Thursday, December 29, 2011

Nipe, nipe, nipe!!. Nipe Uprofesa wa Heshima



Ati mwashangaa!! Ndiyo, wakati mwaka 2011 unapofikia mwishoni, Chokoraa wa Muhangaikaji wa Pangu pakavu, wa Mlalahoi, wa Kabwela, wa Mdangayika nimepata faida moja kubwa na mwaka huu na hiyo ni kutambua haki yangu ya kupewa taito.

Nasema wewe unayenuna na kukasirika ni kwa sababu hupendi tu nikwambie ukweli kwamba ikiwa unatafuta kufanya tathmini ya mwaka kwa kutumia kigezo cha shekeli ulizonazo kwenye ‘kilindo’ , basi umepotea njia. Ndiyo.  Pamoja na kwamba pesa sabuni ya roho na penye udhia penyeza rupia, lakini kwenye hii dunia gunia yetu ya sasa, unahitaji pia kuwa kwenye ‘lokeisheni’ sahihi ili kuliona tundu la wewe kupenyeza lupia hapo penye udhia ili upate matokeo na kwa kuigundua siri hii nadai kutunukiwa heshima ya uprofesa wa kitaa.  Ngoja kwanza! Bado nakamilisha ‘risachi’ kabla sijaanza kuitumia mbinu hii kwa ajiri ya kujiletea maendeleo, ila nimeamua nikumegee walau kidogo ili usisumbuke kujiuliza ni kwanini waishiwa kila mara wanaonekana kupanda juu ilhali wadharauliwa tukibaki chini siku zote, humu namo simo.
Ikiwa utaamua kubishana na Profesa (mtarajiwa) Chokoraa kwenye hili nasema simo.  Ebu tazama pembeni yako uone. Wangapi umekua nao, umeishi nao na hata kufanya nao kazi na unao uhakika wa ‘asili elfu’ miamoja kwamba ‘kredenshozi’ zao na hata utendaji wao hauna hadhi wala sababu ya ‘kutunukiwa’ shahada ya udaktari ati wa falsafa wa heshima na kutengeneza kundi la mbumbumbu wenye majina yanayoanza na ‘Dk’ utadhani kuitwa ‘Dk’ kunabadili DNA na kumfanya mtu kuwa “royo klasi” kwa usiku mmoja tu, humu namo simo.

Huwezi kuamini kiasi na umbali wanaokwenda hawa jamaa kupata walau hiyo ‘taito’ ya utabibu, naapa utakasirika nikikueleza na ndiyo maana nashona domo langu nisibwabwaje kwa hasara ya kichwa changu na vitegemezi vyangu na hata yule kikongwe mke wa marehemu Muhangikaji, mkamwanae Mlalahoi, mama yangu Shida wa Matatizo.

Ngoja kwanza niendelee kukupa walau topic moja zaidi kwenye hili somo langu la “Kitaaolojia” ili nikiondoka darasani usibaki na maswali ni kwanini nataka ‘taito’ ya Prof. Chokoraa wa Muhangaikaji wa Kabwela wa Mlalahoi.  Ala! Ati washangaa mimi kuitwa Profesa! Washangaa nini ebu nikuulize kama alivyouliza papaa mawani mwaka ule iliponyesha mvua nyingi na watu wakalima na kuvuna sana upande mmoja lakini kwa ubovu wa miundo mbinu na migomo ya yule nyoka wenu wa chuma, wakati upande mwingine misosi ikiozea kwenye maghala,  upande wa pili wanadamu wakidodoka kwa kutokwa uhai kisa njaa na bado ati mwatunukiana shahada za udaktari wa falsafa, naapa simo. 

Ala! Kwani nani hajui kwamba wako baadhi yenu mliolazimika ‘kupolitiki’  ili kupata nafasi za kutunukiwa hizo tunu zilizotengwa kwa ajiri ya wana wa adamu waliojaariwa kuvumilia shida za shule na kukabiliana na magumu ya watu wao hata kupata hadhi ya kutunukiwa shahada zenye shada la maua kwa utumishi uliotukuka!!? Naapa simo humu.

Tena nasema mnitoe miye Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangu pakavu wa Kabwela wa Mdanyanyika. Nani kasema nataka kuhusika kwenye hili! Sasa hivi kila mmoja anataka kuitwa tabibu yaani “dokta’ hata kama anajua nafsini na moyoni kwamba hadi na heshima ya dokta ni mzigo wa mwiba ambao kuubeba kwake kutamuumiza lakini yu tayari kufa kikoloni na tai shingoni, nitoeni humu enyi wana.

Nasema, hizi ‘taito’ siku hizi zimegeuka kuwa ‘frontia’ ya mapambano kwenu wana za gunia hili bovu la dunia na athari zake zimekuja hadi huku kwenu wadanganyika na mimi simo. Kwani si mwanzo mlianza na “Uheshimiwa”!? Kila mmoja kwa juhudi na mbinu alizozijua yeye alipambana kwa kadri awezavyo ili kuwa muheshimiwa na mara mlipofika hapo mkagundua kwamba kumbe hata hapa hakuna jipya hasa kama mafanikio ya nje hayalingani na mafanikio ya ndani na hivyo “yu goti beta” mkaamua kutafuta kiwango kingine cha heshima mradi tu niwaheshimu mimi Mdangayika nisiwaze hata siku moja kuwa kama ninyi na ninaamini wala hamna mpango wa kurudi kujiita tena ndugu maana mnafahamu kwamba mimi na ninyi si ndugu tena, humu namo simo. 

Sasa mmeamua kuwa matabibu. Ha ha ha ha ha Nicheke ninenepe Chokoraa miye. Ati, kila mmoja wenu sasa akiishafika tu kwenye kiwango cha heshima kwenye jamii anadai utabibu wa falsafa!!.
Mwanikera enyi wana wacha niseme ukweli wa moyo ikiwa baada ya hapa sitasema tena walau mjue kwamba Mdanyika miye nakereka na huu upuuzi wenu. Ona hata wale waliopaswa kuchunga kondoo wa Mungu nao wamekuwa walevi. Ndiyo, wamekuwa walevi tena wa ulevi mbaya wa kinywaji kiitwacho uheshimiwa ambacho kikiisha kukuzoea huacha kukulevya na ndipo mnapotaka sasa mpate nyongeza ya ‘alikohili’ ya ‘Udakitari wa Falsafa” nasema simo. 

Kichefuchefu chanipata miye kila nisomapo majina yenu kwenye vyombo vya habari kila mara mkijitahidi kujiita madaktari ilihali nawajua wengi wenu nyie elimu zenu za ngumbalu na hata hayo mliyofanikisha si ninyi bali Mungu na ninayo hakika hakuwatuma muanze ‘kupolitiki’ ili kupata shahada za udaktari wa heshima, si hayo mgewaachia wana wa si hasa!!? Nasema humu simo. 

Utakuta mmeandikwa kwa herufi kubwa na wino uliokoza ‘Reverendi, Dokta Chokoraa wa Muhangaikaji” hivi huu ureverendi tu hauwatoshi mpaka na udaktari naapa ikiwa itakuja “taito alikoho” nyingine mtakuwa wa kwanza kukimbilia. 

Kwani kuchunga kondoo si ilipaswa kuwa kazi ya wito ambayo wale waliotangulia kabla yenu waliikata hadi Mungu (kwa vile yeye hashindwi na jambo) alipowalazimisha kufanya atakavyo yeye? Mbona nyie mwakimbilia kujipa majina makubwa hata kama mwajua mioyoni kwamba hamyastahili? Nasema kwenye hili hata kama mtasema nawakosea adabu, Chokoraa simo.

Mmezidiwa hata na ‘Mzanaki’ ambaye pamoja na kwamba alikuwa mmoja wa wadanganyika wa kwanza kabisa kupata shahada ya uzamivu na hata hiyo ya udakitari bado kwa unyenyekevu aliendelea kutaka aitwe “Mwalimu” hadi mwisho wa uhai wake, ati ninyi mliopaswa kuwa mabingwa wa unyenyekevu mnalilia majina ya utabibu. Nakataa kuhusishwa humu. 

Nimechoka kusema, naamini wanafunzi mmesikia na kuelewa na kama kuna maswali basi tukutane kwenye kipindi kijacho kwenye somo letu hili la “Kitaaolojia” na Profesa wenu Chokoraa wa Muhangaikaji, wa Mlalahoi, wa Pangu pakavu, wa Kabwela, wa Mdanganyika.
Simo humu.

Saturday, December 24, 2011

Igizo la sikuu la Chokoraa.



Aaaaaah ha ha ha ha ha!! Nicheke ninenepe Chokoraa wa Muhangaikaji, kitukuu wa Kabwela. Ati wanishangaa kwa nini naangua kicheko!? Mshangae kwanza na huyu anayedhani ati sina akili miye kucheka bila sababu. Hujui kucheka ni sababu tosha ya kucheka kwa sababu kwa hali ya maisha ya sasa hasa kwa Chokoraa hilo ndilo jambo aghali sana!? Basi pana mengi huyajui, naapa simo.

Nacheka, na si mara zote kucheka ni kufurahi kama ambavyo machozi ya Mamba hayana hata chembe ya huruma na nina hakika hilo walifahamu vyema, lakini humu simo leo.  Nacheka kwa sababu huu ni msimu wa kuigiza na igizo la Chokoraa mara hii ni kicheko.  Ndiyo, moja ya sifa kubwa za Chokoraa miye ni kwujaribu kupata raha kwenye maisha pasina kutumia gharama kubwa na kusema kweli ikiwa raha najipa mwenyewe hizo gharama atanitoza nani!? Niwacheni nicheke miye, ha ha ha ha ha ha!!!!!

Nasema umefika wakati wa maigizo ya Wadanyanyika walipa kodi na juzi nilishirikishwa kwenye ‘shuutingi’ na mama wa kitegemezi changu hasa kwa vile yeye igizo lake ni mlo na mavazi. Wacha kwanza nikupe ‘skriputi’ yanyewe ilivyokuwa.
Mara kisimu change cha mchina kikaanza kunitekenya mfukoni (huwa siweki mlio wa sauti kwa vile kina kelele na mara nyingine nikiwa jalalani kinawashtua paka na mbwa na kuwaambia na mimi nipo jalalani na kusababisha mashindano ya vipande vya mikate kuongezeka na mimi siku hizi kasi inapungua. Hilo nitakuhadithia siku nyinge. Basi bwana, nikakichomoa mfukoni na harakaharaka nikakipachika sikioni.
 “Hivi unajua…!” mama wa kitegemezi changu huwa akisema hivi tayari nakuwa nimejua tu! Lakini sikutaka kumpa ‘krediti’ kwa hiyo nikaigiza “kutojua” wakati nilijua alichotaka kusema. Msimu wa maigizo huu nasema.  “Nimezunguka kwenye maduka ya nguo za watoto na nguo  yaani ya bei ya chini ni elfu thelathini”.  Unaona! Nilijua tu wakati aliposema unajua kwamba alihitaji kunishirikisha kwenye igizo lake na ‘skiript’ yangu ilihusu kutoa hela. Nikaamua kugoma nay eye kanuna hadi siku kuu iiishe.

Ala! Hivi haya maigizo yooote haya kwa ajiri ya siku moja tu!? Kweli umaskini ni mzigo mzito tulioubeba kwa gharama ya ujinga wetu wenyewe, naapa simo humu. Yaani mtoto wa Kabwela havai nguo mpya hadi siku kuu!!? Na hizi nguo za watoto wadogo hata miaka miwili bado mwawanunulia suti za elfu hamsini, ndiyo mapenzi ama!!? Naapa Chokoraa sikipendi kitegemezi changu kama ndiyo hivi.

Nasema msimu huu, nyie igizeni ila msinishirkishe kwenye ‘skript’ zenu kwa vile nimeanza kugundua huu mchezo wa kushirikishana kwenye maigizo ni bora unishirkishe kutia voko kwenye wimbo kuliko hivi.

Huu ni msimu ambao hata akina Chokoraa wa Muhangaikaji wanatumia vile visenti vyao vya akiba walivyoweka chini ya mchago kwa takribani mwaka mzima ati kwa ajiri ya ‘siku kuu’ na baada ya msimu huu tu, wanabaki hoi! Igizo hilo Chokoraa sichezi, niiteni mshamba kama mnadhani mnanikomoa. Ala! Hivi mwaniona sina akili eti!!
Ona hawa wengine, wanaiba, wanakopa na hata kuuza sehemu ya thamani zao ili nao wakaigize furaha kwenye mabaa na vilabu vya kidugugu bila kujua kwamba wanatoboa mifuko kwa ajiri ya wawekezaji wa nje na ndani ilhali wao wakibaki kapuku tu. Nani kasema furaha ni kunywa kidugugu na kulewa ukarudi nyumbani na kuanza kuwasemesha watoto wako ‘kikoloni’ ilhali hela yao ya ada umeinywa kwa kujidanganya ati Mungu anajua! Nasema Mungu anajua. Anajua kwamba kwa ukorofi wako tu umeinywa ada yao na kwamba atakutia adabu kwa kukufanyisha kazi kama punda na hata kukukosesha usingizi usiku ukiwaza ada mwezi mmoja tu baada ya mwezi wa maigizo. Humu namo simo. 

Nakutakieni siku kuu njema enyi waigiza akina Kapuku, Kabwela, Pangu pakavu, na bila kuwasahau wadogo zangu wapenzi Sharobaro na Sista Du ila mwenzenu msimu huu kwenye maigizo yenu sichezi ‘skripti’ hata moja isipokuwa mimi ninalo igizo langu nalo ni kuwachekeni mnavyojitia umaskini kwa jina la sikukuu na kusherehekea.

Aaaaaah ha ha ha ha ha!! Simo, tena simo kabisaaaaa!!!!.

Friday, December 23, 2011

Salaam, nawasalimia.


Ole wangu Chokoraa!!
Ndiyo, nasema mpaka sasa mwaka ulikuwa unakuja vizuri japokuwa kusema kweli hapa kati kati sijapata kuwaandikieni enyi wana wa nchi ya Wadanganyika si kwa  sababu niliwasahau ama niliwadharau, la hasa! Isipokuwa kwa vile nilipata safari ya ghafla sana kuelekea kijiji kimoja kwenye nchi ya Wahangaikaji, kijiji maarufu kuliko vyote ambacho hutembelewa na wenye nazo na wasio nazo kijulikanacho kama “Busy”.

Ndiyo, nilikuwa “busy” japokuwa matamshi ya jina la kijiji ni “Bize”. Basi bwana! Huko kwenye kijiji cha bize nilipata bahati ya kukutana na jamaa zangu wa zamani sana na hata yule dada mkubwa Changudoa nilikutana naye japokuwa kusema kweli kazeeka. Ndiyo.  Uzee huuchakaza mwili japo roho hubaki shujaa labda kwa vile madhira mengi yaupatayo moyo hupitia kwanza kwenye mwili na dada Changudoa mwili wake uliishaikosa thamani siku nyingi pale wazazi wetu walipotuacha wadogo yeye akilazimika 'kutumikia' makafiri ili walau sisi wadogo zake akina Chokoraa tupate kwenda shule. Hayo nitakuadithia siku nyingine.

Lakini nilipofika Bize nikajikuta nimekawia kurudi  kuliko nilivyotarajia na si kwa sababu napapenda huku bize isipokuwa kwa sababu majalala ya huku yanaonekana kila mara misosi inapungua na ninadhani ni kwa sababu ya ongezeko la wadogo zangu wengi ilhali nyie wenye nacho mmeacha kutupa kwenye majalala siku hizi ati kwa ajiri ya kulinda usafi wa miji kwa hivyo msipoteketeza  hayo mabaki ya chakula mnayoita ‘taka’ kwa njia ya ‘kuyainsenereiti’ basi kwa uroho tu wa kutotaka na sisi machokoraa walau tufaudu kile mnachobakiza, ati ‘mnayarisaiko’ ili muendelee kutumia wenyewe kila mnachozalisha na mnachobakiza baada ya matumizi. Humu namo simo. 

Naam, ole hii sasa imenipata baada ya kurudi kwenye jiji langu hili nilipendalo saaana la Bongo mahala ambapo huitaji kuwa na ‘ilimu’ (hasa ya mfumo rasmi) ili kufanikisha mambo na pia hakuna anayejari hata ushauri wa kitaalamu wa watalaamu waliopata utaalamu kwa gharama ya babu yangu Kabwela akiwekeza kwao kwa vile alidhani wangesaidia kuboresha maisha ya mzee wangu Muhangaikaji ili mimi mjukuu wake niionje pepo hapa hapa duniani, ila ujio wa “wabongo” wenye kutumia tu ubongo bila kufuata hata utaratibu na kanuni almuradi wanapata wanachotaka ukaharibu mambo kwenye hii nchi ya Wadangayika Walipa kodi, nasema hili nitakuandikia waraka maalumu nikukumbushe maana najua wajifanya umesahahu.

Nilipoingia tu kwenye jiji la watumia ubongo, ati nikakuta kwa siku mbili mfululizo mbingu zilikuwa na kilio na machozi yake yakawa yanawamwagika kwenye jiji la watumia ubongo ila kutokana na uchungu mwingi uliokuwa kwenye moyo wa mbingu, basi machozi yake yalikuwa mengi yakifanya mifereji mikubwa ya maji kushindwa kutiririsha maji vile yalivyotakiwa na kuvunjilia mbali madaraja, kuingia kwenye vibanda vya walalahoi na kuvivunjilia mbali na japo hilo halikuniuma sana maana mimi nalala popote tu (kama imevunja madaraja nitahamia kwenye mitaro ama sokoni), kilichoniuma ni ukweli kwamba machozi ya mbingu yamefurumusha majalala yote na sasa ninalazimika kurudi bize kwa vile sasa msosi ni ngumu kupatikana kwa  ‘kawaida’ huku bongo.

Kuna swali hata hivyo mzee Kabwela alinituma niwaulize watawala na wakaazi wote  wa  nchi ya Wadangayika nalo ni je! Mmejiandaa kukabiliana na  mlipuko wa magonjwa utakaofuata baada ya mbingu kufuta machozi?” maana mzee Kabwela anasema ndicho kinachofuata na kusema kweli huyu mzee maneno yake huwa hayapotei. 

Salaam, nawasilimia miye Chokoraa wa Muhangaikaji.

Friday, December 9, 2011

"Shikamoo Mheshimiwa."


Nani kasema ati kwa vile mimi ni Chokoraa basi sina adabu!? Ninazo adabu, tena tele na wala usinifananishe Chokoraa mimi na ati hawa muwaitao ‘Sharobaro’. Simo humo. Ala! Ati mwaniona Chokoraa miye kuwa mshamba na wakuja ati kwa vile navaa sarawili ya kitambaa na kuchomekea!!? Kwanza huu si uvaaji wangu, lakini nasema siwezi katu kuita ati ni kupendeza kuvaa nusu uchi, ilhali mtoto wa kiume ukiacha sehemu ya makalio yako nje na kutuonyesha nguo zako za ndani. Si ni u- daudi kameruni sasa huu!! Naapa simo.

Lakini wakati Chokoraa ninapotetea adabu yangu, na kusema kweli adabu ya kwangu si ya vocha ati huwa inaisha mpaka ‘kulichaji’, bado najiuliza; hivi ni kweli kwamba heshima ni Shikamoo!!?.

Nasema Chokoraa miye kwa vile nijuavyo mimi “shikamoo” ni neno lenye asili ya ukoloni ndani yake hasa kwa vile lilitoholewa toka kwa watawala wa Kiarabu na maana yake ni “Niko chini ya miguu yako” na ndiyo maana jibu lake siku zote huwa ni “Marhaba” yaani “sawasawa”. Sasa naomba kuuliza, hivi ni kweli kwamba Chokoraa miye niko chini ya miguu ya mtu yeyote!? Nani kasema? Wengine miguu yao ina machacha na soksi hawafui na mnataka Chokoraa nikae chini ya miguu yao!? Mwaniona sina akili eti!!!.

Wengine nao, miguu yao kutwa kucha kuvaa skuna na wanchoma kumoyo zenye visigino vikali na ole wangu wakinikanyaga katika juhudi yangu ya ‘kuwa chini ya miguu yao’, nitakoma mwana wa Muhangaikaji nasema. Hilo si langu leo, ila naapa nitalizungumzia muda si mrefu hili la ‘heshima ya shikamoo’ lakini leo nataka kumwamkia mheshimiwa. Shikamoo Mheshimiwa.

Nimeona nianze kwa kukuamkia Mheshimiwa, si kwa vile wanizidi umri (hasa kwa sababu kwa mila na desturi hicho pekee kilipaswa kuwa kigezo cha mimi kukuamkua) lakini hasa kwa vile kwa kipindi kifupi tu umeweza kujibadilisha kabisa na kuwa mtu mwingine kabisa. Nasema kama ningekuwa nimesoma sana ningekwambia umepitia kile kiitwacho na wasomi ‘metamorphosis’ kwa sababu kabla ya kuanza ‘kampeni za uchafuzi’ wewe ulikuwa ukiitwa Chokoraa Muhangaikaji na ulijulikana huku mtaani kama  rafiki na kijiweni tulikuita ama ‘mshikaji’ ‘msela’ ‘mwana’ na kwa wale waliokuwa karibu zaidi walikuita ‘jembe’ ingawa nafikiri hukuwa lile la mkono.

Mabadiliko makubwa yaliyofuatia baada ya sisi ndugu, jamaa na marafiki (majembe, washikaji na hata washika dau) kukupigia kampeni ili kukuweka uwe msemaji wetu sisi ndugu zako na kukupa nguvu ya ‘kula’ ili uwe na sauti na nguvu za kututetea kwenye mabaraza ya maamuzi, ghafla umebadilisha jina sasa unaitwa ‘Mheshimiwa’.
Chokoraa mimi sina ugomvi na hilo kwa vile hasa ninaamini kwamba ni kwa sababu nilikuamini na kukuheshimu kiasi cha kuona kwamba wewe ungefaa kuwa mwakilishi wangu huko kwenye baraza la maamuzi hata nikakupa ‘kula’ yangu na kuwaacha vitegemezi vyangu vikifa njaa na hiyo ni heshima kubwa ya kukufanya ustahili kuitwa “Mheshimiwa” na ndiyo maana sipendekezi hata kidogo ubadilishe tena jina, lakini ninachojiuliza ni kwanini umeamua hata kubadili ubini wako ama jina lako lote!? Ndiyo. Hata unapozungumza na mimi, naam, mimi mpiganaji wako, mpiga kura ili kukupa ‘kula’ bado unajiita “Mheshimiwa” kana kwamba unajiheshimu kuliko kusubiri mimi nikuheshimu na hapo naanza kujiuliza hivi unachojaribu kuniambia ni kwamba mimi ndiye “Mdharauliwa” au!!?.

Ala! Wajifanya hunielewi sasa! Naapa dunia hii kweli kigeugeu, nimeona miye kilembwe wa Pangu pakavu.  Kwani hujui kwamba hakuwezi kuwa na mfupi kama hakuna mrefu, mke kama hakuna mume, babu kama hakuna mjukuu, polisi kama hakuna mhalifu na Mheshimiwa kama hakuna mdharauliwa?.

Nakuuliza wewe uliyekosa nidhamu kiasi cha kuniita mimi niliyekusomesha kwa kodi yangu na kukuchagua kwa kura yangu ili upate nguvu ya ‘kula’ upate kunitumikia leo unajiita kwa nguvu zote “Mheshimiwa” hata mbele yangu mimi niliye mwajiri wako, nani unayedhani ni “Mdharauliwa”?.

Unaposimama mbele ya wananchi waliokusikiliza kwenye kampeni na kukupa nguvu yao ya ‘kula’, watu uliozaliwa kwao, ukakulia kwao, ukasoma nao, na mara nyingine umeoa ama kuolewa kwao na kuanza kujitambulisha kwa kusema “Naitwa “Mheshimiwa Chokoraa wa Muhangaikaji” unadhani hawa watu wooote hawakujui kwamba wewe ni “Chokoraa wa Muhangaikaji” na kwamba hilo la Mheshimiwa si jina lako bali cheo chako ambacho huna haja ya kukirudia kwa vile wote tunakifahamu?. Naapa laiti angerudi yule mkufunzi aliyetembea na kifimbo akiwachapa wote walioonyesha kukosa adabu na kuvunja miiko na vijiko vya maadili yetu, angewafunza kwa nini yeye alipendelea kuitwa “Mwalimu” badala ya “Mtukufu” na kwamba mara nyingi alipomzungumzia mkulu wa kaya alimwita “Ndugu” rais. Labda kwa sababu hakujua kwamba kwenye Kaya hii hakukuwa tena na ndugu bali makundi ya watu yakiwekwa kwenye mafungu makubwa mawili ya Waheshimiwa na Wadharauliwa.

Nasema humu simo, ila kwa sababu Chokoraa miye nimefunzwa adabu na huwa sipendi dharau, nakuamkua kwa heshima zote; “Shikamoo Mheshimiwa”.

"Natanguliza Shukrani"

Kumekuwako na huu msemo kwenye Kiswahili kwa miaka mingi sasa na ambao matumizi yake huonekana mara nyingi katika ama maandishi au husikika katika matamshi ya kila siku hasa katika mazungumzo yaliyo ‘rasmi’.  Natanguliza Shukurani.
Msemo huu pamoja na mambo mengine, wanikumbusha kipindi kileeee cha enzi zileeeee wakati shule zetu za msingi zilipokuwa bado na masomo kama ‘Sayansi Kilimo, Maarifa ya Nyumbani, Sanaa na Uchoraji, Mwandiko, Kiswahili na Inglishi’ na kadhalika na mwalimu wangu wa somo la Kiswahili aliponifundisha uandishi wa barua aliniambia zilikuwako aina mbili.
 
Aina ya kwanza ya barua ilikuwa ni “Barua ya Kiofisi” ambayo ilitakiwa kuanza na neno ‘Ndugu’ (hasa kwa sababu sisi wote tulikuwa ndugu kabla ya kuzaliwa kundi la “Waheshimiwa” bila kueleza misingi ya “udharauliwa”) na kisha ilipaswa kufuatiwa na vikokoro vingine ikiwamo cheo cha huyo ‘ndugu’ anuani yake na kadhalika na kadhalika. Mwisho hata hivyo wa barua yenyewe niliambiwa nilipaswa kuandika neno “Natanguliza shukurani” kama njia ya kufunga barua yangu.
Sikuelewa, na kusema kweli hadi sasa sijaelewa ni kwa nini kama kweli natanguliza shukurani nilipaswa kuliandika hili mwisho wa barua wakati nilikuwa ‘naitanguliza’ hiyo shukurani yenyewe!!.

Katika kutafakari kwangu huku kudogo , nimefahamu pia kwamba kutanguliza kitu kwaweza pia kufanyika pale ambapo mwenye kutanguliza anavyo vitu vingi ambavyo anataka kuvibeba na hivyo analazimika kupeleka vitu kadhaa mbele yake ili iwe rahisi kwake kusafirisha vinavyobakia. Hili nalo huweza kueleza thamani  kati ya vile vinavyotangulizwa na vile vinavyobaki hasa kama usalama wa kule vinakotangulizwa hauaminiki sana, bila shaka ungependa kutanguliza vile ambavyo si hatari sana kuibiwa. Hili nitalizungumza siku nyingine lakini leo nataka kutanguliza shukurani
.
Ndiyo, kipaji ndiyo mtaji mkubwa alio nao binadamu, lakini hili ni zaidi sana kwa Chokoraa kama mimi na nafikiri ninacho kipawa cha kuandika. Ona sasa! Unaanza kukataa wakati umesoma mpaka hapa na kama ulidhani ni upuuzi ungekwishaacha zamani za mkoloni!!!. Kwa hiyo, natanguliza shukurani kwanza kwa Mwenyezi Mungu kwa kunijalia Chokoraa miye Mwana wa Muhangaikaji, Mjukuu wa Kabwela, Kitukuu wa Mlalahoi, Kilembwe wa Pangu pakavu, kuwa na kipaji cha kuandika. Natanguliza shukurani pia kwa kuniwezesha kupata nafasi ya kuingiza maandishi haya kwenye mtandao wa teke no lojia ya kisasa kwa ajiri yako ili ubukue kidogo yale ambayo nitakushirikisha kwenye bulogu hii.

Lakini kabla sijasimama kwa leo, nataka nitangulize shukurani kwa Yule ndugu yangu mmoja ambaye ikiwa nitaruhusiwa basi nitalitaja jina lake hadharani kabisa hapa ndani aliyenishauri kuacha kutumia ‘kikoloni’ kwenye maandishi yangu na kuanza kutumia Kiswahili kama lugha yangu ya kuwasilisha. Kwake huyu, naomba kusema: “Natanguliza shukurani zangu, utazikuta uko uendako” ila usiache kurudi hapa kesho maana kutakuwa na makala mpya kwa ajiri yako. Tena, natanguliza shukurani.