Ole wangu Chokoraa!!
Ndiyo, nasema mpaka sasa mwaka ulikuwa unakuja vizuri japokuwa kusema kweli hapa kati kati sijapata kuwaandikieni enyi wana wa nchi ya Wadanganyika si kwa sababu niliwasahau ama niliwadharau, la hasa! Isipokuwa kwa vile nilipata safari ya ghafla sana kuelekea kijiji kimoja kwenye nchi ya Wahangaikaji, kijiji maarufu kuliko vyote ambacho hutembelewa na wenye nazo na wasio nazo kijulikanacho kama “Busy”.
Ndiyo, nilikuwa “busy” japokuwa matamshi ya jina la kijiji ni “Bize”. Basi bwana! Huko kwenye kijiji cha bize nilipata bahati ya kukutana na jamaa zangu wa zamani sana na hata yule dada mkubwa Changudoa nilikutana naye japokuwa kusema kweli kazeeka. Ndiyo. Uzee huuchakaza mwili japo roho hubaki shujaa labda kwa vile madhira mengi yaupatayo moyo hupitia kwanza kwenye mwili na dada Changudoa mwili wake uliishaikosa thamani siku nyingi pale wazazi wetu walipotuacha wadogo yeye akilazimika 'kutumikia' makafiri ili walau sisi wadogo zake akina Chokoraa tupate kwenda shule. Hayo nitakuadithia siku nyingine.
Lakini nilipofika Bize nikajikuta nimekawia kurudi kuliko nilivyotarajia na si kwa sababu napapenda huku bize isipokuwa kwa sababu majalala ya huku yanaonekana kila mara misosi inapungua na ninadhani ni kwa sababu ya ongezeko la wadogo zangu wengi ilhali nyie wenye nacho mmeacha kutupa kwenye majalala siku hizi ati kwa ajiri ya kulinda usafi wa miji kwa hivyo msipoteketeza hayo mabaki ya chakula mnayoita ‘taka’ kwa njia ya ‘kuyainsenereiti’ basi kwa uroho tu wa kutotaka na sisi machokoraa walau tufaudu kile mnachobakiza, ati ‘mnayarisaiko’ ili muendelee kutumia wenyewe kila mnachozalisha na mnachobakiza baada ya matumizi. Humu namo simo.
Naam, ole hii sasa imenipata baada ya kurudi kwenye jiji langu hili nilipendalo saaana la Bongo mahala ambapo huitaji kuwa na ‘ilimu’ (hasa ya mfumo rasmi) ili kufanikisha mambo na pia hakuna anayejari hata ushauri wa kitaalamu wa watalaamu waliopata utaalamu kwa gharama ya babu yangu Kabwela akiwekeza kwao kwa vile alidhani wangesaidia kuboresha maisha ya mzee wangu Muhangaikaji ili mimi mjukuu wake niionje pepo hapa hapa duniani, ila ujio wa “wabongo” wenye kutumia tu ubongo bila kufuata hata utaratibu na kanuni almuradi wanapata wanachotaka ukaharibu mambo kwenye hii nchi ya Wadangayika Walipa kodi, nasema hili nitakuandikia waraka maalumu nikukumbushe maana najua wajifanya umesahahu.
Nilipoingia tu kwenye jiji la watumia ubongo, ati nikakuta kwa siku mbili mfululizo mbingu zilikuwa na kilio na machozi yake yakawa yanawamwagika kwenye jiji la watumia ubongo ila kutokana na uchungu mwingi uliokuwa kwenye moyo wa mbingu, basi machozi yake yalikuwa mengi yakifanya mifereji mikubwa ya maji kushindwa kutiririsha maji vile yalivyotakiwa na kuvunjilia mbali madaraja, kuingia kwenye vibanda vya walalahoi na kuvivunjilia mbali na japo hilo halikuniuma sana maana mimi nalala popote tu (kama imevunja madaraja nitahamia kwenye mitaro ama sokoni), kilichoniuma ni ukweli kwamba machozi ya mbingu yamefurumusha majalala yote na sasa ninalazimika kurudi bize kwa vile sasa msosi ni ngumu kupatikana kwa ‘kawaida’ huku bongo.
Kuna swali hata hivyo mzee Kabwela alinituma niwaulize watawala na wakaazi wote wa nchi ya Wadangayika nalo ni je! Mmejiandaa kukabiliana na mlipuko wa magonjwa utakaofuata baada ya mbingu kufuta machozi?” maana mzee Kabwela anasema ndicho kinachofuata na kusema kweli huyu mzee maneno yake huwa hayapotei.
Salaam, nawasilimia miye Chokoraa wa Muhangaikaji.
No comments:
Post a Comment