Kumekuwako na huu msemo kwenye Kiswahili kwa miaka mingi sasa na ambao matumizi yake huonekana mara nyingi katika ama maandishi au husikika katika matamshi ya kila siku hasa katika mazungumzo yaliyo ‘rasmi’. Natanguliza Shukurani.
Msemo huu pamoja na mambo mengine, wanikumbusha kipindi kileeee cha enzi zileeeee wakati shule zetu za msingi zilipokuwa bado na masomo kama ‘Sayansi Kilimo, Maarifa ya Nyumbani, Sanaa na Uchoraji, Mwandiko, Kiswahili na Inglishi’ na kadhalika na mwalimu wangu wa somo la Kiswahili aliponifundisha uandishi wa barua aliniambia zilikuwako aina mbili.
Aina ya kwanza ya barua ilikuwa ni “Barua ya Kiofisi” ambayo ilitakiwa kuanza na neno ‘Ndugu’ (hasa kwa sababu sisi wote tulikuwa ndugu kabla ya kuzaliwa kundi la “Waheshimiwa” bila kueleza misingi ya “udharauliwa”) na kisha ilipaswa kufuatiwa na vikokoro vingine ikiwamo cheo cha huyo ‘ndugu’ anuani yake na kadhalika na kadhalika. Mwisho hata hivyo wa barua yenyewe niliambiwa nilipaswa kuandika neno “Natanguliza shukurani” kama njia ya kufunga barua yangu.
Sikuelewa, na kusema kweli hadi sasa sijaelewa ni kwa nini kama kweli natanguliza shukurani nilipaswa kuliandika hili mwisho wa barua wakati nilikuwa ‘naitanguliza’ hiyo shukurani yenyewe!!.
Katika kutafakari kwangu huku kudogo , nimefahamu pia kwamba kutanguliza kitu kwaweza pia kufanyika pale ambapo mwenye kutanguliza anavyo vitu vingi ambavyo anataka kuvibeba na hivyo analazimika kupeleka vitu kadhaa mbele yake ili iwe rahisi kwake kusafirisha vinavyobakia. Hili nalo huweza kueleza thamani kati ya vile vinavyotangulizwa na vile vinavyobaki hasa kama usalama wa kule vinakotangulizwa hauaminiki sana, bila shaka ungependa kutanguliza vile ambavyo si hatari sana kuibiwa. Hili nitalizungumza siku nyingine lakini leo nataka kutanguliza shukurani
.
.
Ndiyo, kipaji ndiyo mtaji mkubwa alio nao binadamu, lakini hili ni zaidi sana kwa Chokoraa kama mimi na nafikiri ninacho kipawa cha kuandika. Ona sasa! Unaanza kukataa wakati umesoma mpaka hapa na kama ulidhani ni upuuzi ungekwishaacha zamani za mkoloni!!!. Kwa hiyo, natanguliza shukurani kwanza kwa Mwenyezi Mungu kwa kunijalia Chokoraa miye Mwana wa Muhangaikaji, Mjukuu wa Kabwela, Kitukuu wa Mlalahoi, Kilembwe wa Pangu pakavu, kuwa na kipaji cha kuandika. Natanguliza shukurani pia kwa kuniwezesha kupata nafasi ya kuingiza maandishi haya kwenye mtandao wa teke no lojia ya kisasa kwa ajiri yako ili ubukue kidogo yale ambayo nitakushirikisha kwenye bulogu hii.
Lakini kabla sijasimama kwa leo, nataka nitangulize shukurani kwa Yule ndugu yangu mmoja ambaye ikiwa nitaruhusiwa basi nitalitaja jina lake hadharani kabisa hapa ndani aliyenishauri kuacha kutumia ‘kikoloni’ kwenye maandishi yangu na kuanza kutumia Kiswahili kama lugha yangu ya kuwasilisha. Kwake huyu, naomba kusema: “Natanguliza shukurani zangu, utazikuta uko uendako” ila usiache kurudi hapa kesho maana kutakuwa na makala mpya kwa ajiri yako. Tena, natanguliza shukurani.
binafsi saluti kwako
ReplyDelete