini yaani ‘serikali za kitheokrasia’. Katika serikali hizi, huaminika kwamba Mungu (kwa tafsiri ya watu ama jamii inayoongozwa na mfumo huu) ndiye mwenye kuongoza taifa na kwamba kiongozi mkuu wa nchi ni mteule mwenye mahusiano ya hali ya juu na ya kipekee na mungu huyo na hata maelekezo yake kuhusu jinsi ya kutatua migogoro na matataizo ya jamii yake huaminika kuwa yanatoka kwa Mungu. Mifano iko mingi lakini mfano wa jinsi Mussa alivyowaongoza waisraeli kutoka mikononi mwa Farao ama Firauni kama ajulikanavyo na baadhi ya misahafu, unaweza kutuonyesha vyema jinsi dini ilivyo na siasa ndani yake.
Lakini pia Siasa na Dini vyote hufanana kwa kuzingatia kwamba vyote huishi na kufaulu kwa kutumia nguvu ya ushawishi. Neno siasa linatafsiriwa na msomi wa kiarabu iliyo lugha yenye kuchagia maneno mengi kwenye Kiswahili kuliko lugha nyingine yoyote, Shaikh 'Alee Hassan Al-Halabee ya kwamba “ Ni kuhami na linda masuala ya umma”, neno Politics ambalo hutumiwa kumaanisha siasa kwa kiingereza linatafsiriwa kuwa ni ‘uwezo wa kuhamasisha jamii ya watu ama mtu mmoja katika kufikia malengo ya kiutawala”. Hivyo basi ni sahihi kusema kwamba dini na siasa haviwezi kutenganishwa na maisha ya kila siku ya mwanadamu kwa vile tunafanya vyote viwili kwa wakati mmoja tunapotenda majukumu yetu ya kila siku. 

Hayo hapo juu hata hivyo hayafanyi hoja ya waziri mkuu kuwataka viongozi wa dini wajitafakari wenyewe badala ya kuilaumu serikali kuwa na mashiko sana ila mantiki yake kwamba wala rushwa ni waumini wa dini hizi ndiyo hoja ya msingi. 

Viongozi wa dini ndiyo watu wenye dhamana ya kuamua muelekeo wa kidini wa watu wetu, na si hilo tu lakini kama alivyowahi pia kusema Rais wa awamu ya tatu Mh. Benjamini Mkapa kwamba maneno ya viongozi wa dini yanaaminika kuwa maneno ya Mungu miongoni mwa waumini, ni kweli kwamba sisi wengine kwa ujumla wetu tumewaachia viongozi wa dini watuongoze kuhusu masuala mazima ya kidini na bila kuwaingilia na hivyo ikiwa dini leo inageuka kuwa tatizo zito kiasi cha kutishia utaifa wetu, basi wa kulaumiwa wakiwa wa kwanza ni viongozi wa dini. 

Ndiyo, tunawalaumu wanausalama kunapokuwapo na uzagaaji wa siraha za moto na kuhatarisha usalama wa watu na hata usalama wa taifa si kwa kuwaonea bali kwa sababu kwa mwanachi wa kawaida hapa Tanzania hawezi kutofautisha hata milio ya risasi tu kutoka bunduki moja hadi nyingine kwa vile hiyo ni tasinia iliyo na wenye  taaluma, ujuzi na ufahamu nayo ambayo jamii nzima imewaamini na kuwapa jukumu siyo tu la kumiliki na kutumia siraha hizo kwa niaba yetu, bali kuhakikisha usalama wa siraha zenyewe, sasa kwanini mnataka tusiwalaumu wale waliopewa jukumu la kusimamia na kuhakiki usahihi wa mafundisho yatolewayo kwetu wakati jamii  inapohitaji miongozo ya kiimani?. 

Kuwaweka kando viongozi wa dini na kuilaumu serikali kwenye suala la udini ni sawa na kuibiwa mali kwenye ghala na kumweka kando mtunza ghala na kumlaumu muhasibu ati kwa vile tu majukumu yao yanaingiliana bila kuzingatia kwamba mtunza ghala alikabidhiwa majukumu maalumu kutunza ghala hilo hata kama muhasibu anahusika kusimamia matumizi ya rasilimali za shirika. 

Sisemi serikali haina sehemu katika madhila haya yanayoikumba jamii yetu leo, lakini nasema ikiwa kwa namna yoyote wanasiasa wametumia dini kujipatia matakwa yao ya kisiasa na hivyo kuyumbisha mfumo mzima wa jamii kwa kutojulikana mipaka kati ya dini na siasa, si kosa la wanasiasa bali la wanazuoni wetu ambao kwa makusudi ama kwa uzembe wameshindwa kusimamia misingi ya kiimani kuhusu uwajibikaji binafsi wa waumini wao kwa Mungu wao, waumini ambao ndiyo wanasiasa wanaolaumiwa.

Nasema ikiwa kiongozi anawalaumu wale anaowaongoza kwa kushindwa kutekeleza yale waliyopaswa kuyatekeleza, kiongozi huyu ameshindwa kuongoza hana budi kukaa kando awaanchie wengine waongoze.
Yanayojitokeza leo kwenye majumba ya ibaada ni matokeo ya viongozi wa dini kujichanganya wenyewe na kushindwa kusimamia misingi ya utakatifu na heshima kwa Mungu waliyepaswa kumtumikia. Nani haoni vile ambavyo leo mimbari zimegeuka majukwaa ya kisiasa tena yakitumiwa na wanasiasa ambao wana tuhuma nzito kwenye jamii zao wakiwa wamejichafua kwenye ulingo wa siasa na kukimbilia kujiosha kwenye majumba ya dini!? 

Najua wako ambao mtasema si kazi ya viongozi wa dini kuwatenga wakosefu bali kuwapokea na kuwasaidia lakini nasema Mungu mwenyewe hatoi msamaha kwa wasiotubu na hata manabii na mitume walilifundisha hili na hakuna kati yao aliyesema unaweza kumsamehe mkosefu kimya kimya tu bali “akitubu msamehe” na mimi najiuliza hivi watuhumiwa hawa ambao  wamekataa hata kujibu tuhuma zao (japo kusema kweli si tuhuma za kisheria bali za kijamii) na kujisafisha mbele ya jamii na badala yake kukimbilia mbele ya viongozi wa dini ili wawasafishe, watazuiwa na nini kesho wapatapo nafasi kuvurunda tena na kuwataka muwasafishe kama mwanzo?.

Niseme kama alivyowahi kusema Yesu “…chumvi ikipoteza radha yake yafaa nini….” Na mimi najiuliza viongozi wa dini wanaofanya michezo hii wanajua madhara ya kukumbatia watu wenye tuhuma bila kuwawajibisha ma madhara yake?. Najiuliza itakuwaje ama mtamlaumu nani ikiwa tutafika mahala ambapo watu hasa vijana tutakataa kuja kwenye majumba yenu ya ibada kwa vile kumbe huko nako ni kunajisi kama ilivyo kwenye siasa na badala yake kuamua kubaki nje kwa vile ndani na nje kote kunanyesha na hivyo ni bora kulowa huku ukitembea maana mwisho utakuwa umesogea hatua kuliko kuloa ukiwa mahala pamoja?.
Viongozi hawa wa dini ndiyo wanaoshadidia mafundisho yenye kusababisha mitafaruku mikubwa kwenye jamii yetu na si ajabu kwamba leo vijana wa kitanzania ni wazalendo zaidi kwa dini zao kuliko walivyo wazalendo kwa jamii yao. Si ajabu vijana wengi wa kitanzania wanaamini jamii yao ni wale wenye imani ya kidini sawa na wao na wale wenye imani tofauti si sehemu ya jamii yao na hivyo hakuna ndani ya akili za vijana hawa ile iliyojulikana miongoni mwetu kwa miaka mingi kama jamii ya Kitanzania.

Pita kwenye mahubiri na mihadhara mingi utawasikia viongozi wa dini wakiwahubiri vijana wao juu ya umuhimu wa kujitazama kwa “wao” kwa maana ya dini zao badala ya kutumia mwanya wa kuwafundisha imani ya dini ili kuitumia kutatua matatizo yao na jamii zao. Yako mabaraza mengi ya kidini nchi hii na yote yamengukia kwenye mkumbo ule ule. Si mabara ya maaskofu wala masheihk yanayochukua hatua kuwakemea wajinga wachache, natumia neno wajinga na si wapumbavu, wanaojaribu kueneza chuki miongoni mwetu na ndiyo maana kukawa na wachungaji wenye kutumia vituo vyao vya redio kutukana na kupandisha jazba waumini wa dini nyingine hadi serikali ilipoamua kuvifungia. Nauliza wakati wote wahubiri hawa wanahubiri sumu hizi ndani ya jamii yetu, mabaraza ya kidini ya dini hizi yalikuwa yakifanya kazi gani!? Kwani jukumu la mabaraza haya ni nini kama si pamoja na kuhakikisha kwamba mafunzo ya dini hizi hayapotoshwi?. 

Kwani wale waliojiita masheikh waliokuwa wakiendesha mihadhara yenye kuchochea chuki na kusambaza CD za chuki hizo walikuwa kwa namna yoyote hawawajibiki kwa mabaraza ya kidini? Mbona viongozi wa mabaraza hayo wasikemee upuuzi huo hadi damu zimemwagika ndipo ati polisi inawatafuta na wao kukimbilia nje ya nchi?. Najiuliza je, viongozi wa kidini wanafurahishwa na  mafundisho haya yenye kuibomoa jamii yetu? Kwa faida ya nani!?

Ni unafiki. Ni unafiki leo viongozi wa dini kusimama na bila aibu kuilaumu serikali kwamba ndiyo inayochochea udini wakati dini ni tasnia pekee ambayo kwa miaka mingi haikuingiliwa na serikali ndani ya nchi hii hadi pale wenyewe wanaposhindwa kuendesha mambo yao na kusababisha vurugu. Ni ajabu kwamba hata inapofikia hapo bado serikali inapoingilia utawasikia viongozi hawa hawa wakilalamika kwamba serikali inaingilia uhuru wa kuabudu wakati wameshindwa kuutumia uhuru na kuufanya kuwa uendawazimu. Maana uhuru usio mipaka ni uendawazimu. 

Wakati viongozi wa dini wanapojitafutia umaarufu kwenye vyombo vya habari kwa kuzungumzia masuala yasiyowahusu kana kwamba wao ndiyo wasemaji wa taasisi za umma ama kujitokeza kwenye vyombo vya habari kuzitaka taasisi za umma kujibu hoja zao na bado wakaendelea kudai wasiingiliwe uhuru wao wa kuabudu, binafsi ninaona kama wameiondoa ibada kwenye milango ya mahekalu na masinagogi na kuipeleka kwenye malango ya ikulu jambo ambalo ni kinyume na katiba na ni kuingilia uhuru wa taasisi nyingine.
Wako ambao hadi leo wanalalamikia kauli za kiongozi mmoja wa dini ya kikristo kufuatia vurugu za Mwembechai mnamo February 13, 1998 ambapo baada ya vurugu hizo, kiongozi mmoja wa dini alijitokeza mbele ya waandishi wa habari akisema “jeshi la polisi halikutumia nguvu kubwa bila sababu na kwamba ilikuwa sahihi kutumia siraha za moto kwa sababu raia(akiwataja kwa dini yao) nao walikuwa na mawe na kwamba mawe nayo yanaweza kuua….”. Ni kauli za jinsi hii na zifanazo ambazo zimechangia kuchochea migogoro ya kidini kufikia hapa ilipo leo kwa sababu kiongozi huyu hakupaswa kwa namna yoyote kusema aliyosema hata kama yeye aliamini ni sahihi na hata kama kwa mujibu wa katiba anao uhuru wa kutoa maoni yake, lakini alipaswa kuzingatia nafasi yake na kutafakari madhara ya yeye kutoa maoni hayo maana hekima ni uwezo wa kusema neno sahihi, mahala sahihi kwa wakati sahihi na kwa namna sahihi. Ikiwa utanisalimu salamu ya asubuhi wakati wa machweo, utakuwa umefanya kitu sahihi kwamba umenisalimia, ila utakuwa umekosa hekima kwa kunisalimu salamu ya asubuhi wakati wa jioni. 

Ni wakati sasa viongozi wa dini wajichunguze na warudi nyuma kufanya mambo kadhaa waliyoyaacha. Viongozi hawa waache kukubali kuwa daraja la wanasiasa na wahakikishe kwamba wanawaunga mkono wanasiasa katika mambo ya maendeleo lakini pia wapime upepo na kutazama sifa ya mwanasiasa katika jamii na ni lazima wahakikishe kwamba wanasiasa wanajua kwamba ikiwa watajichafua kwenye utendaji wao, dini hazitakuwa mahala pa kujisafishia. 

Viongozi wa dini wakemee watu wanaoibuka kila leo na kufundisha mambo yaliyo kinyume na upendo na amani na hata mshikamano wa watu wa jamii yao badala ya kuingia kwenye makundi ama kuoneana aibu ati kwa vile huyo anayekosea ni wa mlengo wa dini yangu na hivyo siwezi kumkosoa hadharani. Ni lazima viongozi wa dini wanaopotoka kutoka kwenye misingi ya kidini na kuvunja hata sheria za nchi kwa mahubiri ama mafunsidho yao wakemewe na viongozi wenzao wa dini na ikibidi hadharani ili dini zirudi kuwa mahala ambapo mizaha ya hatari haiwezi kuruhusiwa kamwe. 

Ni lazima tuache kuwashabikia watu wenye kufanya vitendo vya kipuuzi na kuumiza binadamu wenzao ati kwa kisingizio cha dini lakini pia tusiwakalie kimya na kisha kusimama tukijiosha kwamba hao ni “wahuni” maana wanachofanya hakikubaliki na dini, ni lazima tuseme hadharani mapema kwamba hawa wanachofanya hakikubaliki na tuwapinge badala ya ama kuwavisha mavazi ya heshima ama kuwakalia kimya hadi serikali inapoonyesha kukasirika ndipo ati na sisi tunaibuka na kauli za kujiosha. 

Viongozi wa dini walinde heshima ya mimbari na pia wasimame ndani ya mipaka yao badala ya kujitwalia mamlaka ya kusema kuhusu kila kitu maana miluzi mingi humpoteza mbwa na ni busara kunyamaza kuliko kusema ikiwa kusema kwenyewe ni kwenye kuchochea moto unaochoma nyumba tayari. Ikiwa bado viongozi wa dini mnataka kujiingiza kwenye siasa na kisha kuwalaumu wanasiasa mi nadhani ni wakati sasa mfike mahala muone haya kwa haya yanayotokea. 

Ni mimi ndugu yenu Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika, nawasalimia. 

Friday, June 28, 2013

"SHIKAMOO" MKULU WA GUNIA.



Shikamoo Mkulu wa Gunia. 

Shikamoo si salaam mwana wa Muhangaikaji  nilikataa tangu zama ila sasa, shikamoo mkulu wa gunia. Nasema shikamoo si kwa kukuamkua maana ningekuamkua ningesema salaam nakusalimia lakini nasema tena kwa sauti ya juu unisikie ijapo kusema kweli akina kaka Muishiwa wamenifungia juu ya dari ya nyumba tena kwenye paa la choo ili nisionekane mbele yako, ila naamini sauti yangu itakufikia ewe mkuu wa gunia hili tambala bovu tuishilo sisi wana wa Adamu, shikamoo mkulu wa gunia. 

Ha ha ha ha ha ha!!! Nimekumbuka zamani enzi zile wakati wazee wangu hasa mama yangu Shida wa Matatizo wa Taabu Malingumu alipokuwa akiniamsha lukwiri ili niende huko kwenye jando la kikoloni kufundwa ujinga wa kuidharau ‘ilimu’ ya babu na babu zangu kwa kuuita ushenzi ilhali tamaduni za mgeni zikiitwa uungwana, hilo si lengo la waraka huu, shikamoo mkulu wa gunia. 

Nakumbuka enzi hizo ikiwa Mkulu wa kaya ama wasaidizi wake walitembelea kijiji chetu, wote tuliambiwa tuoge, tuchane nywele zetu kwa mitindo ya kurithishwa na wakoloni wenyewe ati wakiita ‘kisasa’ bila kuheshimu ukweli kwamba hakuwezi kuwapo na sasa bila zamani na mjukuu ni matokeo ya babu, humu namo simo ila, shikamoo mkulu wa gunia. 

Tulijipanga mabarabarani na enzi hizo barabara zenyewe zilikuwa za vumbi tupu na ole wetu ikiwa ulikuwa msimu wa mvua na siye na shati zetu nyeupe kwa weupe wa mkorogo, letu lilikuwa tope na maji machafu wakati walinzi wa ‘mkulu wa kaya’ wakipita na magari yao na siye tukijitahidi kupunga mikono na kulazimisha tabasamu nasema enzi ni enzi na kumbe historia hujirudi, shikamoo mkulu wa gunia. 

Mkulu wa Gunia, mwana wa wana wa Hamu ndugu wa Shemu na Yafethi kwa mujibu wa misaafu iliyoletwa na wale uwatawalo leo, nimemua kupaza sauti kwanza nikukumbushe japo najua wajua ya kwamba shikamoo humaanisha niko chini ya miguu yako na hilo ndilo ninalotaka kukwambia leo, niko chini ya miguu yako na kusema kweli unanikanyaga. Sikulaumu. Wala! Hata kidogo. Nani kasema nakulaumu? Miye sikulaumu kwa vile kama walivyofanya babu zako ambao walipokuja wageni wenye pua ndefu na tabasamu za unafiki uonekanao kama urafiki, waliwakuta babu zetu wakiwazika machifu mikononi mwa walio hai na waliozikwa hao ati kumsindikiza chifu kwenye safari yake ya mwisho walikufa kwa ujasiri ati kwa vile walikuwa mashujaa na mimi ni shujaa mtukufu mkulu wa gunia. 

Mimi ni shujaa ila si shujaa wako bali shujaa wa kaka Muishiwa kwa vile tangu ulipotangaza kwamba waja huku kwetu mimi niko chini ya miguu yako na hata mkate wa wanangu niliokuwa nimeukumbatia kifuani kwangu nao sasa umesagika kwa kule tu mimi kuwa chini ya miguu yako. 

Ha ha ha ha ha ha!!! Usitake nikutajia jina la marehemu bibi yangu mzaa mama yangu wewe aliyeniambia mbwa mwitu na mbuzi hukaa kundi moja tena bila kuchokozana ama kuogopana Simba anapoingia kichakani na sasa kwa sehemu nasadiki.

Ati! Nasema uji wako kwenye ardhi ya wadanganyika walipa kodi umenikumbusha mambo mengi mojawapo ni mzee yule aliyekuwa mwenye kigoda cha kijiji chetu. Pamoja na kuwa mtu mkubwa sana wa enzi zake lakini hakuwa na shati hata moja lisilo na tobo mabegani na siku moja Mkufunzi alipotembelea darasa lake na kuamua kukagua usafi, yule mzee kwa vile alijua Mkufunzi angekagua mavazi alikuwa amevaa koti zuri juu ya shati lake ila kwa vile mkufunzi alipoamuru huyo mzee avue koti lake ndipo tukagundua kumbe mabega na mgogo vilikuwa wazi. Ha ha ha ha ha ha!!! Nicheke kama mazuri Chokoraa miye. 

 Najua!!! Najua, najua unashangaa kusikia Mkufunzi alitutembelea na kumvua yule mzee shati lake kwenye ukaguzi wa usafi wakati unajua mkufunzi huwa anakagua wanafunzi pekee ila ulichosahau ama kudharau ni kwamba wakati huo kaya yetu yote ilikuwa shule na mkufunzi alikuwa mmoja akituongoza kama Mussa na Israel hayo unayajua kwa hiyo , shikamoo mkulu wa gunia. 

Wacha nikumalizie kisa hicho halafu ninyamaze maana najua akina kaka Muishiwa kwa sasa wamenuna ati Chokoraa nampigia kele mgeni na ndiyo maana ati kwa vile miye siujui ‘ustaarabu’ wamenikataza kuja mjini. Mkufunzi baada ya kumvua koti yule mzee na kumkuta amevaa shati lililochanika akaamuru atandikwe viboko sita pale pale na mimi nikajihoji, kwanini kumtandika mtu aliyejaribu kujiheshimu mbele ya mgeni!? Mkufunzi akanisikia wakati najihoji inawezekana nilijisahau nikawa nazungumza kwa sauti, akaniita mbele. Weeeee! Hukuwapo maana ungecheke sana jinsi nilivyokuwa nikitetema.

 Nilijua leo na miye vyangu sita ninavipata lakini mzee yule Mkufunzi alikuwa heshi visa, ati akaanza kunifafanulia Chokoraa miye ni kwanini alimtandika mzee yule viboko sita. Akasema kwa kitendo cha mzee yule kuficha shati lake lililochanika, mkufunzi angeondoka kijijini ameridhika kwamba mambo yako barabara maana hata mwenye kigoda kava suti kumbe ndani malapulapu na hivyo asingetuma tena “kilimpilini” pale kijijini mwaka huo labda baada ya miaka sita na hivyo aliamua kumtandika kwa vile mwenyekigoda alimficha ukweli wa mambo. Ha ha ha ha ha ha!!! Natamani na wewe mkulu wa gunia ungekuwa na busara ya kujua kilichojificha nyuma ya jiji safi unalolipitia unapotokea kwenye stendi ya mwewe! Lakini waaaapi! Kwani watakwambia!?.

Hata wakikwambia kwani utawafanyaje zaidi ya kuwapongeza kwa juhudi ya kusafisha jiji? Nasema uchafu waliouondoa ni mimi na ndugu zangu akina Seremala, makenika, machine na yule Ntilie, mdogo wake na mama yao Mama Lishe, na miye nauliza, kwani sisi sasa ni takataka kwenye kaya yetu wenyewe ati kwa ajiri ya ujio wako? Naomba kujua unaoga maji ama maziwa!?. Ila bado zijajiinua wasijeniangushia vitu vilipukavyo, bado niko chini ya miguu yako mkulu wa gunia. 

Nasema kumbe ukweli na uwazi ni mchezo mgumu kuucheza na yawezekana wanaohofia na wanachokihofia miye nakijua. Ati! Sikia huyu naye! Ati wanahofia usalama wako? Nani kasema! Hawana mashaka na usalama wako maana kama wao wenyewe tu wako salama iweje wewe na maguvu yote uliyo nayo na ‘utukutu’ uliojifunika nao usiwe salama katika kaya ya amani na utulivu!? Na huyu, ati wanahofia maandamano na si hasa!? Hilo nalo si kweli maana hayo yaweza kutokea popote na vyovyote ila wadanganyika siye hatuna kawaida ya kuwafanzia fujo wangeni kuuana twauana wenyewe lakini mgeni yuko salama.

 Wanachohofia mimi nitakwambia ijapo najua ukiondoka nitakiona cha mtema kuni. Ndiyo, ukiwapo hawanigusi kwa vile, niko chini ya miguu yako. 

Wanaogopa usije ukawauliza zile shekel, noti na mifedha kedekede uliyowapa walete kuboresha maisha ya wadanganyika imefanya nini ikiwa miaka hamsini ati baada ya bendera bado wadanagnyika wanaishi chini ya nusu dola kwa siku!? Nani kasema wanaishi chini ya dola moja? Kwani dola moja si sawa na “si nyingi” zetu harufu mbili! Naapa wako wadanganyika miongoni mwetu ambao wanaamka na kuzitafuta “si nyingi” tamo mia na wasizipate hao wanaishije chini la dola moja!?.  Wanaogopa utawauliza kuhusu magari yao ya kifahari wanayoendesha ilhali mama Ntilie na Machinga hawajui watakula nini na hivyo wanapotuondoa akina siye mjini utakaoukutana nao ni “wao” na hivyo hutojua kundi la akina siye tuko wapi na kuondoka ukidhani na “sisi” ni kama “wao” kumbe pana tofauti kubwa. Natamani kuendelea kusema lakini naonga kama uzito wako unaongezeka na mimi pumzi zinapungua kwa sababu, niko chini ya miguu yako. 


Wasalaam, ni mimi Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahio wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika nakusalimia. Shikamoo Mkulu wa Gunia.

Thursday, May 23, 2013

Kaka Mkulu wa Kaya, Salaam Nakusalimia.



Kaka  Mkulu wa Kaya, salaam nakusalimia,
Nasema kuwa huru si rahisi kama ilivyo si rahisi kuwa rais na sasa Chokoraa nawasalimia. Kubadili majalala huku kuna siku nitaingia kwenye jalala la tindikali naapa kwa jina la bibi yangu mzaa mama yangu Shida wa Matatizo msinihusishe. Nasema msitake niseme kwa mtiririko maana yaliyonijaa kwenye koo ni mengi na njia ya ama kuyameza ama kuyatema ni ndogo na hivyo wacheni niyatapike liwalo na liwe maana ni bora moja kuliko sifuri na humu miye nahusikaje!?. 

Kwani nani kaiona ramani ya kaya yetu, ile ramani halisi ya Danganyika ya Wadanganyika tuliyoachiwa na wazee wetu kabla haijabadilishwa na hawa wenye kujitangazia uhuru kila uchao kisa “uhuru na haki za raia” na mimi nauliza ni nini uhuru na haki za rais na kwa hili mnitoe maana simo. 

Kaka mkulu wa kaya, nimetumwa na wadogo zangu akina Muuza Mayai na Karanga, na hata mama yangu mdogo Mama Ntilie kanituma nikusalimie.  Hawa wawili wanasema wanakumbuka kabla ya kufariki baba wa kaya yetu na kabla ya wewe kuteuliwa na kikao kilichopita cha ukoo kuwa Mkulu wa Kaya na kuongoza kundi la akina kaka Muishiwa wa Maadili na Kiongozi Mbadhilifu katika kuiwakilisha kaya yetu hii, tulikuwa sisi wote ni wamoja watoto wa mzee Mdanganyika Mlipakodi na mama yetu Bi Mzalendo.  

Ati wanasema baada ya kufariki baba yetu, kundi lenu likiongozwa na akina kaka Muishiwa walimpendekeza kaka yenu mkubwa Mtukutu kutuelekeza kule yalikofichwa maisha tarajari ya kaya yetu na ati baada ya siku chache kaka yetu huyu kujitangaza kuwa ‘Mtukufu’ watu wakaogopa lakini kwa vile ati kilikuwa kizazi kilicholelewa vyema na marehemu baba yetu kwa kutohoji yale yafwanywayo na wale wenye kuvaa lile joho lefu la baba na wenzake lenye rangi ya Kiongozi, basi wakakaa kimya. Hata hivyo yale yaliyotendeka ati yalitendeka na hata akina Mlalahoi wakaanza kujenga maghorofa kwa kuuza vitunguu swaumu nisikuchoshe na historia, salaam nakusalimia. 

Baadaye ndipo kijiti alipopewa kaka mkubwa Muishiwa. Wanasema ati huyu naye kwa sehemu alizingatia sehemu ya mafunzo ya marehemu mama yetu Mzalendo binti Mdanganyika ijapokuwa ni kweli kwamba yeye kijiko chake kilikuwa kikubwa maakulini ukizingatia na sisi wengine, lakini walau alijenga daraja na siyo ukuta, nasema nisikuchoshe ila salaam nakusalimia. 

Sasa kuna Yule dada yetu mkubwa ambaye hasa ndiye aliyenifanya nikuandikie waraka huu hasa kwa vile binafsi naweza nisipate nafasi ya kuonana na wewe mwaka huu, si kwa sababu sipendi ama ati kwa vile naogopa wale walinzi wako kama mjomba, lah! Bali kwa vile lile daraja kutoka huku kwetu kuja huko kwenu lina mushkeli kidogo hasa baada ya juzi tu wadanganyika kuchoshwa na kuamua kutenda watendavyo mradi iwe iwavyo, salaam nakusalimia. 

Nasema watu wakichoshwa ni heri ya punda mzee kubeba mzigo yeye na mwana kuliko mtu ama aliyeshiba mema au asiyekula kabisa maana wote huwa na wazimu kwa sababu tofauti na mimi humu sihusiki. 

Dada yetu mkubwa Mjasiriamali ameniagiza nikusalimie na kisha nikueleze kwamba kwake yeye ijapokuwa hapendi hata kidogo jinsi ati unavyotuhumiwa kwa mjomba na shangazi kuwa na sauti nzito kuliko wewe kwenye  kaya yetu, lakini walau alikuwa bado angali na imani na ile “Siri kali” labda kwa vile ilikuwa imefichwa na haikujulikana kwake na hivyo si kwamba aliiamini “Siri kali” bali aliamini kwamba kuna siku na yeye atakuwa sehemu ya wale wenye kuifahamu siri hiyo ifichwayo kwa udi na uvumba na hilo linanifanya salaam nakusalimia. 

Anasema baada ya hivi majuzi watu wasiojulikana kujitangazia mamlaka bila madaraka na kuufunga mji wa Mtwara tena pasina kupata upinzani wowote kutoka kwa walinzi wa “Siri kali”, dada yangu mjasiriamali amejiuliza maswali kadhaa ambayo machache yake amenitaka nikuulize na mimi sasa nakuuliza; Hivi ni kweli kwamba ile “Siri kali” yetu imevuja na sasa kila aliyeko nje anaona ndani kama aliyeko ndaniaonavyo nje!? Nasema usijesema miye sina adabu ninazo tena tele lakini najiuliza inawezekanaje kwamba genge la “wahuni” linafunga mji kiasi Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika na hata dada yangu chakaramu Mjasiriamali hatuwezi kutoka ndani na kwenda kuokoteza mkate wa siku? .
Samahani unisamehe, si hoja yangu ya msingi ikiwa ni sahihi kwako kujenga njia ya panya na kupitisha gesi, oil ama mafuta hiyo kwangu si hoja. Nasema yafaa nini mimi kuhoji ikiwa hilo ni sahihi ama si sahihi ikiwa mimi Mdanganyika sina haki wala hadhi ya kuhoji usahihi ama tafsiri ya usahihi wenyewe?.

Kinachonikera mimi na dada yangu Mjasilia ni kwanini na hasa inawezekanaje kwamba ‘watu wasiojulikana’ wanaweza kufunga mji na biashara zake zote na hadi sasa wakawa bado “hawajajulikana”?.   

Ati! Utani wa kuniambia tena ati ni “kundi la wahuni” wanaohatarisha maisha ya wadanganyika wa Ntwara tafadhali tuuacheni maana wahuni hawa sasa wamepevuka mno kutoka daraja la kawaida la uhuni sasa wanaelekea kuwa ‘waahini’ na mimi humo sihusiki. Hivi inawezekanaje kwamba watu ‘wasiojulikana’ ama “wahuni” kama ambavyo baadhi yenu mtataka nisadiki, kwa kutumia ‘vikaratasi’tu  wameufunga mji na biashara zote kusimama?. 

Nasema kwa hili msinihusishe hata kidogo. Haya, ebu niwaze kichokoraa. Hivi wakati ‘tanchi’ la kwanza lilipopigwa, vipeperushi si vilikuwa vimeanza kusambazwa tangu jumatatu na tanchi lilipigwa ijumaa! Nani kasema unahitaji ‘kadigirii’ kujua kwamba hapo katikati kulikuwa na jumla ya siku tatu nzima na jumla ya saa sabini na mbili za kuwasaka na kuwatia ‘mtaroni’ agha! Samahani, kuwatia mbaroni ‘wahuni’ wanaoongoza vitendo hivi!? Hivi siku hizi wale ‘sungusungu’ wako wa kaya nao wamekuwa butu hawana meno kazi yao imebakia kututishia siye vitukuu wa mdanganyika lakini linapokuja suala la usalama wa kaya nao hawajui cha kufanya!? Kama ni kweli wanafanya kazi “araundi ze kloku” kama msemavyo ninyi, nini kilifanya hadi ‘tanchi’ la ijumaa 17 likatokea? 

Ha ha ha ha ha ha ha!!! Nicheke kama mazuri. Kwani hamkujua kwamba kwa kuruhusu watu hawa ‘wasiojulikana’ kuufunga mji siku moja mliwatumia salaam kwamba wanaweza kufunga mji wakati wowote watakao! Haya sasa wameanza kuufunga kila wanapotaka na mimi humu sasa nahusikaje?. 

Haya, hili sasa limekwishatokea. Lakini hivi ni kweli kwamba wale wanaohamasisha vurugu hizi wanatumia maneno matupu kama mnavyotaka niamini miye kitukuu wa Pangupakavu!? Naapa humu miye sihusiki. Nakataa kuhusika maana ikiwa ni uhafidhina wangu ama ni kweli waliyosema wale waliosema kale, basi “maneno matupu hayavunji mfupa” sasa nyie mwaniambiaje ati wanaoshawishi vurugu hizi wanasema maneno matupu yasiyo mashiko!? Sasa mbona mfupa unanjika!? Nitoeni nasema. 

Au mwataka niamini upinduzi  kwa kutumia ‘propara lenye maganda’ kwamba  wadogo zake na Nchumali wa Chipoku ni wachoyo wa ‘asili mali’ zilizoko kwenye ardhi yao ilhali wao wamefaidi za wenzao? Nasema na kwa hili mnitoe. Haya, basi tumieni wingi wa busara mlizojaaliwa na hata tukawaamini kuwavisha majoho mvaayo kujibu walau kwa kiwango cha uelewa wao ni kwanini viwanda vya sangara viko Mwanza, migodi ya Dhahabu iko Geita na Mara na viwanda vya Pamba na Kahawa viko mahala pa mazao hayo lakini vile vya kusindika Gesi vyajengwa huko kwingineko!? Sisemi hamna majibu ya swali hili, lakini yatoeni basi na kwa namna ya kueleweka hili na mimi nisishangae kama ninavyoendelea kushangaa. Bhaaaaa!! Mwanishangaza enyi wana.

Nasema mzaha mzaha hutumbua usaa, au kwa vile ninyi ni wa kisasa mwaamini mzaha mzaha huwafanya watu kucheka na hivyo kuongeza siku za kuishi!? Naapa ninyi ni kizazi cha wenye hekima na mtakapokufa ninyi basin a hekima nayo itakoma na humo nitoeni. 

Haya, nijuzeni na nyie wenye kufunga mji mwamkomoa nani!? Nasema hawa waliishauza nafsi zao na konzi la kifaranga halimuumizi Kicheche enyi wana. Kwani mnadhani ikiwa mmefunga bishara na kuharibu uchumi wenu kwa siku kadhaa ndipo mmeweza kuwakomesha hawa ‘wezi’ wenu? Naapa wao walikwishashiba halali na mlungula kilichowasalia wao ni heshima na uishiwa na labda kesho ya vizazi vyao ambayo wao wanakusudia kuipata iwe kwa kumaliza vizazi vyenu ama kuharibu kesho ya wanenu, basi tumieni busara badala ya mabavu ilhali mli hali dhoofu kwa kula kidogo na kutenda kazi sana. 

Wacha niyamaze miye maana nasikia kaya yetu hii mama mkwe akitembea uchi unaruhusiwa tu kuwaza kwamba mama mkwe yu utupu lakini ukisema hivyo dhambi. Ati! Kwani mnadhani kama kweli mngekuwa mnaitia mafuta bawaba enyi wenye nyumba, zingetoka wapi kele za mlango ijapokuwa kusema kweli haziwakoseshi usingizi!?. Simo nasema. 

Basi kaka yetu, mkulu wa kaya hii ya Wadanganyika walipa kodi. Wacha nikomee hapa nikatafute sehemu ya kuegesha kichwa changu maana lile pagala nililokuwa nikilala juzi na jana mmelibomolea mbali wakati wenye “siri kali” mlipokuwa mkipambana na “wahuni” katika kujaribu kulinda “siri kali” yenu isivuje pasina kujiuliza kinachoivujisha ni sakafu iliyoloa ama tundu kwenye chombo chenye kutunza “siri” yenyewe?. Ama kweli fahari wawili wapiganapo, ziumiazo nyasi na mara hii Chokoraa nimekuwa nyasi kavu kwenye uwanja wa vita vya fahari wa Faru na Sisimizi. Simo.

Salaam Mheshimiwa, ni mimi mdharauliwa wako Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika nakusalimia.