Monday, April 22, 2013

TUKANANENI WAKATI WADANGANYIKA TWALIWA.



Salaam nawasalimia.
Nasema tofauti kati ya jana na leo hutambulika na mwerevu kwa mjinga ni usumbufu na mimi sina haja hata kuieleza tofauti yenyewe maana muda na nafasi havinitoshi, hivyo naishia tu kuwasalimu, salaam nawasalimia.
Ingawa Chokoraa mwana wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika nimekuwa mpenzi sana wa kale kamchezo ka kizazi hiki ka kuwa “bize”, kwa hili imenilazimu nikae chini ya ukuta wa pagala hasa baada ya kula kipande cha mkate niliiokota jana, niwatumieni salamu enyi ndugu zangu Wadanganyika walipa kodi. Ati! Wakataa nini kwamba wewe si Mdanganyika ama si Mlipa kodi!. 

Nasema juzi juzi binafsi nimeshuhudia akina kaka na dada ‘Muishiwa’ si tu wakibishana bali nimeshuhudia wakimwagiana mitusi na mara hii siyo tu ya nguoni bali hata ya msalani, mnisamehe.  Nasema ukubwa si miaka wala akili maana ikiwa utaamua kupima akili ya samaki kwa kumlazimisha kupanda mti, utaendelea kuwa mjinga kwa kudhani samaki hana akili na humu mnitoe.  Pia ukubwa si majukumu maana hata mtoto mchanga analo jukumu la kula na kulala na ikiwa atashindwa kulitekeleza vyema basi matabibu wataitwa ili waone kwanini ameshindwa jukumu lake, na humu najitoa. Ukubwa ni kutambua, kukubali na kuheshimu upana na mipaka ya majukumu yako tena kwa uadilifu mkubwa ingawa naapa si hizi uadilifu ni msamiati mpya kwenu nyie wana wa Mdanganyik mlio na umaarufu wa harufu na humu nitoeni. 

Ala! Ati mwataka sasa kwa vile na Chokoraa miye nimeghadhibika kwa kunichafulia shati langu jeusi kwa utomvu wenu wa nidhamu nimwage mitusi ili tufanane!? Sihusiki. 

Nauliza, kwani nyie wenye nguvu ya ukinzani kazi mliyopewa na Mdanganyika ni ipi? Nauliza ikiwa mlitumwa huko kilingeni ili mtumie uwezo wenu wa kukinzana ili mkinzane mpaka na yale yaliyo ya asili yetu kama busara na adabu!?. Nasema kwenye hili mi simo. Kwani hatuwezi kukinzana kwa hoja na hata tukaelewana bila kulazimika kutumia ubabe usio na faida? Si nimeshuhudia baadhi yenu mkitunisha misuli kujaribu kubaki kilingeni baada ya mwenyekigoda kutoa amri ya ‘auti’?.  Nani alidanganya nikadanganyika Chokoraa miye kwamba ati wenye nguvu ya ukinzani basi wanao pia uwezo madhubuti wa kuitumia nguvu hiyo kunitetea mimi na wadogo zangu wale wawili akina Mzembe na Mzururaji?. Si mmechomolewa mjengoni baada ya kupandishwa jazba kidogo na watu wakajipitishia ulaji wao bila hata haraka! Ha ha ha ha ha ha ha ha!!! Kama akili ni nywele basi kumbe ndiyo maana mwenye kigoda wenu naye kaamua kuzitia zake mafuta ya kizungu ili ziwe na mng’aro kwa waonao. Simo humu. Hivi kwani mlichokuwa mkijadili mle ndani ni maonevu mnayotendewa na ‘watwawala” ama mipango ya mapato na matumizi ya kodi ya Mdanganyika mlipa kodi!? Nasema mlipoamua kuendesha gari mkielekea usoni ilhali macho yako kwenye vioo pembe mlinunua shubiri kuitia mahala pa sukari na miye najitoa.

Ha ha ha ha ha ha ha!!! Nicheke kama mazuri mwana wa Kabwela miye. Ala! Kwani hamkujua nyie kwamba wakati jinsi ilipotumika kama kigezo pekee cha kuwachagulia mwenye kigoda, siyo tu makubaliano ya ajira kati yenu na mzee Mlipa Kodi yalivunjika, bali pia mlichumiwa vimbo ya akiba ili iwatieni adhabu pasina sababu wala adabu kwa wakati wake!? Naapa asiyeiona tofauti ya jana na leo kesho yake ina taabu na mimi simo. 

Haya, na nyie wenye kunitawala badala ya kuniongoza najiuliza nini kilikusukumeni na nyie kumwaga mitusi kedekede!?. Wenye ukinzani naweza kuwaelewa ikiwa wanaghadhibika na hata kutupa matusi ijapo kusema kweli sehemu kubwa ya kilichotamkwa ni kile ambacho zamani kiliitwa ‘maoni binafsi’ kwa vile ikiwa ninaamini kwamba ‘mdogo anamtawala mkubwa na nikasema hivyo’ kosa langu ni kuamkia salamu ya mchana ilhali ni asubihi hilo nalo ni ukosefu wa hekima, lakini walau nimekusalimia . Nasema naweza kuwaelewa kwa sababu yawezekana wanataka Mdanganyika mimi mwenye kukasirika nisipige mtu bali kura wakati ukifika wa hasira yangu niwapigie wao badala ya ninyi na hivyo wanchofanya ni kukutieni utomvu wa mashati yenu ‘matukufu’ kwa weupe wa mkorogo ili mchafuke, na mimi nauliza, ilikuwaje basi mkaamua kuyavua na kuyachovya wenyewe kwenye utomvu wa wakinzani wenu!? 

Hii michezo ya kukimbizana na kunguru aliyekwiba taulo lako ukiwa maliwatoni itakuponzeni naapa. Simo.
Hata hivyo si lengo langu kuwakosoeni bali kuwasalimia. Nasema mwisho wa yote binafsi nawasifu kwa ujuzi na weredi mkubwa mliionyesha kwa ama kutiana jazba na kutupana nje ya jengo huku mkiwa mmejipitishia bajeti za kutafuna kodi za wadanganyika bila tafakuri ya kina kwa vile wote mlikuwa kasi kurushiana mitusi na kuzinduka mshapitisha ulaji, na kwa kuwazidi akili Mbwa wa wadanganyika waliokabidhiwa jukumu la kulinda kodi zao hata mkazitafuna huku wao wakiwa bize kupandisha jazba. Ha ha ha ha ha ha ha!!!! Kweli, hamzumgumzi na mbwa na hata wenye mbwa hawana uwezo wa kuzungumza nayi.  Simo humu namo.

Salaama nawasalimia.

Saturday, January 19, 2013

BUNGE LIINGILIE KUPUSHA MGOGORO WA MTWARA




 Wananchi wakiondoka kwa amani kwenye mkutano uliofanyika juzi kwenye viwanja vya Bima ambapo mkutano wa leo umekwisha kwa vurugu..

Kwa sababu dunia imebadilika kiasi cha kuruhusu kila mtu kutoa maoni yake kwa urahisi na uhuru, na kwakuwa matumizi ya mitandao ya kijamii yametengeneza jukwaa pana zaidi kwetu sote kutumia nafasi na vipaji vyetu kuonyesha uwezo wetu, naamini ni kwa sababu hiyo baadhi ya wasomaji wangu japo kusema kweli ni wachache humu mtandaoni wananipa nafasi kubwa ya kusema kwao na hata wakakubali juu ya ninachokisema japo walio wengi wana sifa moja na mimi kwamba sisi ni watu wasio na nafasi huru  za kusema.

Ndiyo maana basi kwa hili nimeona vyema niseme kwa sababu wasomaji wangu hawa wanategemea niwe na cha kusema na kwa hilo Chokoraa nawaandikia. Siwaandikii hili wote mkubaliane na mimi lakini najaribu kwa kadri niwezavyo kupata uhuru wangu wa kusema.

Pamoja na kwamba nimekuwa Mtwara kwa karibu miezi sita sasa, leo nimepita katika mji wa Mtwara ukiwa katika kile ambacho kwangu binafsi kama Chokoraa kimenitisha. Nimeogopa. Nimetishwa na kuamka na kugundua kwamba kumbe Tanzania ile tuliyolala jana, inaweza kuamka ikiwa ni Tanzania nyingine ambayo watu wanaishi kwa hofu na mashaka kiasi hiki?

Mji wa Mtwara ulitanda askari Polisi waliokuwa wamejisheheneza vilivyo kwa ajiri ya kupambana na wananchi wa Mtwara waliokuwa  kwenye mkutano wa kupinga Gesi asilia kuondolewa Mtwara.

Inasemekana maandamano ya leo hayakukusidiwa kuwa maandamano ya fujo bali lengo lilikuwa kufanya mkutano mkubwa ambapo wananchi kutoka wilaya zote za  mikoa ya Lindi na Mtwara wangekutanika kwenye uwanja wa mashujaa ikiwa ni mwendelezo wa kuishinikiza serikali kutokuondoa gesi ghafi Mtwara.

Wakati maandalizi ya mkutano yakiendelea mara umeme ukakatika kwenye eno la mkutano na baadhi ya wananchi wakahisi hiyo ni hujuma kutaka mkutano usiendelee kama ulivyopangwa kwa vile vipaza sauti zisingefanya kazi bila umeme na ndipo kimbembe kilipoanza.  

Wananchi waliteremka mabarabarani na kuanza vurugu na fujo huku wakielekea zilipo ofisi za Tanesco na polisi wakaingia kuwadhibiti, kilichofuata ni milipuko ya mabomu, kurushwa mawe, magogo ya miti kupangwa barabarani na kufunga kabisa mji wa Mtwara. Barabara kuu ya Mtwara ilifungwa kabisa ambapo hakuna gari liliweza kupita barabara hiyo na hata makutano ya barabara eneo la Bima yalifungwa kwa magogo.

Maduka yalifungwa na mji mzima ulikuwa umepooza mnamo wa majira ya saa saba hadi tisa za jioni nilipojichomoa mjini na kuamua kujiridia kibandani kwangu kujificha na yatokanayo.

Si lengo langu kusema juu ya nini msimamo wangu binafsi juu ya hili kwenye makala hii  lakini niseme nilichokiona leo kimenitisha sana. Si kwa sababu nyingine yoyote bali kwa kuwa leo kwa mara ya kwanza (najua wako ambao wameshudia hili mara nyingi) nimeshuhudia barabara zikiwa zimefungwa kwa magogo ya miti, polisi wakiwama na siraha mikononi kukabiliana na wananchi waliokuwa na mawe na fimbo mikononi.

Kauli za waandamanaji wakifananisha mji huu na Libya ni jambo lingine lililonitisha. Wananchi wenye morali walisikika wazi wazi wakisema “Kama Libya…..damu itamwagika sana….” Na wengine kutishia askari Polisi wanaoishi uraiani kuhamishia familia zao kituoni.

Si lengo langu kusema juu ya nini msimamo wangu binafsi juu ya hili kwenye makala hii  lakini niseme nilichokiona leo kimenitisha sana. Si kwa sababu nyingine yoyote bali kwa kuwa leo kwa mara ya kwanza (najua wako ambao wameshudia hili mara nyingi) nimeshuhudia barabara zikiwa zimefungwa kwa magogo ya miti, polisi wakiwama na siraha mikononi kukabiliana na wananchi waliokuwa na mawe na fimbo mikononi.

Kilichonitisha zaidi ni pale ambapo mpaka sasa serikali imekaa kimya bila kutoa majibu yoyote kwa hoja za wananchi hawa na badala yake imeishia kudharau vuguvugu hili huku hali hiyo ikihatarisha usalama wa wananchi na amani ya nchi kwa ujumla.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ndiye kiongozi mkubwa kabisa mkoani humu ambaye kauli yake kwa wananchi imeibua kero na manung’uniko hata miongoni mwa maafisa wa serikali yenyewe pale alipowaita wananchi hawa ‘wapuuzi’ na wasiosoma.

Nasema kwa hili serikali itoe majibu yanayoeleweka kwa wananchi wake ama bunge lichukue hatua ya kuitana haraka na kuzungumza kuhusu jambo hili ama mgogoro mkubwa utakaobadili historia ya nchi unaweza kutokana na ukimya huu. Ikiwa bunge limekuwa likiunda tume kuchungunza mambo kama pesa zilizofichwa nje ambazo bado kitendawili chake hakikajulikana ikiwa ni kweli au si kweli, basi ni wakati bunge lichukue hatua kwa hili.

Wananchi bado wana imani na bunge lao japokuwa hawana imani na serikali na ni wakati wabunge ambao ndiyo waajiriwa wa wananchi kuisimamia serikali, waamke na kufanya kazi waliyotumwa na wananchi wao.

Kazi hii wala wasiachiwe wabunge wa Mtwara peke yao. Nasema hivi kwa sababu inaonekana wazi kwamba kazi hii imewashinda kwa sababu maneno haya hayakufikia hapa kwa kuzaliwa leo asubuhi na kufikia hali hii bali yamekuwako kwa wanajamii muda mrefu na ikiwa ama wabunge hawakujua kwa sababu hawana ukaribu na wananchi wao ama walijua na kudharau kwamba ni maneno ya hovyo, basi wameshindwa kuwa na uwezo wa kuaminiwa tena na wananchi kumaliza suala hili na hivyo ni wakati Bunge kama taasisi ijiingize kwenye hili.

Wananchi wanachotaka ni kusikilizwa na kupewa majibu kwa hoja zao na kwa kuwa wamepoteza imani na majibu yanayotolewa na serikali, ni wakati kwa ajiri ya amani ya nchi, taasisi ya Bunge ijiingize kwenye jambo hili kuepusha umwagaji damu mkubwa.

Nilipotazama kwamba wengi wa waandamanaji ni vijana wadogo ambao hata hawajawa na familia bado, nikajifunza kwamba hili litakuwa jambo gumu sana kulimaliza kwa ubabe kwa sababu kimsingi vijana hawa hawana cha kupoteza kwa kufanya wafanyao.

Wednesday, January 16, 2013

WADANGANYIKA: "GESI KWANZA, VYAMA BAADAYE". NAHUSIKAJE HUMU MIYE!!!?

Simo. Katika kile kinachoonekana kuwa hasira za Wadanganyika wa mkoa huu wa akina Njomba Nchumari, ntoto wa Chipoku kukataa suala la mtambo wa kurudufu Gesi kujengwa wilayani Kibaha Mkoani Pwani badala ya Mtwara, leo mkutano Mkubwa ulifanyika kwenye viwanja vya Bima na kuhudhuriwa na maelefu ya Wadanganyika walipa kodi na Chokoraa wa Muhangaikaji nilikuwapo kushuhudia hali ilivyokuwa japo simo, tena simo kabisaaaa. Ala!
"Kwa wale wote wanaotaka kumtumia salamu 'Mkulu wa kaya' kwamba wananchi wa Mtwara hawakatai gesi kutoka Mtwara bali wanakataa gesi kutoka ikiwa ghafi inueni mikono juu......". Matokeo yake ndiyo yaliyozaa picha hii. Nimo kwani humu?
 Hivi ndivyo wananchi walivyoonyesha hisia zao kwa 'Mkulu wa kaya' na Chokoraa nauliza; "Mkulu wa kaya unawasikia hawa?" ikiwa utaamua kuwapuuza mi sihusiki tena simo kabisaaaaaa.
Wadanganyika waliweka chini tofauti zao za dini, vyama na hata makabila na hapa kulikuwa na lugha moja tu, "Gesi kwanza, vyama baadaye". Simo naapa.
 Mwenyekiti wa Vijana wa Chama cha Wananchi (CUF) taifa Bw. Ahmad Katani alikuwa mmoja wa wazungumzaji kwenye mkutano huu na moja ya kauli zilizowakuna wasikilizaji wake ni hii "Hata akija mwenyekiti wa CUF taifa Prof. Ibrahim Lipumba na kusema Gesi iondoke, mtimueni.....". Nauliza humu Chokoraa nimo?.
 Hapa Bw. Katani akizungumza na Meza kuu.
"Mimi nimejitolea, naamini hata nikifa kwa kupigania maslahi na maendeleo ya watu nitaiona pepo pasipo shaka yoyote".
 Ilikuwa jioni muda wa watu kutoka makazini na hapa wanaonekana maafisa wa benki ya CRDB tawi la Mtwara wakijadiliana jambo pembezoni mwa uwanja wa mkutano. Simo humu namo.
 Pembezoni mwa barabara kuu eneo la Bima, wananchi wakisikiliza kilichokuwa kikiendelea kwenye mkutano wa CUF "Gesi kwanza vyama baadaye" Nahusikaje humu miye.
Mmoja wa wadau wa chokoraa blog naye alipitia hapa kusikia kisemwacho na wale wasemao na mimi sihusiki humu namo. Simo.
 Ha ha ha ha ha!!! Gheshi ra Porisi, ririkuwepo kuhakikisha usarama wa raia na mari sao". Simo humu.
 Mwenyekiti Ahmad akisisitiza jambo.
 Sehemu ya wananchi waliohudhuria.
Salamu za Pongezi zimetumwa kwa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara kwa kutotumia mabavu kwenye mikutano hii ya wananchi na Chokoraa natuma pongezi zangu kwa Kamanda wa Polisi Mkoa Bi. Marry Nzuki. "Hongera Kamanda.

Friday, November 23, 2012

Siraha zote zilinunuliwa kwa ajiri yako. Walalama nini zitumikapo!?



Nasema jina baya umuua mwenye nalo chambilecho wale waliokuwa kabla yetu na humu nasema simo. Kwenye hili la wazee wetu kukupa jina la marehemu babu yake na babu mzaa baba marehemu Mdanganyika, walikutia matatizoni we mwana na humu naapa unitoe. 

Kwani mi si nilikuwa nimekataa kwamba usipewe jina hilo lakini Yule shangazi yetu mke wa baba yetu mdogo Mstahiki wa Mheshimiwa akalazimisha na mwisho ukapewa jina ambalo leo lakusumbua ewe Mdanganyika Mlipakodi na humu mi simo nasema. 

Ebu kwanza nikupe pole maana siku hizi wanao wauana kama wanyama tu bila hata kujali na humu nasema mapema kabisa ili msijesema mi sikusema maana simo tena simo kabisaaa.   Nasema wakati walipotutoza kodi na kununua ‘manati za ndhungu’ nani alikudanganya kwamba zilikuwa kwa ajiri ya kuwindia ndege!? Ndege huwindwa kwa manati za asili na si manati za ndhungu zenye nguvu na mshindo wa radi na humu mi nitoeni. Ati! Msikie huyu naye! Kwamba zilinunuliwa kwa ajiri ya kulinda usalama wa kaya yetu hii!? Ha ha ha ha ha ha ha!! Nicheke miye kitukuu wa Pangupakavu maana nchi haikumaanisha akina nyie mzee Pangupakavu na wenzio bali kundi la akina kaka mkubwa Mheshimiwa na vitegemezi vyao na ndiposa na ninyi mnapotishia usalama wa maslahi ya vitegemezi vyao basi wakudungulieni mbali na humu mi nisihusishwe. 

Kwani si mmekuwa mkidunguliwa kila mwaka na hakuna hatua hata za miguu zinazochukuliwa dhidi ya wale waliopewa dhamana ya kushika manati kwa niaba yenu na kisha kukudungueni!? 

Nasema watu wanatumia vibaya vitu vilivyonunuliwa kwa fedha ya wazazi wako Bi Mwananchi na mzee Mlipakodi na sasa wamevigeuza vyombo hivyo kuwa zana za kukuangamizeni na humu simo.  

Nani kasema nahusika miye humu kwenye hili! Nasema wakati ‘wadunguaji’ hawa wanaendelea kulipwa mishahara ya kuwadungueni kwa fedha za baba yangu mzee Mdanganyika Mlipakodi, wana wa kaya ya wadanganyika sasa wako mashakani si kutoka kwa wale waliotarajiwa maana mvua ya msimu haibomoi nyumba ya mwenye akili kwa vile huchukua taadhari, lakini unafanyaje ikiwa dawa inageuka sumu na humu mi nitoeni. 

Hivi! Mbona mwaishi kama wasi kwao ilhali ninyi ni Wadanganyika na babu wa babu zenu walimwaga damu na hata kuutoa uhai si kwa ajiri yao bali kwa ajiri ya vizazi vyao ambavyo ndiyo mimi na wewe na sasa mwachinjana wenyewe kwa wenyewe kwa faida ya nani? Naapa ni heri muumba alivyokataza wafu kufufuka na kuona yawapatayo watoto wao baada yao maana sidhani Mkwawa, Kinjekitile na wenzao wengine wangekubali haya muyafanyao wacha huyu aliyeondoka juzi juzi tu Mzalendo Mwalimu wa Mkufunzi na humu mi sihusiki. 

Haya, tuwachilie mbali hayo ya wale waliokwenda maana baadhi yenu husema hao huwa wamepumzika na kwa miaka mingi nilikataa lakini sasa navutwa kukubali. Ndiyo. Uzee una mambo we mwana nisikize Chokoraa miye nikupashe leo na unisikize kwa makini. Shida ya uzee si kutojua njia na mwisho wa njia yenyewe isipokuwa nguvu za kuipita na msukosuko wa maisha ni kuona wale uliowapa nguvu na kuwakabidhi kijiti wakiiacha njia na kutumbukia maporini kwa vile huko huwezi kuwaona wafanyao na hata ukisema wanakucheka kwa viule huwezi kuwakimbiza na hapa namtumia salamu za pole mzee wa Uongo  na Uficho  kwa sababu kizazi hiki wazi twaficha na fichu twasema na humu mnitoe. Ala! Si aliwekeza juhudi ili kuifanya Danganyika ya wadanganyika walipa kodi isiitwe bongo ati kwa vile watu walikuwa wakiishi kwa kutegemea bongo sana kiasi cha  kuifanya kaya yetu kuwa pango la wanyang’anyi? Najiuliza, naye anasikitika na mimi ninaposikitika kuona kwamba  sasa hii ndiyo Bongo halisi na hivyo kumbe alishindwa vita vyake, ama nay eye alijigeuza msanii kwenye jengo la sanaa kuniigizia ili niamini maigizo nisione uhalisia? Naapa mi humu najitoa mapema maana simo. 

Ati washangaa! Washangaa nini we mwana ikiwa hadi dawa, narudia tena, dawa yaani ile mizizi niliyofundwa na babu yangu Pangupakavu kwamba ingeweza kutiba homa na tetekuwanga nayo mwaitia sumu almuradi mtajipatia chochote kitu kwa kufanya hivyo? Ha ha ha ha ha ha ha!!! Naapa wana wa kaya hii mmekosa aibu na hofu ya muumba na humu simo. 

Ati mwatengeneza dawa bandia na kuzitia sokon, matabibu mwawa wauaji halafu na nyie mnaketi kwenye viti vyenu vireefu mkigonganisha bilauri na kuwalaumu washika manati kwa kuuwa watu kila siku huku mkisahau ninyi mmeua wangapi! Naapa Nyani kweli huliona kundu la mwenzie na humu mi nitoeni.

Ndiposa Chokoraa nikasema jina baya humuua mwenye nalo maana Mdanyika wewe kweli umedanganyika. Umedanganyika kwamba ati ni kwa ajiri yako watu walinunua manati za ndhungu na kusema kweli zilinunuliwa kwa ajiri yako lakini ulidanganyika kudhani ni kwa ajiri ya kukulinda. Ha ha ha ha ha ha ha!!! Nicheke miye. Ulindwe we mwana wa Mlalahoi wa Kabwela una nini!? Zilinunuliwa kwa ajiri yako kwa vile walijua kwamba utaanza muda si mrefu kuuliza juu ya jinsi wanavyotumia kodi yako uwalipayo kila siku kwa kuendelea kuwa Mdanganyika na hivyo walikununulia wewe manati ya ndhungu. Walalama nini sasa zinapotekeleza lengo la kununuliwa kwake ilhali ulijua wamezinunua kwa ajiri yako? Simo.

Nasema ulidanganyika ulipodhani kwamba wao walio wazima wanajipanga kukutengenezea dawa wewe uliye mgonjwa ili urudie kuwa mzima na ukasahau kwamba kipande cha mkate ni kidogo na humu simo. Ona sasa wanalisha sumu kwa jina la dawa naapa kaya hii imekaa kichwa chini miguu juu. Ati! Matabibu wanapokuwa wauaji na walinzi wanapokuwa wadunguaji nani alaumiwe. Narudi zangu jalalani nisijechelewa vipande vya mkate na mabaki ya siagi ila humu mi simoe tena simo kabisaaaa, sihusiki.

Wasalaam, ni mimi nduguyo Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwelwa Mdanganyika, nakusalimia.

Sunday, November 11, 2012

Salaam za Mwana wa Muhangaikaji.

Kisiwani Mafia, linaonekana Gati la bandari ya kisiwa hiki likiendelea kujengwa. Hata hivyo Chokoraa nahoji juu ya uwepo wa 'utashi wa kisiasa' kulimaliza maana imekuwa muda mrefu tangu mradi huu kuanza. Simo humu namo.
 Marafiki wawili katika viunga vya mji wa Mafia.
Meli ya Black Tiger ikiwa imepaki kwenye pwani ya Bandari Salama. Meli hii hutumiwa na kampuni ya Alphagroup kusafirisha mizigo yake kati ya Daressalaam na Mafia.
 Ilikuwa ni siku ya Ijumaa, Chokoraa akitoka kisiwa cha Mafia kuelekea jiji la Daressalaam alipata nafasi ya kumshuhudia Mjasiriamali huyu akitoka kuchukua bidhaa kwa ajiri ya 'kibanda' chake akipishana na mabinti waliokuwa wakielekea kunako ibaada ya Ijumaa. 

Mojawapo ya misikiti ambayo hukosi kuishuhudia kwenye Barabara ya Dar- Mtwara kwenye eneo la Mkuranga Mkoani Pwani.
Mkoa wa Pwani pamoja na kuwa kandoni mwa Bahari una shida kubwa ya maji safi na salama kwa wakaazi wake wengi. Pembeni ya barabara kuu itokayo Mtwara kuelekea Dar, mkokoteni wa maji ukiwa umepaki kusubiri "oda" wa huduma zake. Dumu moja la maji huuzwa kati ya shilingi miambili na miatano kwa kutegemea uhitaji wa maji na eneo husika.
Kwenye eno la Mkuranga mkoani Pwani, biashara ya matunda kando ya barabara si jambo la kuuliza. Ha ha ha ha!! Chokoraa nilijichukulia matunda kwa ajiri ya kujenga afya.
Wilaya ya Mkuranga inavyo vituo vingi vya mafuta. Hapa ushushaji wa mafuta ulikuwa ukiendelea katika kukabiliana na tatizo la mafuta lililoikumba kaya yetu hii kwa wiki tatu mfululizo sasa. Hata hivyo ushushaji huo uliambatana na utoaji huduma jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa watu na mali na sijui kama mamlaka husika zinajua na kuchukua hatua japo za miguu tena za makusudi. Simo.
Katika maeneo ambayo watu wamejenga holela na kuingia hadi ndani ya hifadhi ya barabara ni pamoja na mkoa wa Pwani. Maeneo na majengo mengi yamepigwa alama za X kuonyesha kwamba yamejengwa kinyume na sheria kwenye hifadhi ya barabara, lakini hii ndiyo Danganyika ya Wadanganyika walipa kodi, usishangae mwenye bango akaliandika upya na baadaye likapigwa tena X. Ni mchezo wa kuku na yai. Simo.
Nilipata pia nafasi ya kushuhudia Kondakta wa daladala akimuaga abiria wake huku gari likianza mwendo. Pamoja na hatari ya mchezo huu wa kuchungulia nje gari likitembea, makondakta wengi wanaonekana kutojali madhara yake na hapo ndipo Chokoraa ninapojitoa. Simo.
Atimaye tukasimama kwenye Bar ya dream Pub kwa ajiri ya kujipatia chochote kitu. Karibu tule kama jasho la mtu laliwa yakhe!!!!
Baada ya misosi, tulikipita pia kituo hiki ambacho kingali kikiendelea kujengwa.
Mkombozi wa Chokoraa katika safari zake za hapa na pale katika chakura chakura yangu majalalani. Ha ha ha ha ha!!! Jina la Kiswahili lakini hii siyo 'made in Kipawa bali made in China na hapo ndipo ninapojitoa, simo..

MSAFIRI KAFIRI

Ha ha ha ha ha ha ha! Naapa kwa hili hata kama mkigombana nami sitajari maana simo. Ati wadanganyika wanao msemo wao 'ma harufu' kwamba Msafiri Kafiri na mimi nauliza mwamaanisha nini enyi wana!?. Je! Kwamba msafiri kwa sababu ya shida za kushindwa kwenu kuwa ma mifumo bora ya usafiri, basi humlazimu kuweka kando imani ya dini yake na kuwa Kafiri!? Au kwamba ...........................
Wiki hii Chokoraa naye alikuwa "Kafiri"
Rubani wa 'boti' itokayo kisiwa cha Mafia kuelekea Nyamisati na mimi nauliza kama hawa waitwa Marubani, wa gari mwaita Madereva, mwendesha Baiskeli aitwaje!? Simo.

Hii ndiyo 'Festi Klass' na Chokoraa nauliza 'Thedi Klasi' ina hali gani!!!? Simo.
 Kwa ulingano huu wa idadi ya Abiria na Maboya, ajali ikitokea mtasema "Kazi ya Mungu haina makosa" kana kwamba na yeye ni mzembe kama ninyi. Simo humu naapa.
Mheshimiwa Diwani mtaasu wa kata ya Kilindoni naye alikuwamo kwenye msafara huu akielekea Dodoma kwenye mkutano mkuu wa  CCM

Tuesday, October 16, 2012

Nasema tena kama nilivyowahi ksema ili msijesema mi sikusema wakati watakaposema wale waliosema mapema, kuchanganya "si hasa" na taaluma ndiyo ugonjwa unaowaumiza wadanganyika walipa kodi na mimi humu Simo. Haya tena, Dk. Robert Ntakamulenga awafungulia SBS baada ya kuwa wamefungiwa kwa tuhuma za kuchafua mazingira. Chokoraa nilikuwapo kushuhudia na humu mi simo.
Dk. Ntakamulenga akitoa maelekezo kwa mkurugenzi Mtendaji wa Supply Base Solutions (SBS) Ltd kuhusu hatua za kuchukua kuhakikisha usalama wa mazingira kwenye eneo la Mdenga, kata ya Likonde wilaya ya Mtwara Mikindani.

Dk. Ntakamulenga (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa SBS Bw. Ganeshani Vedagiri na mshauri mwelekezi wa mazingira Bw. Abel Sikaona wakitazama bwawa maalumu la kuchuja maji kwenye kiwanda cha kutekeketeza takataka kinachomilikiwa na SBS.

Afisa Mwandamizi wa mazingira kutoka baraza la mazingira Tanzania (NEMC) Bi. Nengia Mollel (kushoto), mwanasheria wa NEMC Bw. Heche (kulia) na mtaalamu kutoka ofisi ya mkemia mkuu (mwenye Tshirt ya blue bahari) wakisikiliza maelekezo kutoka mmoja wa Wakurugenzi wa NEMC Dk, Robert Ntakamlenga.
Mafundi wa kampuni ya SBS wakiwa kazini kwao wakati wa ziara ya Dk. Ntakamlenga kwenye kiwanda chao.
Afisa Mwandamizi kutoka NEMC Bi. Nengia Mollel akirekodi kumbukumbu zake wakati wa ziara ya wataalamu hao kwenye kiwanda cha uchomaji taka cha SBS kwenye mtaa wa Mdenga, Manispaa ya Mtwara Mikindani.



Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya SBS Bw. Ganeshan Vedagiri akitoa maelezo kwa mkurugenzi wa NEMC wakati wa ziara ya mkurugenzi huyo kiwandani hapo.
Bi. Nengai Mollel akitoa maelekezo kwa wenyeji wake wakati wa ziara hiyo. Huyu Mrembo, duh!!!. Sisemi. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa SBS akimsikiliza kwa makini.

Mshauri mwelekzi wa mazingira wa SBS Bw. Abel akijieleza mbele ya Dk. Ntikamlenga.

Sikiliza hii. Simo.

NA KUTOKA MKOANI MWANZA UCHAGUZI WA NDANI WA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) WAIBUA MAMBO MAZITO.

Jiji la mwanza, hasa huku kwetu uswazi, Ha ha ha ha ha ha!!! Simo.

Waziri na Mbunge wa Zamani wa Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza Bw. Antony Diallo, aibuka mshindi wa kiti cha mwenyekiti.
"Muishiwa" sana Antony Diallo akitoa neno la shukurani kwa wajumbe baada ya kuchaguliwa, kulia kwake ni 'Muishiwa' wazi hili Lukuvi.

Mh. Lukuvi naye alikuwa na neno kwa wajumbe.


Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza na Diwani wa Kata ya Mkolani Mh. Stanslausi S. Mabula naye alikuwapo kushuhudia kinyang'anyiro hicho. Sihusiki.