Sunday, November 11, 2012

Salaam za Mwana wa Muhangaikaji.

Kisiwani Mafia, linaonekana Gati la bandari ya kisiwa hiki likiendelea kujengwa. Hata hivyo Chokoraa nahoji juu ya uwepo wa 'utashi wa kisiasa' kulimaliza maana imekuwa muda mrefu tangu mradi huu kuanza. Simo humu namo.
 Marafiki wawili katika viunga vya mji wa Mafia.
Meli ya Black Tiger ikiwa imepaki kwenye pwani ya Bandari Salama. Meli hii hutumiwa na kampuni ya Alphagroup kusafirisha mizigo yake kati ya Daressalaam na Mafia.
 Ilikuwa ni siku ya Ijumaa, Chokoraa akitoka kisiwa cha Mafia kuelekea jiji la Daressalaam alipata nafasi ya kumshuhudia Mjasiriamali huyu akitoka kuchukua bidhaa kwa ajiri ya 'kibanda' chake akipishana na mabinti waliokuwa wakielekea kunako ibaada ya Ijumaa. 

Mojawapo ya misikiti ambayo hukosi kuishuhudia kwenye Barabara ya Dar- Mtwara kwenye eneo la Mkuranga Mkoani Pwani.
Mkoa wa Pwani pamoja na kuwa kandoni mwa Bahari una shida kubwa ya maji safi na salama kwa wakaazi wake wengi. Pembeni ya barabara kuu itokayo Mtwara kuelekea Dar, mkokoteni wa maji ukiwa umepaki kusubiri "oda" wa huduma zake. Dumu moja la maji huuzwa kati ya shilingi miambili na miatano kwa kutegemea uhitaji wa maji na eneo husika.
Kwenye eno la Mkuranga mkoani Pwani, biashara ya matunda kando ya barabara si jambo la kuuliza. Ha ha ha ha!! Chokoraa nilijichukulia matunda kwa ajiri ya kujenga afya.
Wilaya ya Mkuranga inavyo vituo vingi vya mafuta. Hapa ushushaji wa mafuta ulikuwa ukiendelea katika kukabiliana na tatizo la mafuta lililoikumba kaya yetu hii kwa wiki tatu mfululizo sasa. Hata hivyo ushushaji huo uliambatana na utoaji huduma jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa watu na mali na sijui kama mamlaka husika zinajua na kuchukua hatua japo za miguu tena za makusudi. Simo.
Katika maeneo ambayo watu wamejenga holela na kuingia hadi ndani ya hifadhi ya barabara ni pamoja na mkoa wa Pwani. Maeneo na majengo mengi yamepigwa alama za X kuonyesha kwamba yamejengwa kinyume na sheria kwenye hifadhi ya barabara, lakini hii ndiyo Danganyika ya Wadanganyika walipa kodi, usishangae mwenye bango akaliandika upya na baadaye likapigwa tena X. Ni mchezo wa kuku na yai. Simo.
Nilipata pia nafasi ya kushuhudia Kondakta wa daladala akimuaga abiria wake huku gari likianza mwendo. Pamoja na hatari ya mchezo huu wa kuchungulia nje gari likitembea, makondakta wengi wanaonekana kutojali madhara yake na hapo ndipo Chokoraa ninapojitoa. Simo.
Atimaye tukasimama kwenye Bar ya dream Pub kwa ajiri ya kujipatia chochote kitu. Karibu tule kama jasho la mtu laliwa yakhe!!!!
Baada ya misosi, tulikipita pia kituo hiki ambacho kingali kikiendelea kujengwa.
Mkombozi wa Chokoraa katika safari zake za hapa na pale katika chakura chakura yangu majalalani. Ha ha ha ha ha!!! Jina la Kiswahili lakini hii siyo 'made in Kipawa bali made in China na hapo ndipo ninapojitoa, simo..

MSAFIRI KAFIRI

Ha ha ha ha ha ha ha! Naapa kwa hili hata kama mkigombana nami sitajari maana simo. Ati wadanganyika wanao msemo wao 'ma harufu' kwamba Msafiri Kafiri na mimi nauliza mwamaanisha nini enyi wana!?. Je! Kwamba msafiri kwa sababu ya shida za kushindwa kwenu kuwa ma mifumo bora ya usafiri, basi humlazimu kuweka kando imani ya dini yake na kuwa Kafiri!? Au kwamba ...........................
Wiki hii Chokoraa naye alikuwa "Kafiri"
Rubani wa 'boti' itokayo kisiwa cha Mafia kuelekea Nyamisati na mimi nauliza kama hawa waitwa Marubani, wa gari mwaita Madereva, mwendesha Baiskeli aitwaje!? Simo.

Hii ndiyo 'Festi Klass' na Chokoraa nauliza 'Thedi Klasi' ina hali gani!!!? Simo.
 Kwa ulingano huu wa idadi ya Abiria na Maboya, ajali ikitokea mtasema "Kazi ya Mungu haina makosa" kana kwamba na yeye ni mzembe kama ninyi. Simo humu naapa.
Mheshimiwa Diwani mtaasu wa kata ya Kilindoni naye alikuwamo kwenye msafara huu akielekea Dodoma kwenye mkutano mkuu wa  CCM

Tuesday, October 16, 2012

Nasema tena kama nilivyowahi ksema ili msijesema mi sikusema wakati watakaposema wale waliosema mapema, kuchanganya "si hasa" na taaluma ndiyo ugonjwa unaowaumiza wadanganyika walipa kodi na mimi humu Simo. Haya tena, Dk. Robert Ntakamulenga awafungulia SBS baada ya kuwa wamefungiwa kwa tuhuma za kuchafua mazingira. Chokoraa nilikuwapo kushuhudia na humu mi simo.
Dk. Ntakamulenga akitoa maelekezo kwa mkurugenzi Mtendaji wa Supply Base Solutions (SBS) Ltd kuhusu hatua za kuchukua kuhakikisha usalama wa mazingira kwenye eneo la Mdenga, kata ya Likonde wilaya ya Mtwara Mikindani.

Dk. Ntakamulenga (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa SBS Bw. Ganeshani Vedagiri na mshauri mwelekezi wa mazingira Bw. Abel Sikaona wakitazama bwawa maalumu la kuchuja maji kwenye kiwanda cha kutekeketeza takataka kinachomilikiwa na SBS.

Afisa Mwandamizi wa mazingira kutoka baraza la mazingira Tanzania (NEMC) Bi. Nengia Mollel (kushoto), mwanasheria wa NEMC Bw. Heche (kulia) na mtaalamu kutoka ofisi ya mkemia mkuu (mwenye Tshirt ya blue bahari) wakisikiliza maelekezo kutoka mmoja wa Wakurugenzi wa NEMC Dk, Robert Ntakamlenga.
Mafundi wa kampuni ya SBS wakiwa kazini kwao wakati wa ziara ya Dk. Ntakamlenga kwenye kiwanda chao.
Afisa Mwandamizi kutoka NEMC Bi. Nengia Mollel akirekodi kumbukumbu zake wakati wa ziara ya wataalamu hao kwenye kiwanda cha uchomaji taka cha SBS kwenye mtaa wa Mdenga, Manispaa ya Mtwara Mikindani.



Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya SBS Bw. Ganeshan Vedagiri akitoa maelezo kwa mkurugenzi wa NEMC wakati wa ziara ya mkurugenzi huyo kiwandani hapo.
Bi. Nengai Mollel akitoa maelekezo kwa wenyeji wake wakati wa ziara hiyo. Huyu Mrembo, duh!!!. Sisemi. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa SBS akimsikiliza kwa makini.

Mshauri mwelekzi wa mazingira wa SBS Bw. Abel akijieleza mbele ya Dk. Ntikamlenga.

Sikiliza hii. Simo.

NA KUTOKA MKOANI MWANZA UCHAGUZI WA NDANI WA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) WAIBUA MAMBO MAZITO.

Jiji la mwanza, hasa huku kwetu uswazi, Ha ha ha ha ha ha!!! Simo.

Waziri na Mbunge wa Zamani wa Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza Bw. Antony Diallo, aibuka mshindi wa kiti cha mwenyekiti.
"Muishiwa" sana Antony Diallo akitoa neno la shukurani kwa wajumbe baada ya kuchaguliwa, kulia kwake ni 'Muishiwa' wazi hili Lukuvi.

Mh. Lukuvi naye alikuwa na neno kwa wajumbe.


Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza na Diwani wa Kata ya Mkolani Mh. Stanslausi S. Mabula naye alikuwapo kushuhudia kinyang'anyiro hicho. Sihusiki.


Thursday, October 11, 2012

Chokoraa nahama 'Mjini'.



Nawaomba msihoji uzalendo wangu na wala msinione mwoga ila nasema wazi Chokoraa nahama mjini.  Naapa kwa jina lake mama yangu Shida wa Matatizo binti Huzuni wa Sikitiko wa Taabu Mateso Mengi humu simo , tena simo kabisaaa. 

Nasema tena msijesema sikusema na naweka kumbukumbu sawa kabla sijafunga vilango kurejea zangu shamba kwenye kile kibanda cha marehemu bibi yangu alichoachiwa na marehemu mumewe Kabwela wa Mdanganyika, na hapo ni ikiwa hakijauzwa kwa bei chee kwa mkulima wa matuta hamsini ya nyanya ila mwenye umaarufu wa harufu kwa vile anapaka yale marashi ya siku hizi yajulikanayo humu mjini kwenu kama ‘Ukewenzaji’ na humu simo.  Simo.
Salaale!! Mwanitisha enyi wana na sasa sijui ikiwa nikitoka kwenye pagala langu kwenda kuokoteza majalalani niwaambieje wadogo zangu akina Mzembe na Mzururaji ama kwamba ‘tutaonana jioni’ ama niage kabisa!? 

Ati washangaa!? Washangaa nini ikiwa siku hizi kukiwako tu na taarifa za “kiintelijensia” kwamba Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika anaunda mabomu ya ‘nyuki hulia’ hakuna anayejali hata kutaka kutumia walau sehemu kiduchu ya ‘intelijensi’ yake kupima ikiwa kweli ‘intelijensia’ hizo ni sahihi anachofanya ni kuvuta  “manati ya ndhungu” na halengi miguu bali kichwa!? Naapa, kaya ya wadanganyika si salama kwa akina Chokoraa, labda kaka zetu akina Mstahiki na Muishiwa wao kwa vile wanafanya makosa yaliyofanyiwa upembuzi yakinifu. Wallahi twahitaji tena akina Nyerere na Kwame Nkurumah na humu mi naapa sihusiki. 

Kwani mmeanza leo enyi walinzi wa amani mliogeuka kuwa wavuruga amani na sasa mmekuwa tishio la raia!? Nani hajui  Wambeya walivyopoteza vitegemezi vyao kwenye ‘risero’ na bado tukaambiwa na ‘kamati teule’ juu ya ‘makosa ya kiufundi’ na kwamba hatua za miguu zimechukuliwa kukomesha vifo hivi!? Hamkutosheka enyi wana na sasa kila aliye na “manati ya ndhungu” akijisikia anadungua yeyeote amtakaye!  Naapa kwa Muumba wa mbingu na ardhi Chokoraa nina mashaka na kichwa changu maana mawe ya manati zenu yanaviona zaidi vichwa vya Kunguru kuliko Mbuni kisa si kwamba Kunguru ni mwizi sana, lakini anawanyima usingizi akina Mbuni waishio kwenye majumba ya starehe na humu miye simo. 

Kwani nini tofauti kati ya Punda na Farasi au Kunguru na Mbuni isipokuwa aina ya maisha waishiyo ilhali wote wakiwa ni ndege na wayama na humu miye nahusika kwani!? Kama haikuwatosheni enyi wenye dhamana ya uhai na mamlaka ya kuutwaa wa kwetu na kuutoa sadaka huku mkijisafi kwa ‘mizimu weupe’ kwa damu zetu na wao wakiwapa ‘manati’ zaidi kwa vile hilo hasa lawaongezeeni ninyi uishiwa na wao ‘shekeli’ zitokanazo na ‘mali asili’ za ardhi yenu hii ya wana wa Hamu, mkawachukua baadhi ya kaka zetu na kuwapeleka kwenye ule msitu mkuubwa mtoleako sadaka za damu ya wana wa Adamu na kuwachinjilia mbali na kisha mkatwambia  “yarikuwa yakipambana na ‘hofu ya raia” tukakaa kimya si kwa vile tuliwakubalia bali kwa vile tuliogopa kesho isiwe zamu yetu. 

Nasema hata pale mlipoanza kuchunguzana huku mkikonyezana na kuzungumza kwa uchungu wa kujifanya, Chokoraa nilijua igizo hili limemkosa tu Muhogo Mchungu lingenoga lakini sikufumbua kinywa hadi ati “siri kali” ilipopoteza kwenye shauri hilo watoto na wake wa ‘wajasiria mlo’ wale wakabaki wajane na yatima likaisha. Nina uchungu lakini simo. 

Kama haikuwatosha ni hivi majuzi tu mkaamua kumuua sisimizi kwa risasi ya Tembo ati kwa vile sisimizi huyu ni mmoja wa wale wenye kupanda kwa siri kwenye nguo zenu na kuyajua yale tusiyoyajua na kisha kuyaanika hadharani, naapa hii tabia ya “hivi unanijua!” itawamaliza wanaobaki mjini maana Chokoraa siji tena mjini na humo wala msinihusishe maana simo. 

Haya, jiosheni muosheke basi kwa wana na mjane wa Yule mliyemtandika bomu la machozi na kumtoa damu ya uhai kama mwaweza.  

Haya, tena juzi juzi  tu wanafunzi wakiwa kwenye michezo ya kujificha kwenye eno la hifadhi, wenye manati za ndhungu, tena za ‘siri kali’ ya kaya yao, wamewakomelea hadi umauti na Chokoraa nauliza, hivi mwawapima vyema hawa mnaowakabidhi hizi manati au kila mmoja sasa anaweza kubeba manati na akiogopa kidogo tu basi anadungua!? Jibu msinipe, lakini wafundeni basi walau kwamba watumia ‘intelijensi’ zao kuamua ikiwa intelijensia wanazopata zinatosha kuwapa kibali cha kudungua ama lah, vinginevyo Chokoraa sirudi mjini na humu mi sihusiki.


Ni mimi ndugu yenu Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa mDanganyika nawasalimia. Simo.

Thursday, September 27, 2012

Mji wa Mafia (Kilindoni) na viunga vyake.

Nauliza hivi! Mafia si mji wa utalii!!? Inakuwaje mwaliacha soko la mji huu kuwa chafu kiasi hiki? Haya siyo maji yaliyotuama kwa sababu ya mvua maana msimu wa mvua kisiwani hapa bado, lakini ni maji kutoka kwenye vibanda vya 'Mama Lishe' walioko ndani ya soko kuu la Mafia. Simo humu naapa.

Tungali bado kwenye viunga vya mji wa Mafia na hapa ni sokoni. Ha ha ha ha ha ha!!! Nicheke ninenepe Chokoraa wa watu.
Huku ni mwendo wa "ushungi" aisee, Usije na vimini na vipedo vyenu mnavyovalishana mkituonyesha siri zenu enyi wana na humu mi simo.

Chokoraa nilipata pia nafasi ya kutembelea ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mafia na hili ndilo jengo la "Muishiwa" huyu. Ha ha ha ha ha! Ati hapo inapopepea bendera ya kaya yetu hii, miaka kadhaa kabla ya 1961 ilipepea bendera ya "mkoloni". Simo humu miye.

Usiache kunitumia barua na hata kifurushi kutokea huko kwenu ughaibuni kwa anuani ifuatayo: Mheshimiwa Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika, S.L.P .....Mafia, Pwani ya Wadanganyika. Pia biashara ya kuuza vocha inaendelea hapa na mimi nauliza haya makampuni ya simu yanalipia ushuru!!!!? Simo.
'Prezidenti' wa Wilaya, D.C ama ukipenda Mkulu wa Kaya wa Mafia ana ofisi zake hapa na hili lote ni jengo la ofisi za "muishiwa" huyu. Ati! Mtu mmoja jengo lote hili na mwalimu aliwahi kuuliza "...kwani mi tembo?". Na hii je!!!!!? Sihusiki naapa, simo.
Usitie shaka kuja na Njuluku, Pesa, Sinyingi, Hela, Chokoraa naita "Shekeli" zako huku kwetu maana hata sisi tunayo "Nyumba ya hela" na inayo "Ei tii Emu" inayofanya kazi saa 24 mfululizo. Sihusiki bado.
Uwanja wa ndege wa Mafia. Jengo hili halitumiki kwa sasa kwa sababu uwanja uko kwenye matengenezo makubwa ukitarajiwa kuwa na jengo la kisasa kabisa lakini hii ndiyo hali halisi miaka 50 baada ya uhuru. Sihusiki mimi humu..
'Muishiwa' Batuli, Diwani wa Kata ya Kirongwe, Kata ya Kaskazini Mafia akielezea jambo tulipokutana naye kwenye kijiji cha Jimbo huko Mafia. Wa kwanza kulia ni Dk. Kiwia, mtaalamu wa Uvuvi wenyewe twaita Fisheries. Nahusika kwani miye humu!!!? Simo.
 Dk. Kiwia kutoka Fisheries, Ndg Makongoro mtaalamu wa mazingira, Chokoraa wa Muhangikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika, 'Muishiwa Diwani wa Kirongwe, Muishiwa Mwenyekigoda wa Kijiji cha Banja wakimsikiliza mwananchi akidadavua mada kwenye mkutano. Ha ha ha ha ha!!! Nijitoe na humu?. Simo.

FOTOA FOTO YA CHOKORAA KISIWANI MAFIA.

Nasema humu Chokoraa sihusiki na simo tena simo kabisaaaaa!!! Ala! Nani kakwambia Chokoraa nakaa jalala moja!? Nilikwenda kisiwa cha Mafia juma lililopita na katika pita pita yangu kwenye majalala yangu nikakutana na hali hii, nikaamua kufanya katabia kangu kaleeee ka zamani nilikokatazwa nisisikie yaanI "FOTOA FOTO". We kuwamo humu japo mi simo tena simo kabisaaaaaaa.
Kwanza ni "Usafiri" wetu. Hapa kwetu Mafia hatuna "Teksi" na wala huo upuuzi wenu wa kutumia magari hata kwa safari fupi kisa mwaonyesha ufahari wa kuwa na mafedha kedekede sisi hatumo na humu Chokoraa nilikataa kuhusika. Kuna njia mbili tu za kuingia kisiwa hiki chenye utajiri wa mali na utu na mara unapofika ama kwenye bandari yetu kongwe isiyoendelezwa bado ukitumia usaifiri wa "boti" kutokea Nyamisati au wale "waishiwa" msiochoka kuishiwa mkijifanya kutumia "ulozi wa ndhungu" kwa kupanda 'ungo' mchana kweupeeeee! Na humo simo, hata hivyo usaifiri wako wa kuzunguka mjini humu ni pikipiki iwe ya matairi mawili almaarufu "Bodaboda" ama matairi matatu almaarufu "Bajaji". Teksi zenu tupa kule!!! Simo nasema.
Halafu! Huku kwetu ule uchafu wenu muutiao barabarani mkiifanya nyeusi tiii kama mkaa ati wenyewe mwaita lami huku sisi upuuzi huo hatuna hata mmoja. Huu mji wa kitalii bwana lazima uwe "nechuro". Ha ha ha ha ha ha!!! Sihusiki miye humu naapa.
Halafu nani kasema ati wanawake wa Pwani hawajui kutafuta pesa ila akina "Manka" peke yao!!!? Nyooo!! Simo. Hapa kwetu sokoni kwa lugha ya 'Ami' yangu wa kule Mchambawima paitwa "Malikiti" akina mama wanauza kitoweo. Yaani akina baba wavua, na akina mama wauza na wote watia kipato ndani ya nyumba sasa hilo la haki sawa mwalikataa kwanini!!!? Simo humu miye.


"Si hasa" za Kaya yetu nazo zatuhusu na sisi twahusika. Hapa ni kikao cha kamati za vijiji vya Banja na Jojo kilichofanyika shule ya msingi Banja ambapo wanavijiji hawa walikutana na wataalamu wa mazingira na hapa mmoja wa wanakamati akihoji swali na kutoa maoni yake. Ha ha ha ha ha!! Nisifurahi kwanini Chokoraa miye.


Kwenye kikao hiki, ndugu yenu Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika nilikaribishwa niketi na mimi pamoja na wakuu na sikufungua kinywa kunena bali kusikiza yale yaliyosemwa na wana kaya maana simo.

 Huyu si mgonjwa jamani kwamba anakandwa mkono umevunjika ama kakutwa na madhila. La hasha! Anapambwa mtoto wa kike kabla ya harusi na kama huyajui haya basi hujafika Pwani weye na mi humo simo, tena simo kabisaaaaaaaa.

 Haya tena, kishapendeza mtoto wa kike asubiriwa somo hapa mambo yaanze. Ha ha ha ha ha ha! Tembea ulishe macho yako wewe! Kila siku kumshangaa Chokoraa, ohoo! mara Chokoraa ana maneno mengi! Si nimeona mengi!!!? Simo humu miye.

Somooooooooo!!!! Yuko wapi somoye harusi jamani aje hapa tuhangaike naye, nasema aje hapaa, nasema aje hapaa, nasema aje hapaaa!!!!!!!! Nahusika humu kwani miye!? Simo.



Haya, kwa leo nakomea hapa. Ni mimi ndugu yenu Chokoraa wa Muhangaikaji wa Mlalahoi wa Pangupakavu wa Kabwela wa Mdanganyika, nawasiliamia.

Saturday, July 14, 2012

Chokoraa na 'Fotoa Foto'

Hapa ni "Ng'wanza" wenyewe mwaita 'Mwanza'. Tumekuja kushuhudia mchakato wa BSS chini ya udhamini wa Zantel.
Ha ha ha ha ha ha!!! Ati wajiuliza namaanisha nini? Kwani mbona wewe hutambai tena siku hizi!? Ndiyo, nasema na Chokoraa anakua na kuongezeka na hizo ni baraka za jalali na kama unabisha basi kwenye huo ubishi mi simo tena simo kabisa. Ala!. Haya basi, kuanzia sasa naanza kuwaletea picha kadha wa kadha ambazo Chokoraa wa Kabwela amekutana nazo kwenye kuchakulachakula majalalani huku na huko, walau kila mwisho wa Wiki.

Wiki hii, meli maarufu kwa kusaifirisha mizigo toka Bandari Salama hadi kisiwa cha Mafia iliteketea kwa moto baada ya mmoja wa wafanyakazi wake kujaribu kuwasha jenereta ili ku-pump nje shehena ya mafuta ya Tanesco yaliyokuwa ndani ya meli hiyo.

Wananchi wakishuhudia meli hiyo ikiteketea kwa moto. Wananchi wamekitupia lawama kikosi cha Zimamoto wilayani Mafia kwa kushindwa kuonyesha makeke yoyote kwenye tukio hilo. Hata hivyo, shehena ya mafuta iliyokuwemo kwenye meli hiyo iliokolewa yote ilhali kiasi cha pikipiki mbili, na gari moja vilivyokuwa mali ya watu binafsi vinaripotiwa kuteketea kabisa. Hili ni tukio la pili kwa meli iliyobeba shehena ya mafuta ya Tanesco kupata mushkeli ambapo miaka kadhaa meli nyingine ikiwa na shehena ya mafuta ya Tanesco ilizama baharini ikitokea Dare salaam kwenda kisiwani Mafia.