Friday, December 9, 2011

"Shikamoo Mheshimiwa."


Nani kasema ati kwa vile mimi ni Chokoraa basi sina adabu!? Ninazo adabu, tena tele na wala usinifananishe Chokoraa mimi na ati hawa muwaitao ‘Sharobaro’. Simo humo. Ala! Ati mwaniona Chokoraa miye kuwa mshamba na wakuja ati kwa vile navaa sarawili ya kitambaa na kuchomekea!!? Kwanza huu si uvaaji wangu, lakini nasema siwezi katu kuita ati ni kupendeza kuvaa nusu uchi, ilhali mtoto wa kiume ukiacha sehemu ya makalio yako nje na kutuonyesha nguo zako za ndani. Si ni u- daudi kameruni sasa huu!! Naapa simo.

Lakini wakati Chokoraa ninapotetea adabu yangu, na kusema kweli adabu ya kwangu si ya vocha ati huwa inaisha mpaka ‘kulichaji’, bado najiuliza; hivi ni kweli kwamba heshima ni Shikamoo!!?.

Nasema Chokoraa miye kwa vile nijuavyo mimi “shikamoo” ni neno lenye asili ya ukoloni ndani yake hasa kwa vile lilitoholewa toka kwa watawala wa Kiarabu na maana yake ni “Niko chini ya miguu yako” na ndiyo maana jibu lake siku zote huwa ni “Marhaba” yaani “sawasawa”. Sasa naomba kuuliza, hivi ni kweli kwamba Chokoraa miye niko chini ya miguu ya mtu yeyote!? Nani kasema? Wengine miguu yao ina machacha na soksi hawafui na mnataka Chokoraa nikae chini ya miguu yao!? Mwaniona sina akili eti!!!.

Wengine nao, miguu yao kutwa kucha kuvaa skuna na wanchoma kumoyo zenye visigino vikali na ole wangu wakinikanyaga katika juhudi yangu ya ‘kuwa chini ya miguu yao’, nitakoma mwana wa Muhangaikaji nasema. Hilo si langu leo, ila naapa nitalizungumzia muda si mrefu hili la ‘heshima ya shikamoo’ lakini leo nataka kumwamkia mheshimiwa. Shikamoo Mheshimiwa.

Nimeona nianze kwa kukuamkia Mheshimiwa, si kwa vile wanizidi umri (hasa kwa sababu kwa mila na desturi hicho pekee kilipaswa kuwa kigezo cha mimi kukuamkua) lakini hasa kwa vile kwa kipindi kifupi tu umeweza kujibadilisha kabisa na kuwa mtu mwingine kabisa. Nasema kama ningekuwa nimesoma sana ningekwambia umepitia kile kiitwacho na wasomi ‘metamorphosis’ kwa sababu kabla ya kuanza ‘kampeni za uchafuzi’ wewe ulikuwa ukiitwa Chokoraa Muhangaikaji na ulijulikana huku mtaani kama  rafiki na kijiweni tulikuita ama ‘mshikaji’ ‘msela’ ‘mwana’ na kwa wale waliokuwa karibu zaidi walikuita ‘jembe’ ingawa nafikiri hukuwa lile la mkono.

Mabadiliko makubwa yaliyofuatia baada ya sisi ndugu, jamaa na marafiki (majembe, washikaji na hata washika dau) kukupigia kampeni ili kukuweka uwe msemaji wetu sisi ndugu zako na kukupa nguvu ya ‘kula’ ili uwe na sauti na nguvu za kututetea kwenye mabaraza ya maamuzi, ghafla umebadilisha jina sasa unaitwa ‘Mheshimiwa’.
Chokoraa mimi sina ugomvi na hilo kwa vile hasa ninaamini kwamba ni kwa sababu nilikuamini na kukuheshimu kiasi cha kuona kwamba wewe ungefaa kuwa mwakilishi wangu huko kwenye baraza la maamuzi hata nikakupa ‘kula’ yangu na kuwaacha vitegemezi vyangu vikifa njaa na hiyo ni heshima kubwa ya kukufanya ustahili kuitwa “Mheshimiwa” na ndiyo maana sipendekezi hata kidogo ubadilishe tena jina, lakini ninachojiuliza ni kwanini umeamua hata kubadili ubini wako ama jina lako lote!? Ndiyo. Hata unapozungumza na mimi, naam, mimi mpiganaji wako, mpiga kura ili kukupa ‘kula’ bado unajiita “Mheshimiwa” kana kwamba unajiheshimu kuliko kusubiri mimi nikuheshimu na hapo naanza kujiuliza hivi unachojaribu kuniambia ni kwamba mimi ndiye “Mdharauliwa” au!!?.

Ala! Wajifanya hunielewi sasa! Naapa dunia hii kweli kigeugeu, nimeona miye kilembwe wa Pangu pakavu.  Kwani hujui kwamba hakuwezi kuwa na mfupi kama hakuna mrefu, mke kama hakuna mume, babu kama hakuna mjukuu, polisi kama hakuna mhalifu na Mheshimiwa kama hakuna mdharauliwa?.

Nakuuliza wewe uliyekosa nidhamu kiasi cha kuniita mimi niliyekusomesha kwa kodi yangu na kukuchagua kwa kura yangu ili upate nguvu ya ‘kula’ upate kunitumikia leo unajiita kwa nguvu zote “Mheshimiwa” hata mbele yangu mimi niliye mwajiri wako, nani unayedhani ni “Mdharauliwa”?.

Unaposimama mbele ya wananchi waliokusikiliza kwenye kampeni na kukupa nguvu yao ya ‘kula’, watu uliozaliwa kwao, ukakulia kwao, ukasoma nao, na mara nyingine umeoa ama kuolewa kwao na kuanza kujitambulisha kwa kusema “Naitwa “Mheshimiwa Chokoraa wa Muhangaikaji” unadhani hawa watu wooote hawakujui kwamba wewe ni “Chokoraa wa Muhangaikaji” na kwamba hilo la Mheshimiwa si jina lako bali cheo chako ambacho huna haja ya kukirudia kwa vile wote tunakifahamu?. Naapa laiti angerudi yule mkufunzi aliyetembea na kifimbo akiwachapa wote walioonyesha kukosa adabu na kuvunja miiko na vijiko vya maadili yetu, angewafunza kwa nini yeye alipendelea kuitwa “Mwalimu” badala ya “Mtukufu” na kwamba mara nyingi alipomzungumzia mkulu wa kaya alimwita “Ndugu” rais. Labda kwa sababu hakujua kwamba kwenye Kaya hii hakukuwa tena na ndugu bali makundi ya watu yakiwekwa kwenye mafungu makubwa mawili ya Waheshimiwa na Wadharauliwa.

Nasema humu simo, ila kwa sababu Chokoraa miye nimefunzwa adabu na huwa sipendi dharau, nakuamkua kwa heshima zote; “Shikamoo Mheshimiwa”.

1 comment:

  1. du kaka uynanikosha sana kama c kunifunza kwa kauli zako zilizojaa ubunifu na kila aina ya mafunzo lakini shikamoo muheshimiwa kama sijakosea

    ReplyDelete