Aaaaaah ha ha ha ha ha!! Nicheke ninenepe Chokoraa wa Muhangaikaji, kitukuu wa Kabwela. Ati wanishangaa kwa nini naangua kicheko!? Mshangae kwanza na huyu anayedhani ati sina akili miye kucheka bila sababu. Hujui kucheka ni sababu tosha ya kucheka kwa sababu kwa hali ya maisha ya sasa hasa kwa Chokoraa hilo ndilo jambo aghali sana!? Basi pana mengi huyajui, naapa simo.
Nacheka, na si mara zote kucheka ni kufurahi kama ambavyo machozi ya Mamba hayana hata chembe ya huruma na nina hakika hilo walifahamu vyema, lakini humu simo leo. Nacheka kwa sababu huu ni msimu wa kuigiza na igizo la Chokoraa mara hii ni kicheko. Ndiyo, moja ya sifa kubwa za Chokoraa miye ni kwujaribu kupata raha kwenye maisha pasina kutumia gharama kubwa na kusema kweli ikiwa raha najipa mwenyewe hizo gharama atanitoza nani!? Niwacheni nicheke miye, ha ha ha ha ha ha!!!!!
Nasema umefika wakati wa maigizo ya Wadanyanyika walipa kodi na juzi nilishirikishwa kwenye ‘shuutingi’ na mama wa kitegemezi changu hasa kwa vile yeye igizo lake ni mlo na mavazi. Wacha kwanza nikupe ‘skriputi’ yanyewe ilivyokuwa.
Mara kisimu change cha mchina kikaanza kunitekenya mfukoni (huwa siweki mlio wa sauti kwa vile kina kelele na mara nyingine nikiwa jalalani kinawashtua paka na mbwa na kuwaambia na mimi nipo jalalani na kusababisha mashindano ya vipande vya mikate kuongezeka na mimi siku hizi kasi inapungua. Hilo nitakuhadithia siku nyinge. Basi bwana, nikakichomoa mfukoni na harakaharaka nikakipachika sikioni.
“Hivi unajua…!” mama wa kitegemezi changu huwa akisema hivi tayari nakuwa nimejua tu! Lakini sikutaka kumpa ‘krediti’ kwa hiyo nikaigiza “kutojua” wakati nilijua alichotaka kusema. Msimu wa maigizo huu nasema. “Nimezunguka kwenye maduka ya nguo za watoto na nguo yaani ya bei ya chini ni elfu thelathini”. Unaona! Nilijua tu wakati aliposema unajua kwamba alihitaji kunishirikisha kwenye igizo lake na ‘skiript’ yangu ilihusu kutoa hela. Nikaamua kugoma nay eye kanuna hadi siku kuu iiishe.
Ala! Hivi haya maigizo yooote haya kwa ajiri ya siku moja tu!? Kweli umaskini ni mzigo mzito tulioubeba kwa gharama ya ujinga wetu wenyewe, naapa simo humu. Yaani mtoto wa Kabwela havai nguo mpya hadi siku kuu!!? Na hizi nguo za watoto wadogo hata miaka miwili bado mwawanunulia suti za elfu hamsini, ndiyo mapenzi ama!!? Naapa Chokoraa sikipendi kitegemezi changu kama ndiyo hivi.
Nasema msimu huu, nyie igizeni ila msinishirkishe kwenye ‘skript’ zenu kwa vile nimeanza kugundua huu mchezo wa kushirikishana kwenye maigizo ni bora unishirkishe kutia voko kwenye wimbo kuliko hivi.
Huu ni msimu ambao hata akina Chokoraa wa Muhangaikaji wanatumia vile visenti vyao vya akiba walivyoweka chini ya mchago kwa takribani mwaka mzima ati kwa ajiri ya ‘siku kuu’ na baada ya msimu huu tu, wanabaki hoi! Igizo hilo Chokoraa sichezi, niiteni mshamba kama mnadhani mnanikomoa. Ala! Hivi mwaniona sina akili eti!!
Huu ni msimu ambao hata akina Chokoraa wa Muhangaikaji wanatumia vile visenti vyao vya akiba walivyoweka chini ya mchago kwa takribani mwaka mzima ati kwa ajiri ya ‘siku kuu’ na baada ya msimu huu tu, wanabaki hoi! Igizo hilo Chokoraa sichezi, niiteni mshamba kama mnadhani mnanikomoa. Ala! Hivi mwaniona sina akili eti!!
Ona hawa wengine, wanaiba, wanakopa na hata kuuza sehemu ya thamani zao ili nao wakaigize furaha kwenye mabaa na vilabu vya kidugugu bila kujua kwamba wanatoboa mifuko kwa ajiri ya wawekezaji wa nje na ndani ilhali wao wakibaki kapuku tu. Nani kasema furaha ni kunywa kidugugu na kulewa ukarudi nyumbani na kuanza kuwasemesha watoto wako ‘kikoloni’ ilhali hela yao ya ada umeinywa kwa kujidanganya ati Mungu anajua! Nasema Mungu anajua. Anajua kwamba kwa ukorofi wako tu umeinywa ada yao na kwamba atakutia adabu kwa kukufanyisha kazi kama punda na hata kukukosesha usingizi usiku ukiwaza ada mwezi mmoja tu baada ya mwezi wa maigizo. Humu namo simo.
Nakutakieni siku kuu njema enyi waigiza akina Kapuku, Kabwela, Pangu pakavu, na bila kuwasahau wadogo zangu wapenzi Sharobaro na Sista Du ila mwenzenu msimu huu kwenye maigizo yenu sichezi ‘skripti’ hata moja isipokuwa mimi ninalo igizo langu nalo ni kuwachekeni mnavyojitia umaskini kwa jina la sikukuu na kusherehekea.
Aaaaaah ha ha ha ha ha!! Simo, tena simo kabisaaaaa!!!!.
No comments:
Post a Comment