Saturday, January 14, 2012

Wadanganyika na Kelele za Mlango.

Ngoja kwanza nicheke. Ha ha ha ha ha ha ha!!! Nacheka miye Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangu Pakavu wa Kabwela wa Mdanganyika.  Leo, tofauti na siku zote ni furaha. Ndiyo, mwaka huu umeanza kwa mafanikio makubwa na kwa hilo namshukuru ‘Mulungu’. Ona huyu naye anakereka ati  kwa vile nimemwita kikwetu huyu ambaye yeye angetaka aitwe “God” ili ajiridhishe kwamba yeye ni mtumwa. Naapa simo. 


Nina furaha kwa vile mwaka huu Chokoraa nimepanda daraja, halafu nimepanda daraja mwanzoni mwa mwaka, ha ha ha ha ha ha!! Unashangaa!! Kwa sasa Chokoraa silali tena kwenye mitaro na huko hunikuti, nimepanga kichumba changu kimoja huku kwetu Uswazi kwenye kajumba ka mama Chausiku na hivyo silali tena chini ya daraja. Nani kasema hilo ni jambo dogo!?
Japo misosi yangu ni kule kule majalalani kama kawaida, lakini mara hii nafikiri hata majalala yangu itabidi yabadilike kidogo hasa kwa vile inabidi niwe kibiashara zaidi ili niweze kulipa kodi. Hilo nitakuhadithia ila leo, nataka kukueleza kero moja tu iliyonikuta. Kero ya mlango.


Kila mara “Ng’waaaaa!! Ng’waaaaaa!! Mlango huu wa bati unapiga kelele kila unapofunguliwa na Chokoraa hili linanikera  lakini kinachonishangaza ni kwamba mama Chau na watoto wake wala hilo haliwasumbui, nasema kweli mi nashangaa sana.  Ene wei, baada ya kuishi hapa walau kwa wiki mbili, nimeanza kuzoea hali hii na hivyo na mimi sasa naweza kulala na hiyo kelele hainisumbui sana isipokuwa pia hunisaidia nyakati fulani fulani, hilo nitakueleza siku nyingine.
Ndipo siku moja nikiwa nimejilaza hapa kwenye kitanda change cha kamba na hasa kwa vile siku hiyo nilikuwa sijatia kitu kinywani hadi hiyo saa sita ya usiku, nikabaki kuhesabu ‘kenchi’ na misumari na kupata nafasi ya kutafakari na hata kuzilinganisha kero za hapa kwa mama Chau na kero za kelele za wadanganyika walipa kodi kama ambavyo nimekuwa nikishuhudia kwenye kurasa za magazeti. 


Ngoja kwanza! Nani kasema Chokoraa huwa sisomi magazeti!? Mwongo. Huwa sinunui magazeti hasa kwa vile matukio mengi yanayotokea huku mtaani huwa nayaona mwenyewe na sitaki kuyanunua tena yakishatiwa nakshi za wino hasa kwa vile huwa tayari yamechakachuliwa ili kuleta radha ya si hasa, lakini huwa nasoma magazeti na hapa kwangu si ajabu ukakuta magazeti kadha wa kadha  kuanzia yale yaliyofungiwa maandazi, vitumbua, samaki au hata chips dume na kila nipatapo nafasi huwa najisomea hivyo vipande na usiniambie eti siyo magazeti. 


Ndiyo. Nakumbuka Wadanganyika walivyokuwa wamedanganyika na kuhamasika hadi kutaka kuingia barabarani  kuandaa mana ili iliwe na watoto wao baada yao ati kwa vile walichoshwa kula nyama ilhali wakifyatua matofari ya utumwa na hivyo wakajiandaa kuandaa mana. Weeee!!! Koma. Kwani waliandaa mana hata hivyo!? Wapiii!! Walifanya maandalizi yao yoote na matangazo na kila kitu halafu ati kuna jamaa mmoja mwema katika wema wake akagundua kuna mashababi mjini wanataka ati kuwadungua wadanganyika wote watakao andaa mana, basi kwa wema wake akawaonya wadangayika na wao wakanyewa kimyaaa!!  Ama kweli rahisi sana kuwadanganya wadanganyika.


Ni juzi tu wakati nasoma hiki kipande cha gazeti kuhusu hayo maandalizi ya kuandaa mana na jinsi yalivyozimwa kwa wema wa mwema na vijana wake, ndipo nilipogundua kumbe  wadanganyika wengi wanaishi kama milango ya nyumba ya mama Chausiku. Nasema usidhani nakutusi ewe mdanganyika mlipa kodi, lakini nakuuliza, ziko wapi zile hasira ulizokuwa nazo na kampeni kubwa ulizofanya ili kuandaa mana kwa ajiri ya kizazi kijacho baada yako hasa kwa kuzingatia kwamba ikiwa hivyo vijisenti yako uchwara vingelipwa kwa ajiri ya kusafisha hilo “Doa la Nzi” kwenye shati jeusi lenye harufu ya kinyesi, basi vizazi vijavyo vingepata hasira itokanayo na hasara na hata kufikia kuukana udanganyika wao?! Kwani hao mashababi walikuwa wangapi hata nchi nzima inasiamama wima kuwaacha hawa jamaa wapite!? Hata kama walikuwa wengi na waliojisheheneza sira nzitonzito na za maangamizi, walikuwa wapi na walikusudia kukaa muda gani au ndiyo wamehamia na hivyo sasa hatuwezi kufanya lolote kwa sababu kila tutakapojaribu kutoka nje ya milango yetu basi tutapambana na hawa mashababi!!? Nafikiri katika wema wake, huyu nduyu yetu mwema angetwambia basi kwamba hawa mashababi ama wamedibitiwa au wamekwishaondoka na hivyo tuendelee na maandalizi yetu ya kuandaa mana ili kizazi chetu kisifie jangwani kwa ukosefu wa chakula!. Humu mimi simo. 


Nikakumbuka pia kwamba baada ya maandalizi ya mana kushindikana,  waheshimiwa wawili akina Mbu na Nge nao wakaja kwa umoja wao wa Mbu-Nge kutaka nyogeza ya posho na hapa wadanganyika wakakasirika hadi povu kuwatoka midomoni. Nikahisi labda mara hii, wadanganyika hawa hawatadangayika. Wapi!! Kwa mara nyingine wakazidiwa na kile kibinti huwa nakiona kwenye vile visanduku vya picha kikisema kwa sauti kubwa “Sidanganyikiii” maana wandanganyika ghafla wakadanganyika na matukio ya mafuriko na mengineyo na kusahahu kwamba kuna visenti vyao kibao vyaliwa na ule umoja wa “Mbu-Nge”  na wao wakibakia kuwa wadanganyika walipa kodi. 


Mara mlango wa nje wa hapa nyumbani kwa mama chiku ukasukumwa ila mara hii polepole nafikiri kwa vile huyu anayefungua anajua kwamba watu wameanza kulala na hataki kuwasumbua na hivyo japo ulipiga kelele kama kawaida yake, lakini bado nasikia mikoromo ya usingizi ya mama Chiku na vitegemezi vyake ndipi nikakumbuka, kweli kele za mlango, hazimzuii mwenye nyumba kuuchapa.

Mi ninaomba kuuliza, hivi Wadanganyika mnaugua ugonjwa gani huu!!? Nasema usikasirike na wala usininune na hata ukinuna mi nina manati ya ndhungu sikuogopi ng'o! wacha nikuuliza na jibu nalitaka. Kwanza, mlitaka kuandamana ili kushinikiza sirikali isiwalipe "Doa la Nzi" mabilioni ya visenti vyenu vya madafu, mkachapwa mkwara na yule jamaa mwema mwenye kuwatendea wema hata wasio wema akiwaambia ati kulikuwa na tishio la wale mashababi, mkanywea. Hivi hilo tishio halijesha au ndo mmekubali kuliwa enyi 'wapinga kula'!? Nasema yule mwema katika wema wake atwambie kama wale mashababi wamekwishaondoka na kurudi kupamba na Kenya na Amisomi ili Chokoraa niandamane maana bado nataka kuandamana. Hamtaki kuhoji nawauliza wadanganyika mwaumwa ugonjwa gani?!. Wabunge walipojiongezea posho, mkaandika mpaka kwenye bulogu zenu, mkanuna hadi sura kuwavimba na kisha haoooo mkanywea. Nawauliza, hivi juhudi zenu zimefikia wapi ama mmebakia kuwa milango ya bati na bawaba kavu zenye kupiga kelele nyingi hata kwa kuguswa na mende ilhali mkiwaacha wenye nyumba yenye siri kali walele fofofo!!? Simo, nasema simo tena mntioe humu simo kabisaaaaaaaa.

Salaam nakusamilia,  ni mimi nduguyo Chokoraa wa Muhangaikaji ,wa Mlalahoi, wa Pangu Pakavu, wa Kabwela ,wa Mdanganyika.

Tuesday, January 3, 2012

Usalama usio salama wa Barabarani.


Kiherehere hiki!
Leo ati Chokoraa na mimi nimejikusanya na baadhi ya wananzengo hapa mtaani kwetu, tumekazunguka haka kasanduku kanakoonyesha sura za watu wakiongea na sauti zao twazisikia ati ninyi mwaita tivii. Uliza sasa tunaangalia nini! Duh! Nachoka miye mwana wa Muhangakaji kitukuu  wa Kabwela. 

Tumekaa tunaangalia Taarifa na Habari. Wewee!! Nani kasema nimekosea?! Nani!!! Tena!!! Angalia usiniudhi mapema nikazira kukuhadithia hata tukio lenyewe. Kwani ile ni “Taarifa ya Habari, Taarifa za Habari, Taarifa na Habari?!!. Nadhani lile baraza la wanaokifahamu Kiswahili kuliko sisi wengine inabidi watusaidie kwenye hili. 

Ala! Unaona sasa!! Hadi nimesahau nilichotaka kukwambia kwa vile umenitia hasira. Hata hivyo nadhani nimejaribu sana kutumia lugha yenu ya kistaarabu sana ilhali mi siifahamu hiyo lugha yenyewe. Wacha nitwange kichokoraa sasa ndo tuelewane. Simo.

Nasema kwenye hili la kulalamika na kunung’unika kwa kila kitu simo, tena simo hata kidogo, simo kabisaaaaa! Ala! Hivi, si kila mwisho na mwanzo wa mwaka kumekuwapo na lundo la ajari barabarani na nyingi zikisababishwa pamoja na mambo mengine uzembe wa madereva na kukosa ujuzi na sifa stahiki za kuendesha magari!? Kwani kuna mtu kati yetu hajui kwamba hali hii imechangiwa kwa kiasi kikubwa na uzembe wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama hasa wa barabarani yaani  ile mamlaka ya kuzibiti barabara na maji almaarufu kama ‘chuma tule’  na vikosi vya ‘usaha alama za barabarani’ kwa umoja wao? Hilo halinikasirishi hata hivyo.

Linalonikasirisha hadi nimewaandikia waraka huu, ni hili la wadanganyika walipa kodi kujifanya kulaumu “sirikali” kwa kila kinachofanywa hata kama ni kizuri. Hivi si nimeona mkipaza sauti mishipa ya shingo kuwasimama mkilalamikia kukatizwa safari zenu kwa sababu ya zoezi la ukaguzi wa “liseni’ za udereva ili kujua wale walio ‘liseni’ darasani kabla ya kuanza kuendesha na wale ambao wanaendesha bila kuanza ‘kuliseni’!! Nasema kwa hili mnitoe. 

Ona sasa. Yaani wakati watendanaji wa ‘sirikali’ walipojipanga ki ‘stratejiki’ kabisa kwa kuzingatia ‘taimingi’ ya muda ambao ajari zinazidi na kujaribu kuokoa maisha ya wadanganyika, mwalalama! Mwalalama nini enyi wana wa danganyika yetu!? Naapa simo humu.  Ona hyu naye anachukia ati kwa vile nachanganya kikoloni katikati ya sentensi zangu. Utajuaje kwamba “Nshomile mpaka fomu fooo!!!” Kalagabaho kama hujaelewa, kwani hilo mi Chokoraa lanihusu!? Simo nasema.

Nasema kwenye hili, badala ya hasira zangu kuzielekeza kwa hawa wana usalama japo si salama, ningezielekeza kwa wamiliki wa haya madude yaliyofanyika wajumbe wa malaika mtoa roho kila mwanzoni mwa kila mwaka. Washangaa nini!! Ningezielekeza hasira zangu kwao kwa vile kila mwajiri anapomwajiri dereva anamuuliza kuhusu leseni na ikiwa mwenye gari anaruhusu dereva asiye na leseni kuendesha gari lake, mwataka nisimwelekezee hasira zangu kwa nini!!? Naapa kwa hili tutashindana sana, lakini simo.

Halafu!! Ebu niwaulize enyi wana wa usalama japo si salama, huu utaratibu wenu wa kuvamia tu maeneno na kuanza kutekeleza majukumu yenu bila hata kuzingatia kwamba Chokoraa miye mwana wa Muhangaikaji, naam, mimi huyu mjukuu wa Mlalahoi kilembwe wa Kabwela, mara nyingine ninatoka nyumbani na tiketi tu na ziada ya shilingi elfu mbili kwa ajiri ya maji na nauli ya ‘bodaboda’ nikifika huko niendako na hayo mengine namuachia maulana, mmeianza lini!?

Naapa kwa ubabe huu sina hakika kama mnafanya ‘upolisi jamii’ kwa sababu mnashindwa kuzingatia mahitaji ya jamii yenyewe katika utekelezaji wa majumu yenu kwa sababu hasa mahitaji ya Chokoraa miye hayaishii kwenye kusafiri na kufika salama bali pia kuzingatia matumizi ya kila ‘shekeli’ (iite ‘sinyingi’ kama hilo ndilo jina ulipendalo) ninayoitumia na ninavyoitumia wakati wa safari na ndiyo maana japo naona kama lengo lilikuwa zuri lakini kwenye utekezaji wake simo, tena simo kabisaaa!.

Nasema iweni na huruma na maisha ya sisi wajukuu wa Pangu Pakavu kwa sababu kila mara tumekuwa tukisema tieni mchuzi lakini hamtaki, naapa simo. Hivi mnadhani wale wadogo zangu akina Mzembe na Mzururaji ambao walikuwa wameng’ng’ana kuishi mjini humu kwa kuningezea shughuli ya kuwalinda na kuwahudumia mimi kaka yao Mkubwa, tajiri wa ukoo kwa kipato cha kunanga, Chokoraa wa Kabwela, na sasa walikuwa wameamua kurudi kijijini, si wamehairisha baada ya magari kuchelewa kuondoka na wamerudi  kwenye lile pagala tunakojikusanya usiku na kujirundika tukipitiwa na usingizi ilhali tukiita huko ni kulala!?. Nasema hamjui ni kiasi gani ya gharama na maumivu ya moyo mmeniongezea mwaka huu na ndiyo kwanza unaanza. Naapa mpaka umelizike, tutaonana wabaya. Simo. 

Na nyie ‘chuma tule’ hivi kweli na akili zenu zoote  mmeshindwa kutengeneza ‘mpango mkakati’ (naogopa kusema ‘sitrateji’ msijesema napenda sana kikoloni) wa jinsi ya kukagua walio ‘liseni’ na kuwa lessen wale wasio nazo bila kunisumbua miye Mdanganyika Mlipa kodi!!? Naapa utaalamu umesafiri kwenye inchi ya wadanganyika walipa kodi. Simo, tena simo kabisaa.

Haya, tekelezeni majukumu yenu na wala msijesema mimi nawakataza kutekeleza majukumu yenu maana nafahamu mnayo sheria ya kuitumia kuniyamazisha miye hati kwa vile nimekuwa domo kaya wakati huyo ni mpwa wangu mimi jina langu ni lile lile le siku zote, Chokoraa wa Mdanganyika wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangu pakavu wa Kabwela.

Haha ha ha ha ha ha ha! Nicheke niongeze siku miye.

Salaam nawasalimia, 

Chokoraa wa Muhangaikaji.

Thursday, December 29, 2011

Nipe, nipe, nipe!!. Nipe Uprofesa wa Heshima



Ati mwashangaa!! Ndiyo, wakati mwaka 2011 unapofikia mwishoni, Chokoraa wa Muhangaikaji wa Pangu pakavu, wa Mlalahoi, wa Kabwela, wa Mdangayika nimepata faida moja kubwa na mwaka huu na hiyo ni kutambua haki yangu ya kupewa taito.

Nasema wewe unayenuna na kukasirika ni kwa sababu hupendi tu nikwambie ukweli kwamba ikiwa unatafuta kufanya tathmini ya mwaka kwa kutumia kigezo cha shekeli ulizonazo kwenye ‘kilindo’ , basi umepotea njia. Ndiyo.  Pamoja na kwamba pesa sabuni ya roho na penye udhia penyeza rupia, lakini kwenye hii dunia gunia yetu ya sasa, unahitaji pia kuwa kwenye ‘lokeisheni’ sahihi ili kuliona tundu la wewe kupenyeza lupia hapo penye udhia ili upate matokeo na kwa kuigundua siri hii nadai kutunukiwa heshima ya uprofesa wa kitaa.  Ngoja kwanza! Bado nakamilisha ‘risachi’ kabla sijaanza kuitumia mbinu hii kwa ajiri ya kujiletea maendeleo, ila nimeamua nikumegee walau kidogo ili usisumbuke kujiuliza ni kwanini waishiwa kila mara wanaonekana kupanda juu ilhali wadharauliwa tukibaki chini siku zote, humu namo simo.
Ikiwa utaamua kubishana na Profesa (mtarajiwa) Chokoraa kwenye hili nasema simo.  Ebu tazama pembeni yako uone. Wangapi umekua nao, umeishi nao na hata kufanya nao kazi na unao uhakika wa ‘asili elfu’ miamoja kwamba ‘kredenshozi’ zao na hata utendaji wao hauna hadhi wala sababu ya ‘kutunukiwa’ shahada ya udaktari ati wa falsafa wa heshima na kutengeneza kundi la mbumbumbu wenye majina yanayoanza na ‘Dk’ utadhani kuitwa ‘Dk’ kunabadili DNA na kumfanya mtu kuwa “royo klasi” kwa usiku mmoja tu, humu namo simo.

Huwezi kuamini kiasi na umbali wanaokwenda hawa jamaa kupata walau hiyo ‘taito’ ya utabibu, naapa utakasirika nikikueleza na ndiyo maana nashona domo langu nisibwabwaje kwa hasara ya kichwa changu na vitegemezi vyangu na hata yule kikongwe mke wa marehemu Muhangikaji, mkamwanae Mlalahoi, mama yangu Shida wa Matatizo.

Ngoja kwanza niendelee kukupa walau topic moja zaidi kwenye hili somo langu la “Kitaaolojia” ili nikiondoka darasani usibaki na maswali ni kwanini nataka ‘taito’ ya Prof. Chokoraa wa Muhangaikaji wa Kabwela wa Mlalahoi.  Ala! Ati washangaa mimi kuitwa Profesa! Washangaa nini ebu nikuulize kama alivyouliza papaa mawani mwaka ule iliponyesha mvua nyingi na watu wakalima na kuvuna sana upande mmoja lakini kwa ubovu wa miundo mbinu na migomo ya yule nyoka wenu wa chuma, wakati upande mwingine misosi ikiozea kwenye maghala,  upande wa pili wanadamu wakidodoka kwa kutokwa uhai kisa njaa na bado ati mwatunukiana shahada za udaktari wa falsafa, naapa simo. 

Ala! Kwani nani hajui kwamba wako baadhi yenu mliolazimika ‘kupolitiki’  ili kupata nafasi za kutunukiwa hizo tunu zilizotengwa kwa ajiri ya wana wa adamu waliojaariwa kuvumilia shida za shule na kukabiliana na magumu ya watu wao hata kupata hadhi ya kutunukiwa shahada zenye shada la maua kwa utumishi uliotukuka!!? Naapa simo humu.

Tena nasema mnitoe miye Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangu pakavu wa Kabwela wa Mdanyanyika. Nani kasema nataka kuhusika kwenye hili! Sasa hivi kila mmoja anataka kuitwa tabibu yaani “dokta’ hata kama anajua nafsini na moyoni kwamba hadi na heshima ya dokta ni mzigo wa mwiba ambao kuubeba kwake kutamuumiza lakini yu tayari kufa kikoloni na tai shingoni, nitoeni humu enyi wana.

Nasema, hizi ‘taito’ siku hizi zimegeuka kuwa ‘frontia’ ya mapambano kwenu wana za gunia hili bovu la dunia na athari zake zimekuja hadi huku kwenu wadanganyika na mimi simo. Kwani si mwanzo mlianza na “Uheshimiwa”!? Kila mmoja kwa juhudi na mbinu alizozijua yeye alipambana kwa kadri awezavyo ili kuwa muheshimiwa na mara mlipofika hapo mkagundua kwamba kumbe hata hapa hakuna jipya hasa kama mafanikio ya nje hayalingani na mafanikio ya ndani na hivyo “yu goti beta” mkaamua kutafuta kiwango kingine cha heshima mradi tu niwaheshimu mimi Mdangayika nisiwaze hata siku moja kuwa kama ninyi na ninaamini wala hamna mpango wa kurudi kujiita tena ndugu maana mnafahamu kwamba mimi na ninyi si ndugu tena, humu namo simo. 

Sasa mmeamua kuwa matabibu. Ha ha ha ha ha Nicheke ninenepe Chokoraa miye. Ati, kila mmoja wenu sasa akiishafika tu kwenye kiwango cha heshima kwenye jamii anadai utabibu wa falsafa!!.
Mwanikera enyi wana wacha niseme ukweli wa moyo ikiwa baada ya hapa sitasema tena walau mjue kwamba Mdanyika miye nakereka na huu upuuzi wenu. Ona hata wale waliopaswa kuchunga kondoo wa Mungu nao wamekuwa walevi. Ndiyo, wamekuwa walevi tena wa ulevi mbaya wa kinywaji kiitwacho uheshimiwa ambacho kikiisha kukuzoea huacha kukulevya na ndipo mnapotaka sasa mpate nyongeza ya ‘alikohili’ ya ‘Udakitari wa Falsafa” nasema simo. 

Kichefuchefu chanipata miye kila nisomapo majina yenu kwenye vyombo vya habari kila mara mkijitahidi kujiita madaktari ilihali nawajua wengi wenu nyie elimu zenu za ngumbalu na hata hayo mliyofanikisha si ninyi bali Mungu na ninayo hakika hakuwatuma muanze ‘kupolitiki’ ili kupata shahada za udaktari wa heshima, si hayo mgewaachia wana wa si hasa!!? Nasema humu simo. 

Utakuta mmeandikwa kwa herufi kubwa na wino uliokoza ‘Reverendi, Dokta Chokoraa wa Muhangaikaji” hivi huu ureverendi tu hauwatoshi mpaka na udaktari naapa ikiwa itakuja “taito alikoho” nyingine mtakuwa wa kwanza kukimbilia. 

Kwani kuchunga kondoo si ilipaswa kuwa kazi ya wito ambayo wale waliotangulia kabla yenu waliikata hadi Mungu (kwa vile yeye hashindwi na jambo) alipowalazimisha kufanya atakavyo yeye? Mbona nyie mwakimbilia kujipa majina makubwa hata kama mwajua mioyoni kwamba hamyastahili? Nasema kwenye hili hata kama mtasema nawakosea adabu, Chokoraa simo.

Mmezidiwa hata na ‘Mzanaki’ ambaye pamoja na kwamba alikuwa mmoja wa wadanganyika wa kwanza kabisa kupata shahada ya uzamivu na hata hiyo ya udakitari bado kwa unyenyekevu aliendelea kutaka aitwe “Mwalimu” hadi mwisho wa uhai wake, ati ninyi mliopaswa kuwa mabingwa wa unyenyekevu mnalilia majina ya utabibu. Nakataa kuhusishwa humu. 

Nimechoka kusema, naamini wanafunzi mmesikia na kuelewa na kama kuna maswali basi tukutane kwenye kipindi kijacho kwenye somo letu hili la “Kitaaolojia” na Profesa wenu Chokoraa wa Muhangaikaji, wa Mlalahoi, wa Pangu pakavu, wa Kabwela, wa Mdanganyika.
Simo humu.

Saturday, December 24, 2011

Igizo la sikuu la Chokoraa.



Aaaaaah ha ha ha ha ha!! Nicheke ninenepe Chokoraa wa Muhangaikaji, kitukuu wa Kabwela. Ati wanishangaa kwa nini naangua kicheko!? Mshangae kwanza na huyu anayedhani ati sina akili miye kucheka bila sababu. Hujui kucheka ni sababu tosha ya kucheka kwa sababu kwa hali ya maisha ya sasa hasa kwa Chokoraa hilo ndilo jambo aghali sana!? Basi pana mengi huyajui, naapa simo.

Nacheka, na si mara zote kucheka ni kufurahi kama ambavyo machozi ya Mamba hayana hata chembe ya huruma na nina hakika hilo walifahamu vyema, lakini humu simo leo.  Nacheka kwa sababu huu ni msimu wa kuigiza na igizo la Chokoraa mara hii ni kicheko.  Ndiyo, moja ya sifa kubwa za Chokoraa miye ni kwujaribu kupata raha kwenye maisha pasina kutumia gharama kubwa na kusema kweli ikiwa raha najipa mwenyewe hizo gharama atanitoza nani!? Niwacheni nicheke miye, ha ha ha ha ha ha!!!!!

Nasema umefika wakati wa maigizo ya Wadanyanyika walipa kodi na juzi nilishirikishwa kwenye ‘shuutingi’ na mama wa kitegemezi changu hasa kwa vile yeye igizo lake ni mlo na mavazi. Wacha kwanza nikupe ‘skriputi’ yanyewe ilivyokuwa.
Mara kisimu change cha mchina kikaanza kunitekenya mfukoni (huwa siweki mlio wa sauti kwa vile kina kelele na mara nyingine nikiwa jalalani kinawashtua paka na mbwa na kuwaambia na mimi nipo jalalani na kusababisha mashindano ya vipande vya mikate kuongezeka na mimi siku hizi kasi inapungua. Hilo nitakuhadithia siku nyinge. Basi bwana, nikakichomoa mfukoni na harakaharaka nikakipachika sikioni.
 “Hivi unajua…!” mama wa kitegemezi changu huwa akisema hivi tayari nakuwa nimejua tu! Lakini sikutaka kumpa ‘krediti’ kwa hiyo nikaigiza “kutojua” wakati nilijua alichotaka kusema. Msimu wa maigizo huu nasema.  “Nimezunguka kwenye maduka ya nguo za watoto na nguo  yaani ya bei ya chini ni elfu thelathini”.  Unaona! Nilijua tu wakati aliposema unajua kwamba alihitaji kunishirikisha kwenye igizo lake na ‘skiript’ yangu ilihusu kutoa hela. Nikaamua kugoma nay eye kanuna hadi siku kuu iiishe.

Ala! Hivi haya maigizo yooote haya kwa ajiri ya siku moja tu!? Kweli umaskini ni mzigo mzito tulioubeba kwa gharama ya ujinga wetu wenyewe, naapa simo humu. Yaani mtoto wa Kabwela havai nguo mpya hadi siku kuu!!? Na hizi nguo za watoto wadogo hata miaka miwili bado mwawanunulia suti za elfu hamsini, ndiyo mapenzi ama!!? Naapa Chokoraa sikipendi kitegemezi changu kama ndiyo hivi.

Nasema msimu huu, nyie igizeni ila msinishirkishe kwenye ‘skript’ zenu kwa vile nimeanza kugundua huu mchezo wa kushirikishana kwenye maigizo ni bora unishirkishe kutia voko kwenye wimbo kuliko hivi.

Huu ni msimu ambao hata akina Chokoraa wa Muhangaikaji wanatumia vile visenti vyao vya akiba walivyoweka chini ya mchago kwa takribani mwaka mzima ati kwa ajiri ya ‘siku kuu’ na baada ya msimu huu tu, wanabaki hoi! Igizo hilo Chokoraa sichezi, niiteni mshamba kama mnadhani mnanikomoa. Ala! Hivi mwaniona sina akili eti!!
Ona hawa wengine, wanaiba, wanakopa na hata kuuza sehemu ya thamani zao ili nao wakaigize furaha kwenye mabaa na vilabu vya kidugugu bila kujua kwamba wanatoboa mifuko kwa ajiri ya wawekezaji wa nje na ndani ilhali wao wakibaki kapuku tu. Nani kasema furaha ni kunywa kidugugu na kulewa ukarudi nyumbani na kuanza kuwasemesha watoto wako ‘kikoloni’ ilhali hela yao ya ada umeinywa kwa kujidanganya ati Mungu anajua! Nasema Mungu anajua. Anajua kwamba kwa ukorofi wako tu umeinywa ada yao na kwamba atakutia adabu kwa kukufanyisha kazi kama punda na hata kukukosesha usingizi usiku ukiwaza ada mwezi mmoja tu baada ya mwezi wa maigizo. Humu namo simo. 

Nakutakieni siku kuu njema enyi waigiza akina Kapuku, Kabwela, Pangu pakavu, na bila kuwasahau wadogo zangu wapenzi Sharobaro na Sista Du ila mwenzenu msimu huu kwenye maigizo yenu sichezi ‘skripti’ hata moja isipokuwa mimi ninalo igizo langu nalo ni kuwachekeni mnavyojitia umaskini kwa jina la sikukuu na kusherehekea.

Aaaaaah ha ha ha ha ha!! Simo, tena simo kabisaaaaa!!!!.

Friday, December 23, 2011

Salaam, nawasalimia.


Ole wangu Chokoraa!!
Ndiyo, nasema mpaka sasa mwaka ulikuwa unakuja vizuri japokuwa kusema kweli hapa kati kati sijapata kuwaandikieni enyi wana wa nchi ya Wadanganyika si kwa  sababu niliwasahau ama niliwadharau, la hasa! Isipokuwa kwa vile nilipata safari ya ghafla sana kuelekea kijiji kimoja kwenye nchi ya Wahangaikaji, kijiji maarufu kuliko vyote ambacho hutembelewa na wenye nazo na wasio nazo kijulikanacho kama “Busy”.

Ndiyo, nilikuwa “busy” japokuwa matamshi ya jina la kijiji ni “Bize”. Basi bwana! Huko kwenye kijiji cha bize nilipata bahati ya kukutana na jamaa zangu wa zamani sana na hata yule dada mkubwa Changudoa nilikutana naye japokuwa kusema kweli kazeeka. Ndiyo.  Uzee huuchakaza mwili japo roho hubaki shujaa labda kwa vile madhira mengi yaupatayo moyo hupitia kwanza kwenye mwili na dada Changudoa mwili wake uliishaikosa thamani siku nyingi pale wazazi wetu walipotuacha wadogo yeye akilazimika 'kutumikia' makafiri ili walau sisi wadogo zake akina Chokoraa tupate kwenda shule. Hayo nitakuadithia siku nyingine.

Lakini nilipofika Bize nikajikuta nimekawia kurudi  kuliko nilivyotarajia na si kwa sababu napapenda huku bize isipokuwa kwa sababu majalala ya huku yanaonekana kila mara misosi inapungua na ninadhani ni kwa sababu ya ongezeko la wadogo zangu wengi ilhali nyie wenye nacho mmeacha kutupa kwenye majalala siku hizi ati kwa ajiri ya kulinda usafi wa miji kwa hivyo msipoteketeza  hayo mabaki ya chakula mnayoita ‘taka’ kwa njia ya ‘kuyainsenereiti’ basi kwa uroho tu wa kutotaka na sisi machokoraa walau tufaudu kile mnachobakiza, ati ‘mnayarisaiko’ ili muendelee kutumia wenyewe kila mnachozalisha na mnachobakiza baada ya matumizi. Humu namo simo. 

Naam, ole hii sasa imenipata baada ya kurudi kwenye jiji langu hili nilipendalo saaana la Bongo mahala ambapo huitaji kuwa na ‘ilimu’ (hasa ya mfumo rasmi) ili kufanikisha mambo na pia hakuna anayejari hata ushauri wa kitaalamu wa watalaamu waliopata utaalamu kwa gharama ya babu yangu Kabwela akiwekeza kwao kwa vile alidhani wangesaidia kuboresha maisha ya mzee wangu Muhangaikaji ili mimi mjukuu wake niionje pepo hapa hapa duniani, ila ujio wa “wabongo” wenye kutumia tu ubongo bila kufuata hata utaratibu na kanuni almuradi wanapata wanachotaka ukaharibu mambo kwenye hii nchi ya Wadangayika Walipa kodi, nasema hili nitakuandikia waraka maalumu nikukumbushe maana najua wajifanya umesahahu.

Nilipoingia tu kwenye jiji la watumia ubongo, ati nikakuta kwa siku mbili mfululizo mbingu zilikuwa na kilio na machozi yake yakawa yanawamwagika kwenye jiji la watumia ubongo ila kutokana na uchungu mwingi uliokuwa kwenye moyo wa mbingu, basi machozi yake yalikuwa mengi yakifanya mifereji mikubwa ya maji kushindwa kutiririsha maji vile yalivyotakiwa na kuvunjilia mbali madaraja, kuingia kwenye vibanda vya walalahoi na kuvivunjilia mbali na japo hilo halikuniuma sana maana mimi nalala popote tu (kama imevunja madaraja nitahamia kwenye mitaro ama sokoni), kilichoniuma ni ukweli kwamba machozi ya mbingu yamefurumusha majalala yote na sasa ninalazimika kurudi bize kwa vile sasa msosi ni ngumu kupatikana kwa  ‘kawaida’ huku bongo.

Kuna swali hata hivyo mzee Kabwela alinituma niwaulize watawala na wakaazi wote  wa  nchi ya Wadangayika nalo ni je! Mmejiandaa kukabiliana na  mlipuko wa magonjwa utakaofuata baada ya mbingu kufuta machozi?” maana mzee Kabwela anasema ndicho kinachofuata na kusema kweli huyu mzee maneno yake huwa hayapotei. 

Salaam, nawasilimia miye Chokoraa wa Muhangaikaji.