Tuesday, May 1, 2012

Ama kweli hamna adabu enyi wana.


Najua! Najua umekuwa muda sasa tangu nimepitia kijiweni hapa walau kukusalimia na si kwamba nilikusahau, ila nilikuwa kwenye ule mchezo wa sasa ambao kila mtu ni lazima acheze tangu mdogo hata mkubwa, maskini ama tajiri, msomi kama wewe ama mbumbumbu kama Chokoraa, nao ni mchezo wa kuwa “bize’. Naapa simo. Si kwamba simo kwenye mchezo wenyewe, isipokuwa kwa vile wako ambao wako ‘bize’ kila siku na wapata chochote kitu ilhali wengine wako ‘bize’ waambulia umaarufu wa harufu, humu namo simo. 

Ha ha ha ha ha ha!! Nicheke miye Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangu pakavu wa Kabwela wa Mdanganyika si kana kwamba nina furaha, lakini nani kasema hii “gunia” yetu ni kama ile ya babu yangu Pangu pakavu ambapo walioweza kupata habari, wachilia mbali walioweza kutoa habari walikuwa wachache sana na wenye daraja fulani katika jamii!!? Washangaa nini! Nakumbuka miaka hiyo kulikuwa na vyombo vichache sana vya habari na vyote vilikuwa kwenye ‘siri kali’ vikitumiwa tu na ‘watwawala’ kuwapelekea amri ‘watwaliwa’ na hata sheria ikaweka kwamba ili iwe sheria ni lazima kwanza itangazwe kwenye gazeti la ‘siri kali’. Ha ha ha ha ha ha!!! Leo watu wasema na sisi kupitia ‘ubunifu wa Buibui’ na mwana wa Muhangaikaji nasikika kupitia kamchezo hako ka mdudu Buibui na bado wataka ati nisicheke! Simo humu.   

Haya, wacha basi nikupe pole kwa msiba maana siku hizi kwa ajiri ya wadanganyika woote kuhama mitaani na vijijini kwao wakishinda “bize” na kurudi jioni ama usiku mwingi, basi utamaduni wetu umebadilika na hata misiba haihudhuriwi kama ilivyokuwa zama na ndiyo maana hata Chokoraa sikuwa nimepata nafasi ya kukupa pole ya misiba. He! Ona huyu ati hajui kwamba kwenye ‘inji’ hii tumepata misiba mikubwa kadhaa na ya kitaifa kwa sababu ati naye alikuwa ‘bize’ kiasi cha kushindwa kusoma ‘udaku’ na kutazama kasanduku ka picha ama kusikiliza ile radio ya mwenyekigoda wa kijiji chao, hata alipoingia kwenye makaazi ya Buibui yaani ‘mtandaoni’ hakupata nafasi ya kusoma ‘niuzi’ zaidi ya kupata ‘esi emu esi’ kadhaa kwa BBM na kuishia kulala ili adamke mapema na kukimbilia ‘bize’, naapa utamaduni wa binadamu unafirisika kila kukicha na humu simo. 

Nasema mnitoe kwenye huu mufirisi wa ustaarabu wenu enyi wadanganyika maana mtu asite utamaduni ni mfungwa wa kifungo cha nyumbani walau hivyo ndivyo nijuavyo Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi na kwa hili naapa tutashindana sana lakini simo. Hivi si ulikuwa utamaduni wenu enyi wadanganyika wa kuheshimu watangulizi wenu iwe ni wazazi nyumbani ama viongozi kwenye hizo ‘siri’ zenu ‘kali ‘ na hata mlikuwa na ‘proto kali’ ya kutokunywa kahawa kama mwenyekigoda hajafika? Nasema huo unaoonekana kama upuuzi kwenu ninyi masharo wa sasa ndiyo ulikuwa misingi ya uzalendo wa watu wa  inji hii na hata kujitolea kufa kwa ajiri ya ‘udanganyika’ wao kwa sababu walau walijua ‘legasi’ yao ingebaki. Sasa naapa kila mmoja anataka kuwa “msanii” na nimtumie pole ‘mzee wa ukweli usio wazi’ kwa juhudi zake za kutaka ati kuifanya ‘danganyika’ yake isiitwe tena ‘bongo’ kwa vile ati ‘usanii’ ulizidi. Nani anataka kuwa ‘hiro ov ze nesheni’ (naonyesha msisitizo) kwa kutumikia inji hii ilhali anaweza kuacha ‘ligasi’ kwa watoto wake kwa kuwa muuza sura luningani nasema mnitoe. Ati wakulu wote wa kaya wakajikusanya na kujirundika kwenye msiba wa ‘msanii’ na kuishushia heshima ya ‘kiifitaki’ misiba ya mashujaa wa inji hii hadi wale walioliongoza ‘geshi la waheshiwa tangu zamani’ naapa humu simo. Nasema kwa hili Chokoraa nitasema na kurudia kwamba adabu si shikamoo na uungwana ni vitendo, kizazi hiki kimekosa adabu kwa watangulizi wake na namuomba jalali awajaalie mzeeke ili muone jinsi inavyoumiza kwa kizazi kinachofuata baada yenu ‘kuikanya legasi’ yenu chini ya nyao za miguu, siyo nawalaani nawaombea maisha mema na ya neema ila kwenye hili la dharau mimi simo, tena simo kabisaaa. 

Nasema kama mgekubali kuwa wanafunzi mgejifunza maana waalimu wako wengi waliotenda vyema kabla yenu ili muone na kujifunza kwao lakini nani kasema adabu inauzwa ama hukwanguliwa kama vocha!? Naapa simo. Ala! Kwani wakati ‘mzee wa kuruhusu’ alipoamua ‘kushtuka’ (naogopa kusema kizanaki msijesema natumia vibaya lugha ya taifa) na kujiweka pembeni ‘kuepusha msongamano’ ilimnyima nini kuwa ‘mkulu wa kaya’ wakati ulipowadia!? Au ni kwa sababu ninyi sasa mmeendela sana na mnaamini “riziki kama ipo ichukue kama haipo ilazimishe” na hivyo mwaona kung’atuka ni aibu?. 

Labda ni kweli kwamba hamna heshima kwa ‘wazee’ wenu tena enyi wana wa danganyika maana nani hakusikia wakati mlipowatazama usoni wazee wenu na kuwahoji sababu ya wao kutotumia hayo mawazo mazuri wanayokupeni kipindi cha ‘wakati wao’ mkisahau kwamba wakati ukuta?. Naapa mna zaidi ya kiburi enyi wana. Nasema kama ilivyokwisha kusemwa kwamba sokoni hupatikana vyote yaani chakula na uchafu na cha pili si aghali kupatikana kwake japo matumizi yake ni adimu na ninyi mmejifunza kwa watangulizi wenu lakini kama waenda sokoni mmechukua uchafu mkaacha chakula ashakumu si matusi, humu simo. Ala! Kwani si mmeamua kwa makusudi kujifunza kwa wale waliojitokeza hadharani mbele ya visanduku vyetu vya picha, tena tunavyoviwasha kwa umeme tunaoulipia sisi wakitwambia wala si kutuomba kwamba tugeuke mbuzi na ng’ombe tule nyasi lakini wao wanunue “mwewe” kwa ajiri ya ‘mkulu wa kaya?”. Nasema mmejifunza kwa hao na mmefaulu na humu mimi nakataa kuhusika, simo tena simo kabisa.
Ni hivi juzi tu, mlikulana na kuparurana makucha huko kwenye jumba la maamuzi na kutaka hata kuvuana nguo na wala hii si mara ya kwanza ama ya pili walau kwa siku za karibuni, lakini tofauti na mwanzo wakati watu walipojipachika majina kama “Bangusiro’ na mengineyo, ninyi mmekataa kuwa ‘mbuzi wa sadaka’ na badala yake mmekuwa ‘ngangari’ kwenye kuendeleza ‘yale yote ambayo kwa moyo na nia thabiti mmekuwa mkiitendea inji hii’ na kwa hili nakupongezeni ila mi mnitoe maana simo. Naam, mioyo na nia zenu ni thabiti katika kutenda lakini mnatenda kama waenda sokoni maana pana faida gani kuendelea kuonyesha njia mbele ya mtu ambaye hayuko tayari kukufuata?  Naapa nilidanganyika. Ndiyo, ni uzembe wangu kwamba nilidanganywa nikadanganyika kwamba kiongozi wa domo daraja la kwanza ama domo class A huzingatia misingi ya ‘domo class A’ yaani utawala wa watu kupitia watu kwa ajiri ya watu, kumbe sivyo na humu simo tena simo kabisa. Nakataa kuwamo kwa sababu kama watu (kupitia mawakala wao) wamekataa kwamba fulani na fulani hatutaki muendelee kutangulia huko mbele, si adabu basi kwamba mjitenge na kuwaacha watu wachague watu wengine wa kuongoza njia ya watu kwa ajiri ya watu ama ninyi mnayo tafsiri nyingine ya ‘domo krasi ei’? 

Sitaki kuongea sana wacha haya machache yatoshe kwa leo na niwape pole wadanganyika walipa kodi kwa misiba mikubwa ya kitaifa iliyowakuteni ikiwamo kuondokewa na wazee wetu, waliojitolea kufa na kupona, waliorudisha fedha za serikali kwa sababu waliamini kwamba wamelipwa zaidi ya walivyotumia na hatuwezi kwa na mfano bora zaidi wa uwajibikaji na uzalendo kama huu. Nasema jifunzeni kwa hawa kama bado mmebakiza sehemu ya kuingiza mafunzo mapya kwenye fahamu zenu lakini ikiwa tayari mmekwishakuwa mbwa wazee wasiofunzwa mbinu mpya, sina jingine la kuwaambieni isipokuwa kuwasalimiwa.
Wasalaaam, ni mimi ndugu yenu Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangu pakavu wa Kabwela wa Mdanganyika, nawasalimia.

Wednesday, March 7, 2012

Ati! Una "mawazo"!? Kwani ulitakaje?.

Salaam,
Leo siandiki ati kwa sababu nahitaji msomaji, na wala sina kile kiherehere cha kujaribu kujithibitishia kwamba naweza kuandika. Lah! Ninaandika kwa sababu ya kuandika tu hasa kwa vile kuandika kama kusema huyatoa yale yaliyoko moyoni yaani huyafanya mawazo kuwa maneno na ustaarabu wote wa binadamu umejengwa juu ya mambo mawili makubwa, mawazo yaliyotendwa ambayo kifupi huitwa matendo, na mawazo yaliyosemwa ambayo kifupi huitwa maneno na neno hili maneno hutumika mara nyingine kuelezea mawazo yaliyoandikwa kama haya ya kwangu ambayo mara nyingi huitwa maandiko.

Tofauti iliyoko hata hivyo kati ya maandiko, maneno na matendo ni muda wa kudumu na kukumbukwa kwa hizi njia zote tatu za kuwasilisha mawazo. Matendo, hudumu muda mrefu na huonwa na wengi, hata hivyo kwa kadri kizazi kimoja kinavyoondoka na kuruhusu kizazi kingine, basi yale yaliyokuwa matendo makubwa na yenye nguvu na maana kwa kizazi kimoja hubadilika kuwa tu msingi wa matendo bora zaidi, lakini hayaleti tena ule msisimko wa awali.

Fikiria  kwa mfano juu ya  wazo la mvumbuzi wa simu. Wakati alipowaza kwamba binadamu wangeweza kuwa na njia bora ya kuwasiliana kwa mazungumzo wajapokuwa umbali fulani ikiwa tu watakuwa na chombo chenye uwezo wa kusafirisha mazungumzo yao kutoka upande mmoja hadi mwingine na kurudi, bila shaka kama angerudi leo kwenye dunia yetu hii na kuona jinsi ambavyo sasa teknolojia ya mawasiliano imekuwa hata kizazi chetu hiki kinaamini kwamba kinaishi katika ulimwengu wa teknolojia ya habari na mawasiliano, asingeshangazwa kuona wazo lake la msingi kuwa likiishi hadi sasa, bali angeshangazwa na ukweli kwamba matendo yake yaani chomo alichotengeneza hakitumiki kabisa leo.  Mifumo na vyombo vitumikavyo leo kwenye mawasiliano kama tuyajuavyo leo, ni matokeo ya uboreshaji wa mawazo ya yule aliyewaza kwanza juu ya mfumo huo na kuyatia mawazo yake katika vitendo. Ni jambo linaloshawishi kuamini kwamba hakuwa akiwaza mawasiliano kwa mifumo na viwango tulivyo navyo sasa. Na hivyo kazi yake kwa maana ya vile alivyoyatendea kazi mawazo yake vile alivyoyawaza imesahahulika na leo wako wengine wanaoutukuzwa kwa uvumbuzi bora wa mifumo na vyombo vya mawasiliano kuliko Alexander Bell ambaye mtambo wake aliotengeneza yaweza kuwa kwamba hauko leo hata kwenye majumba ya makumbusho . Kinachosemwa hapa ni kwamba matendo japo huwa makubwa na huacha nyuma yake mchango usiopingika, lakini usahauliwa upesi zaidi katika mifumo yote hii mitatuu ya uwasilishaji wa mawazo.

 Maneno ya hekima huwa kama msumari uliogongomewa sana katika mioyo ya wale wasikiao, lakini maneno husahaulika haraka zaidi na utuzanji wake hata kwenye ulimwengu ulioendelea kama huu wa kwetu wa sayansi na teknolojia bado ni mgumu sana ukilinganisha na maandiko. Inawezekana pia kwamba maneno hupata zaidi maana yake kutoka kwenye sauti na nota wakati wa kutamka na hivyo japo ni rahisi kusema fulani kasema hivi ama vile, lakini si rahisi kuwasilisha kwa jinsi alivyosema yeye wakati aliposema kwa vile sauti yake ni yake na mvumo wa sauti hiyo wakati akisema neno hilo ulikuwa wa maana sana ili kulipa neno lenyewe maana.

Ndiposa binaadam tangu kale amefahamu umuhimu wa kuandika na sehemu kubwa ya historia ya binadamu iliyotunzwa hata sasa imetunzwa kwa kuandika japo si kuandika kule tukujuako leo. Wamayani kwa mfano, ndiyo jamii yenye historia tajiri kuliko nyingi na ambayo yaonekana kuwa na mchango mkubwa kwenye mambo mengi yatumikayo na binaadamu wa leo, na sehemu kubwa ya maandiko yao yameendelea kutafsiriwa kizazi hadi kizadi yakitufunulia kile walichokijua wakati huo na walichokitegemea kwenye ulimwengu ujao baada yao.

Imani zote za dini duniani, zimejengwa pia kwenye maandiko yaliyoandikwa na wale waliokuwako kabla ya baba zetu na hata sisi na yatakuwako baada yetu na watoto wetu japo imani na uchaji wake hutofautiana toka kizazi hadi kizazi.

Kwa kutambua maana, heshima na nafasi ya kuandika ndiyo maana leo naandika.

Kama unasoma maandiko haya yamkini swali lako ni naadika nini juu ya nini!? Mimi nasema unauliza swali hili kwa kutegemea tu uzoefu wako juu ya maandiko na unadhani kila kinachoandikwa ni lazima kwanza kiwe na jina na kifuate aina fulani ya uandishi na mtiririko ndipo kistahili kusomwa na huu ni udadidi usio faida. Ebu fikiri kwamba kama ningesema naandika kuhusu dini kwa mfano, wale wasioamini katika dini wangeacha kusoma maandiko haya kwa vile yanazungumza kitu ambacho hakina maana kwao. Vivyo kama ningesema naandika kuhusu vita, mapenzi, sayansi kwa aina zake na kadhalika, ningepata kwenye kila jamii ya watu ambao maandiko hayo yasingewagusa hata kidogo na hivyo ningekuwa nimeyafungia mawazo yangu kwenye jamii moja ama mbili au zaidi kidogo za watu na kusema kweli mimi ningepeda kuandikia watu wa jamii zote, rika zote na hata ikibidi lugha zote na ndiyo maana ninaandika juu ya mawazo.

Naandika mawazo kwa vile kila binadamu huwaza, naam, hata wale ambao wanadhani hawana muda wala haja ya kusoma, kusikia ama kufahamu mawazo ya wengine, nao huwaza na wanalo hitaji la kufahamiwa na hata kuheshimiwa mawazo yao na ingewasaidia kujua kwamba wako watu wengine wawazao kama wao au hata kinyume chao juu ya mambo kadha wa kadha katika ubinadamu wao.

Kama umesoma mpaka hapa, maana yake umekubali kwamba na wewe huwaza na kwamba unalo hitajio la kujua mawazo ya wengine hata kama hukubaliani nayo na ama unayaona kuwa ni upuuzi lakini bado unajua kwamba ni mawazo.

Labda sasa umebaki ukihitaji kujua ni mawazo juu ya nini? Hili jibu lake ni rahisi tu. Ni mawazo juu ya mawazo kwa sababu maisha yote na ustaarabu wote wa binadamu ni mawazo yaani matendo ni mawazo yaliyotendwa, maneno ni mawazo yaliyosemwa na hata maadiko ni mawazo yaliyoandikwa na hivyo huwezi kumtenga binadamu na mawazo.

Hivyo leo nimeamua  wakati nilipoamua kuandika, hilo lilikuwa ni wazo lililotokana na wazo juu ya muda na hivyo nitakushirikisha mawazo yangu kuhusu muda.

Miasha ya binadamu yanaonekana kupata tafsiri yake kwa kutumia muda walau hayo ndiyo mawazo yangu. Wakati tunapozungumzia umri wa mtu, kitu ama taasisi, tunazungumzia muda  ambao mtu, kitu ama taasisi husika imekuwapo.

Pia muda ni moja ya vitu adimu lakini visivyohitaji fedha kuwa navyo na ndiyo maana watu wote dunia kote wamepewa muda kwa kiasi sawa. Binadamu na awe upande wowote wa dunia, rangi yoyote ya ngozi yake na hata jinsi yoyote ya maumbile yake, anazo saa kumi na mbili za mchana na saa kumi na mbili za usiku. Katika saa hizi, binadamu hupata nafasi ya kuwaza na kusema ama kutenda mawazo yake.

Wakati binadamu anapofanya shughuli yoyote, anachofanya ni ama kutumia muda wake kutekeleza mawazo yake ama ya wengine. Ukweli unabaki kuwa kwamba binadamu anatumia muda kutekeleza mawazo iwe ni kwa kutenda ama kusema.

Kwa hiyo, kama maisha ya binadamu yangekuwa chakula ama kinywaji, basi tungesema kinywaji hiki kinahitaji mchanganyiko bora wa vitu viwili tu, navyo ni mawazo na muda na kwamba  uchanganyaji wa muda na mawazo ndivyo huamua ikiwa maisha ya binadamu huyu yatakuwa mazuri ama mabaya.

Uko msemo miongoni mwetu uliosemwa na wale waliokuwa kabla yetu usema “Hekima ni uwezo wa kutenda ama kusema neno sahihi, mahala sahihi, kwa watu ama mtu sahihi, kwa wakati sahihi, na lugha sahihi”. Ni mawazo yangu kwamba usahihi woote unaweza kuharibiwa tu ikiwa tutapatia maeneo mengine ya kauli hiyo tukakosea usahihi wa muda.

Kwa hiyo kwa maelezo hayo tumeona kwamba mawazo na muda huwekwa pamoja kuleta ama madhara au faida kwa binadamu.

Ni mawazo yangu kwamba muda ni sawa na fedha iwekwayo kwenye akaunti ya benki. Ebu fikiri hivi, kwamba kila siku asubuhi, fulani hukuwekea fedha kiasi cha shilingi themanini na sita elfu na mia nne,  na kukwambia utumie fedha hizo kwa kila siku na kwamba ikiwa utabakisha, kiasi utakachobakisha hakitaweza kuingizwa kwenye akaunti yako kesho, bali kesho utapewa kiwango kile kile cha fedha.

Hii ingemaanisha kwamba ungetumia shilingi elfu tatu na mia sita kwa saa moja na kile ambacho ungenunua kwa fedha hizo ni juu yako. Ndivyo na muda. Unazo sekunde 3600 kwa kila saa moja na unachofanyia sekunde zote hizo ni juu yako. Kwa mfano, muda unaotumia kusoma makala haya, utakuwa umetumika kabisa na kuptea milele na ikiwa hutapata faida yoyote kwa kusoma makala haya, basi utakuwa umepata hasara ya muda wote uliotumia kuisoma.

Wakati nikiwaza haya na jinsi muda ulivyo wa muhimu katika matumizi yake, nikaona nikuandikie ili nikueleze ujibidishe kutumia muda wako kuwaza na kutekeleza mawazo yako. Mimi nimewaza kuandika makala haya na nimekuandikia.

Wasalaam,
Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangu pakavu wa Kabwela wa Mdanganyika.

Saturday, February 4, 2012

NAWEKA MOJA CHEMBA.


Chokoraa wa Muhangaikaji wa Kabwela wa Mlalahoi nilipoamua kuwa natembea nimeshikilia "manati ya ndhungu", kuna waliodhani sasa nimeanza kuingia kwenye kutafuta shekeli kwa matumizi ya mabavu, humu nakataa simo. Simo kwa sababu matumizi ya mabavu kwa kutumia hii manati ni hatua nisiyoitaka kabisa, lakini leo nimekuja kijijini hapa kutangaza rasmi kwamba naweka moja chemba. Ndiyo, naweka moja chemba kwa sababu naona sasa ama kuna watu kwa maskudi kabsaaa wanamchezea kichwa mkulu wa kaya na kwa hivyo wanatuchezea vichwa wanakaya wote ama mkulu wa kaya mwenyewe hajali matatizo ya wadanganyika walipa kodi wake na humu naapa sihusiki. Ala! Hivi mwataka ati niendelee kuelekeza mtutu wa hii manati chini ilhali "waishiwa" wanyonya damu ya wadanganyika (mbu) na watema sumu hatari (nge) wamekutana kwa karibu siku saba sasa na hawataki kuzungumzia hali ya afya ya vitegemezi vyangu ilhali wao ndiyo walikuwa tegemeo langu la mwisho kwenye ulimwengu huu wa kupiga domo class 'A'. Nakataa simo. Hivi mnachotaka kuniambia Chokoraa miye mwana wa Kabwela ni kwamba ile timu nzima ya 'ivitaki' pale kwenye "chikale" haijui kwamba wadanganyika tumekuwa kwa juma zima tukimsubiria mkulu wa kaya aseme kitu kuhusu hawa akina "kalumanzila" wa kaya yetu waliogoma kuzama porini kuchimba mizizi na kutoa michemsho kwa matumbo ya watoto!!?. Ati anakuja na nyie mwampeleka moja kwa nne kwenye kufungua majumba ya hela!? Hela gani mtaweka humo ikiwa wadanganyika nguvu kazi ya kaya yetu wanakufa kwa vile hakuna "mshana" unaotolewa huko kilingeni?? Nitoeni humu. Simo, tena simo, simo, simo kabisaaaaaaaaaaaaa. 
Naapa mwaka huu mtakiona cha moto wadanganyika walipa kodi nyie maana mmekuwa nyasi kwenye uwanda wa mapambano ya mafahali wa Nyati na Faru na humu simo.  Bhaaaa!! Yaani ati kwa vile ninyi mwatibiwa nje ya mipaka ya kaya yetu hii mkituacha wadanganyika tukitaabika, basi mwatuona pia hatuna akili wala uwezo wa kupambanua mambo! Ama kweli ukitaka kumuua mbwa ua kwanza pua zake, nanyi mmeshindwa kunusa harufu ya hasira na chuki za wadanganyika na kwa hili simo.
Nasema, wadanganyeni wengine wooote lakini si mimi mwana wa Muhangaikaji maana mimi ninayo macho, tena makubwa kama ya bundi naona vyema usiku kuliko mchana na hivyo hamnidanganyi enyi mchekao nasi mchana ilhali usiku mwatuua gizani na kuhudhuria mazishi mchana mkivalia sura za uongo na kweli muonekane wahuzunika nasi, nasema simo. 

Ha ha ha ha ha, nacheka miye kitukuu wa Kabwela kwa sababu nawajua ninyi hata kutokea mbali maana macho yangu ya ndani yanaona hata mjapo ninyima kuona kwa macho ya nje  mtendapo mtendayo  kwa siri na hila, lakini nikiuona mwisho, naujua mwanzo wake na kwa hili nasema mnitoe!.  Ala! Kwani si ni nyie wenyewe wana wa ‘ifitaki’ mliokuwa hapo mwanzo mkimweka mkulu wa kaya mbele ya luninga zetu huku mkimfanya kuongelea mambo ambayo yalipaswa kuongelewa na liwali wala si mkulu wa kaya na kutufanya wenye akili kushangaa kwa nini mwamvunjia heshima namna hii!!? Yuko wapi sasa kuzungumzia madhira yenye kuwagusa wadanganyika, madhira ambayo neno lake tu, roho za wadanganyika arobaini milioni na ushee zingepona, nasema kwa hili mimi nakuwa wa kwanza kusema “Amina”. 

Ndiyo nasema amina maana musa alitangulia kuwajua enyi wana na akaandika akigiaza walaaniwe wampotezao mgeni njia na watu wote waseme amina na mimi kwenye hili ni wa kwanza “Amina”.

Najua mtasema nabwabwaja mambo nisiyoyajua lakini haya ninayoyajua ninayajua na ninayasema kwa usahihi ili mwenye masikio asikie, mmempoteza njia aliyepaswa kuongoza njia na humu simo. Nasema simo kwa vile wote twasafiri na tuendako wote twapajua, basi kelele na manung’uniko haya sit u ni mazao ya ‘ domo ghasia’ kama msemavyo ili msadikiwe na wazandiki wenye kuwapa vipande vya chupa ilhali wakiondoka na almasi yenu, bali ni hisia za wazi kwamba wadanganyika waliokuwa siku zote wakijua kwamba ni wadanganyika na kujivunia kudanganyika, sasa wamechoka na wanataka uhakika na kwenye hili nasema mnitoe.

Mnitoe, tena simo kabisa. Naam, kwa sababu najua mnajua ya kwamba hamna majibu ya maswali yaulizwayo na sasa mnataka tunyamaze tusiulize si kwa vile tunauliza upuuzi bali kwa vile hamkujua kwamba wakati unakuja tutawauliza kwa habari ya talanta ya “kula” mlizopewa na wenye kukasirika na kupiga ‘kura’ ili wapate kula kuambulia kuliwa, humu namo simo.
Ala! Hivi nyie ndugu wawili wa mdanyika yaani Mbu na Nge mmeanza lini tabia hii!!? Ha ha ha ha ha ha ha ha, nacheka miye maana najua wadanganyika walidanganyika walipodhani kwamba wakiwaweka ninyi pamoja yaani mbu kwa sababu ya sauti yako nzuri ya kubembeleza huku ukinyonya damu na kuwacha virusi, basi ungenyonya kwa wanyonyaji na kuacha virusi kwao ili ulete faida kwa wadanganyika, sasa najua kwamba walidanganyika, na ninaapa simo. Walidanyika walipodhani Mbu na Nge wakiwekwa pamoja wataleta uwezo wao wa kunyonya damu na kutema sumu hili kuleta nafuu kwa niaba ya wadanganyika walipa kodi kumbe hawakujua kwamba kwenye kijiji cha waishiwa kuna kaugonjwa ka ‘metamofisisi’ kanakowabadili wadanganyika wanaoingia kijijini humo kuwa ‘waishiwa’ na kusahau udanganyika wao na humu nakataa kuwamo. 

Wacha nicheke miye maana najua sasa wakati u karibu. Ndiyo, wakati wa Chokoraa kuambiwa anyamaze na asiseme anayosema na kama bado anataka kusema basi aseme watakayosema wale wenye mamluki na si mamlaka ya kusema na humu nasema sitakuwamo maana simo.  Nasema wakati wanaosema sasa watakapotakiwa kunyamaza na walionyama kutakiwa kusema, wanaodanganyika sasa watakapotakiwa kuambiwa ukweli na wakweli kudanganywa, wakati huo mjomba shangazi na binamu hawatafanya tena maamuzi kwenye jumba kuu la mashauri na hapo walau hadhi na heshima ya mdanganyika itarejea, lakini kwa vile njia ni ndefu yenye kugharimu machozi jasho na damu, Chokoraa najitoa, simo, tena simo kabisaaaaaaa!!

Salaam, ni mimi nduguyo wa damu, Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangu pakavu wa Kabwela wa Mdangayika, nakusalimia.

Saturday, January 14, 2012

Wadanganyika na Kelele za Mlango.

Ngoja kwanza nicheke. Ha ha ha ha ha ha ha!!! Nacheka miye Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangu Pakavu wa Kabwela wa Mdanganyika.  Leo, tofauti na siku zote ni furaha. Ndiyo, mwaka huu umeanza kwa mafanikio makubwa na kwa hilo namshukuru ‘Mulungu’. Ona huyu naye anakereka ati  kwa vile nimemwita kikwetu huyu ambaye yeye angetaka aitwe “God” ili ajiridhishe kwamba yeye ni mtumwa. Naapa simo. 


Nina furaha kwa vile mwaka huu Chokoraa nimepanda daraja, halafu nimepanda daraja mwanzoni mwa mwaka, ha ha ha ha ha ha!! Unashangaa!! Kwa sasa Chokoraa silali tena kwenye mitaro na huko hunikuti, nimepanga kichumba changu kimoja huku kwetu Uswazi kwenye kajumba ka mama Chausiku na hivyo silali tena chini ya daraja. Nani kasema hilo ni jambo dogo!?
Japo misosi yangu ni kule kule majalalani kama kawaida, lakini mara hii nafikiri hata majalala yangu itabidi yabadilike kidogo hasa kwa vile inabidi niwe kibiashara zaidi ili niweze kulipa kodi. Hilo nitakuhadithia ila leo, nataka kukueleza kero moja tu iliyonikuta. Kero ya mlango.


Kila mara “Ng’waaaaa!! Ng’waaaaaa!! Mlango huu wa bati unapiga kelele kila unapofunguliwa na Chokoraa hili linanikera  lakini kinachonishangaza ni kwamba mama Chau na watoto wake wala hilo haliwasumbui, nasema kweli mi nashangaa sana.  Ene wei, baada ya kuishi hapa walau kwa wiki mbili, nimeanza kuzoea hali hii na hivyo na mimi sasa naweza kulala na hiyo kelele hainisumbui sana isipokuwa pia hunisaidia nyakati fulani fulani, hilo nitakueleza siku nyingine.
Ndipo siku moja nikiwa nimejilaza hapa kwenye kitanda change cha kamba na hasa kwa vile siku hiyo nilikuwa sijatia kitu kinywani hadi hiyo saa sita ya usiku, nikabaki kuhesabu ‘kenchi’ na misumari na kupata nafasi ya kutafakari na hata kuzilinganisha kero za hapa kwa mama Chau na kero za kelele za wadanganyika walipa kodi kama ambavyo nimekuwa nikishuhudia kwenye kurasa za magazeti. 


Ngoja kwanza! Nani kasema Chokoraa huwa sisomi magazeti!? Mwongo. Huwa sinunui magazeti hasa kwa vile matukio mengi yanayotokea huku mtaani huwa nayaona mwenyewe na sitaki kuyanunua tena yakishatiwa nakshi za wino hasa kwa vile huwa tayari yamechakachuliwa ili kuleta radha ya si hasa, lakini huwa nasoma magazeti na hapa kwangu si ajabu ukakuta magazeti kadha wa kadha  kuanzia yale yaliyofungiwa maandazi, vitumbua, samaki au hata chips dume na kila nipatapo nafasi huwa najisomea hivyo vipande na usiniambie eti siyo magazeti. 


Ndiyo. Nakumbuka Wadanganyika walivyokuwa wamedanganyika na kuhamasika hadi kutaka kuingia barabarani  kuandaa mana ili iliwe na watoto wao baada yao ati kwa vile walichoshwa kula nyama ilhali wakifyatua matofari ya utumwa na hivyo wakajiandaa kuandaa mana. Weeee!!! Koma. Kwani waliandaa mana hata hivyo!? Wapiii!! Walifanya maandalizi yao yoote na matangazo na kila kitu halafu ati kuna jamaa mmoja mwema katika wema wake akagundua kuna mashababi mjini wanataka ati kuwadungua wadanganyika wote watakao andaa mana, basi kwa wema wake akawaonya wadangayika na wao wakanyewa kimyaaa!!  Ama kweli rahisi sana kuwadanganya wadanganyika.


Ni juzi tu wakati nasoma hiki kipande cha gazeti kuhusu hayo maandalizi ya kuandaa mana na jinsi yalivyozimwa kwa wema wa mwema na vijana wake, ndipo nilipogundua kumbe  wadanganyika wengi wanaishi kama milango ya nyumba ya mama Chausiku. Nasema usidhani nakutusi ewe mdanganyika mlipa kodi, lakini nakuuliza, ziko wapi zile hasira ulizokuwa nazo na kampeni kubwa ulizofanya ili kuandaa mana kwa ajiri ya kizazi kijacho baada yako hasa kwa kuzingatia kwamba ikiwa hivyo vijisenti yako uchwara vingelipwa kwa ajiri ya kusafisha hilo “Doa la Nzi” kwenye shati jeusi lenye harufu ya kinyesi, basi vizazi vijavyo vingepata hasira itokanayo na hasara na hata kufikia kuukana udanganyika wao?! Kwani hao mashababi walikuwa wangapi hata nchi nzima inasiamama wima kuwaacha hawa jamaa wapite!? Hata kama walikuwa wengi na waliojisheheneza sira nzitonzito na za maangamizi, walikuwa wapi na walikusudia kukaa muda gani au ndiyo wamehamia na hivyo sasa hatuwezi kufanya lolote kwa sababu kila tutakapojaribu kutoka nje ya milango yetu basi tutapambana na hawa mashababi!!? Nafikiri katika wema wake, huyu nduyu yetu mwema angetwambia basi kwamba hawa mashababi ama wamedibitiwa au wamekwishaondoka na hivyo tuendelee na maandalizi yetu ya kuandaa mana ili kizazi chetu kisifie jangwani kwa ukosefu wa chakula!. Humu mimi simo. 


Nikakumbuka pia kwamba baada ya maandalizi ya mana kushindikana,  waheshimiwa wawili akina Mbu na Nge nao wakaja kwa umoja wao wa Mbu-Nge kutaka nyogeza ya posho na hapa wadanganyika wakakasirika hadi povu kuwatoka midomoni. Nikahisi labda mara hii, wadanganyika hawa hawatadangayika. Wapi!! Kwa mara nyingine wakazidiwa na kile kibinti huwa nakiona kwenye vile visanduku vya picha kikisema kwa sauti kubwa “Sidanganyikiii” maana wandanganyika ghafla wakadanganyika na matukio ya mafuriko na mengineyo na kusahahu kwamba kuna visenti vyao kibao vyaliwa na ule umoja wa “Mbu-Nge”  na wao wakibakia kuwa wadanganyika walipa kodi. 


Mara mlango wa nje wa hapa nyumbani kwa mama chiku ukasukumwa ila mara hii polepole nafikiri kwa vile huyu anayefungua anajua kwamba watu wameanza kulala na hataki kuwasumbua na hivyo japo ulipiga kelele kama kawaida yake, lakini bado nasikia mikoromo ya usingizi ya mama Chiku na vitegemezi vyake ndipi nikakumbuka, kweli kele za mlango, hazimzuii mwenye nyumba kuuchapa.

Mi ninaomba kuuliza, hivi Wadanganyika mnaugua ugonjwa gani huu!!? Nasema usikasirike na wala usininune na hata ukinuna mi nina manati ya ndhungu sikuogopi ng'o! wacha nikuuliza na jibu nalitaka. Kwanza, mlitaka kuandamana ili kushinikiza sirikali isiwalipe "Doa la Nzi" mabilioni ya visenti vyenu vya madafu, mkachapwa mkwara na yule jamaa mwema mwenye kuwatendea wema hata wasio wema akiwaambia ati kulikuwa na tishio la wale mashababi, mkanywea. Hivi hilo tishio halijesha au ndo mmekubali kuliwa enyi 'wapinga kula'!? Nasema yule mwema katika wema wake atwambie kama wale mashababi wamekwishaondoka na kurudi kupamba na Kenya na Amisomi ili Chokoraa niandamane maana bado nataka kuandamana. Hamtaki kuhoji nawauliza wadanganyika mwaumwa ugonjwa gani?!. Wabunge walipojiongezea posho, mkaandika mpaka kwenye bulogu zenu, mkanuna hadi sura kuwavimba na kisha haoooo mkanywea. Nawauliza, hivi juhudi zenu zimefikia wapi ama mmebakia kuwa milango ya bati na bawaba kavu zenye kupiga kelele nyingi hata kwa kuguswa na mende ilhali mkiwaacha wenye nyumba yenye siri kali walele fofofo!!? Simo, nasema simo tena mntioe humu simo kabisaaaaaaaa.

Salaam nakusamilia,  ni mimi nduguyo Chokoraa wa Muhangaikaji ,wa Mlalahoi, wa Pangu Pakavu, wa Kabwela ,wa Mdanganyika.

Tuesday, January 3, 2012

Usalama usio salama wa Barabarani.


Kiherehere hiki!
Leo ati Chokoraa na mimi nimejikusanya na baadhi ya wananzengo hapa mtaani kwetu, tumekazunguka haka kasanduku kanakoonyesha sura za watu wakiongea na sauti zao twazisikia ati ninyi mwaita tivii. Uliza sasa tunaangalia nini! Duh! Nachoka miye mwana wa Muhangakaji kitukuu  wa Kabwela. 

Tumekaa tunaangalia Taarifa na Habari. Wewee!! Nani kasema nimekosea?! Nani!!! Tena!!! Angalia usiniudhi mapema nikazira kukuhadithia hata tukio lenyewe. Kwani ile ni “Taarifa ya Habari, Taarifa za Habari, Taarifa na Habari?!!. Nadhani lile baraza la wanaokifahamu Kiswahili kuliko sisi wengine inabidi watusaidie kwenye hili. 

Ala! Unaona sasa!! Hadi nimesahau nilichotaka kukwambia kwa vile umenitia hasira. Hata hivyo nadhani nimejaribu sana kutumia lugha yenu ya kistaarabu sana ilhali mi siifahamu hiyo lugha yenyewe. Wacha nitwange kichokoraa sasa ndo tuelewane. Simo.

Nasema kwenye hili la kulalamika na kunung’unika kwa kila kitu simo, tena simo hata kidogo, simo kabisaaaaa! Ala! Hivi, si kila mwisho na mwanzo wa mwaka kumekuwapo na lundo la ajari barabarani na nyingi zikisababishwa pamoja na mambo mengine uzembe wa madereva na kukosa ujuzi na sifa stahiki za kuendesha magari!? Kwani kuna mtu kati yetu hajui kwamba hali hii imechangiwa kwa kiasi kikubwa na uzembe wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama hasa wa barabarani yaani  ile mamlaka ya kuzibiti barabara na maji almaarufu kama ‘chuma tule’  na vikosi vya ‘usaha alama za barabarani’ kwa umoja wao? Hilo halinikasirishi hata hivyo.

Linalonikasirisha hadi nimewaandikia waraka huu, ni hili la wadanganyika walipa kodi kujifanya kulaumu “sirikali” kwa kila kinachofanywa hata kama ni kizuri. Hivi si nimeona mkipaza sauti mishipa ya shingo kuwasimama mkilalamikia kukatizwa safari zenu kwa sababu ya zoezi la ukaguzi wa “liseni’ za udereva ili kujua wale walio ‘liseni’ darasani kabla ya kuanza kuendesha na wale ambao wanaendesha bila kuanza ‘kuliseni’!! Nasema kwa hili mnitoe. 

Ona sasa. Yaani wakati watendanaji wa ‘sirikali’ walipojipanga ki ‘stratejiki’ kabisa kwa kuzingatia ‘taimingi’ ya muda ambao ajari zinazidi na kujaribu kuokoa maisha ya wadanganyika, mwalalama! Mwalalama nini enyi wana wa danganyika yetu!? Naapa simo humu.  Ona hyu naye anachukia ati kwa vile nachanganya kikoloni katikati ya sentensi zangu. Utajuaje kwamba “Nshomile mpaka fomu fooo!!!” Kalagabaho kama hujaelewa, kwani hilo mi Chokoraa lanihusu!? Simo nasema.

Nasema kwenye hili, badala ya hasira zangu kuzielekeza kwa hawa wana usalama japo si salama, ningezielekeza kwa wamiliki wa haya madude yaliyofanyika wajumbe wa malaika mtoa roho kila mwanzoni mwa kila mwaka. Washangaa nini!! Ningezielekeza hasira zangu kwao kwa vile kila mwajiri anapomwajiri dereva anamuuliza kuhusu leseni na ikiwa mwenye gari anaruhusu dereva asiye na leseni kuendesha gari lake, mwataka nisimwelekezee hasira zangu kwa nini!!? Naapa kwa hili tutashindana sana, lakini simo.

Halafu!! Ebu niwaulize enyi wana wa usalama japo si salama, huu utaratibu wenu wa kuvamia tu maeneno na kuanza kutekeleza majukumu yenu bila hata kuzingatia kwamba Chokoraa miye mwana wa Muhangaikaji, naam, mimi huyu mjukuu wa Mlalahoi kilembwe wa Kabwela, mara nyingine ninatoka nyumbani na tiketi tu na ziada ya shilingi elfu mbili kwa ajiri ya maji na nauli ya ‘bodaboda’ nikifika huko niendako na hayo mengine namuachia maulana, mmeianza lini!?

Naapa kwa ubabe huu sina hakika kama mnafanya ‘upolisi jamii’ kwa sababu mnashindwa kuzingatia mahitaji ya jamii yenyewe katika utekelezaji wa majumu yenu kwa sababu hasa mahitaji ya Chokoraa miye hayaishii kwenye kusafiri na kufika salama bali pia kuzingatia matumizi ya kila ‘shekeli’ (iite ‘sinyingi’ kama hilo ndilo jina ulipendalo) ninayoitumia na ninavyoitumia wakati wa safari na ndiyo maana japo naona kama lengo lilikuwa zuri lakini kwenye utekezaji wake simo, tena simo kabisaaa!.

Nasema iweni na huruma na maisha ya sisi wajukuu wa Pangu Pakavu kwa sababu kila mara tumekuwa tukisema tieni mchuzi lakini hamtaki, naapa simo. Hivi mnadhani wale wadogo zangu akina Mzembe na Mzururaji ambao walikuwa wameng’ng’ana kuishi mjini humu kwa kuningezea shughuli ya kuwalinda na kuwahudumia mimi kaka yao Mkubwa, tajiri wa ukoo kwa kipato cha kunanga, Chokoraa wa Kabwela, na sasa walikuwa wameamua kurudi kijijini, si wamehairisha baada ya magari kuchelewa kuondoka na wamerudi  kwenye lile pagala tunakojikusanya usiku na kujirundika tukipitiwa na usingizi ilhali tukiita huko ni kulala!?. Nasema hamjui ni kiasi gani ya gharama na maumivu ya moyo mmeniongezea mwaka huu na ndiyo kwanza unaanza. Naapa mpaka umelizike, tutaonana wabaya. Simo. 

Na nyie ‘chuma tule’ hivi kweli na akili zenu zoote  mmeshindwa kutengeneza ‘mpango mkakati’ (naogopa kusema ‘sitrateji’ msijesema napenda sana kikoloni) wa jinsi ya kukagua walio ‘liseni’ na kuwa lessen wale wasio nazo bila kunisumbua miye Mdanganyika Mlipa kodi!!? Naapa utaalamu umesafiri kwenye inchi ya wadanganyika walipa kodi. Simo, tena simo kabisaa.

Haya, tekelezeni majukumu yenu na wala msijesema mimi nawakataza kutekeleza majukumu yenu maana nafahamu mnayo sheria ya kuitumia kuniyamazisha miye hati kwa vile nimekuwa domo kaya wakati huyo ni mpwa wangu mimi jina langu ni lile lile le siku zote, Chokoraa wa Mdanganyika wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangu pakavu wa Kabwela.

Haha ha ha ha ha ha ha! Nicheke niongeze siku miye.

Salaam nawasalimia, 

Chokoraa wa Muhangaikaji.

Thursday, December 29, 2011

Nipe, nipe, nipe!!. Nipe Uprofesa wa Heshima



Ati mwashangaa!! Ndiyo, wakati mwaka 2011 unapofikia mwishoni, Chokoraa wa Muhangaikaji wa Pangu pakavu, wa Mlalahoi, wa Kabwela, wa Mdangayika nimepata faida moja kubwa na mwaka huu na hiyo ni kutambua haki yangu ya kupewa taito.

Nasema wewe unayenuna na kukasirika ni kwa sababu hupendi tu nikwambie ukweli kwamba ikiwa unatafuta kufanya tathmini ya mwaka kwa kutumia kigezo cha shekeli ulizonazo kwenye ‘kilindo’ , basi umepotea njia. Ndiyo.  Pamoja na kwamba pesa sabuni ya roho na penye udhia penyeza rupia, lakini kwenye hii dunia gunia yetu ya sasa, unahitaji pia kuwa kwenye ‘lokeisheni’ sahihi ili kuliona tundu la wewe kupenyeza lupia hapo penye udhia ili upate matokeo na kwa kuigundua siri hii nadai kutunukiwa heshima ya uprofesa wa kitaa.  Ngoja kwanza! Bado nakamilisha ‘risachi’ kabla sijaanza kuitumia mbinu hii kwa ajiri ya kujiletea maendeleo, ila nimeamua nikumegee walau kidogo ili usisumbuke kujiuliza ni kwanini waishiwa kila mara wanaonekana kupanda juu ilhali wadharauliwa tukibaki chini siku zote, humu namo simo.
Ikiwa utaamua kubishana na Profesa (mtarajiwa) Chokoraa kwenye hili nasema simo.  Ebu tazama pembeni yako uone. Wangapi umekua nao, umeishi nao na hata kufanya nao kazi na unao uhakika wa ‘asili elfu’ miamoja kwamba ‘kredenshozi’ zao na hata utendaji wao hauna hadhi wala sababu ya ‘kutunukiwa’ shahada ya udaktari ati wa falsafa wa heshima na kutengeneza kundi la mbumbumbu wenye majina yanayoanza na ‘Dk’ utadhani kuitwa ‘Dk’ kunabadili DNA na kumfanya mtu kuwa “royo klasi” kwa usiku mmoja tu, humu namo simo.

Huwezi kuamini kiasi na umbali wanaokwenda hawa jamaa kupata walau hiyo ‘taito’ ya utabibu, naapa utakasirika nikikueleza na ndiyo maana nashona domo langu nisibwabwaje kwa hasara ya kichwa changu na vitegemezi vyangu na hata yule kikongwe mke wa marehemu Muhangikaji, mkamwanae Mlalahoi, mama yangu Shida wa Matatizo.

Ngoja kwanza niendelee kukupa walau topic moja zaidi kwenye hili somo langu la “Kitaaolojia” ili nikiondoka darasani usibaki na maswali ni kwanini nataka ‘taito’ ya Prof. Chokoraa wa Muhangaikaji wa Kabwela wa Mlalahoi.  Ala! Ati washangaa mimi kuitwa Profesa! Washangaa nini ebu nikuulize kama alivyouliza papaa mawani mwaka ule iliponyesha mvua nyingi na watu wakalima na kuvuna sana upande mmoja lakini kwa ubovu wa miundo mbinu na migomo ya yule nyoka wenu wa chuma, wakati upande mwingine misosi ikiozea kwenye maghala,  upande wa pili wanadamu wakidodoka kwa kutokwa uhai kisa njaa na bado ati mwatunukiana shahada za udaktari wa falsafa, naapa simo. 

Ala! Kwani nani hajui kwamba wako baadhi yenu mliolazimika ‘kupolitiki’  ili kupata nafasi za kutunukiwa hizo tunu zilizotengwa kwa ajiri ya wana wa adamu waliojaariwa kuvumilia shida za shule na kukabiliana na magumu ya watu wao hata kupata hadhi ya kutunukiwa shahada zenye shada la maua kwa utumishi uliotukuka!!? Naapa simo humu.

Tena nasema mnitoe miye Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangu pakavu wa Kabwela wa Mdanyanyika. Nani kasema nataka kuhusika kwenye hili! Sasa hivi kila mmoja anataka kuitwa tabibu yaani “dokta’ hata kama anajua nafsini na moyoni kwamba hadi na heshima ya dokta ni mzigo wa mwiba ambao kuubeba kwake kutamuumiza lakini yu tayari kufa kikoloni na tai shingoni, nitoeni humu enyi wana.

Nasema, hizi ‘taito’ siku hizi zimegeuka kuwa ‘frontia’ ya mapambano kwenu wana za gunia hili bovu la dunia na athari zake zimekuja hadi huku kwenu wadanganyika na mimi simo. Kwani si mwanzo mlianza na “Uheshimiwa”!? Kila mmoja kwa juhudi na mbinu alizozijua yeye alipambana kwa kadri awezavyo ili kuwa muheshimiwa na mara mlipofika hapo mkagundua kwamba kumbe hata hapa hakuna jipya hasa kama mafanikio ya nje hayalingani na mafanikio ya ndani na hivyo “yu goti beta” mkaamua kutafuta kiwango kingine cha heshima mradi tu niwaheshimu mimi Mdangayika nisiwaze hata siku moja kuwa kama ninyi na ninaamini wala hamna mpango wa kurudi kujiita tena ndugu maana mnafahamu kwamba mimi na ninyi si ndugu tena, humu namo simo. 

Sasa mmeamua kuwa matabibu. Ha ha ha ha ha Nicheke ninenepe Chokoraa miye. Ati, kila mmoja wenu sasa akiishafika tu kwenye kiwango cha heshima kwenye jamii anadai utabibu wa falsafa!!.
Mwanikera enyi wana wacha niseme ukweli wa moyo ikiwa baada ya hapa sitasema tena walau mjue kwamba Mdanyika miye nakereka na huu upuuzi wenu. Ona hata wale waliopaswa kuchunga kondoo wa Mungu nao wamekuwa walevi. Ndiyo, wamekuwa walevi tena wa ulevi mbaya wa kinywaji kiitwacho uheshimiwa ambacho kikiisha kukuzoea huacha kukulevya na ndipo mnapotaka sasa mpate nyongeza ya ‘alikohili’ ya ‘Udakitari wa Falsafa” nasema simo. 

Kichefuchefu chanipata miye kila nisomapo majina yenu kwenye vyombo vya habari kila mara mkijitahidi kujiita madaktari ilihali nawajua wengi wenu nyie elimu zenu za ngumbalu na hata hayo mliyofanikisha si ninyi bali Mungu na ninayo hakika hakuwatuma muanze ‘kupolitiki’ ili kupata shahada za udaktari wa heshima, si hayo mgewaachia wana wa si hasa!!? Nasema humu simo. 

Utakuta mmeandikwa kwa herufi kubwa na wino uliokoza ‘Reverendi, Dokta Chokoraa wa Muhangaikaji” hivi huu ureverendi tu hauwatoshi mpaka na udaktari naapa ikiwa itakuja “taito alikoho” nyingine mtakuwa wa kwanza kukimbilia. 

Kwani kuchunga kondoo si ilipaswa kuwa kazi ya wito ambayo wale waliotangulia kabla yenu waliikata hadi Mungu (kwa vile yeye hashindwi na jambo) alipowalazimisha kufanya atakavyo yeye? Mbona nyie mwakimbilia kujipa majina makubwa hata kama mwajua mioyoni kwamba hamyastahili? Nasema kwenye hili hata kama mtasema nawakosea adabu, Chokoraa simo.

Mmezidiwa hata na ‘Mzanaki’ ambaye pamoja na kwamba alikuwa mmoja wa wadanganyika wa kwanza kabisa kupata shahada ya uzamivu na hata hiyo ya udakitari bado kwa unyenyekevu aliendelea kutaka aitwe “Mwalimu” hadi mwisho wa uhai wake, ati ninyi mliopaswa kuwa mabingwa wa unyenyekevu mnalilia majina ya utabibu. Nakataa kuhusishwa humu. 

Nimechoka kusema, naamini wanafunzi mmesikia na kuelewa na kama kuna maswali basi tukutane kwenye kipindi kijacho kwenye somo letu hili la “Kitaaolojia” na Profesa wenu Chokoraa wa Muhangaikaji, wa Mlalahoi, wa Pangu pakavu, wa Kabwela, wa Mdanganyika.
Simo humu.