Salaam nawasalimia! Najua wako baadhi yenu ambao mmepita
kijiweni kwangu mara nyingi na kunikosa na hata wengine nasikia walishakula
wali wa hitima. Si makosa yenu, ila miye salaam nawasalimia. Nasema sionekani
kijiweni si kwa sababu sipo ila kwa sababu hamnioni. Labda pia sipendi mnione
maana si siku hizi hata upele mwaita jipu na kila mmoja atafuta kuonekana
tabibu na anaweza kutumbua! Nani kakwambia na miye jipu! Naapa mwanitafuta
ubaya enyi wana na miye humo simo ila salaam tu miye nawasalimia.
Ala! Kwani mi si nimekuwa nakuoneni tu tangu mlipomaliza ule
mchezo wwenu kichaa jinsi ambavyo nyote mmehamia huku kwetu ‘bize’ mkimwagiana “majitaka”
ilhali mwajua fika kwamba muda wa kuchafuana ushakwisha!?. Haya, endeleeni
kumwagiana majitaka tu midhali si mtindi mkali, lakini nawaapia enyi wana
msipokubaliana kutokukubaliana na mkasonga mbele hata kama kwa mwendo wa Kobe,
huko mwendako nachelea mtaanza tumbuana wenyewe kwa wenyewe ila miye humo
nahusikaje! Simo naapa.
Leo miye nimekuja tu huku mjini kwenu mara moja kumletea salaam za heri Mkulu wa kaya ya
Wadanganyika walipakodi; ikiwa heri ni kunyamaa usinene yale wasiyopenda
kuyasikia akina kaka mkubwa Muishiwa wa Mdanganyika wa Mlakodi, , salaam
nakusalimia.
Muishiwa sana Mkulu wa kaya yetu, miye ni yule nduguyo
Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika
Mlipakodi, ambaye siku si nyingi wapambe wako walipita kijiweni kwangu na
baragumu kunitaka nikusanyike kwenye uwanja wa ‘mkung’utano’; nishuhudie jinsi
mlivyokuwa mkiucheza ule mchezo wenu maarufu kwa harufu, muupendao wewe na
waishiwa wenzio, mchezo wa kuchafuana.
Ha ha ha ha ha!!! Sikuwa nimevaa rangi rangi, na sauti ya
kijiweni haitoki kwa mvaa suti kwa hiyo kama hukunitambua kwa masempele yangu
niliyokuwa nimejifunika ili walau msiseme natembea uchi japo kusema kweli
sikuwa nimevaa, basi itakuwa shida kweli kunikumbuka, ila salaam nakusalimia,
shikamoo mkulu wa kaya.
Sitaki nikukumbushe zamani maana najua wewe waifahamu vyema
historia ya kaya yetu hii na jinsi ambavyo kaka mkubwa, Mkufunzi wa Mdanganyika
wa Mlipakodi alivyotuasa na kutuacha, ila miye nimekuja tu hapa mtaani kwako
nikuletee salaam za wadogo zangu wale
akina Mtafutaji na Mjasiria, na hata yule aliyepewa jina la babu wa babu yake
na babu mzaa baba, Mlalahoi.
Wala sina haja ya kukumbusha jinsi Mlalahoi alivyo mtundu na
hata bibi yake yaani mama yenu mkubwa Mchakarikaji anasema amechoshwa na kelele
na vurugu za huyu mtoto, ila hayo unayajua.
Juzi tu wakati nafunga safari kuja mjini, mlalahoi akaniijia
na majani mabichi mkononi, unaweza
kudhani nilimdharau tu kwa vile ni mtoto anacheza, lakini mimi namfahamu vyema
mlalahoi, akifanya jambo ujue anataka kusema jambo. Asivyo na adabu, ati nayo
akayaweka kwenye kimfuko changu cha Rambo nilimoweka pia vidaso vyangu vya
kubadilisha, hapo sasa nikakasirika, nikataka kumzaba kofi, lakini kabla hata
sijanyanyua mkono akanitazama na kutabasamu kitoto, kisha akasema “Kaka, hiyo dawa
hiyo, uende nayo huko mjini”.
“Dawa ya nini wewe
Mlalahoi, mbona weshi vituko we mtoto?” Nikamuuliza na hata mimi sasa
nilitabasamu maana kumbe ule niliowaza kuwa uchafu, ilikuwa namna yake ya
kunijali nisiugue niendako.
“Dawa ya majipu kaka,
huko mjini nasikia huo ugonjwa umeenea na hata kaka yetu Muishiwa sana mkulu wa
kaya, siku hizi anatumbua majipu tu...”. Nikamtazama huyu mtoto, kisha nikaanza
kujihoji ameyatoa wapi mawazo hayo kichanga huyu asiyejua chochote katika dunia
hii ya “si hasa” za kuchafuana hata baada ya “uchafuzi mkuu”?
Nadhani mlalahoi aliouna wasiwasi wangu, akanishika mkono na
kuniashiria nikae chini, nikaketi na kumsikiza, ndipo aliponiambia nikifika
mjini nikusalimu na ati nikwambie ingawa ni kweli kwamba dawa yoyote ni chungu
wakati wa kunywewa kwake, na kwamba dawa ya jipu kutumbuliwa, lakini tumeagana
na nyonga katika mbio hizi!?.
Ndiyo, maana huku kwetu sasa wale watoto watukutu wa mzee
Mhalifu wameanza tena zile tabia mbaya za kumpiga dada “Fatuma” na ati ukiuliza
unaambiwa “hali ngumu sasa tukale wapi?”, na miye swali ambalo sijalipatia jibu
hadi sasa ni ikiwa ‘kumpiga fatuma’ ndiyo suluhu ya njaa yao, ila miye salaam
nakusalimia.
Nasema hili ongezeko la kile ambacho sungusungu wa kijiji
wanakiita “uhalifu mdogo mdogo” siyo hasa jipu, bali ni dalili za kansa
inayomea na kukua upesi, na naapa mwaniapisha ikiwa hamtafuti dawa yake,
tumbueni majipu lakini kansa haitumbuliwi.
Ati! Najua wako wanaosema kwani anajua nini bananga huyu, na
wako wengine watatafuta kunitumbua na miye kwa kutumia ile sindano yao ya “swahiba
klaimu”, lakini miye sivunji sheria bali ni salaam tu nawasalimia.
Ala! Kwani mmepofuka lini msione kwamba ama ongezekeo hili
la ‘vibakaji’ vinavyobaka hata chakula chetu tulichokitolea jasho na damu, ni
dalili ama kwamba ile bana matumizi sasa inaanza kutufikia hata sisi tuliokuwa
tukipiga kelele za ufisadi bila kujua kwamba hata kuishi mjini kwa ‘misheni
tauni’ ni ufisadi, ama kwamba wahalifu papa hasa wauzao sembe wameamua
kuanzisha mbinu ya kuhamisha ‘atensheni’ yenu mkimbizane na ‘vijitu
vidogovidogo’ ili wao wasage na kuuza sembe lao kwa amani!? Ha ha ha ha ha
ha!!! Nacheka mwanichekesha miye!
Nasema ya wauza sembe msiniulize maana miye si mla nyama,
mchicha na tembele ndiyo mboga yangu, lakini sembe simo hata kidogo, na hapa
salaam nawasalimia, ila fumbueni macho muikate kansa hii kabla haijaenea sana
na kuwazidi kimo enyi wana maana mchelea mwana kulia hulia yeye.
Ala! Kwani hamjui kwamba kuna waliokuwa wakiishi mjini kwa
misimu ya sikuu za kitaifa na sasa hawana la kufanya ili wanunue ugali kwa mama ntilie!? Ama
mwajifanya mmesahau kwamba walipoamua kutoendesha magari yao kwa vile mafuta
yamekuwa aghali, na vipuri vimeacha kuharibika na hivyo gereji hazina kazi!?.
Nasema simo humu namo!. Mwashangaa ati inakuwaje sasa mnasikia kilio, fatuma
kapigwa mtaani kwenu!? Mwashangaa nini!?
Sisemi kati msibane matumizi na wala msitumbue majibu
uchungu maana dawa ya ugonjwa tiba,
lakini nauliza tu ikiwa kuna mipango mbadala ya kukabiliana na madhara
yatokanayo na hatua chanya hizi ama wote tufumbe macho tusali!?
Ni mimi ndugu yenu Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa
Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika Mlipakodi, salaam nawasalimia.